Saturday, April 25, 2015

Utitiri wa Blogu

Siku hizi, wa-Tanzania tuna utitiri wa blogu, blogu za kila aina. Pamoja na hayo, blogu zinaendelea kuibuka, kama uyoga. Mimi mwenyewe nimechangia utitiri huo. Nina blogu mbili: hii ya hapakwetu na nyingine ya ki-Ingereza.

Mtu akitaka, anaweza kushinda, na hata kukesha, anazisoma hizi blogu, na hataweza kuzimaliza. Wenye blogu na wadau tunaandika usiku na mchana, kwani tumeenea sehemu mbali mbali za dunia. Inapokuwa usiku Tanzania, huku ughaibuni ndio kwanza tunaamka, au ni mchana, alasiri au jioni, bado tuko kazini kwenye blogu. Mtu atasoma hadi achoke, hali sisi tunaendelea kudunda, kama wasemavyo mitaani.

Je, kuna ubaya wowote kuwa na utitiri wa blogu? Ni jambo jema, au ni jambo lisilostahili hata kuzungumzwa? Hili ndilo suali kuu ninalotaka kulitafakari, au kulianzishia mjadala.

Kwa upande mmoja, utitiri wa blogu ni jambo jema. Kumiliki blogu kunampa mtu fursa kamili ya kujieleza bila vizuizi ambavyo vinakuwepo kwenye magazeti na vyombo vingine vya habari ambavyo vinatawaliwa na watu wengine, kama vile wamiliki na wahariri. Kwa maana hiyo, blogu zinapanua uwanja wa uhuru na demokrasia ya kutoa maoni.

Kwa upande mwingine, kwa kuwa yeyote anaweza kuanzisha na kuendesha blogu, hata kama ni mbumbumbu, blogu zimekaribisha uwepo wa mambo ya kila aina, yakiwemo yasiyo na faida kwa umma, au ya ovyo. Ulimwengu wa blogu ni sawa na soko huria. Kuna vitu vya maana, mitumba michakavu, na bidhaa feki.

Utitiri wa blogu una athari zingine pia. Utitiri unasababisha ushindani mkubwa na imekuwa ni hali ya "mwenye mbavu mpishe." Wasomaji wanachagua blogu za kusoma, na kuna blogu ambazo hazijulikani sana, au zinajulikana na wenye blogu na wasomaji wachache.

Kutokana na hii hali ya "mwenye mbavu mpishe," blogu nyingi zinaibuka, na baada ya muda zinakufa. Zingine zinatoweka baada ya kitambo kifupi au kirefu, na baadaye zinajitokeza tena. Zingine zinaendelea kupumua na kujikongoja, ingawa mahututi, ila hazifi.

Bila shaka msomaji utakuwa na mtazamo wako. Kama unapenda kuchangia, nakukaribisha sana.


 

2 comments:

Anonymous said...


Athari za utitiri wa blog unaweza kuendana na athari za ugunduzi wa kuchapisha vitabu miaka 600 iliyopita. Kwani iisababisha vitabu kuwa vingi na kila mwenye uwezo aliweza kuandika na pia utamaduni wa kumiliki vitabu ukaanza kujengeka. Vitabu vileta mapinduzi makubwa ya fikra na ndio msingi mkubwa wa ustaarabu wa kimagharibi. Vitabu viliifanya ulaya kuwa na nguvu tena, baada ya kudidimia kwa muda.

Tofauti na internet na matokeo yake kama blogs ambazo vimeleta kitu kinaitwa Digital Distraction. Ambayo athari zake ni kupunguza umakini na kujenge kizazi cha watumwa wa mtandao na kompyuta. Mimi mwenyewe toka nianze kumiliki kompyuta na zaidi ni we na mtandao, kimeathiri sana uwezo wangu wa kujisomea na kufanya utafiti.

Mbele said...

Ndugu Anonymous wa April 26, 2015 at 7:37 AM, shukrani kwa ujumbe wako, ambao umeibua aina ya masuala ambayo tungepaswa kuwa tunayajidili enzi zetu hizi za utandawazi wa leo, ambamo intaneti ina athari kubwa sana.

Tungepaswa kuwa tunaongelea masuala hayo katika hizi blogu, katika makongamano, katika makala za kitaaluma, na hata vitabu, kama ilivyo katika kitabu maarufu cha Patricia Wallace kiitwacho The Psychology of the Internet

Lakini sisi, kwa uvivu wetu, hatuna fikra hizo za kutafakari mfumo huu tunamoishi na kutumia hizi tekinolojia. Tunazitumia tu, kama tunavyozitumia hizi blogu, huku tukijidanganya na kudanganyana kwamba tunaelimishana katika hizi blogu.

Inanisikitisha ninapoona watu wanadhani kuwa ninapoandika katika blogu ninaandika kama profesa, na kama hawaridhiki na yale ninayosema, wanahoji na kukebehi, profesa gani huyu?

Huu ni ujinga na utumwa ambao umeongelea. Kuingia kwenye blogu yangu kama vile unaingia darasani kwangu ni kosa na hatari. Watu wanapaswa wasome makala zangu za kitaaluma wakitaka kujua mchango wangu katika taaluma. Kwa kawaida, wenye blogu ninakuwa kama vile niko kijiweni au kwenye kikao cha arusi au kwenye mjadala mtaani kuhusu msondo ngoma.

Sikatai, mara moja moja, kwenye blogu zangu, huwa natoa vidokezo vyenye uzito kitaaluma, au naongelea vitabu ninavyofundisha au kusoma, bila kuvichambua ipasavyo taaluma.

Nakubaliana nawe kuwa hizi blogu zina tabia ya kuwachepusha watu lengo, hiyo unayoiita "digital distraction," na pia kuwadumaza akili.

Blogu kwa ujumla zinachangia uvivu kwa kuwafanya watu wajiziuke nazo badala ya kusoma vitabu. Kutokana na tabia yake ya kuwa "addictive" (yaani kuteka akili kama vile kilevi au bangi) blogu zinapoteza muda ambao tungeweza kuutumia kwa kujielimisha.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...