Saturday, February 28, 2015

Kitabu Kinapoingia Amazon

Kati ya majina yanayojulikana sana mtandaoni ni Amazon, duka la mtandaoni ambamo vinapatikana vitu mbili mbali. Wengi wetu, kama sio wote, tunalihusisha jina la Amazon na vitabu.

Wanunuaji wa vitabu mtandaoni moja kwa moja huwazia duka la Amazon. Mimi mwenyewe, katika matamasha ya vitabu ninayoshiriki, nimezoea kuulizwa na watu iwapo vitabu yangu vinapatikana Amazon. Hao ni watu ambao wangependa kununua vitabu vyangu ila hawana hela wakati huo. Waandishi wanaitegemea Amazon kama sehemu ya kuuza vitabu kwa urahisi, hasa ikizingatiwa kwamba Amazon imejijenga sehemu nyingi za dunia.

Binafsi, sikutaka kuviweka vitabu vyangu Amazon. Sikupendezwa na jinsi kampuni hii kubwa inavyowaharibia biashara wauzaji wadogo wadogo, kama yanavyofanya makampuni makubwa katika mfumo wa ubepari.

Nilitaka vitabu vyangu viuzwe na maduka madogo madogo, ya watu wa kawaida au taasisi za kawaida. Niliridhika kuona vitabu yangu vinauzwa na duka la vitabu la Chuo cha St. Olaf, kwa mfano.

Lakini, nilikuja kushangaa baadaye kuwa, ingawa sikuvipeleka vitabu yangu Amazon, vilianza kuonekana kule. Hapo nilitambua kuwa Amazon ina nguvu au mvuto kuliko nilivyodhania. Ni kama kifaru anayetembea nyikani bila kubughudhiwa na wanyama wadogo wadogo.

Amazon inauza vitabu vipya na pia nakala zilizotumika. Mtu akishanunua na kusoma nakala yake, anaweza kuiuza Amazon. Ukiangalia tovuti ya Amazon, utaona vitabu vyangu vipya vinauzwa sambamba na vilivyotumika.

Kutokana na hali halisi ya ushindani katika uchumi wa kibepari, Amazon inauza au inaweza kuuza vitabu kwa bei ya chini kidogo au sana, ukifananisha na wauzaji wengine, kuanzia wachapishaji hadi hasa wauzaji wadogo wadogo. Vile vile, malipo ("royalties") anayopata mwandishi kutokana na mauzo ya vitabu vyake Amazon huwa ni pungufu kuliko yale ayapatayo au anayoweza kuyapata kutoka kwa wachapishaji, ingawa nayo si makubwa, bali ni asilimia ndogo ya bei ya kitabu.

Pamoja na yote hayo, Amazon imetamalaki katika uwanja huu wa uuzaji wa vitabu mtandaoni. Ingawa kuna makampuni mengine pia, kama vile Barnes and Noble, Amazon ndio inayoonekana kutawala vichwani mwa watu.

Amazon inauza vitabu halisi, yaani vya karatasi, na vitabu pepe. Ni juu ya mwandishi kuamua kama anataka kukiweka kitabu chake katika mtindo wa kielektroniki. Inavyoonekana, kadiri siku zinavyopita, watu wengi zaidi na zaidi wanaingia katika mkondo huu wa kununua vitabu pepe. Mimi mwenyewe nimeshuhudia hayo, na nimekuwa nikijitahidi kwenda na wakati. Baadhi ya vitabu vyangu vinapatikana kama vitabu pepe kwenye mtandao wa lulu na mtandao wa Amazon.

Hata hivi, kuna mjadala mkubwa unaoendelea kuhusu hatima ya vitabu tulivyovizoea, yaani vya karatasi. Wakati wengine wanaamini kuwa vitabu hivi vitadidimizwa na vitabu pepe, wengine wanasema kuwa hilo halitawezekana, kutokana na mazoea na mapenzi yaliyojengeka kwa vitabu kama vitabu. Wanasema kuwa hivi vitabu vya jadi vitakuwepo sambamba na hivi vya kielektroniki.

Nimeona niseme hayo, kwa manufaa ya wengine ambao ni waandishi au wanawazia kuwa waandishi.

Thursday, February 26, 2015

Leo Nimefundisha Darasa Kwa Kutumia "Skype"

Asubuhi ya leo, nimefundisha darasa kwa kutumia "Skype." Ni darasa la Mwalimu Kristofer Olsen la somo la "Mythologies," katika Chuo Kikuu cha Montana, Marekani. Chuo hiki kiko mjini Bozeman, maili 995 kutoka hapa nilipo, Northfield, Minnesota. Niliandika kuhusu mpango wa kufundisha darasa hili katika blogu hii.

Katika mawasiliano ya barua pepe na Mwalimu Olsen, aliniuliza iwapo ningeweza kuongea na darasa lake la "Mythologies," ambalo lilikuwa linasoma kitabu changu cha Matengo Folktales. Aliniletea silabasi ya somo, inayoonyesha kuwa tarehe 24 na 26 wangejadili Matengo Folktales.

Jana jioni, binti yangu Zawadi alinielekeza tena namna ya kutumia "Skype," na alinisajili. Leo asubuhi, kipindi kilianza kama ilivypoangwa, saa nne na nusu za hapa Minnesota, ambayo ni saa tatu na nusu kule Montana. Nilikuwa mbele ya kompyuta, na wanafunzi na profesa wao walikuwa wananiona na kunisikia, nami nilikuwa nawaona na kuwasikia.

