Wednesday, September 29, 2010

Programu za Kupeleka Wanafunzi Tanzania

Leo hapa chuoni St. Olaf tulikuwa na shughuli ya kuzitangaza programu za masomo ambamo chuo kinapeleka wanafunzi wake.

Tunafanya hivyo mara moja kwa mwaka. Walimu washauri wa programu tunakuwepo na taarifa mbali mbali za programu tunazohusika nazo, na wanafunzi wanakuja kupata taarifa hizo, na pia kujiandikisha iwapo wana nia ya kujiunga na programu hizo.

Vyuo vingi hapa Marekani vina programu za aina hiyo, na vyuo kadhaa vinapeleka wanafunzi Tanzania. Hii inatokana na kufahamu faida wanayopata wanafunzi kwa kwenda kuishi na kujifunza katika nchi zingine. Inapanua akili na upeo. Kuishi miongoni mwa watu wa utamaduni tofauti kunampa kijana fursa ya kukomaa kwa namna mbali mbali na kuwa tayari kwa maisha ya zama zetu za utandawazi wa leo. Programu hizi zinachangia maelewano mema duniani.

Pamoja kazi yangu ya kufundisha katika idara ya ki-Ingereza hapa St. Olaf, ninashughulika katika program zinazopeleka wanafunzi nchi za ki-Afrika, ikiwemo Tanzania. Nimefanya shughuli hii kwa miaka yote niliyofundisha hapa ughaibuni, katika programu kama LCCT, ACM Tanzania, na ACM Botswana. Leo nilijipanga kwenye meza kama inavyoonekana katika picha, nikingojea wanafunzi, nimwage sera.

Hii ni fursa ya kuitangaza nchi. Kama nilivyowahi kusema kwenye blogu hii, picha ni vielelezo murua kabisa. Ni lazima niseme kuwa shughuli hii ya kuitangaza Tanzania ilikuwa inanipendeza sana miaka ya mwanzo, wakati Tanzania ilipokuwa kweli nchi ya kupigiwa mfano, ambayo nilikuwa najivunia. Tanzania ile, ya Mwalimu Nyerere, inatoweka. Nchi inazidi kuwa ya matabaka ya wenye mali wanaostarehe, na maskini wanaoteseka. Badala ya jamii yenye amani na utulivu, tunaendelea kuona kushamiri kwa ukatili kama ule unaofanywa dhidi ya albino na wale wanaoitwa vibaka. Program hizi za kuleta wanafunzi Tanzania zinaiingizia nchi hela nyingi, lakini naogopa kuwa hela hizi zinachotwa na mafisadi. Siku hizi, ninapowaambia wanafunzi hao kwenda Tanzania, ninasema nikiwa na wasi wasi. Lakini naendelea kufanya shughuli hii, kwani ni muhimu, sio tu kwa hao wanafunzi, bali kwa nchi yetu na yao, na dunia kwa ujumla, kama nilivyoandika hapa.

Sunday, September 26, 2010

Ujumbe Kuhusu Vitabu

Leo nilienda mji wa Duluth kwa matembezi ya masaa machache nikiwa na mwalimu mwenzangu katika idara yetu. Baada ya kuzunguka na gari sehemu kadhaa za mji huo, niliegesha gari kwenye mtaa uitwao Superior Street, unaoonekana katika picha hizi mbili, tukaanza kutembea katika mtaa huu, kuangalia mazingira.

Hatukwenda mbali, tukaona duka la vitabu na moja kwa moja tukaingia humo.

Humo ndani kulikuwa na vitabu vingi sana na vitu vingine vidogo vidogo vya nyumbani, kama vile sahani, glasi, mishumaa, na maua ya mapambo.

Nilipoingia tu, kwenye meza moja karibu na mlango niliona ujumbe uliowekwa kwenye fremu, kuhusu vitabu. Nilivutiwa sana na ujumbe ulioandikwa na Clarence Day, Jr.

Nilimwuliza mama mhudumu humo dukani kama naweza kupiga picha. Alisema kwa uchangamfu kuwa ni sawa kabisa.

