Wednesday, April 29, 2015

Maelezo Zaidi Kuhusu Filamu ya "Papa's Shadow"

Wakati huu ninapoandika makala hii niko na binti zangu Deta na Zawadi, tunaangalia filamu ya Papa's Shadow, iliyotngenezwa na Jimmy Gildea, aliyekuwa mwanafunzi katika kozi niliyofundisha Tanzania Januari, 2013. Nimeshaitaja filamu hii katika blogu hii

Maelezo yanayoambatana na filamu ni haya:

FEATURING AN EXCLUSIVE TESTIMONY GRANTED BY HIS SON, PATRICK HEMINGWAY, PAPA'S SHADOW DIVES HEAD FIRST INTO AUTHOR ERNEST HEMINGWAY'S HUNTING EXPEDITIONS IN EAST AFRICA AND THEIR DEFINING ROLE IN SHAPING A LEGEND.

YOUNG FILMMAKER JIMMY GILDEA DOCUMENTS HIS EXPERIENCE WHILE STUDYING HEMINGWAY UNDER THE INSTRUCTION OF AFRICAN AUTHOR JOSEPH MBELE, JOURNEYING ACROSS MIDWEST AMERICA, THROUGH THE SERENGETI PLAIN AND UP THE STEEP CLIFFS OF MT. KILIMANJARO.

HEMINGWAY'S SON PATRICK AND MBELE ENGAGE IN AN INSPIRATIONAL AND REVEALING CONVERSATION REGARDING THE FAMOUS AUTHOR'S FASCINATING RELATIONSHIP WITH EAST AFRICA.

THIS PERSONAL AND EMOTIONAL FILM EXPOSES MANY ANSWERS TO QUESTIONS HEMINGWAY FANS HAVE ALL BEEN WAITING FOR.

Hii ni mara yangu ya pili kuiangalia filamu hii, na kuona jinsi Mzee Patrick Hemingway na mimi tunavyomwongelea Ernest Hemingway: maisha yake, uandishi wake, na falsafa yake. Ninajionea faida ya kusoma, kusoma kwa dhati, bila kuchoka. Ninafurahi kuwa wanangu wanajifunza jambo kutoka kwangu.

Lengo langu kuu katika kuunda kozi yangu, ambayo ni chimbuko la filamu hii, lilikuwa kuuelimisha ulimwengu kuhusu namna Hemingway alivyoipenda Afrika Mashariki. Kwa upande wa Tanzania, nilitaka walimwengu wafahamu namna Hemingway alivyoandika kuhusu Serengeti, Mlima Kilimanjaro, na kadhalika. Huu ni ukweli juu ya Hemingway ambao haufahamiki vizuri, au umefunikwa kwa makusudi kwani wengi, wamezoea tangu zamani kuiona Afrika kwa dharau. Filamu hii itasaidia kurekebisha jadi hiyo.

Tuesday, April 28, 2015

Leo Nimeonana na Mtengeneza Filamu ya Hemingway

Leo nimeonana na Jimmy Gildea, mtengenezaji wa filamu ya Papa's Shadow. Jimmy alikuwa mmoja wa wanafunzi wa Chuo cha St. Olaf waliokuja Tanzania, Januari 2013, kwenye kozi yangu Hemingway in East Africa.

Filamu yake imetokana na kozi ile, na watakaobahatika kuiangalia watajifunza mengi kutoka kwa Mzee Patrick Hemingway, motto pekee aliyebaki wa Ernest Hemingway aliyebaki,  na mimi, ambao ni wazungumzaji wakuu.

Tumeongea kwa saa moja na robo hivi, kuhusu filamu yake na masuala yanayohusika nayo. Tumeongelea mikakati ya kuitangaza filamu hiyo, fursa za kuionyesha katika matamasha, vyuoni, na kadhalika.

Tumeongelea safari yetu ya Montana tulipoenda kuongea na Mzee Patrick Hemingway, na jinsi alivyotufanyia wema wa kutueleza mengi juu ya baba yake. Tumejikumbusha jinsi alivyotugusa alipoelezea  hisia zake kuhusu hali ya baba yake iliyotokana na unywaji uliokithiri na pia ajali za ndege nchini Uganda zilizohujumu afya yake kwa miaka yote hadi kifo chake. Niliyafahamu mambo hayo kutokana na kusoma mimi mwenyewe, na wanafunzi niliwaeleza, lakini kumsikiza Mzee Patrick Hemingway akiyaelezea ilitugusa kwa namna ya pekee.

Tumeelezana kuridhika kwetu na filamu hii, nami nimemweleza Jimmy kuwa yote aliyokumbana nayo katika kuitengeneza filamu hii ni mafundisho yatakayomsaidia katika kutengeneza filamu zingine. Jimmy, kama anavyofanya siku zote anashukuru kuwa katika kozi yangu, ambayo ilikuwa mwanzo wa yeye kuifahamu Afrika, ambayo imemgusa na kubadili mtazamo wake wa maisha, na imekuwa chachu ya yeye kuitengeneza filamu hii.

Ni mwalimu yupi asiyefurahi kuona matunda mema namna hii ya kazi yake? Ni furaha kwangu kuongea na wanafunzi wangu na kuwahamasisha katika mkondo wa maisha waliojichagulia. Nimemhakikishia Jimmy, kama ilivyo desturi yangu, kwamba wakati wowote akihitaji ushauri au barua ya utambulisho ajisikie huru kuwasiliana nami.