Tulifanya mengi. Niliombwa kusimulia hadithi mojawapo, ambayo ingechukua muda mfupi, nami nikasimulia hadithi ya "Hawk and Crow," iliyomo kitabuni. Niliwaambia wanafunzi kuwa kokote niendako kuongelea hadithi za jadi, huzisimulia papo kwa papo, badala ya kuzisoma. Katika kusimulia hadithi ya "Hawk and Crow," niliwaeleza machache kuhusu namna hadithi inavyosimuliwa, tofauti na inavyoonekana kimaandishi.

Masuali yao yalikuwa ya maana sana. Suali moja lilihusu jinsi nilivyorekodi hadithi na kuandaa kitabu cha Matengo Folktales. Suali jingine lilihusu mchakato wa kutafsiri. Jingine lilihusu vifo na mauaji katika hadithi hizo. Jingine lilihusu mhusika mjanja ("trickster") katika hadithi, kama vile Anansi na Sungura.

Niliwaeleza mambo kadhaa kuhusu mhusika huyu, katika tamaduni mbali mbali. Mhusika huyu hujitokeza kama mnyama (kama vile Anansi au Gizo, Kobe na Sungura), na katika tamaduni zingine hujitokeza katika umbo la binadamu, kama vile Nasreddin Hodja na Abu Nuwas. Niliongelea asili na maana ya mhusika huyu katika jamii, kwa kutumia nadharia za kisaikolojia za Carl Jung.

Niliguswa kwa namna ya pekee nilipoulizwa nifafanue dhana iliyomo katika blogu yangu kwamba ninaliona darasa kuwa ndio mahali pekee penye uhuru kamili wa kufikiri na kujieleza. Kumbe kuna watu wanaosoma blogu yangu kwa makini kiasi hiki.

Mawasiliano kama haya ya kutumia "Skype" ni maendeleo ya tekinolojia, ambayo yanatuwezesha kufanya mambo ambayo hatukuweza kuyafanya kabla. Jambo moja la kujifunza ni kuwa tunaweza kuendesha darasa bila kukutana katika chumba kimoja. Mimi kama mwalimu, ninaweza kuwafundisha wa-Tanzania ingawa niko nje ya Tanzania. Tuachane na mawazo kwamba sherti nirudi Tanzania ili kujenga nchi.

Wakati tekinolojia inasonga mbele na kutufungulia milango mipya, inashangza kuona jinsi wa-Tanzania kwa ujumla wanavyoendelea kuwa na mawazo yaliyopitwa na wakati. Kila ninapowasikia wakidai kuwa wataalam walioko nje warudi nyumbani wakajenge Taifa, nawazia suala hilo. Najiuliza ni lini wataamka usingizini na kutambua kuwa maendeleo ya tekinolojia ya mawasiliano yanazidi kuififisha mipaka ya kijiografia tuliyoizoea. Tunaingia kwenye dunia isiyo na mipaka, dunia ambamo mtu popote alipo anaweza akatoa mchango wake kwa walimwengu popote.

Wednesday, February 25, 2015

Yatokanayo na Mihadhara ya Jana Chuoni South Central

Tangu nilipomaliza ziara yangu chuoni South Central jana, nimekuwa na furaha kutokana na mafanikio ya ziara ile. Kuanzia jana ile ile, taarifa zimeenea za kuisifia ziara ile. Mfano ni namna mwenyeji wangu, Mwalimu Becky Fjelland Davis, alivyoandika katika blogu yake. Ninafurahi kuwa sikumwangusha, kwani katika kuandaa ujio wangu, alikuwa ameutangazia umma kama ifuatavyo:

Come one, come all, to hear what he has to say. You'll be touched by his wisdom and wit, as well as his gentle demeanor.

Mwalimu Fjelland Davis aliandika hivyo kwa kujiamini, kwani alishanialika mwaka 2013 kuongea na wanafunzi wake, kama alivyoripoti katika blogu yake.

Kwa kuwa nilialikwa ili nikaongelee masuala yaliyomo katika kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, nimefurahi kuona jinsi ziara yangu ilivyotekeleza mategemeo ya waandaaji na wote waliohudhuria  mihadhara yangu.

Ninafurahi kuwa ziara ya jana imefanyika mwezi huu, ambapo ninasherehekea kutimia kwa miaka kumi tangu nilipochapisha kitabu hiki. Pia ni faraja kwangu, baada ya miezi mingi ya kuwa katika matatizo ya afya. Nakumbuka kauli ya wahenga kuwa baada ya dhiki, faraja.

Makala hii fupi haiwezi kumaliza tathmini ya ziara ya jana. Kumbukumbu itaendelea mawazoni mwangu na katika jamii. Ila kuna jambo moja ambalo napenda kulitaja. Duka la vitabu la chuoni South Central lilikuwa linauza kitabu changu kwa dola 17.95. Ukifananisha na bei yake ya dola 13 niliyoweka mtandaoni, ni wazi kuwa mwuzaji anajipatia faida. Hakuna kizuizi kwa muuzaji yeyote kujipangia bei yake.