Jioni hii, wakati naandika habari hii kwenye blogu, nimetafuta taarifa nikagundua kuwa Clarence Day, Jr. aliandika ujumbe wake mwaka 1920. Kwa jinsi nilivyoupenda, nimeona niuweke hapa na nijaribu kuutafsiri kwa ki-Swahili. :


VITABU

Ulimwengu wa vitabu ni kitu kilichotukuka kwa namna ya pekee kilicholetwa na binadamu. Hakuna anachounda binadamu ambacho kinadumu hivyo: majengo ya kumbukumbu huanguka, mataifa hutokomea, himaya za ustaarabu hupitwa na wakati na kutoweka duniani; kufuatia zama za giza, mataifa mapya hujenga himaya zingine. Lakini ulimwengu wa vitabu una majuzuu yanayodumu daima, yakiwa na upya na ubichi kama siku yalipoandikwa, na yanaendelea kuelezea mioyoni mwa wanadamu kuhusu yaliyojiri hata mioyoni mwa wanadamu waliokwishafariki karne za zamani.

Thursday, September 23, 2010

Nimeipata Nakala ya "Tendehogo."

Nilipokuwa Tanzania mwaka huu, nilikutana na rafiki yangu, mwandishi Edwin Semzaba, kama nilivyoandika hapa. Jambo moja tuliloongelea ni kutafsiri tamthilia yake ya Tendehogo. Basi, niliporejea hapa chuoni St. Olaf ninapofundisha, nilienda maktaba na kuagiza nakala ya tamthilia hii. Kwa vile nakala haiko hapa, waliniagizia kutoka Maktaba ya Congress iliyoko Washington DC.

Nimeshapata nakala hiyo, na sasa inabidi nianze mikakati ya kuitafsiri. Kazi ya kutafsiri kazi ya fasihi ni ngumu, yenye changamoto nyingi, hata kama mtu unazijua lugha husika vizuri sana. Hata kama lugha husika ni zako za kuzaliwa nazo au za tangu utotoni, kama kilivyo ki-Matengo na ki-Swahili kwa upande wangu.

Ninasema hivyo kutokana na uzoefu. Nimejishughulisha na kutafsiri tungo za ki-Swahili na hadithi za ki-Matengo kwenda ki-Kiingereza. Niliwahi hata kuandika makala kuhusu kutafsiri hadithi ya ki-Matengo. Soma hapa.

Miaka michache iliyopita nilianza kutafsiri Tendehogo, lakini nakumbuka nilitafsiri kurasa labda mbili au tatu. Sasa, pamoja na wasi wasi nilio nao kuhusu uwezo wangu, itabidi nijipige moyo konde na kuanza kuogelea.

Tuesday, September 21, 2010

Kiboko ya Wachawi

Nilipokuwa Tanzania mwaka huu, nilipata wazo la kupiga picha za matangazo mbali mbali ya waganga wa kienyeji, ambayo ni mengi kwenye miji kama Dar es Salaam. Matangazo hayo yanahusu uponyaji wa magonjwa na matatizo mengine ya afya, mafanikio ya biashara na maisha, kuwavuta wapenzi, na kadhalika.

Tangazo hili la "Kiboko ya Wachawi" nililiona Kibamba, kandokando ya barabara itokayo Dar es Salaam kwenda Morogoro, tarehe 28 Julai. Nilipita hapo na walimu wengine watatu kutoka Marekani, kutembelea shule ya sekondari ya Shulua ambayo iko maeneo hayo.

Friday, September 17, 2010

Kwa Nini Ninablogu

Jana niliandika makala, lakini nadhani nilikosea wakati wa kuichapisha, maana naona imeenda bila kichwa. Nimeona kwenye blogu za wengine hakuna kichwa, bali jina la blogu tu. Kwa hivi nimeona nilete taarifa kuwa makala ilikuwa na kichwa, "Kwa nini ninablogu." Soma hapa.

Thursday, September 16, 2010

Kwa Nini Ninablogu

Wiki kadhaa zilizopita, wanablogu watatu tulikutana Sinza, Dar es Salaam, tukaongea kuhuau masuala mbali mbali. Kati ya mambo mengi, tuliondoka na suali: kwa nini tunablogu? Bofya hapa. Baada ya kulitafakari suali hili kiasi, napenda kuelezea kidogo kwa nini ninablogu.

Kwanza, nakumbuka kuwa nilianza kublogu baada ya kuhamasishwa na ndugu Freddy Macha na Jeff Msangi, mmiliki wa Bongo Celebrity. Hao wawili walifahamu kuhusu maandishi yangu, wakanishawishi nianzishe blogu. Nami nilifuata ushauri wao.