Monday, April 27, 2015

Ushauri kwa Waandishi Chipukizi

Mara kwa mara, ninapata ujumbe kutoka kwa waandishi chipukizi wa-Tanzania wakiniomba ushauri kuhusu masuala ya uandishi, uchapishaji, na uuzaji wa vitabu. Ninafurahi kuwapa ushauri wowote ninaoweza, kutokana na uzoefu wangu.

Ninataka wafanikiwe. Kwa mfano, ninajisikia vizuri ninapoona mafanikio ya mwandishi chipukizi Bukola Oriola kutoka Nigeria, ambaye anaonekana nami pichani hapa kushoto. Nilisoma katika gazeti hapa Minnesota kuwa alikuwa na mswada, ila hakujua afenyeje ili kuuchapisha. Niliona ni lazima nimsaidie.

Ingawa hatukuwa tunafahamiana, nilimwandikia na kumweleza kuwa nilikuwa tayari kumsaidia kuchapisha kitabu chake, bila usumbufu wala gharama. Tulipanga siku, akaja ofisini kwangu, nikamwelekeza namna ya kutumia tekinolojia ya uchapishaji mtandaoni kwenye tovuti ya lulu.

Kitabu alichapisha, Imprisoned: The Travails of a Trafficked Victim, ambacho kimechangia kumpa umaarufu hapa Minnesota. Anaalikuwa kutoa mihadhara; anahojiwa katika televisheni, na anaendesha kipindi chake cha televisheni. Kila ninaposoma habari zake au ninapomwona katika televisheni napata raha moyoni kwa kuwa nimechangia mafanikio yake.

Hao waandishi chipukizi wa Tanzania nao napenda wafanikiwe. Nawaambia kuwa, pamoja na kuandika kama ninavyoandika, ninajielimisha kuhusu uandishi, uchapishaji, na uuzaji vitabu, kwa kununua na kusoma vitabu. Nao wafanye hivyo hivyo.

Nawaambia kuwa yale ninayojifunza nawafundisha wengine, katika maandishi yangu, kama vile kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, na katika blogu hii ya hapakwetu. Hakuna jambo ambalo nalijua ambalo sijalianika hadharani, liwafaidie wengine.

Juzi, nimepata ujumbe kutoka Tanzania, kwa mwandishi chipukizi mwingine. Ameniuliza nini cha kufanya, kwani amekuwa akiandika sana, na watu wanapenda maandishi yake, ila hajachapisha kitabu, kwa sababu hana uwezo. Nimemwambia kuwa itabidi tuwasiliane siku za usoni, kwa vile masuali yake ni mengi. Lakini, kwa vile anataka ushauri wangu,  aanze kwa kusoma kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii  na pia blogu yangu.

Nimemwambia kuwa ni lazima awe msomaji sana wa vitabu, kama nilivyosema katika blogu hii. Nakumbuka fundisho ambalo mwandishi Ernest Hemingway alimpa kijana mwandishi chipukizi aliyemwulizia ushauri. Hemingway alimwambia kuwa ni lazima asome vitabu vyote muhimu vilivyowahi kuandikwa, ili atambue mtihani ulio mbele yake wa kushindana na waandishi wale.

Kwa waandishi chipukizi wa Tanzania, napenda kuzingatia ushauri huo wa Hemingway. Wasome maandishi ya waandishi maarufu. Kama wana ndoto ya kuwa washairi, wasome Hamziya, Al Inkishafi, Utendi wa Mwana Kupona, Diwani ya Muyaka bin Haji al-Ghassaniy, Utendi wa Ras il Ghuli, Utendi wa Masahibu, Utendi wa Ngamia na Paa, mashairi ya Shaaban Robert, ya Gora Haji Gora, na kadhalika. Kama wanataka kuandika riwaya, wasome maandishi ya Shaaban Robert, Shafi Adam Shafi, Said A. Mohamed, Euphrase Kezilahabi, na kadhalika. Kwa juhudi hizi, waandishi chipukizi watajipatia ufahamu wa kuwawezesha kuandika kazi zitakazodumu kihistoria.

Saturday, April 25, 2015

Utitiri wa Blogu

Siku hizi, wa-Tanzania tuna utitiri wa blogu, blogu za kila aina. Pamoja na hayo, blogu zinaendelea kuibuka, kama uyoga. Mimi mwenyewe nimechangia utitiri huo. Nina blogu mbili: hii ya hapakwetu na nyingine ya ki-Ingereza.

Mtu akitaka, anaweza kushinda, na hata kukesha, anazisoma hizi blogu, na hataweza kuzimaliza. Wenye blogu na wadau tunaandika usiku na mchana, kwani tumeenea sehemu mbali mbali za dunia. Inapokuwa usiku Tanzania, huku ughaibuni ndio kwanza tunaamka, au ni mchana, alasiri au jioni, bado tuko kazini kwenye blogu. Mtu atasoma hadi achoke, hali sisi tunaendelea kudunda, kama wasemavyo mitaani.

Je, kuna ubaya wowote kuwa na utitiri wa blogu? Ni jambo jema, au ni jambo lisilostahili hata kuzungumzwa? Hili ndilo suali kuu ninalotaka kulitafakari, au kulianzishia mjadala.

Kwa upande mmoja, utitiri wa blogu ni jambo jema. Kumiliki blogu kunampa mtu fursa kamili ya kujieleza bila vizuizi ambavyo vinakuwepo kwenye magazeti na vyombo vingine vya habari ambavyo vinatawaliwa na watu wengine, kama vile wamiliki na wahariri. Kwa maana hiyo, blogu zinapanua uwanja wa uhuru na demokrasia ya kutoa maoni.

