Kwanza, nakumbuka kuwa nilianza kublogu baada ya kuhamasishwa na ndugu Freddy Macha na Jeff Msangi, mmiliki wa Bongo Celebrity. Hao wawili walifahamu kuhusu maandishi yangu, wakanishawishi nianzishe blogu. Nami nilifuata ushauri wao.
Nilianzisha blogu mbili: ya ki-Swahili, na ya ki-Ingereza. Nilijifunza na naendelea kujifunza huku nikiblogu. Katika harakati hiyo, Dada Subi, mmiliki wa Wavuti amekuwa akinisaidia, kama anavyowasaidia wanablogu wengine.
Kwangu mimi blogu ni ukumbi wa kuelezea mawazo, hisia, fikra na mambo yangu mengine, na hivi kuyahifadhi na kuwashirikisha wengine. Siblogu kwa imani kuwa nina ujuzi au busara kuliko watu wengine. Blogu ni baraza inayonikutanisha na wengine kwa mazungumzo, mijadala na kubadilishana mawazo.
Vile vile, ninablogu kwa sababu nimeona umuhimu wa blogu kwa upande wa lugha. Ninavyoandika ki-Swahili najiongezea uzoefu wa kutumia lugha hiyo ipasavyo. Hiyo ndio jitihada yangu, na hili ndilo lengo langu.
Mazoezi ni mazoezi. Tunapofanya mazoezi ya viungo daima, tunajijengea afya bora, na tunaanza kuusikia mwili ukikaa sawa. Kwa namna hiyo hiyo, kuandika kwa ki-Swahili kumenifanya niisikie akili yangu ikizidi kukaa sawa, kwa upande huu wa matumizi ya lugha. Nazidi kujiamini katika utumiaji wa lugha hii.
Katika blogu yangu ya ki-Ingereza, naandika kwa lengo la kuonyesha uandishi bora wa ki-Ingereza. Ni lugha ambayo nimeipenda tangu nilipoanza kujifunza, darasa la tatu, na naifundisha hapa katika Chuo cha St. Olaf, Minnesota.
Kublogu kumeniunganisha na watu wengi ambao wanasoma blogu zangu, kutoka pande zote za dunia. Inaleta faraja, kwa mfano, ninapotambua kuwa kitu fulani nilichoandika katika blogu kimekuwa ni msaada kwa mtu fulani. Kwa mfano, miezi kadhaa iliyopita, nilipata ujumbe kutoka kwa mama mmoja aliyeko Ujerumani.
Aliulizia namna ya kufika Mbamba Bay na mahali pa kulala akishafika kule, kwani alikuwa anapangia kuja Tanzania. Alisema kuwa aliniuliza kwa vile alisoma habari za Mbamba Bay kwenye blogu yangu. Nilimpa maelezo aliyohitaji. Wakati huu wote yeye alikuwa Ujerumani na mimi nilikuwa Marekani. Alikuja Tanzania mwaka huu na familia yake, wakati nami niko nchini. Tulionana Ubungo, kwenye kituo cha mabasi, kama inavyoonekana katika picha hii, wakiwa wamefurahi kununua nakala ya Matengo Folktales