Watu wengi wanabadili dini. Nikitoa mfano wa wa-Islam na wa-Kristu, wa-Kristu kwa maelfu wanabadili dini na kuwa wa-Islam, na wa-Islam kwa maelfu wanabadili dini na kuwa wa-Kristu. Kuna taarifa nyingi za watu hao mtandaoni.
Katika mtandao wa YouTube, unaweza kuwasikiliza watu wa aina hiyo wakijieleza. Kwa mfano, unawasikia watu wakielezea jinsi dini ya u-Islam ilivyoshindwa kukidhi mahitaji yao ya kiroho na kadhalika. Na unawasikia wengine wakielezea jinsi dini ya u-Kristo ilivyoshindwa kukidhi mahitaji yao ya kiroho na kadhalika. Nimewasikiliza baadhi kutoka pande zote, na nimeona jinsi wanavyoongea kwa masikitiko na hata jazba kuhusu dini walizozihama. Watu hao wanajisikia kuwa kubadili dini kumewapa mwanga na amani moyoni.
Kama nilivyosema, taarifa hizi zimezagaa mtandaoni. Sijui unajisikiaje endapo mtu wa dini yako akihamia dini nyingine. Wa-Islam wanajisikiaje pale wa-Islam wenzao wanapohamia katika u-Kristu? Wa-Kristu wanajisikiaje pale wenzao wanaposilimu? Naona hili ni suala la kusisimua akili, na ndio maana nimeamua kuliweka hadharani.
Tujaribu kulitafakari suala hili kwa undani. Binafsi natambua kuwa dini ni suala la imani ya mtu. Ni suala la mtu na dhamiri yake, yeye na Mungu. Endapo mtu akifikia hatua ya kuamini kwa dhati kabisa, katika dhamiri yake, kwamba akiwa katika dini fulani anakuwa karibu zaidi na Mungu kuliko katika dini yake ya sasa, halafu akahamia ile dini nyingine, kilichopo kwa sisi wengine ni kumwombea na kumtakia mema.
Wa-Islam na wa-Kristu tunajisikia sana kuwa msikitini na wa-Islam wenzetu, au kuwa kanisani na wa-Kristu wenzetu. Dini zetu zinajitahidi kwa namna mbali mbali kuwapata waumini zaidi. Utawasikia waumini wakitamba jinsi dini yao inavyoenea kuliko dini nyingine. Kwa upande wa Tanzania, utawasikia watu wakilumbana kuhusu dini ipi ina wafuasi wengi zaidi Tanzania. Suala la hizi takwimu limefanywa kuwa muhimu sana.
Lakini je, siku ya kiyama, tutasimama mbele ya Mungu na kuongelea haya masuala ya takwimu? La hasha. Wewe mu-Islam hutaweza kujikinga na hukumu ya Mungu kwa kuongelea umati wa wa-Islam uliokuwa nao hapa duniani. Na wewe m-Kristu itakuwa ni hivyo hivyo. Hutaweza kujinasua na hukumu ya Mungu kwa kuongelea utitiri wa wa-Kristu uliokuwa nao kanisani kwako au jimboni kwako. Itakuwa ni kila mtu kuchunguzwa yeye binafsi, imani yake, matendo yake, na maisha yake.
Ni kutokana na masuala kama haya ndio nasema kuwa tuwe waangalifu sana kuhusu suala la watu kubadili dini.
10 comments:
Mimi naamini dini ni moja tu duniani kwasababu muumba ni mmoja ambae tunapaswa kumuabudu.Lakini dini vilevile ni somo kama masomo mengine tunayojifunza hivo kuitafuta dini ya ukweli ni muhimu kusoma vitabu mbalimbali kuliko watu kufarakana.Mwenyezi mungu ndie atakae toa hukumu siku ya kiama na sio mashekhe wala mapadri.Kwa hivo watu wanaobadili dini ni watu waliosoma labda chaguo lao limefika sehemu waliokuwa wanaitafuta.Kwasababu sisi wanadamu tumetofautiana kwa mengi na sio vizuri kumhukumu mtu kwa kile alichochagua.Kwani ukristo na uisilamu hata mayahudi dini hizi tatu zimekulia sehemu moja kwasababu hata nabii Musa-Moses(piece be upon him)alituletea amri kumi kutoka kwa mwenyezi mungu ambazo sote tunaziamini.
http://www.youtube.com/watch?v=AD2EgGG5iUQ&feature=related
Tatizo moja ni kuwa watu tukishakuwa waumini wa dini fulani, tunaanza kujifanya polisi wa dini hiyo. Ukiangalia humo mtandaoni, utaona kuna watu wengi ambao, baada ya kubadili dini, wananyanyaswa na kutishwa. Mapolisi hao wako tayari hata kuwaua.
Yaani inatisha jinsi binadamu anavyojitwalia madaraka ambayo ni ya Mungu peke yake, yaani madaraka ya kuwahukumu na kuwaadhibu binadamu wengine katika masuala haya ya imani.
