Tuesday, April 28, 2015

Leo Nimeonana na Mtengeneza Filamu ya Hemingway

Leo nimeonana na Jimmy Gildea, mtengenezaji wa filamu ya Papa's Shadow. Jimmy alikuwa mmoja wa wanafunzi wa Chuo cha St. Olaf waliokuja Tanzania, Januari 2013, kwenye kozi yangu Hemingway in East Africa.

Filamu yake imetokana na kozi ile, na watakaobahatika kuiangalia watajifunza mengi kutoka kwa Mzee Patrick Hemingway, motto pekee aliyebaki wa Ernest Hemingway aliyebaki,  na mimi, ambao ni wazungumzaji wakuu.

Tumeongea kwa saa moja na robo hivi, kuhusu filamu yake na masuala yanayohusika nayo. Tumeongelea mikakati ya kuitangaza filamu hiyo, fursa za kuionyesha katika matamasha, vyuoni, na kadhalika.

Tumeongelea safari yetu ya Montana tulipoenda kuongea na Mzee Patrick Hemingway, na jinsi alivyotufanyia wema wa kutueleza mengi juu ya baba yake. Tumejikumbusha jinsi alivyotugusa alipoelezea  hisia zake kuhusu hali ya baba yake iliyotokana na unywaji uliokithiri na pia ajali za ndege nchini Uganda zilizohujumu afya yake kwa miaka yote hadi kifo chake. Niliyafahamu mambo hayo kutokana na kusoma mimi mwenyewe, na wanafunzi niliwaeleza, lakini kumsikiza Mzee Patrick Hemingway akiyaelezea ilitugusa kwa namna ya pekee.

Tumeelezana kuridhika kwetu na filamu hii, nami nimemweleza Jimmy kuwa yote aliyokumbana nayo katika kuitengeneza filamu hii ni mafundisho yatakayomsaidia katika kutengeneza filamu zingine. Jimmy, kama anavyofanya siku zote anashukuru kuwa katika kozi yangu, ambayo ilikuwa mwanzo wa yeye kuifahamu Afrika, ambayo imemgusa na kubadili mtazamo wake wa maisha, na imekuwa chachu ya yeye kuitengeneza filamu hii.

Ni mwalimu yupi asiyefurahi kuona matunda mema namna hii ya kazi yake? Ni furaha kwangu kuongea na wanafunzi wangu na kuwahamasisha katika mkondo wa maisha waliojichagulia. Nimemhakikishia Jimmy, kama ilivyo desturi yangu, kwamba wakati wowote akihitaji ushauri au barua ya utambulisho ajisikie huru kuwasiliana nami.

No comments: