Monday, January 23, 2012

Mwandishi Lazima Awe Msomaji Sana

Yule mwandishi maarufu sana, Ernest Hemingway, alikuwa na mawazo ya kusisimua kuhusu masuala mbali mbali, likiwemo suala la uandishi. Aliandika sana kuhusu uandishi: mbinu za uandishi, uandishi bora, changamoto za uandishi na namna ya kuzikabili, raha na machungu ya kuandika. Aliongelea kazi za waandishi mbali mbali, na hakuficha hisia na mtazamo wake kuhusu ubora au mapungufu ya waandishi hao.

Kuna mengi sana ya kuongelea, kuhusu suala hilo la Hemingway na uandishi. Lakini hapa nataka kutaja jambo moja tu, nalo ni kauli ya Hemingway kwamba mwandishi ana wajibu wa kusoma kazi za waandishi wote waliomtangulia, ili ajue kazi inayomkabili ya kuwafunika hao waandishi.

Napenda kunukuu maneno ya Hemingway aliyomjibu kijana kutoka Minnesota aliyemfuata Hemingway umbali mkubwa ili kuuliza masuali kuhusu uandishi. Kiutani, Hemingway alimpa kijana huyo jina la Mice.

Mice alimwuliza Hemingway masuali mengi, ila suali ninalotaka kulileta hapa ni, "What books should a writer have to read?" Hemingway akajibu, "He should have read everything so he knows what he has to beat."(Ernest Hemingway, By-Line, New York: Touchstone, 1998, p. 217)

Kwa tafsiri ya juu juu, suali lilikuwa, "Je, mwandishi anapaswa asome vitabu gani?" Na Hemingway alijibu kwamba awe amesoma kila kitu ili afahamu kazi inayomkabili ya kuwashinda waliomtangulia.

Tuangalie kauli hizi kwa kuzingatia hali ya Tanzania. Kila mchunguzi anakubali kuwa utamaduni wa kusoma vitabu unazidi kufifia au umefifia Tanzania. Taarifa zinaeleza kuwa hata uwezo wa kusoma na kuandika unazidi kufifia. Asilimia ya waTanzania wasiojua kusoma na kuandika inaongezeka. Kwa maneno mengine, Tanzania inazidi kuwa nchi ya ngumbaru.

Katika hali hiyo, na kwa kuzingatia kauli ya Hemingway, tutawezaje kutegemea kuwa na waandishi wa kiwango cha juu kabisa? Kwa mujibu wa Hemingway, mwandishi m-Tanzania, ambaye labda tuseme anaandika kwa ki-Swahili, anapaswa kuwa amesoma waandishi wote waliotangulia. Kwa mfano awe amesoma Tambuka, Al-Inkishafi, Mwana Kupona, Miraji, Masahibu, Ngamia na Paa, Muyaka bin Haji, Rasi l'Ghuli, Shufaka, Fumo Liyongo, Maisha ya Tippu TIp, vitabu vyote vya Shaaban Robert, na kadhalika. Anapaswa afahamu jadi hiyo vizuri, apambane kiuandishi ili awe juu zaidi, aweze kweli kutoa mchango unaotupeleka mbele.

Sitaki kudanganya. Lazima nikiri kuwa Hemingway alitoa mtihani mkubwa sana. Kwa mfano, sijui kama kuna mtu leo anayeweza kumfikia Muyaka, au Mgeni bin Faqihi. Lakini Hemingway alifanya vizuri kuweka kigezo cha juu kabisa, hata kama kukifikia ni taabu sana au haiwezekani. Ni vibaya sana kujiwekea viwango vya chini na kisha kujipongeza kwa kufikia viwango hivyo. Naamini hili ndilo tatizo letu: tunajiwekea viwango vya chini, au tunababaisha bila viwango, na bado tunajipongeza au tunapongezana.

3 comments:

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Ilikuwa ni Shule ya Sekondari ya Kahororo -shule mojawapo mashuhuri sana kule Bukoba. Mtihani wa kumaliza kidato cha nne ulikuwa unabisha hodi.