Kwa upande mwingine, kwa kuwa yeyote anaweza kuanzisha na kuendesha blogu, hata kama ni mbumbumbu, blogu zimekaribisha uwepo wa mambo ya kila aina, yakiwemo yasiyo na faida kwa umma, au ya ovyo. Ulimwengu wa blogu ni sawa na soko huria. Kuna vitu vya maana, mitumba michakavu, na bidhaa feki.

Utitiri wa blogu una athari zingine pia. Utitiri unasababisha ushindani mkubwa na imekuwa ni hali ya "mwenye mbavu mpishe." Wasomaji wanachagua blogu za kusoma, na kuna blogu ambazo hazijulikani sana, au zinajulikana na wenye blogu na wasomaji wachache.

Kutokana na hii hali ya "mwenye mbavu mpishe," blogu nyingi zinaibuka, na baada ya muda zinakufa. Zingine zinatoweka baada ya kitambo kifupi au kirefu, na baadaye zinajitokeza tena. Zingine zinaendelea kupumua na kujikongoja, ingawa mahututi, ila hazifi.

Bila shaka msomaji utakuwa na mtazamo wako. Kama unapenda kuchangia, nakukaribisha sana.


 

Wednesday, April 22, 2015

Filamu Inayoongelea Kozi Yangu Ya Hemingway

Leo, Jimmy Gildea, mmoja wa wanafunzi waliofika Tanzania mwezi Januari 2013, kwenye kozi yangu ya Hemingway in East Africa ameniletea nakala ya awali ya Papa's Shadow, filamu ambayo ameitengeneza kutokana na kozi ile. Nimeiangalia leo hii na binti yangu Zawadi, na tumeifurahia.

Wakati nilipokuwa nawachagua wanafunzi wa kuwepo katika kozi hii, Jimmy aliomba awemo katika msafara wetu ili akarekodi kumbukumbu ("documentary"). Alikuja na vifaa vyake, akawa anarekodi matukio na sehemu mbali mbali tulizotembelea, kama vile Arusha mjini, hifadhi za Ngorongoro na Serengeti, Karatu, na Longido.

Baada ya kozi kwisha, wazazi wa Jimmy, kaka yake na dada yake walifika kumchukua Jimmy wakaenda kupanda Mlima Kilimanjaro. Filamu inaonyesha safari hiyo pia, sambamba na maneno maarufu ya Hemingway aliyoyaweka mwanzoni mwa hadithi yake maarufu, The Snows of Kilimanjaro:

Kilimanjaro is a snow-covered mountain 19,710 feet high, and is said to be the highest mountain in Africa. Its western summit is called the Masai "Ngaje Ngai," the House of God. Close to the western summit there is the dried and frozen carcass of a leopard. No one has explained what the leopard was seeking at that altitude.

Jimmy alikuwemo katika safari yangu ya Montana kuonana na Mzee Patrick Hemingway. mtoto pekee aliyebaki wa Ernest Hemingway. Pichani hapo kushoto tunaonekana nyumbani kwa Mzee Hemingway katika mji wa Craig. Kuanzia kushoto ni Clay Cooper, Jimmy, Mzee Hemingway, na mimi. Clay alikuwa mmoja wa wanafunzi waliokuja kwenye kozi yangu Tanzania.

Pamoja na yote hayo, filamu inajumlisha pia sehemu alipozaliwa Ernest Hemingway, yaani Oak Park, na sehemu alipofia na kuzikwa, jimbo la Idaho. Filamu ina maelezo mengi ya Mzee Patrick Hemingway na mimi kumhusu Ernest Hemingway na maandishi na fikra zake. Jimmy aliwahi kunihoji kabla ya safari yetu ya Montana, na amejumlisha mengi niliyoyasema katika mahojiano yale.

Filamu hii ni kumbukumbu nzuri sana. Kwa namna ya pekee, inaitangaza Tanzania na Mlima Kilimanjaro, na inaitangaza kozi yangu, ambayo lengo lake lilikuwa kuuelimisha ulimwengu kuhusu jinsi Ernest Hemingway alivyoandika kwa umakini, ufahamu, na upendo mkubwa kuhusu watu wanyama, na mazingira kama alivyoshuhudia katika safari na kuishi kwake Afrika Mashariki miaka ya 1933-34 na 1953-54.

Kuna sehemu katika filamu ambapo Mzee Patrick Hemingway anakitaja kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho anakipenda, na tunamwona akisoma sehemu ya kitabu hicho, ukurasa 89, ambayo nimenukuu makala ya Ronald G. Ngala, iliyoandikwa kwa ki-Swahili. Mzee Patrick Hemingway anasoma nukuu hii pamoja na tafsiri yangu.

Ingawa tulimshuhudia Mzee Patrick Hemingway akisoma, mimi kama mwandishi wa kitabu hiki nimeguswa kuona tukio hili limo katika filamu. Baada ya kazi ngumu ya zaidi ya miaka miwili, filamu imekamilika, na inategemewa kupatikana siku za karibuni. Nitaleta taarifa.

Saturday, April 18, 2015

Misahafu na Balaa Linaloitwa Dini

Si kila kinachoitwa dini ni dini. Katika historia, kumekuwepo na uovu mwingi ambao umefanyika kwa jina la dini. Hadi leo, uovu wa aina hiyo unaendelea kufanyika. Siku nyingine, panapo majaliwa, nitaleta na kuongelea mifano, kwa uwazi na haki.

Misahafu imetumika na inaendelea kutumika kuhalalisha uovu. Kwa kiasi fulani hii ni kwa sababu mtu anaweza kuzipata nukuu kutoka katika msahafu ambazo zinapingana au zina utata. Lakini vile vile ni suala la tafsiri. Wataalam wa lugha wanatueleza kuwa matumizi ya lugha yanatoa mwanya wa tafsiri mbali mbali.  