Nilianzisha blogu mbili: ya ki-Swahili, na ya ki-Ingereza. Nilijifunza na naendelea kujifunza huku nikiblogu. Katika harakati hiyo, Dada Subi, mmiliki wa Wavuti amekuwa akinisaidia, kama anavyowasaidia wanablogu wengine.

Kwangu mimi blogu ni ukumbi wa kuelezea mawazo, hisia, fikra na mambo yangu mengine, na hivi kuyahifadhi na kuwashirikisha wengine. Siblogu kwa imani kuwa nina ujuzi au busara kuliko watu wengine. Blogu ni baraza inayonikutanisha na wengine kwa mazungumzo, mijadala na kubadilishana mawazo.

Vile vile, ninablogu kwa sababu nimeona umuhimu wa blogu kwa upande wa lugha. Ninavyoandika ki-Swahili najiongezea uzoefu wa kutumia lugha hiyo ipasavyo. Hiyo ndio jitihada yangu, na hili ndilo lengo langu.

Mazoezi ni mazoezi. Tunapofanya mazoezi ya viungo daima, tunajijengea afya bora, na tunaanza kuusikia mwili ukikaa sawa. Kwa namna hiyo hiyo, kuandika kwa ki-Swahili kumenifanya niisikie akili yangu ikizidi kukaa sawa, kwa upande huu wa matumizi ya lugha. Nazidi kujiamini katika utumiaji wa lugha hii.

Katika blogu yangu ya ki-Ingereza, naandika kwa lengo la kuonyesha uandishi bora wa ki-Ingereza. Ni lugha ambayo nimeipenda tangu nilipoanza kujifunza, darasa la tatu, na naifundisha hapa katika Chuo cha St. Olaf, Minnesota.

Kublogu kumeniunganisha na watu wengi ambao wanasoma blogu zangu, kutoka pande zote za dunia. Inaleta faraja, kwa mfano, ninapotambua kuwa kitu fulani nilichoandika katika blogu kimekuwa ni msaada kwa mtu fulani. Kwa mfano, miezi kadhaa iliyopita, nilipata ujumbe kutoka kwa mama mmoja aliyeko Ujerumani.

Aliulizia namna ya kufika Mbamba Bay na mahali pa kulala akishafika kule, kwani alikuwa anapangia kuja Tanzania. Alisema kuwa aliniuliza kwa vile alisoma habari za Mbamba Bay kwenye blogu yangu. Nilimpa maelezo aliyohitaji. Wakati huu wote yeye alikuwa Ujerumani na mimi nilikuwa Marekani. Alikuja Tanzania mwaka huu na familia yake, wakati nami niko nchini. Tulionana Ubungo, kwenye kituo cha mabasi, kama inavyoonekana katika picha hii, wakiwa wamefurahi kununua nakala ya Matengo Folktales.

Sunday, September 12, 2010

Nimekutana na Mwandishi Edwin Semzaba

Katika mizunguko yangu Tanzania mwaka huu, nilitembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mara kadhaa, kwa shughuli rasmi na pia shughuli binafsi. Kwa vile nilisoma na kufundisha hapo, daima ninakutana na watu wengi tuliosoma au kufundisha pamoja au niliowafundisha ambao baadhi yao ni walimu pale. Kwa mfano, soma hapa na hapa.

Mmoja wa wale niliokutana nao mwaka huu ni Edwin Semzaba, mwandishi maarufu wa tamthilia na riwaya na ni mwigizaji hodari. Anaandika kwa ki-Swahili. Tamthilia zake, kama vile Ngoswe, zinafahamika Tanzania nzima na nje.













Baadhi ya riwaya zake, ambazo ninazo, ni Tausi Wa Alfajiri (Heko Publishers Limited, 1996), na Funke Bugebuge (Dar es Salaam University Press, 1999).

Semzaba ni rafiki yangu wa siku nyingi. Tulisoma darasa moja, kuanzia Mkwawa High School, Iringa, 1971-72, hadi Chuo Kikuu Dar es Salaam, 1973-76. Mwaka huu, aliposikia kuwa niko nchini, Semzaba alinipa nakala mpya ya Ngoswe, iliyochapishwa na Nyambari Nyangwine Publishers, 2008.