Tuesday, February 24, 2015

Ziara Yangu Mankato Imeenda Vizuri


Ziara yangu Mankato, kutoa mihadhara katika
Chuo cha South Central, imekuwa njema kabisa. Shughuli yangu ya kwanza ilikuwa ni kukukutana na wanafunzi wa Mwalimu Fjelland Davis, kama inavyoonekana pichani hapa kushoto. Wanafunzi hao walikuwa wamesoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Kwa sababu hiyo, sikutaka kutoa mhadhara, bali nilitoa maelezo mafupi juu yangu na shughuli zangu za uelimishaji wa jamii, kisha nikatoa fursa ya masuali. Tulitumia zaidi ya saa nzima kwa masuali na majibu.
Baada ya hapo, nilipelekwa katika ukumbi mkubwa uliojaa watu, nikatoa mhadhara kuhusu "Writing About Americans."  Katika picha hapo kushoto ambayo nimeitoa kutoka ukurasa wa Facebook wa Chuo Cha South Central ninaonekana nikitoa mhadhara huo.
Hapa kushoto ni picha nyingine ya mhadhara wa "Writing About Americans," ambayo nimeitoa kutoka ukurasa wa Facebook wa Mwalimu Davis.

Baada ya kumaliza mhadhara huu, katika ukumbi uliojaa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, Mwalimu Davis alitangaza kuwa vitabu vyangu viko katika duka la vitabu hapa chuoni, na kwamba nilikuwa tayari kusaini vitabu hivyo. Ndivyo ilvyokuwa. Watu walikimbilia dukani, wakanilietea nakala niwasainie.  Pichani hapa kushoto ninaonekana nimesimama na dada mmoja kutoka Peru, akiwa ameshika nakala yake niliyomsainia.

Katika kuandaa na kutoa mhadhara wa "Writing About Americans," na kwa jinsi watu walivyoufurahia, nimepata motisha ya kuandika kijitabu kuhusu mada hiyo.

Alasiri hii, niliporejea hapa kazini kwangu,  mjini Northfield, nimeanza kuona taarifa katika mtandao wa Facebook, kuhusu ziara yangu. Watu wamefurahia maongezi yangu, na wamemshukuru Mwalimu Becky Fjelland Davis kwa kunialika.

Monday, February 23, 2015

Mihadhara ya Mankato ni Kesho

Siku zinakwenda kasi. Naona kama ndoto, kwamba safari yangu ya kwenda Chuo cha South Central, mjini Mankato, kutoa mihadhara ni kesho asubuhi.

Ninangojea kwa hamu kutekeleza majukumu yaliyoko mbele yangu, ambayo ni kwanza kuongea na wanafunzi wanaojiandaa kwa safari ya Afrika Kusini kimasomo, na pili ni kutoa mhadhara kwa jumuia ya chuo ambao mada yake itakuwa "Writing About Americans."

Maongezi yote hayo yatahusu masuala ya tofauti za tamaduni na athari zake ulimwenguni. Wanafunzi wanaokwenda Afrika Kusini wanajiandaa kuishi na kushughulika na wa-Afrika, katika utamaduni ambao ni tofauti na ule wa Marekani. Utaratibu huu wa maandalizi, ambao umeshakuwa jambo la kawaida hapa Marekani, ingekuwa bora ufuatwe na wengine, kama nilivyowahi kuwaasa wa-Tanzania wenzangu.

Katika maandalizi hayo, hao wanafunzi wanasoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kitabu ambacho, japo kidogo, kinawagusa watu, tangu nilipokichapisha, tarehe 5 Februari, 2005. Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kukiandika kama nilivyoandika, hadi kimekuwa msingi wa mialiko ya kwenda kuongelea yaliyomo na yatokanayo.

Katika mhadhara wa "Writing About Americans," ninapangia kuelezea mchakato wa kuandika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kuanzia chimbuko la wazo la kukiandika, mchakato wa kukiandika, mambo muhimu niliyojifunza katika kuandika huku, hadi jinsi kitabu kilivyopokelewa na jamii, hasa wa-Marekani, ambao ndio wanaoongoza katika usomaji wake.

Jambo moja kubwa nililojifunza katika kutafakari na kuandika ni kuheshimu tamaduni, pamoja na tofauti zake. Shaaban Robert angeishi miaka mingi zaidi ya ile aliyoishi, angetufundisha mengi kuhusu suala hilo.

Panapo majaliwa, nikikamilisha ziara ya kesho, nitaandika taarifa katika hii blogu yangu.

Saturday, February 21, 2015

Lugha na Mwamko wa Elimu Tanzania

Katika kuendelea kutekeleza ombi nililopata kutoka kwa mdau wa blogu hii, juu ya sera ya lugha ya kufundishia nchini Tanzania, napenda kuongelea suala la lugha na mwamko wa elimu. Huu ni mwendelezo wa ujumbe nilioandika katika makala yangu, "Tatizo si Lugha ya Kufundishia, ni Uzembe." ambayo niliichapisha katika blogu hii.

Kwanza, nasisitiza mtazamo wangu kuwa tatizo si lugha ya kufundishia, bali uzembe.

Mimi kama mwelimishaji, nimeshuhudia tatizo hili lilivyo katika jamii ya wa-Tanzania. Nitaanza kwa kutoa mfano. Mwaka 1980, nilipokuwa mhadhiri katika idara ya "Literature" ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nilifika kusomea shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, Marekani.