Kwa msingi huo, watu waovu wanaweza kutafsiri nukuu za msahafu kwa namna ya kuhalalisha uovu. Katika tamthilia ya Shakespeare, The Merchant of Venice, Antonio anasema, "The devil can cite Scripture for his own purpose." Shetani anaweza kunukuu msahafu kwa faida yake mwenyewe. Historia imethibitisha ukweli huo tena na tena.
 

Tatizo jingine ni imani miongoni mwa waumini wa dini kwamba kila kilichomo katika misahafu sherti kikubaliwe na kufuatwa kilivyo, bila mabadiliko. Imani hii ni chanzo cha matatizo makubwa.

Mtu ukiusoma msahafu wowote bila upendeleo wala ushabiki, utaona kuwa msahafu ulitokea katika mazingira maalum ya kihistoria, kijamii, na kitamaduni. Kuna mambo katika misahafu ambayo yalikusudiwa kwa jamii za zamani, na hayatuhusu sisi watu wa leo.

Kwa msingi huu, ni muhimu tujijengee utamaduni wa kuichambua misahafu ili tuone ni yepi yanatufaa na yepi yaliwafaa watu wa zamani lakini hayatufai sisi watu wa leo.


Mungu ametujalia akili. Tuzitumie. Mungu ametuweka katika dunia tofauti na ile ya watu wa zamani. Tuna ufahamu  na akili tofauti na watu wa zamani, katika masuala kama haki za binadamu.

Utandawazi wa leo na tekinolojia imetupa ufahamu tofauti wa ulimwengu na watu wake, ufahamu wa mahusiano tunayoyahitaji katika dunia ya leo ambayo siku hadi siku inageuka kuwa kijiji.

Je, katika mazingira hayo, ni sahihi kuishikilia misahafu neno kwa neno, kikasuku, badala ya kupambanua yale yanayotuhusu na yale yaliyowahusu watu wa zamani? Je, ukasuku huu, unaosababisha au kuhalalisha balaa juu ya balaa, na maovu ya kila aina, ndio dini?

Kwa kumalizia ujumbe wangu, napenda kusisitiza mtazamo wangu kuwa mijadala ya dini ni muhimu, kama nilivyowahi kuelezea katika blogu hii.

 

Wednesday, April 15, 2015

Soma Misahafu Upate Akili, Halafu Changanya na Zako

Kati ya vitabu vinavyochangamsha na kutajirisha sana akili ni misahafu ya dini mbali mbali. Hayo ni maoni yangu, yanayotokana na uzoefu wangu. Ninayo misahafu ya dini kadhaa. Ninayo Qur'an, kwa miaka zaidi ya thelathini. Kabla ya kuipata Qur'an, nilikuwa na Biblia.

Qur'an niliipata kwenye mwaka 1984 nilipokuwa masomoni Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison. Kati ya marafiki zangu walikuwepo wa-Islam, na mmoja wao kutoka Sudan, alinitafutia Qur'an ilivyotafsiriwa kwa ki-Ingereza na Abdullah Yusuf Ali. Uzuri wa tafsiri hii ni kuwa ina maelezo mazuri ya vipengele mbali mbali.


Bhagavad Gita, msahafu maarufu wa u-Hindu, nilijipatia miaka ya hivi karibuni, sambamba na vitabu vingine vya dini hii.

Kwa nini mimi, ambaye ni m-Kristu (m-Katoliki) niwe na misahafu ya dini zingine? Kwa nini ninasoma, angalau kidogo kidogo, misahafu ya dini mbali mbali? Nina sababu zangu, na Mungu anajua, na ndiye atakayenihukumu.

Kwanza, ninatambua wajibu wa kuwaheshimu wanadamu wote. Mimi kama m-Kristu, nakumbuka Yesu alitupa changamoto kubwa pale alipotuasa kumpenda Mungu na kuwapenda watu wote, hata maadui zetu. Nina wajibu wa kuwafahamu wanadamu bila mipaka.

Mimi ni mwalimu wa fasihi za kimataifa. Ninaposoma na kufundisha fasihi za mataifa mbali mbali, ninapata fursa ya kuwafahamu wanadamu wa tamaduni mbali mbali. Kuzifahamu imani za dini zao ni hivyo hivyo. Ni muhimu kusoma misahafu ya dini mbali mbali, kama namna ya kuchangia maelewano.

Fasihi aghalabu zimefungamana na imani za dini. Bila kuyaelewa angalau mambo ya msingi ya u-Islam, kwa mfano, utafundishaje riwaya kama Twilight in Delhi, ya Ahmed Ali wa India na Pakistan; Minaret, ya Leila Aboulela wa Sudan; au The Fall of the Imam, ya Nawal el Saadawi wa Misri? Bila kuelewa angalau misingi ya u-Hindu, utafundishaje riwaya kama Untouchable, ya Mulk Raj Anand wa India? Bila kuielewa misingi ya u-Kristu, utafundishaje utungo wa Paradise Lost wa John Milton? Jawabu ni wazi: sherti nisome hiyo misahafu.

Sunday, April 12, 2015

Mazungumzo Kufuatia Mhadhara Lands Lutheran Church

Mhadhara wangu jana kwenye mkutano uliofanika katika kanisa la Lands Lutheran mijini Zumbrota, Minnesota, ulienda vizuri. Kulikuwa na mambo kadhaa katika ajenda, kama vile hotuba na ripoti mbali mbali, muziki na nyimbo. Halafu nilitambulishwa, nikatoa hotuba yangu fupi.

