Sunday, January 29, 2012

Mwandishi Shafi Adam Shafi

Tanzania tuna waandishi wengi maarufu katika lugha ya ki-Swahili. Mmoja wao ni Shafi Adam Shafi, kutoka Zanzibar, ambaye anaonekana nami pichani hapa kushoto. Tulikuwa New Africa Hotel, Dar es Salaam mwaka 2004 wakati wa tamasha la vitabu.







Shafi Adam Shafi anafahamika sana kwa riwaya zake. Riwaya aliyoichapisha kwanza ni Kasri Ya Mwinyi Fuad (Tanzania Publishing House, 1978). Ilikuwa maarufu tangu mwanzo. Sikupata muda wa kuisoma. Halafu, mwaka 1980 niliondoka Tanzania, kuwenda masomoni Marekani, hadi mwaka 1986.

Baada ya kukaa Marekani miaka sita hiyo, nilivyorejea Tanzania nilifanya juhudi ya kujipatia vitabu vya ki-Swahili. Nilinunua nakala ya Kasri Ya Mwinyi Fuad tarehe 28 Oktoba, 1987, ikasainiwa na Shafi Adam Shafi tarehe 29. Nina risiti ya kununulia kitabu, kutoka Tanzania Publishing House. Kwa hivyo, nina ushahidi kuwa nimeonana na Shafi Adam Shafi mara mbili.

Ingawa mara kwa mara ninapoongelea vitabu katika blogu zangu huwa naandika kuhusu yaliyomo, na uchambuzi wangu, leo nimependa tu kuchangia kumtangaza Shafi Adam Shafi na kazi zake. Nitakapokuwa nimezisoma kazi zake, Insh'Allah, nitaweza kuandika kwa undani zaidi.

Shafi Adam Shafi ameandika pia Kuli (Dar es Salaam: Tanzania Publishing House, 1979) , Vuta N'kuvute (Dar es Salaam: Mkuki na Nyota Publishers, 1999), na Haini (Nairobi: Longhorn Publishers, 2003).

Kuna taarifa ya mahojiano ya kina baina ya Shafi Adam Shafi na Freddy Macha ambayo unaweza kuyasoma hapa.

5 comments:

Anonymous said...

PROFESSOR UMENIKUMBUSHA MBALI SANA KWA KUMZUNGUMZIA SHAFI NA HUSUSAN KITABU CHAKE CHA KULI.NASIKITIKA SANA KUWA WAKATI MIMI NIKO SEC NILIKUWA NIMEKIPA KIINGEREZA KIPAUMBELE SANA AU NAWEZA KUSEMA WENGI WA RIKA LANGU TULIKUWA HIVYO. YAANI ILIKUWA UKIJUA KIINGEREZA BASI WEWE UNAAKILI WAKATI WAKO WAINGEREZA WENYEWE NA WENGI TU BAADA YA KUINGIA NAO MADARASANI UNAWAONA NI MBUMBUMBU.SASA PROFESSOR HIVI KUNA VITABU GRAMMAR YA KISWAHI NA WAPI VINAPATIKANA. MAANA JUZI KULIKUWA NA MJADALA KUWA JEE PREPOSITION NI KIHUSISHI AU KIUNGANISHI MIMI NILIKAA KIMYA SIKUCHANGIA LAKINI MOYONI NILISIKIA AIBU.

Mbele said...

Ndugu anonymous, shukrani kwa ujumbe. Mimi mwenyewe nililikuwa naongoza darasani, hadi chuo kikuu, masomo hayo ya kiIngereza. Lakini, ki-Swahili nilikuwa siwezi kukitumia vizuri kama ki-Ingereza. Na kwa vile nilijiaminisha kuwa siwezi, hata juhudi sikuwa nafanya.

Hatimaye, rafiki yangu Mugyabuso Mulokozi, ambaye amestaafu kama profesa pale Chuo Kikuu Dar, alianza kunielimisha umuhimu wa kukienzi ki-Swahili. Alianza kufanya hivyo tangu tulipokuwa tunasoma Mkwawa High School, mwaka 1971. Nilimsikiliza, nikaanza kujibidisha. Hatimaye nikawa mtafiti ninayetambuliwa kimataifa katika tenzi za kale za ki-Swahili.