Niliondoka Tanzania wakati jamii ikiwa bado inazingatia mafundisho ya Mwalimu Nyerere kuhusu elimu. Kwa miaka sita niliyokuwa masomoni, nilifanya bidii katika masomo na pia nilinunua vitabu vingi sana, nikijua kuwa ndio nyenzo itakayonifanya nifundishe kwa kiwango cha juu kabisa pindi nitakaporejea tena Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Nilipohitimu masomo, nilirejea nchini nikiwa na shehena yangu ya vitabu. Badala ya kuniulizia kuhusu masomo niliyosomea au elimu niliyoipata, watu waliniuliza kama nimeleta "pick-up." Walinishangaa kwa kuleta vitabu badala ya gari. Haikutegemewa kuwa mtu ukae "majuu" miaka yote ile halafu usirudi na gari.

Hapo nilitambua wazi kabisa kuwa mwamko wa elimu, ambao alikuwa ameuchochea Mwalimu Nyerere, ulikuwa umedidimia. Niliendelea kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam huku nikishuhudia mwamko wa elimu ukiendelea kudidimia nchini.

Jadi ya kuthamini mali na vitu badala ya elimu iliendelea kushamiri. Wasomi wakipata fursa ya kwenda nje, inayojulikana kama "sabbatical," walitegemea na walitegemewa kutumia fursa hiyo kujitafutia vitu, hasa magari. Mwenye kuleta gari au magari alionekana ndiye msomi bora. Ni tofauti kabisa na hapa Marekani, ambapo profesa unathaminiwa kwa ujuzi wako, hata kama unatembelea baiskeli au unapekua kwa miguu. Binafsi, kwa kuwa kipaumbele changu elimu na taaluma nimeridhika kufundisha hapa Marekani, tangu nilipoanza, mwaka 1991.

Tanzania, ilikuwa ni jambo la kawaida kwa walimu kushughulikia shughuli zao za kujipatia pesa hata kama walipaswa wawe darasani wakifundisha. Jambo hili limekuwa likitajwa na wanafunzi wetu wa ki-Marekani tunaowapeleka kusoma Tanzania, kwani katika vyuo vyao hapa Marekani, profesa hawezi kukosa kuingia darasani bila sababu ya maana kama vile kuumwa. Na akikosa kipindi, hufanya mpango wa kukifidia.

Katika jamii ya wa-Tanzania, nilishuhudia kushamiri utamaduni wa kutafuta vyeti kwa njia yoyote, badala ya kutafuta elimu. Nilishuhudia jinsi watu walivyokuwa tayari kutafuta hata vyeti feki. Hata baadhi ya wale wanaoitwa viongozi wamejipatia hivyo vyeti feki, kutoka  vyuo ambavyo havina hadhi itambulikanayo katika ulimwengu wa taaluma.

Kama ambavyo nimekuwa nikilalamika tena na tena katika blogu hii, utamaduni wa kununua na kusoma vitabu umekosekana katika jamii ya wa-Tanzania. Wazazi, ambao wangetegemewa kuwa wanunuaji wa kuaminika wa vitabu na wawe wanawasomea vitabu watoto wao, kama wafanyavyo wa-Marekani, hawafanyi hivyo.

Hao tunaowaita viongozi Tanzania, na wa-Tanzania wengine wengi, hutembelea nchi za nje. Sijui ni wangapi wanatumia fursa hii kununua vitabu na kurudi navyo Tanzania. Katika miji wanayopita na katika viwanja vya ndege, kuna maduka ya vitabu. Sijui ni wangapi wanapita katika maduka hayo na kununua vitabu. Nimewahi kusafiri mara kwa mara na wa-Tanzania, na nimeona kuwa zawadi wanazonunua ni vitu kama vipodozi, marashi, na mizinga ya vinywaji vikali. Wa-Tanzania hupenda zawadi za aina hiyo. Vitabu je? Jibu mwenyewe.

Sijui ni nyumba zipi katika Tanzania ambazo zina maktaba. Sijui ni nyumba ngapi ambazo zina vitabu angalau 50 au 100, kwa ajili ya watoto na wazazi. Kutegemea kuwa utamwona m-Tanzania amekaa sebuleni, bustanini, ufukweni, ndani ya basi au ndege, anasoma kitabu, ni kama kutegemea kumwona jogoo amevaa suruali.

Niliwahi kuhudhuria tamasha la vitabu Dar es Salaam, mwaka 2004. Watoto walikuwepo, na waalimu, lakini watu wazima walikuwa wachache sana. Hata hao wanaoitwa viongozi, wa ngazi yoyote, hawakuwepo. Watoto walifanya maonesho mbali mbali na waliimba nyimbo. Katika wimbo mmojawapo, waliwasihi wazazi wawe wananunua vitabu na kusoma pamoja na watoto wao majumbani. Wazazi wenyewe hawakuwepo kwenye tamasha. Lakini jioni, nilipokuwa naelekea nyumbani, niliwaona hao watu wazima wamekusanyika kwenye mabaa.

Katika hali hii, tatizo linalohitaji kushughulikiwa ni mwamko wa elimu. Bila mwamko wa elimu, hata lugha ya kufundishia ikibadilishwa mara ngapi, hata tukisema tutumie lugha zetu za ki-Nyaturu, ki-Nyasa, ki-Zaramo, na kadhalika, tusitegemee kuwa tutaleta mapinduzi yatakiwayo. Kinachohitajika ni mwamko wa elimu. Huu ndio msingi, ambao tumeuharibu.