Mada yangu ilikuwa "The Dilemma of Cultural Differences: Challenges and Opportunites," ambayo inaendana na utafiti, uandishi, na mihadhara ambayo nimekuwa nikitoa sehemu mbali mbali. Niliongelea umuhimu wa kuzingatia athari za tofauti za tamaduni katika ulimwengu wa utandawazi wa leo. Kwa vile nilikuwa naongea katika mkutano wa waumini wa dini, nilisisitiza kuwa utandawazi huu unatuhitaji tutafakari namna ya kuthibitisha imani ya dini yetu, kwani kuwepo kwa tamaduni mbali mbali ni mtihani anaotushushia Mungu.

Kwa kuzingatia kuwa wote waliokuwa wananisikiliza ni wazungu, katika eneo la mashambani, na ambao wanajua propaganda zilizopo Marekani kuhusu wageni wanaoendelea kuingia nchini, niliwakumbusha kuwa Yesu tunayemwabudu alikuwa mchokozi na mkorofi alyewatibua watu kwa fikra na kauli zake. Angekuwepo leo hapa Zumbrota, hapa Marekani, bila shaka angebadilisha hadithi yake ya m-Samaria mwema, na badala yake angewatibua kwa kusimulia habari ya mu-Islamu mwema.

Basi, kwa hoja za aina hiyo, nilichochea fikra miongoni mwa wasikilizaji. Tulipomaliza mkutano, tulienda kula chakula cha mchana na watu wakaendelea kuongea nami. Kwa vile kulikuwa nakala za kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences mezani, kama ilivyotangazwa na mratibu wa mkutano wakati alipokuwa ananitamulisha, baada ya kula nilikwenda kwenye ile meza na kuwauzia na wengine kuwasainia.

Napenda kumalizia kwa kuleta mfano moja wa maongezi yaliyofanyika pale kwenye meza. Mama mmoja alipokiona kile kitabu, hakuchelewa kuniambia kuwa kitabu kile kiko katika maktaba ya kanisa lao la Zumbro. Nilifurahi nikamwambia kuwa nilifahamu jambo hilo. Aliponiuliza nilifahamuje, nilimweleza kuwa nilisoma katika kijarida cha kanisa la Zumbro uchambuzi wa kitabu changu, na mwandishi alikuwa amesema kuwa kitabu kiko katika maktaba ya kanisa lile. Aliniambia kuwa aliyeandika uchambuzi ule ni mchungaji mstaafu, akaongeza kuwa atamweleza kuwa tumeonana hapa mkutanoni Lands Lutheran Church.

Huo ni mfano mmoja tu wa mazungumzo ya jana na watu mbali mbali. Kweli dunia hii ni ndogo, na wanadamu hukutana kwa namna tusiyotegemea. Mambo ya aina hii ni mengi, na ndio yananipa hamasa ya kwenda popote kushiriki mambo ya aina hii ya manufaa kwa jamii.

(Picha ya kanisa la Lands Lutheran nilipiga wakati naondoka hapa mahali)

Thursday, April 9, 2015

Mipango ya Mhadhara wa Keshokutwa Imekamilika

Jioni hii, nimepigiwa simu na Marci Irby wa First English Lutheran Church, Faribault, kunipa taarifa kuwa mipango ya mhadhara wangu wa keshokutwa, imekamilika. Mada yangu itakuwa kama ilivyopangwa, "The Dilemma of Cultural Differences: Challenges and Opportunities."

Hadi leo, watu 40 wameshajiandikisha kuhudhuria mkutano. Lakini, kama ilivyokuwa miaka iliyopita, wengine hungoja mpaka dakika ya mwisho, na wengine hujisajili hapo hapo kwenye mkutano.

Mama Irby kaniuliza aseme nini juu yangu wakati wa kunitambulisha. Nimemwambia kuwa ninapenda kutambulishwa au kujitambulisha kifupi, bila madoido mengi. Itatosha akitaja jina langu, uraia wangu kama m-Tanzania, na kwamba ninafundisha Chuo cha St. Olaf.

Anaweza kuongeza kuwa, zaidi ya kufundisha darasani, ninatoa ushauri kuhusu masuala ya utamaduni kwa wa-Marekani wanaoenda Afrika, iwe ni kusoma, kujitolea, au kutalii, na ninatoa ushauri huo kwa wa-Afrika wanaofika au wanaoishi Marekani.

 Mkutano utaanza saa tatu asubuhi, kama ilivyopangwa. Kwa kuzingatia kwamba zitakuwepo shughuli nyingine pia, tangu hiyo saa tatu hadi saa sita na nusu mchana, nitakuwa na muda wa nusu saa hivi kwa ajili ya mhadhara wangu. Huenda yakatokea mabadiliko.

Amesema amemaliza tu kusoma upya kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, akaburudika na michapo iliyomo. Kwenye mkutano ataweka meza niweke vitabu hivi, kwa ajili ya wale watakaopenda kuvinunua.

Kuna uwezekano kuwa nitaonana na watu ambao wameshafika Tanzania, kama yeye mwenyewe Mama Irby, na labda wawili watatu ambao tumewahi kuonana, kama Mchungaji Joy Bussert, ambaye aliwahi kunialika kutoa mhadhara kuhusu kitabu changu kanisani kwake Immanuel Lutheran mjini St. Paul, kisha akatembelea Tanzania akiwa na binti yake mdogo.

Tuesday, April 7, 2015

Mhadhara Ujao, Lands Lutheran Church

Siku zimekwenda kasi. Wiki kadhaa zimepita tangu nilipopata mwaliko wa kwenda kutoa mhadhara katika mkutano wa Sinodi ya Kusini Mashariki ya Minnesota. Mkutano ulipangwa kufanyika mjini Zumbrota, kwenye Kanisa la Lands Lutheran, tarehe 11 Aprili.