Binadamu, kiumbe dhalili, anajipa madaraka ambayo ni ya Mungu. Ni ajabu sana.
Mwenyezi mungu ni mkubwa wa yote na anasifa za kila aina na ndie atakae tuhukumu kwa yote tuliotenda duniani ktk uhai wetu.Mimi kama muisilamu naamini kama sisi wanaadamu hatujakamilika isipokuwa mwenyezi mungu.Na utawaona wanaadamu wa kila aina wazuri na wabaya ktk dini zote lakini tunachohitaji ni kujielimisha na kuwapuuza wale wenyekukiuka.Wapo watu wanaodhani dini yao ndio dini aliyokuwa nayo ndio dini nzuri kuliko ya mwingine lakini hata undani wake wa dini anayoifuata hajawahi kuisoma ila anaisikia tu ikihubiriwa na kuifuata.Na hatimae kuidharau dini yako na kukuona kama taahira.Sasa husema kwamba sio ubinaadamu kumdharau mtu kwa dini yake au rangi yake ila napenda kuona watu wanaelimishana kidini japo tofauti.Profesa niliwahi kupata marafiki wawili wazungu walikuwa watu wa dini sana walifanya kazi Kanisani ni mtu na mkewe.Hawa watu walinipenda sana na walikuwa wanapita dukani kwangu japo mara 3 au 4 kwa wiki kuja kunisalimia na waliniheshimu kwasababu niliwaheshimu.Kwani walijua mimi ni muisilamu na ninavaa hijab na walipenda kuongelea uisilamu na kutaka kujua zaidi.Walikuwa wananiachia vitabu nivisome kama magazine lakini za kikristo.Hivi ndio inapendeza kumuheshimu mtu anapokuheshimu.Lakini anaweza kutokea mtu anakuuliza maswali ya kebehi to be honest huwa sipendi.Huwezi kumchagulia mtu dini,kama anaamua kubadili bila ya kulazimishwa basi aachiwe na uhuru wake na mungu ndie atakaemuamulia kama kakosea au kapatia.
Asante kwa mchango wako murua. Naona wadau sasa wamepata mengi ya kuyatafakari, na ingekuwa vizuri iwapo nao wangechangia. Nikizingatia kauli yako kuhusu umuhimu wa kujielimisha, napenda kuongezea kuwa jukumu la kujielimisha na kuelimishana ni msingi wa maelewano, na kwa maana hii, ni wajibu katika dini.
Mimi mwenyewe ni m-Kristu na papo hapo ninashukuru kuwa nilijipa jukumu, miaka mingi kidogo iliyopita, la kusoma maandishi ya dini mbali, na hiyo imenisaidia kuzielewa na kuziheshimu. Na naendelea na juhudi hiyo.
ila mimi huwa ninamshangaa anaye badili dini halafu akaanza kutukana dini aliyohama.maana mimi nilibadiri dini kutoka ukristo kwenda uislam basi baadhi ya wakristo wenzangu wakataka kuniogopa kwakufuata yale wayasikiayo kutoka kwa waislam.Mimi nikaona hapana kwani kubadili dini hakuondoi ubinadamu nikawa nawakaribisha nyumbani kwangu vizuri,tunashirikiana kwa kila kitu kumbe kubadili dini hakuna kinachobadilrika bado wewe unakuwa ni yuleyule zaidi imani.Na wanaotukana dini za wengine ni wale ambao hawajazisoma hata dini zao wala hawazielewi tena dini zote mbili.Kumbe mimi mwanzo nilidhani wakristo wana mitume wao na waislam wana mitume wao,kumbe mitume ni walewale labda utaratibu wa kufanya ibada ndio tofauti tangu hapo hata mambo ya dini sipendi kuyabishania sana zaidi ni kumwelewesha mtu.Ilatu bado dini zetu za asili ninazifuatilia hasa mambo ya matambiko maana nazo zilikuwa zinamtambua mungu tena sana ukiondoa hizi za mapokeo ya waarabu na wazungu
Anonymous, shukrani kwa mchango wako murua, wenye kuboresha mjadala. Nimevutiwa na kila ulilosema.
sasa sijui kuhusu mimi mfuasi wa dini zoote duniani hata nisizozijua nazifuata tu
Ndugu Kamala, naona unaongoza njia. Mimi mwenyewe nasoma vitabu vya dini mbali mbali ili nizielewe. Vile vile nafuatilia masimulizi ya dini ambazo hazina vitabu, yaani ni masimulizi ya mdomo na kurithi kutoka kizazi hadi kizazi. Huenda, mwisho wa safari, nikawa nami mfuasi wa dini zote.
ndio waweza kuwa kwani utakachogudnua ni kuwa zoote zinaongelea kitu kile kile kwa mazingira na tamaduni tofauti
Huwa nashangaa xana wazazi akiingilia kati ukiwa unauamuzi wa kubadili dini.....wakati haya mambo ya imani ni ww na iman yako wazazi wanayafuatilia nn xaxa
Post a Comment