Tuesday, February 17, 2015

Tatizo si Lugha ya Kufundishia, ni Uzembe

Jana, katika blogu hii, mdau mmoja aliniomba niandike makala kuhusu lugha ya kufundishia nchini Tanzania. Aliandika hivi:

Prof Mbele. Pole na kazi za kila siku.
Ningependa kujua nini maoni yako kuhusu kutumia kiswahili kama lugha kuu ya kufundishia mpaka chuo kikuu. Je unalionaje hili, unaona kutakuwa na athari zozote kutokana na elimu?. Je ni kweli tutakuwa tumejitenga na dunia?.

Ningeomba kama ungepata nafasi basi ukaliandika hili kama post katika blog na wala si comment. Nakutakia siku njema


Kwa kweli mada hii ya lugha ya kufundishia Tanzania imejadiliwa sana, katika vitabu, majarida, magazeti, mitandao, mikutano, na kadhalika. Siamini kama ninaweza kusema lolote ambalo halijasemwa. Hata hivi, nina mtazamo wangu, kama watu wengine.

Ninaamini kwa dhati kuwa tatizo si lugha ya kufundishia bali uzembe. Ingekuwa watu wanatambua umuhimu wa elimu, kwa maana halisi ya elimu, hawangekuwa wanatoa visingizio au lawama kama wanavyofanya. Hawangekuwa wanatumia muda wao katika kulalamika. Wangeelekeza nguvu zao na akili zao katika kutatua matatizo yoyote na kusonga mbele.

Kwamba mwanafunzi anafanya vizuri akifundishwa kwa lugha yake, ni hoja inayovutia, lakini sina hakika kama ninaikubali sana. Ingekuwa ninaikubali sana au kabisa, ningesema basi tuwafundishe watoto wetu kwa ki-Nyakyusa, ki-Sukuma, ki-Yao, na kadhalika. Kwa wengi, ki-Swahili ni lugha yao ya pili. Sisi hatukufundishwa kwa lugha mama, bali tulifundishwa kwa lugha ngeni ya ki-Swahili na baadaye ki-Ingereza, na hatukutetereka. Kwa nini mambo yawe kinyume leo, kama si uzembe?

Kama lugha ya ki-Ingereza ni tatizo, jawabu ni kufanya bidii kujifunza lugha hiyo. Kusema kwamba tuache kufundishia kwa ki-Ingereza eti kwa vile ufahamu wa ki-Ingereza ni mdogo ni kuhalalisha uzembe. Kinachotakiwa ni kufanya bidii kujifunza lugha hiyo kama tulivyokuwa tunafanya sisi.

Uzembe umetufikisha hapa tulipo. Kwa nini majirani zetu wa Malawi, Kenya, na Uganda hawatoi visingizio kama wanavyotoa wa-Tanzania? Ki-Ingereza sio lugha ya wenzetu hao, bali ki-Chewa, ki-Yao, ki-Ganda, ki-Acholi, ki-Kamba, Kikuyu, na kadhalika, kama ilivyo kwetu ki-Pare, ki-Luguru, ki-Makonde na kadhalika.

Kwa nini hao majirani zetu wawe wanatumia ki-Ingereza hadi chuo kikuu bila malalamiko kama wanayotoa wa-Tanzania? Enzi zetu, tulikuwa tunasomeshwa kwa ki-Ingereza sekondari (au kabla?)na kuendelea. Tulisoma chuo kikuu na hao wenzetu kutoka nchi za jirani, kwa ki-Ingereza bila matatizo. Leo ki-Ingereza kimekuwa shida. Ni nini kimetokea, kama si uzembe?

Ingawa nina mengine ya kusema, ninaamini kuwa blogu ni mahali pa makala fupi fupi, tofauti na kitabu. Kwa leo naona niishie hapa. Nitaendelea kuandika, ili kuongelea vipengele vya ujumbe wa mdau ambavyo sijavigusia hapa.

Sunday, February 15, 2015

Hadithi za Wa-Matengo Chuoni Montana

Leo nimepata ujumbe wa barua pepe kutoka kwa mwalimu mmoja wa Chuo Kikuu cha Montana.Ananiambia kuwa muhula huu anafundisha kozi ya Mythologies, na kati ya nyenzo anazotumia ni kitabu changu cha Matengo Folktales. Ananiulizia kama nitaweza kuongea na wanafunzi wake kwani itawafaidia sana kuweza kuongea na mtafiti aliyeandaa kitabu, akatoa maelezo kuhusu mambo kadha wa kadha, kama vile mchakato wa utafiti. Amependekeza kuwa ikiwezekana, tupange siku waweze kuongea nami kwa njia ya Skype.

Nimemjibu kuwa niko tayari kutoa mchango wangu, na kuwa ninafurahi kusikia kuwa anafundisha masimulizi ya wa-Matengo, sambamba na yale ya wa-Griki wa kale na wengine. Ingawa binti yangu Zawadi alishanionyesha namna ya kutumia Skype na akanisajili, sijawahi kutumia tekinolojia hii. Wengi wa rika langu au wale wanaotuzidi umri, tumezoea mambo ya zamani. Lakini dunia inavyobadilika, hasa tekinolojia, tunalazimika kukiri mazoea yana taabu.

Ujumbe niliopata leo umenifanya niwazie mambo kadhaa. Kwanza, ni kwamba nilifanya utafiti na kuandaa kitabu hiki kwa miaka yapata 23. Wakati nachapisha kitabu hiki, nilikuwa tayari ninafundisha huku Marekani, baada ya kufundisha Chuo Kukuu Cha Dar es Salaam. Nilikuwa na hamu kuwa kitabu kiwe mchango wangu kwa elimu Tanzania, kwa ufundishaji wa chuo kikuu, kwani hapakuwa na kitabu cha aina ile nchini, kilichofaa kufundishia somo hili la hadithi za mapokeo ("folktales"). Nilijua hayo, kwa vile mimi ndiye nilikuwa mhadhiri wa somo la fasihi simulizi, sambamba na somo la nadharia ya fasihi.

Kilichotokea ni kuwa kitabu hiki kinatumika au kimetumika katika vyuo vikuu vya Marekani. Vyuo ninavyovifahamu ni Wichita State University, University of California San Diego, St. Olaf College, Colorado College, na College of St. Benedict/St. John's University. Niliwahi kualikwa na hicho chuo cha St. Benedict/St. John's kutoa mhadhara katika darasa la "fairy tales," ambalo lilikuwa linasoma kitabu cha Matengo Folktales, kama nilivyoripoti katika blogu yangu, na nilitoa pia mhadhara kwa jumuia ya chuo kuhusu kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Hayo ni baadhi ya mawazo yaliyomo akilini mwangu, wakati huu ninapofikiria ujumbe niliopata leo. Ingawa kwa upande mmoja ninafurahi, sijawahi kuridhika na hali hii ya vitabu vyangu kuwa vinawafaidia wa-Marekani, lakini sio wa-Tanzania. Hata hivi, kosa si langu. Mimi natimiza wajibu wangu wa kufanya utafiti, kuandika, na kuchapisha maandishi. Baada ya hapo, mwenye macho haambiwi tazama.

Saturday, February 14, 2015

Miaka Kumi ya Kitabu: Shukrani Wanablogu

Katika kusherehekea miaka kumi tangu nilipochapisha kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, nawajibika kuwakumbuka watu wengi waliokuwa nami bega kwa bega katika kunitangazia kitabu hiki. Leo napenda kuwakumbuka wanablogu wa ki-Tanzania, ambao wamechangia katika kunihamasisha na kuniunga mkono miaka yote hii.

Pichani hapa kushoto anaonekana mwanablogu Simon Kitururu, ambaye amewahi kuniambia mara kadhaa kuwa anasoma maandishi yangu kila yanapopatikana. Anaonekana ameshika vitabu vyangu viwili: Matengo Folktales na Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Picha hiyo aliichapisha katika blogu yake ya Mawazoni.

Mwanablogu Issa Michuzi amefanya juhudi kubwa kutangaza shughuli zangu, kama vile warsha na mihadhara. Ni mfuatiliaji wa blogu yangu, na mara kwa mara huamua kuchapisha baadhi ya makala zangu katika blogu yake. Hata leo amechapisha makala yangu kuhusu kitabu changu kutimiza miaka kumi.

Subi Nukta naye ametoa mchango wake, ikiwemo kutangaza kitabu hiki kinachotimiza miaka kumi. Katika blogu yake, aliandika hivi:

Africans and Americans: Embracing Cultural Differences is a book by Professor Joseph Mbele that I would recommend to anybody willing to learn something about a culture that is different fro theirs.

Since Tanzania is my home country, I'd ask anybody planning to travel to Tanzania, or anybody unsure on what to do when in a different culture to buy this book. To order your copy, simply click on the book's image and you will be taken to lulu.com where you can purchase it
.

Jeff Msangi ni mwanablogu mwingine ambaye ananiunga mkono kwa dhati. Aliandika kuhusu kitabu changu hapa. Hakuishia hapo, bali siku nyingine alandika hivi:

Now, if you live or have lived in the US in the past, you will agree with me that there are a lot of things or let me call them cultural differences between Africans and Americans. There is a lot of learning and adjustment for newcomers/immigrants from Africa. The same applies to Americans going or rather growing up in Africa. My good friend, Prof. Joseph Mbele, highlights these cultural differences very well in his famous book titled “Africans and Americans-Embracing Cultural Differences”. I recommend everyone to read this book.

Christian Bwaya ameandika mara kadhaa kuhusu kitabu hiki, kwa mfano hapa. Wanablogu wengine wametoa mawazo yao kuhusu kitabu hiki katika maoni kwenye mijadala. Mfano ni Sophie Becker ambaye aliandika katika blogu ya Jielewe:

Hiki kitabu kifundisha na kuburudisha. Kinakuelezea mambo ambayo yangekuchukua miaka kadhaa kuyaelewa au usiyaelewe kabisa harafu Prof.Mbele kakiandika with sense of humor utacheka sana.nimekipenda sana.

Ningeweza kuendelea kuwataja wanablogu wengine, kama vile Rachel Siwa Isaac, Profesa Masangu Matondo, na Yasinta Ngonyani, ambaye aliandika maoni yake hapa. Naamini kuwa wanablogu niliowataja na hata ambao nimeshindwa kuwataja, hawajaishia kuandika tu kuhusu kitabu changu. Bila shaka, kama ilivyo ada kwetu wanadamu, wamekiongelea na wanakiongelea katika mazingira mengine pia, kwa marafiki na watu wengine. Ninawashukuru wote kwa kuniunga mkono katika jukumu hili la kujenga mahusiano mema baina ya watu wa tamaduni tofauti.

Thursday, February 12, 2015

Kitabu Kimetimiza Miaka Kumi

Kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kimetimiza miaka kumi tangu nilipokichapisha, tarehe 5 Februari, mwaka 2005. Siku hiyo niliuingiza muswada katika mtandao wa lulu nikalipia namba ya utambulisho wa kitabu, yaani ISBN. Siku hiyo hiyo niliagiza nakala ya kwanza, nikaipata baada ya wiki moja hivi. Wiki hii ni kumbukumbu ya miaka kumi ya kuwepo kwa kitabu hiki.

Mambo mengi yametokea katika miaka hii kumi kuhusiana na kitabu hiki. Nimepata fursa ya kusikia maoni ya wasomaji wengi. Baadhi wameandika maoni hayo na kuyachapisha, kama vile katika tovuti, blogu, na majarida. Wengine wameniandikia maoni yao katika barua pepe. Wengine wamenieleza maoni yao katika maongezi ya ana kwa ana.

Watu waliotoa maoni yao kuhusu kitabu hiki ni wa aina mbali mbali. Baadhi nawakumbuka vizuri, kama vile Mhashamu Askofu Owdenburg Mdegella wa dayosisi ya Iringa ya Kanisa la Kiluteri Tanzania, ambaye alisema kuwa kitabu kimemfurahisha sana na anataka wageni wakisome ili watuelewe wa-Tanzania. Aliniambia hayo siku tulipokutana kwenye chuo cha Peace House, Arusha, na alikuwa anaongea kutokana na uzoefu wake mkubwa wa kuwapokea na kushughulika na wa-Marekani wanaokuja Tanzania katika mpango wa ushirikiano baina ya waumini wa-Marekani na wa-Tanzania uitwao Bega kwa Bega.

Mwingine ninayemkumbuka vizuri ni Balozi Mstaafu Andrew Daraja. Alikisoma kitabu hiki wakati akiwa balozi wa Tanzania hapa Marekani, na alinipigia simu akaniambia jinsi alivyokipenda kitabu hiki kama nyenzo ya kuweka maelewano baina wa wa-Marekani na sisi wa-Afrika.

Mzee Patrick Hemingway, katika maongezi naye, amekuwa akikisifia kitabu hiki. Siku tulipomtembelea, alisema kuwa kitabu hiki ni "tool of survival." Mzee huyu m-Marekani anajua anachokisema, kwani aliishi Tanganyika (baadaye Tanzania) kwa miaka yapata 25. Ninaguswa na maoni ya watu kama yeye, ambao wanajua hali halisi ya tofauti baina ya utamaduni wao na wetu.

Katika miaka hii kumi, nimepata mialiko kadha wa kadha kutoka kwenye vyuo, taasisi, makampuni, na vikundi, kwenda kutoa mihadhara kuhusu masuala ya tofauti za tamaduni na athari zake. Ingawa kitabu hiki ni kifupi tu kilichoandikwa kwa lugha rahisi, wala si cha kitaaluma, kimenisaidia kuendesha mihadhara hiyo na pia warsha, na hata kutatua migogoro ya kutoelewana baina ya wa-Marekani na wahamiaji na wakimbizi kutoka Afrika.

Ninawashukuru kwa namna ya pekee watu waliochangia kwa namna moja au nyingine kwa kukisoma kitabu, kuwaelezea wengine, na kunipa maoni yao. Wiki hii nitawakumbuka kwa namna ya pekee.

Mambo ni mengi sana yaliyotokea katika miaka hii kumi, ambayo ningeweza kuyaandikia kitabu. Panapo majaliwa, nitafanya hivyo.

Sunday, February 8, 2015

Mwenyeji Wetu Longido, Tanzania

Picha hii ilipigwa Januari, 2013, nilipokuwa Longido, Tanzania. Niko na Ndugu Ally Ahamadou, mkurugenzi wa programu ya utalii wa utamaduni hapa Longido. Yeye ndiye alikuwa mwenyeji wa misafara yangu katika kozi kuhusu safari na maandishi ya Ernest Hemingway.

Programu ya utalii wa utamaduni Longido ni moja kati ya programu maarufu za aina hii nchini Tanzania. Taarifa kuhusu program hii zinapakana kirahisi mtandaoni.

Binafsi nimeshuhudia jambo hili kwa jinsi makala niliyochapisha katika blogu yangu ya ki-Ingereza kuhusu utalii wa utamaduni Longido inavyotembelewa na wasomaji wengi. Hali hii imenithibitishia kuwa blogu inaweza kuwa nyenzo yenye uwezo mkubwa wa kutangaza utalii.

Ingawa Ndugu Ally Ahmadou si mzaliwa wa Longido, bali Tanga, niliona anakubalika sana na watu wa Longido. Hata kwa kuongea naye muda mfupi tu, unapata picha kuwa huyu ni mpenzi Longido na shughuli za utalii wa utamaduni. Programu hii ya utalii wa utamaduni Longido niliona inapendwa na watu wa Longido, kwa kuwa faida zake katika jamii yao wanaziona.

Ndugu Ally Ahmadou nilimwona kuwa mtu mwepesi wa kuangalia fursa mpya katika shughuli ya utalii. Mfano ni jinsi tulivyoongelea suala la vitabu katika utalii, suala ambalo nimeliongelea katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii na nililigusia pia katika blogu hii. Ndugu Ally alipofahamu kuwa nimechapisha vitabu vinavyoweza kuchangia katika sekta hiyo, alichukua nakala za kutosha za Matengo Folktales na Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kwa ajili ya watalii ambao wangependa kuvinunua.