Nilikuwa na nakala ya Ngoswe tangu zamani, toleo lililochapishwa na Education Services Centre Ltd, 1988. Vile Vile, miaka kadhaa iliyopita, Semzaba alinipa nakala ya video ya tamthilia hii.








Mwaka huu alinipa pia nakala ya riwaya yake mpya, Marimba ya Majaliwa. Sikujua kuwa alikuwa ameandika riwaya hii. Alinieleza kwamba ni riwaya aliyoshinda kwenye shindano la hadithi za kusisimua, mwaka 2007. Shindano hili lilifadhiliwa na SIDA na kusimamiwa na Mradi wa Vitabu vya Watoto, Tanzania.



Nilifurahi kusikia hivyo, kwani nafahamu alivyo makini na kazi yake, na jinsi alivyochangia fasihi na sanaa Tanzania na duniani kwa miaka mingi. Nafurahi kuwa mchango wake unatambuliwa kwa namna hiyo.

Kwa miaka kadhaa nimewazia kutafsiri baadhi ya maandishi ya Semzaba. Nilianza kutafsiri Mkokoteni, ila sikumaliza. Lakini katika kuongea na Semzaba mwaka huu, ilionekana kuwa tafsiri ya Tendehogo inahitajika mapema zaidi. Kazi hizi, na za waandishi wengine wa nchi yetu, inafaa zitafsiriwe, kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Friday, September 10, 2010

Upatikanaji wa Vitabu Vyangu

Kutokana na maulizo ya wadau, napenda kutangaza kuwa vitabu vyangu vinapatikana Tanzania, sehemu zifuatazo:

Arusha (Kimahama Literature Center)
0786242222

Dar es Salaam (Sinza)
0754 888 647
0717 413 073

Bagamoyo
0754445956

Karatu (Bougainvillea Lodge)
0754576783

Longido (Cultural Tourism Program)
0787855185

Mto wa Mbu (Cultural Tourism Program)
0786373099

Walioko ughaibuni wanaweza kuvipata sehemu hizi:

Duka la mtandaoni, Bofya hapa

St. Olaf College Bookstore, Fax 507 786 3779, simu 1-888-232-6523

Africonexion (info@africonexion.com, simu 507 403 9756)

Tuesday, September 7, 2010

Watoto wa Tanzania Wanapenda Vitabu

Wengi wetu tunalalamika kuhusu kufifia au kutoweka kwa utamaduni wa kununua na kusoma vitabu miongoni mwa wa-Tanzania. Inaonekana kuwa hata pale ambapo vitabu vipo, kama vile maktaba, wa-Tanzania hawaendi kusoma.

Ukweli ni kuwa tabia hii inajengeka na umri. Watoto wa Tanzania, wanapenda vitabu, sawa na watoto wengine popote. Nimeshuhudia hayo katika pita pita zangu Tanzania. Kwa mfano, ukienda kwenye maonesho ya vitabu Tanzania, utawaona watoto.

Mwanzoni mwa Septemba, 2004, kulikuwa na maonesho ya vitabu katika uwanja wa hifadhi ya kumbukumbu za Taifa, Dar es Salaam. Kama kawaida, waliohudhuria zaidi ni watoto.

Katika maonesho hayo, watoto wa shule walifanya michezo ya kuigiza, kuhusu umuhimu wa vitabu.
Waliimba pia nyimbo, wakiwahamasisha wazazi kuweka vitabu nyumbani na kuwa na utaratibu wa kusoma pamoja na watoto. Lakini, ujumbe wao uliishia hewani, kwani wazazi wenyewe hawakuwepo.

Wakati wa kuigiza mchezo, watoto hao walishika vitabu, kama vilelelezo. Nilimwona mtoto mmoja ameshika kijitabu changu kuhusu Things Fall Apart. Anaonekana hapa juu, wa pili kutoka kulia. Niliguswa na jambo hilo.

Mwaka huu, tarehe 24-25 Juni nilishiriki maonesho ya elimu na ajira, ambayo yaliandaliwa na Tripod Media. Yalifanyika Diamond Jubilee Hall, Dar es Salaam.
Nililipia banda, nikaweka vitabu vyangu na machapisho mengine, nikawa naongea na watu kwa siku zote mbili.

