
Ninataka wafanikiwe. Kwa mfano, ninajisikia vizuri ninapoona mafanikio ya mwandishi chipukizi Bukola Oriola kutoka Nigeria, ambaye anaonekana nami pichani hapa kushoto. Nilisoma katika gazeti hapa Minnesota kuwa alikuwa na mswada, ila hakujua afenyeje ili kuuchapisha. Niliona ni lazima nimsaidie.
Ingawa hatukuwa tunafahamiana, nilimwandikia na kumweleza kuwa nilikuwa tayari kumsaidia kuchapisha kitabu chake, bila usumbufu wala gharama. Tulipanga siku, akaja ofisini kwangu, nikamwelekeza namna ya kutumia tekinolojia ya uchapishaji mtandaoni kwenye tovuti ya lulu.
.jpg)
Hao waandishi chipukizi wa Tanzania nao napenda wafanikiwe. Nawaambia kuwa, pamoja na kuandika kama ninavyoandika, ninajielimisha kuhusu uandishi, uchapishaji, na uuzaji vitabu, kwa kununua na kusoma vitabu. Nao wafanye hivyo hivyo.
Nawaambia kuwa yale ninayojifunza nawafundisha wengine, katika maandishi yangu, kama vile kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, na katika blogu hii ya
.jpg)
Nimemwambia kuwa ni lazima awe msomaji sana wa vitabu, kama nilivyosema katika blogu hii. Nakumbuka fundisho ambalo mwandishi Ernest Hemingway alimpa kijana mwandishi chipukizi aliyemwulizia ushauri. Hemingway alimwambia kuwa ni lazima asome vitabu vyote muhimu vilivyowahi kuandikwa, ili atambue mtihani ulio mbele yake wa kushindana na waandishi wale.
Kwa waandishi chipukizi wa Tanzania, napenda kuzingatia ushauri huo wa Hemingway. Wasome maandishi ya waandishi maarufu. Kama wana ndoto ya kuwa washairi, wasome Hamziya, Al Inkishafi, Utendi wa Mwana Kupona, Diwani ya Muyaka bin Haji al-Ghassaniy, Utendi wa Ras il Ghuli, Utendi wa Masahibu, Utendi wa Ngamia na Paa, mashairi ya Shaaban Robert, ya Gora Haji Gora, na kadhalika. Kama wanataka kuandika riwaya, wasome maandishi ya Shaaban Robert, Shafi Adam Shafi, Said A. Mohamed, Euphrase Kezilahabi, na kadhalika. Kwa juhudi hizi, waandishi chipukizi watajipatia ufahamu wa kuwawezesha kuandika kazi zitakazodumu kihistoria.
4 comments:
Professor Mbele,
Nakujulia hali. Kila la kheri.
Shaaban Fundi
www.kibogoji.com
Ndugu Kibogoji
Shukrani kwa ujumbe wako. Mara baada ya kuuona ujumbe wako, nimeanza kuangalia tovuti ya kibogoji. Nimeona kazi nzuri unayofanya.
Mimi kama mwalimu nimevutiwa na kampeni yako ya kuchangia vitabu mashuleni Tanzania. Nami nimekuwa nikifanya hivyo, kufuatana na kile kidogo ninachoweza kumudu katika kugharamia usafirishaji wa vitabu.
Tuendelee kuwasiliana, Insha Allah.
Moyo wa pekee wa kujitoa kwa wengine pasipo mtazamo wowote wa maslahi ya kifedha,Muwa chache wa aina yako mzee Mbele hasa kwa nyakati hizi.kila la kheri .
Ndugu Mfuko,
Shukrani kwa ujumbe wako. Kujitolea ni jambo rahisi sana, na kwa sisi tunaosema tuna dini, tungekuwa mfano wa kuigwa katika kujitolea. Badala yake, tunanaringiana kuhusu misahafu, kuhusu msahafu upi unasema ukweli, kuhusu dini ipi ni ya kweli, badala ya kudhihirisha kimatendo kwamba tuna dini.
Wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere, utamaduni wa kujitolea aliuhimiza na ulikuwepo, angalau miaka ya mwanzo ya Uhuru.
Leo watu hata kusafisha mitaro mtaani kwao hawataki. Wanangojea halmashauri ya mji.
Wamarekani wanatuzidi kwa hilo. Wana utamaduni wa kujitolea, mashuleni, mahospitalini, mitaani. Wanawasaidia wenye shida kama chakula. Utawakuta wanajitolea kakika nchi yao na nchi zingine.
Hata Tanzania utawakuta wakijitolea, kwenye program kama Peace Corps, Global Volunteers, Global Service Corps, na Cross Cultural Solutions. Mtandaoni utaona taarifa za program hizo, hao wa-Marekani utawakuta hadi mbali vijijini, katika mazingira magumu.
Ninakumbuka nilivyofundishwa katika shule za Kanisa Katoliki kule mkoani Ruvuma na mapadri, mabruda, na masista. Walikuwa hawalipwi, lakini walikuwa wanajituma sana katika kutufundisha, na shule zetu zilikuwa tishio nchini kwa ufaulu. Tulikuwa tunazipiga chini shule za serikali ambako waalimu walikuwa wanalipwa mishahara.
Ninaamini kwa dhati kuwa unapojitolea kwa hali na mali kwa manufaa ya binadamu mwenzako au wanadamu wenzako, Mungu anakubariki. Mambo yako yanakunyookea kwa namna ambayo hukutegemea. Huu ni ushuhuda wangu wa dhati.
Post a Comment