Mama aliyenialika, kwa niaba ya kamati ya maandalizi, alisema kuwa wangependa niongelee masuala ambayo yameanza kujitokeza katika sharika mbali mbali za sinodi kutokana na kuingia kwa watu kutoka tamaduni mbali mbali. Aliniambia kuwa aliwahi kunisikiliza miaka kadhaa iliyopita katika kanisa lake la First English Lutheran Church, mjini Farbault, nikiongelea masuala hayo, akanunua kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Wiki zilizofuata, mama huyu nami tuliwasiliana ili kupanga mada ya mhadhara wangu. Nilitoa mapendekezo, naye aliyawasilisha kwenye kamati yao. Pendekezo walilolichagua ni "The Dilemma of Cultural Differences: Challenges and Opportunities."

Niliandika taarifa ya mwaliko katika blogu yangu ya ki-Ingereza. Sasa siku imekarbia, nami nangojea kwa hamu kwenda kujumuika na waumini hao kutoka makanisa mbali mbali, na kuwapa mawazo na mawaidha yangu kuhusu hali wanayoikabili ya kujikuta wana watu wa tamaduni mbali mbali. Azma yao ya kutaka kujua nini cha kufanya ni mfano wa kuigwa.

Kadiri dunia inavyoendelea kubadilika kutokana na utandawazi wa leo, jamii zote zitalazimika kutafuta njia za kuishi pamoja na watu wa tamaduni tofauti. Hili ni suala ambalo nimelitafiti, kulitafakari, na kuliongelea kwa miaka mingi.

Kama ilivyo kawaida hapa Marekani, niliulizwa malipo yangu ni kiasi gani. Nilijibu kama nilivyozoea, kwamba waamue wenyewe, kufuatana na uwezo wao. Nasukumwa na dhamiri yangu, kutumia vipaji alivyonipa Mungu kwa manufaa ya wanadamu. Pesa si msingi.

Ningekuwa na uchu wa pesa, kama fisadi, ningesema ngoja niwakamue. Lakini mtu unayemtegemea Mungu unajiuliza: Je, tunabarikiwa kwa kutanguliza pesa mbele badala ya ubinadamu? Ninashukuru ninavyofanikiwa kuwagusa wanadamu.

Monday, April 6, 2015

Bemidji Yamwenzi Mary, Mke wa Hemingway

Jioni ya tarehe 4 Aprili, baada ya kurejea kutoka Leech Lake Tribal College karibu na mji wa Bemidji, niliingia mtandaoni nikiwa na lengo la kuona kama kuna taarifa zozote kuhusu mkutano wetu. Katika ukurasa wa Facebook wa Chuo, niliona taarifa na picha za mkutano ule:

Hilo lilinivutia. Lakini niliona pia taarifa nyingine, kuhusu namna mji wa Bemidji unavyomwenzi Mary Welsh, aliyekuwa mke wa nne na wa mwisho wa Ernest Hemingway. Mary Welsh alizaliwa karibu na Bemidji akakulia na kusoma mjini hapo.

Kisha alienda kusoma katika Chuo Kikuu cha Northwestern karibu na Chicago. Alikuja kuwa mwandishi katika magazeti hapo Chicago na hatimaye London, akajipambanua kama mwandishi wa habari za vita. Huko ndiko alikokutana na Ernest Hemingway na baadaye wakafunga ndoa.

Nilifahamu hayo yote na mengine mengi, kutokana na utafiti wangu wa miaka kadhaa. Nilifahamu tangu zamani kuwa Mary Welsh alizaliwa eneo la Bemidji, na nilikuwa nawazia kwenda kule kufanya utafiti juu yake. Mary Welsh Hemingway alitanguzana na Ernest Hemingway katika safari ya Afrika Mashariki mwaka 1953-54. Walizunguka Kenya, Tanganyika, hadi Uganda, ambako walipata ajali mbili za ndege, mfululizo.

Mary Hemingway alisafiri hadi Mbeya, na ameelezea hayo na mengi mengine katika kitabu chake kiitwacho How it Was. Nasikitika kuwa wa-Tanzania, kwa kukosa utamaduni wa kununua na kusoma vitabu, hawafahamu hayo. Wangekuwa wana utamaduni huo, wangeweza kutumia habari na maandishi kama haya ya Mary Welsh Hemingway na Hemingway mwenyewe kwa manufaa makubwa, hasa katika utalii. Hali ni mbaya kwamba wa-Tanzania hawashtuki wakielezwa habari za vitabu namna hii. Nimethibitisha hayo, kama nilivyoandika katika blogu hii.

Wenzetu katika nchi kama Cuba, Hispania na Marekani wanafaidika sana na maandishi ya Hemingway. Cuba wanaitunza sana nyumba ya Hemingway, Finca Vigia, na hata baa alimokuwa anakunywa, mjini Havana, ni kivutio kikubwa cha watalii. Kule Hispania kuna mji wa Pamplona ambao ulipata umaarufu duniani na umaarufu huu unaendelea, baada ya Hemingway kuutembelea na kuangalia mchezo wa "bull fighting," akaandika juu yake katika riwaya iitwayo The Sun Also Rises. Maelfu ya watalii wanafurika Pamplona. Hapa Marekani, nyumba alimoishi Hemingway, kama vile kule Oak Park (Illinois)na Key West (Florida), ni vivutio vikubwa kwa watalii.

Hayo ndio yaliyonijia akilini wakati nasoma taarifa ya mji wa Bemidji kumwenzi Mary Welsh Hemingway. Jambo moja kubwa lililoelezwa katika taarifa ile ni utunzi wa tamthilia juu ya Mary Welsh Hemingway, unaofanywa na Catie Belleveau baada ya utafiti wa muda mrefu.

Hoja sio kwamba ni lazima nasi tujitose na kujishughulisha na Hemingway na mke wake, ingawa kufanya hivyo kungetuletea manufaa kama wanayopata wenzetu wa Cuba, Pamplona, Oak Park na Key West. Ninachotaka kusisitiza ni umuhimu wa kujifunza kutoka kwa hao wenzetu.

Sisi tunao waandishi maarufu kama Mgeni bin Faqihi wa Bagamoyo, aliyetunga Utenzi wa Ras il Ghuli. Je, tunajua habari zake? Tunaye Shaaban Robert. Je, ni wa-Tanzania wangapi wanajua angalau mahali alipozaliwa, sehemu alimoishi, na mahali alipozikwa? Je? wahusika katika wizara za utalii na utamaduni wanafahamu habari hizo? Na je, wanafahamu kuwa taarifa hizo ni hazina ambayo tungeweza kuitumi? Binafsi ninatekeleza wajibu wangu kwa kuandika kuhusu mambo haya, kama nilivyofanya katika kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, ambacho nitashangaa kikipata wasomaji Tanzania.

Saturday, April 4, 2015

Nimerejea Salama Kutoka Leech Lake Tribal College

Nilirejea jana jioni kutoka Leech Lake Tribal College, kwenye mkutano kuhusu "Narratives of Identity." Nilikuwa mmoja wa wanajopo wanne waliotoa mada, na mada yangu ilikuwa "Being African in America."

Niliongelea uzoefu wangu katika miaka mingi ya kuishi na kufundisha hapa Marekani, nikielezea kazi kubwa isiyoisha ya kujitambulisha kama mu-Afrika, ambaye ni tofauti na mu-Amerika Mweusi. Nilielezea jinsi suala hilo linavyosabisha mikanganyiko na kutoelewana baina ya wa-Marekani Weusi na wa-Afrika tuishio Marekani.

Nilisema wazi kuwa namna wanavyojiita na kujitambulisha wa-Marekani Weusi ni tofauti na namna tunavyojiita na kujitambulisha sisi wa-Afrika. Nilimnukuu Chimamanda Ngozi Adichie wa Nigeria ambaye katika mahojiano na katika riwaya yake maarufu ya Americanah, ameelezea vizuri suala hilo.

Nilimnukuu pia mwandishi Jamaica Kincaid wa Antigua, pande za Caribbean, ambaye pamoja na kuwa ni mweusi pia, hakuwahi kujiita kama wanavyojiita  wa-Marekani Weusi. Hayo mawazo yake niliyasoma katika mahojiano yaliyochapishwa mwaka 1991 katika jarida la Mississippi Review.

Nilisisitiza umuhimu wa kuheshimu haki ya kila jamii kujiita au kujitambulisha kwa majina wanayoyataka au yanayowaridhisha wenyewe. Watu wengine sherti wafuate njia hiyo badala ya kuwapachika watu majina ya utambulisho kama walivyofanya wakoloni.

Nilienda mbali zaidi na kuelezea suala la haki ya kila jamii kujieleza wenyewe, sio kuzimishwa kama walivyotuzimisha wakoloni, na wao wakawa wanaandika juu yetu.

Siwezi kuelezea hapa yote niliyosema. Nawazia kuendelea kutafakari suala hilo na kujisomea zaidi, na kuwasoma upya watu kama Frantz Fanon, Aime Cesaire, na Ngugi wa Thiong'o, ili hatimaye niandike makala kamili.

Hiyo jana, wakati nilipokuwa najitambulisha mkutanoni, nilisema kuwa nimeleta vitabu vyangu viwili kama zawadi kwa maktaba ya chuo cha Leech Lake Tribal College. Vitabu hivyo ni Africans and Americans: Embracing Cultural Differences na Matengo Folktales. Vitabu hivi vilipokelewa kwa furaha na shukrani tele.

Nina hakika kuwa mkutano ule umesisimua watu. Jana hiyo hiyo, katika ukurasa wa Facebook wa Leech Lake Tribal College iliandikwa taarifa hii:

We had some great speakers on campus today for the Narratives of Identity presentations. One of the many memorable remarks from today's visit was by Joseph Mbele, St Olaf College- “I am not a person of color. I am Tanzanian which is a concept of colonization. Only when I came to America was I referred to as black. Naming yourself, knowing yourself, is a right…Construction of identities are not fixed and it’s our right to identify ourselves.”

(Picha ya juu kabisa na ya katikati ni kutoka Leech Lake Tribal College)

Thursday, April 2, 2015

Mijadala Kuhusu Vitabu Katika Maktaba ya Bemidji, Minnesota

Ni usiku saa saba kasoro, nami nimo chumbani mwangu katika Hampton Inn hapa mjini Bemidji. Ninasoma gazeti la hapa liitwalo "The Bemidji Pioneer" la jana, yaani tarehe 2.

Nimevutiwa sana na habari kuhusu utaratibu walio nao katika mji huu wa kukusanyika katika maktaba yao na kufanya mijadala kuhusu vitabu. Nanukuu habari nzima, ambayo iko ukurasa wa 2:

Public Library book discussion set

BEMIDJI--The Bemidji Public Library offers a monthly book discussion program--the next session will take place at noon April  13. The program will run for approximately an hour.

The book for discussion will be "The Devil in the White City: Murder, Magic and Madness at the Fair that Changed America" by Eric Larson.