Walifika watoto wengi, na hapo nilijionea mwenyewe jinsi watoto walivyo na ari ya vitabu. Walikuwa wanaviangalia na waliniuliza masuali kem kem.
Nami nilitumia fursa hii kuwaelezea umuhimu wa kusoma na kutafuta elimu kwa dhati muda wote.



Nilipata faraja kubwa katika kuwa na watoto hao na kuona moyo wao juu ya vitabu.



Suali la msingi linabaki: Tufanyeje ili watoto waweze kukua na moyo huu walio nao bila kulegea au kufifia? Kuna njia gani ya kuwafanya watu wazima wahudhurie maonesho ya vitabu?

Katika jarida la Tanzania Schools Collection, toleo la kwanza, Moris Mwavizo anaripoti, ukurasa 12, kuwa katika maonesho fulani ya vitabu Dar es Salaam, mratibu mmoja alimwona mtoto akizunguka mwenyewe katika viwanja. Alipomwuliza kwa nini baba yake hakuja naye, mtoto alijibu kuwa baba yake angekuja kama kungekuwa na bia hapa kwenye maonesho. Je, hii si aibu?

Monday, September 6, 2010

Mh. Balozi Peter Kallaghe Afutarisha UK

Haya ndio mambo yanayotakiwa Tanzania. Nimevutiwa na kila kitu katika video hii, kuanzia ule wimbo mtamu wa kuienzi nchi yetu na utambulisho wetu kama wa-Tanzania, hadi mshikamano baina ya wa-Tanzania, na nasaha murua zilizotolewa na wasemaji. Mungu Ibariki Tanzania.

Sunday, September 5, 2010

Aliyosema Marando Jangwani

Nimeiona video hii katika blogu ya Kulikoni Ughaibuni, nikaona niiweke hapa kwangu. Natanguliza shukrani kwa ndugu Chahali, kwa kuchangia suala la kupeana habari na kuelimishana. Ni haki ya msingi. Bofya hapa

Wednesday, September 1, 2010

Nimepiga Picha Nyingi Tanzania

Kila mwaka, ninapokuwa Tanzania, napiga picha nyingi niwezavyo na kuja nazo huku Marekani. Mwaka huu nimepiga picha nyingi sehemu nilizopata fursa ya kuzitembelea: Arusha, Dar es Salaam, Lushoto, Morogoro, Moshi, na Tanga.

Watu ambao wameishi Tanzania tu wanaweza kuuliza kwa nini napiga picha hata sehemu ambazo si za pekee au muhimu. Siwezi kuwalaumu. Huku ughaibuni mambo ni tofauti, na napenda nitoe fununu kidogo.

Mbali na kufundisha hapa katika chuo cha St. Olaf, ninashughulika na programu zinazopeleka wanafunzi Tanzania na sehemu zingine za Afrika. Kazi yangu ni kuwaandaa hao wanafunzi, kwa kuwaeleza mambo ya utamaduni, maisha, elimu, na kadhalika yahusuyo nchi hizo wanakokwenda.

Picha zangu hizi ni hazina inayonisaidia katika shughuli hizi. Mbali ya kuwaelimisha, zinawahamasisha katika kupenda kuja Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Wiki iliiyopita, niliporejea hapa chuoni kutoka Tanzania, mkuu wa idara yangu ya ki-Ingereza aliomba nitundike picha za Tanzania kwenye ubao wetu wa matangazo. Niko katika harakati ya kuziandaa. Ni fursa ya kuitangaza Tanzania, nami nimeipokea kwa furaha. Picha hizi zitakaa hapo kwa wiki kadhaa, labda miezi.

Napangia kutundika picha za Chuo Kikuu Dar es Salaam, maeneo ya miji niliyoitembelea na vijiji mbali mbali. Nitatundika picha za matukio mbali mbali. Nitatundika picha za makanisa na misikiti, nikizingatia kuwa wa-Marekani hawajazoea kuona misikiti, na mbaya zaidi, wengi wana mawazo potofu kuhusu misikiti na u-Islam, kama nilivyogusia hapa. Hizi picha zitachangia kuwaelimisha.

Jambo la ziada ni kuwa ninazunguka sehemu mbali mbali hapa Marekani nikitoa mihadhara kuhusu masuala kama elimu na tamaduni, kama inavyoonekana katika blogu zangu. Basi, katika mizunguko hiyo, picha zangu ni hazina mojawapo na nyenzo ya kuelimishia.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...