Mkuu wetu wa shule wa wakati ule (Mungu Amlaze Mahali Pema Peponi) alituasa sisi watahiniwa kwa kutumia maneno yafuatayo:

"Ukitaka kupima ubora wa afya yako, KAMWE usijilinganishe na mgonjwa" Aliendelea kutuambia kwamba ukijilinganisha na mgonjwa daima afya yako itaonekana kuwa bora hata kama nawe una ndwele kibao zinazokuandama. Alituasa kwamba tusijisomee kwa lengo la kupata vyeti vya daraja la pili au la tatu. Kama kweli tuna nia na malengo thabiti, mbona tusijiandae na kujiweka tayari kupata vyeti vya daraja la kwanza ?

Japo nilikuwa bado tineja lakini maneno haya yaliniingia sana, sijayasahau na yamekuwa yakiniongoza katika mambo yangu mengi.

Leo hii tukifanikiwa kidogo tu basi tunakaa chini na kuangusha bonge la pati kujipongeza bila kujiuliza tumefanikiwa kwa kiwango kipi?

Mifumo yetu mingi ya kijamii inakwenda mrama na siye, kama vile mazuzu,tumekazania kupongezana kwa vitone vidogo tu vya mafanikio vinavyoonekana katikati ya jangwa la ufisadi, uzembe, utoto na kutojali. Mfano, hatuoni aibu kusimama kidete na kujipiga kifua kwamba tumefanikiwa kujenga mashule ya kata karibu kila kona bila kujiuliza kuhusu kiwango cha elimu kinachotolewa katika mashule hayo.

Kuhusu uandishi na uhakiki katika Fasihi ya Kiswahili, Kezilahabi aliwasha moto alipotoa novela zake mbili - Nagona na Mzingile. Wasomaji na wahakiki wazembe walikuwa wamezoea kusoma kazi za moja kwa moja na kuandika tahakiki zenye mlengo wa ki-Marx. Katika kazi hizi walipigwa dafrau na kujikuta hoi bin Taaban kwani bila kuelewa mikondo mikuu ya kifalsafa, kufanya uchambuzi au uhakiki wa maana wa Nagona na Mzingile ilikuwa haiwezekani. Kumbe ni yale yale ya kujilinganisha na mgonjwa.

Ngoja nikome hapa ili nisije kuonekana kama ninayelalama. Mada hii imetonesha hisia zangu na kunikumbusha asubuhi ile tulivu kule Bukoba, siku ambayo mkuu wetu wa shule alitupa ule ushauri muhimu wa kutojilinganisha na mgonjwa kama kweli tulikuwa tuna dhamira ya kupima ubora wa afya zetu na kufanya mabadiliko ya maana !

Mbele said...

Mwalimu Matondo, shukrani kwa kutukumbusha hayo mambo. Nimemkumbuka marehemu baba yangu. Mimi ni mtoto wake wa kwanza. Tangu aliponipeleka kuanza darasa la kwanza, mwaka 1959, alipoangalia daftari zangu, alitaka aone nimepata 100% kila ukurasa au kila zoezi. Kama nilipata kitu kama 95% alihoji kwa nini.

Sasa fikiria, mimi ni mtoto mdogo, na kama ilivyokuwa miaka ile, tulikuwa tunawaogopa baba zetu. Kwa hivi, kazi niliyokuwa nayo ni ya kufurukuta nipate 100% siku zote, ingawa haikuwezekana kupata hivyo kila siku. Lakini kutokana na msukumo wa baba, maisha yangu yote shuleni hadi kwenye vyuo vikuu, nilikuwa naharakatika ili niongoze kwa kufaulu.

Laiti kama moyo huu tungeujenga katika vijana wetu wa Tanzania. Badala yake, siku watu wanapopata shahada zao, utakuta hata yule aliyeambulia "C" kwenye mitihani anashangiliwa na umati wa ndugu, jamaa, na marafiki kwa vigelegele na hoi hoi, na ngoma. Jioni ni kreti za bia za kumwaga, na kuruka majoka hadi asubuhi. Kisa, mtu kaibuka na ushindi mkubwa wa "C," wakati ilitakiwa akazane kupata "A."

Unknown said...

Ahsante sana Prof. Nimefaidi sana darasa hili. Kwakuwa ninapenda kufanya vizuri katika kuandika, nitajibidiisha kujisomea kila kitu.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...