Nimejikuta nawazia mengi. Je, utaratibu wa aina unawezekana katika miji ya Tanzania? Kuna maktaba katika miji kama Dar es Salaam, Arusha, Tanga, Mwanza, Iringa, Songea, Lushoto, Mbinga, Karatu, na Mbulu. Hizo nimeziona mwenyewe, sio za kusikia.

Je utaratibu wa kuchagua na kujadili kitabu fulani kila mwezi unawezekana? Tusianze kutoa visingizio. Makampuni ya vitabu kama Mkuki na Nyota, Tanzania Publishing House, Dar es Salaam University Press, Ndanda Mission Press, na E&D Publishers yamechapisha na yanaendelea kuchapisha vitabu vingi sana.

Kampuni ya Mkuki na Nyota, kwa mfano imekuwa ikichapisha  vitabu vya Shaaban Robert kwa wingi, na kwa jamii yetu inayodai kuwa inakienzi ki-Swahili, mtu ungetegemea kuwa vitabu hivyo vinawindwa kama tunavyowinda kitimoto au bia za baridi.

Kuhusu gharama, wa-Tanzania kwa ujumla hawawezi kushindwa kuvinunua. Angalia jinsi wanavyochangia sherehe, jinsi wanavyofurika kwenye mechi za kabumbu, jinsi wanavyofurika kwenye burudani mbali mbali. Hela sio tatizo; ziko tele.

Nini kinazuia kuwepo katika jamii yetu kwa utamaduni kama huu wa jamii ya Bemidji wa kujadili vitabu?


Nimewasili Bemidji, Minnesota

Alasiri hii, nimewasili mjini Bemidji, nikiwa njiani na wenzangu watatu, ambao tumesafiri pamoja kutoka Minneapolis. Tutalala hapa, na kesho asubuhi tunakwenda Leech Lake Tribal College kwenye mkutano  kuhusu "Narratives of Identity." Mimi ni mmoja wa watoa mada wanne. Mada yangu itakuwa "Being African in America."

Tulipokuwa tunakuja, tulisimama kidogo katika mji uitwao Akeley, ili kuona sanamu ya Paul Bunyan, mhusika maarufu katika masimulizi ya jadi ya sehemu hii ya Minnesota, ambaye anajulikana sana pia Marekani na ulimwenguni. Sanamu hii inamwonyesha akiwa ameshika shoka lake. Ili kujionea jinsi sanamu hii ilivyo kubwa, ifananishe na sisi watatu ambao tumesimama hapo Mbele yake.


Tulipoingia Bemidji, tulikwenda moja kwa moja kwenye sanamu nyingine ya Paul Bunyan, ambayo inamwonyesha akiwa na fahali wake wa buluu ambaye ni sehemu muhimu ya masimulizi kuhusu mhusika huyu. Sanamu hiyo, sawa na ile ya Akeley, ni kubwa sana.

Kwa mujibu ya masimulizi, Paul Bunyan alikuwa jitu kubwa la ajabu, nadhani kumzidi hata Liongo Fumo, shujaa katika masimulizi ya jadi ya wa-Swahili, wa-Pokomo, na wengine katika mwambao wa Kenya.

Bemidji ni mahali ambapo niliwahi kufika miaka mitatu hivi iliyopita, lakini tangu muda mrefu kabla ya hapo nimetamani kuja kwa shughuli za utafiti wangu juu ya mwandishi Ernest Hemingway.

Mary Welsh, mke wa nne na wa mwisho wa Ernest Hemingway alizaliwa na kukulia eneo hili la Bemidji, kabla hajaenda kusoma katika Chuo Kikuu cha Northwestern, karibu na Chicago. Katika safari zake Kenya, Tanganyika, na Uganda, mwaka 1953-54, Hemingway alitanguzana na mke wake huyu.

Panapo majaliwa, nitakuja Bemidji kufanya utafiti huo. Kwa leo nimefurahi kuziona hizi sanamu, na kujionea jinsi Paul Bunyan alivyo maarufu eneo hili. Jina lake liko kila mahali. Nimeona mtaa wenye jina hilo, biashara mbali mbali, hata kampuni ya mawasiliano ya intanenti.

Hata katika hoteli tunamolala usiku huu, Hampton Inn, nimeona picha kubwa ya Paul Bunyan katika ukuta wa mgahawa. Kwangu mimi kama mtafiti wa masimulizi na mambo mingine ya jadi ("folklore"), nimeguswa sana na kupata hamasa ya kufanya utafiti juu ya Paul Bunyan.


Wednesday, April 1, 2015

Tunahitaji Demokrasia, Lakini Tunahitaji Vyama vya Siasa?

Bila shaka tutakubaliana kuwa tunahitaji demokrasia, yaani mfumo wa utawala ambao ni wa umma, unaendeshwa na umma, kwa maslahi ya umma. Kwa ki-Ingereza wanasema "rule of the people, by the people and for the people."

Hii ndio maana na tafsiri ya demokrasia. Lakini je, tunahitaji chama cha siasa? Tunahitaji vyama vya siasa? Ni lini wa-Tanzania walikaa na kulitafakari suali hili? Kwa kweli hawajawahi kufanya tafakari hii. Badala yake wamekurupuka na wazo la chama au vyama, kikasuku tu.

Hata wale tunaowaita wasomi wetu nao wameshindwa kuhoji hali hii. Wameshindwa kujinasua kutokana na mtazamo huu, badala ya kufanya kile kinachoitwa kwa ki-Ingereza "thinking outside the box."

Nimeelezea zaidi huu ukurupukaji, mkanganyiko, na ukasuku wa wa-Tanzania katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...