Pia, kutokana na shinikizo la Mulokozi, nilianza kufanya bidii katika kuandika kwa ki-Swahili. Tayari nimechapisha kitabu kiitwacho CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Ninayo pia hii blogu ya Hapa Kwetu.

Kwa miaka hii niko hapa Marekani katika chuo cha St. Olaf. Ingawa nafundisha kiIngereza, sirudi nyuma katika ufahamu wangu wa ki-Swahili. Kila ninapokuwa Tanzania, nanunua vitabu vya waandishi maarufu wa ki-Swahili. Ninavyo hapa, na nashukuru kuwa binti yangu, ambaye alikulia Tanzania, huwa anaviazima na kuvisoma pia.

Kuhusu upatikanaji wa vitabu vya sarufi ya ki-Swahili, ningependekeza uulizie Chuo Kikuu Dar es Salaam ile taasisi iliyokuwa inaitwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. Duka la Chuo Kikuu Dar es Salaam pia huenda wanavyo vitabu vya aina hiyo. Nilipita pale mwaka jana, ila nilikuwa natafuta vitabu vya fasihi.

Kuhusu "preposition" kama ni kihusishi au kiunganishi, ndio aina ya masuala ambayo tunatakiwa kujibidisha kujifunza. Mimi naweza kuelezea vizuri masuala hayo yalivyo katika ki-Ingereza. Lakini kwenye ki-Swahili nakwama. Kama ulivyokiri mwenzangu katika sentensi yako ya mwisho, nami ni lazima nikiri kuwa hii ni aibu kwangu na kwa wasomi wengine ambao wanakwama katika ufahamu na matumizi ya ki-Swahili.

Narudia, shukrani kwa mchango wako.

Unknown said...

Prof. Mbele, shukrani sana kwa post hii. Huku Dar, sisi vijana, kwa kutumia klabu yetu ya usomaji wa vitabu ya KITABU NILICHOSOMA, tumeandaa mjadala wa siku ya SHAFI ADAM SHAFI utaofanyika siku ya tarehe 05/09/2015.
Jambo la kupendeza Shafi mwenyewe atahudhuria siku hiyo.
Nduguyo,
Ado Shaibu.

Mbele said...

Ndugu Ado Shaibu

Shukrani kwa ujumbe wako. Mimi ni mfuatiliaji makini sana wa shughuli zako kama unavyozielezea mitandaoni, hasa Facebook. Nafurahi ulivyo karibu na "watu wangu," kama vile Profesa Issa Shivji, Dr. Lwaitama, Mwalimu Richard Mabala, bila kuwasahau akina Demere Kitunga na Elieshi Lema ambao walikuwa wanafunzi wangu hapa UDSM.

Kwa msingi huo, hata hizo taarifa za mjadala wa siku ya Shafi Adam Shafi nilizipata mara mlipozitangaza. Sipitwi na kitu kwa kweli, labda kiwe hamjakitangaza.

Mna bahati sana kujumuika na gwiji Shafi Adam Shafi. Ni mwandishi mahiri, na mwenye ufahamu wa mambo mengi. Mtaelimika sana kutoka kwake.

Ni jambo jema sana kuwa na mkutano na mwandishi maarufu kwa mtindo huo. Ni namna ya kuwaenzi waandishi ambayo wenzetu huku Marekani ni sehemu ya utamaduni wao. Nawapeni hongera na kuwatakieni kila la heri.

Mohan said...

Lugha ni sehemu kubwa Sana ya utamaduni wa jamii au taifa lolote. Kukibeza Kiswahili ni kuubeza utamaduni . Tatizo limekuwa kubwa Sana Kwa nyakati hizi Kwa kuwa vijana wanakiharibu Kiswahili kuanzia mtaani,magazetini,radioni nahilo ndiyo dhoruba.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...