Thursday, February 5, 2015

Kitabu Kimemgusa Mdau wa Bangladesh

Leo asubuhi nimepigiwa simu na mama mmoja kutoka Bangladesh anayefanya kazi katika benki ninayoitumia. Wiki kadhaa zilizopita, baada ya kufahamu kuwa hakuwa amekaa sana hapa Marekani, nilimwazimisha nakala ya kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ili aone mambo yalivyokuwa kwangu katika utamaduni huu mgeni. Nilihisi kuwa kingemsaidia kwa namna moja au nyingine.

Siku nyingine, nilipokwenda benki kwa shughuli zangu, tulionana, na aliniambia kuwa kitabu amekipenda, ila kilikuwa nyumbani. Basi nilimwambia kuwa tutafanya mpango nikichukue siku nyingine.

Jana nilimpigia simu kazini kwake, na kwa vile hakuwepo, niliacha ujumbe kwenye simu kwamba ninashiriki maonesho Jumamosi hii na, ikiwezekana, ningechukua kile kitabu; la sivyo, akitaka, anaweza kukilipia katika akaunti yangu na kukichukua moja kwa moja.

Leo asubuhi amenipigia simu, tukaongelea suala la kitabu. Alisema amekipenda na angetaka kumpelekea kaka yake aliyeko Canada, ila sasa hajui itakuwaje kwa vile ninakihitaji kwenye maonesho. Nilimwambia kuwa nina nakala zingine ambazo nadhani zitatosha, naye alisema atalipia kitabu. Nilimshukuru, nikamwuliza iwapo tutaweza kupanga siku tukutane, ili anieleze mawazo yake kuhusu yaliyomo kitabuni. Alikubali hima.

Nimeona niandike kumbukumbu hizi, kama ilivyo kawaida katika hii blogu yangu. Tangu siku ya kwanza mama huyu aliponiambia kuwa kitabu amekipenda, nilitambua kuwa ingawa niliandika kuhusu utamaduni wa mu-Afrika, kitabu kinawagusa watu wasio wa-Afrika pia.

Hili halikuwa jambo la ajabu kwangu, kwani katika kufundisha fasihi za sehemu mbali mbali za dunia, napata fursa ya kuyaelewa mambo kadha wa kadha ya tamaduni hizo. Nimegusia jambo hilo katika utangulizi wa kitabu changu.

Hata hivi, ingawa kusoma fasihi kutoka nchi fulani ni fursa ya kuufahamu utamaduni wa nchi ile, kuongea ana kwa ana na mtu au watu wa nchi ile ni fursa ya aina yake. Nami nangojea kwa hamu kuongea na huyu mama wa Bangladesh kuhusu kitabu changu na utamaduni wa kwao. Ninahisi nitajifunza mengi.

Wednesday, February 4, 2015

Wanachuo wa Gustavus Adolphus, Marekani, Wameifurahia Tanzania

Wanachuo wa Chuo cha Gustavus Adolphus, ambao walikuwa Tanzania mwezi Januari mwaka huu kwa ziara ya kimasomo, wamerejea salama nchini kwao Marekani. Hao ni wale ambao niliongea nao kuhusu tofauti baina ya utamaduni wa Marekani na ule wa kwetu Afrika, katika kuwaandaa kwa safari.

Jana, mmoja wao ameandika ujumbe katika blogu yangu ya ki-Ingereza:

Dr. Mbele,
Thank you very much for meeting with us before we left for Tanzania. We had a wonderful trip and learned so much about the differences and similarities between our two cultures. The Tanzanians are a beautiful people-- so full of happiness and passion for life. I will never forget my time there and hope that I can go back someday! Thanks you also for signing my copy of your book.
Abby Simms


Natafsiri ujumbe huu hivi:

Dr. Mbele,
Asante sana kwa kukutana nasi kabla hatujaondoka kwenda Tanzania. Safari yetu ilikuwa nzuri sana, na tulijifunza mengi kuhusu jinsi tamaduni zetu mbili zinavyofanana na jinsi zinavyotofautiana. Wa-Tanzania ni watu wazuri--wamejaa furaha na ari ya maisha. Sitasahau kamwe muda niliokuwepo kule na natumaini siku moja kwenda tena! Asante pia kwa kusaini nakala yangu ya kitabu chako.
Abby Simms.


Niliandika katika blogu hii kuwa hao wanachuo, kama walivyo wa-Marekani wengine, wana tabia ya kuripoti kuhusu safari na kukaa kwao Tanzania, nikaahidi kuwa nitakavyopata ripoti hizo, nitaziweka hapa katika blogu yangu.

Sidhani kama kuna m-Tanzania ambaye hatafurahi kusoma ripoti kama hii ya Abby Simms, kwa jinsi inavyotukumbusha kuwa tunayo mema na mazuri. Tukiamua, tunaweza kujibadili tukaachana na yale mabaya na tukaendeleza yale mema na mazuri.

Tuesday, February 3, 2015

Wa-Marekani na wa-Tanzania: Tofauti za Tamaduni

Leo, katika ukurasa wake wa "Facebook," Ndugu Maggid Mjengwa aliandika: "Leo Nimepokea Wafanyakazi Wa Kujitolea Kutoka Marekani..."

Wa-Marekani hao, ambao anaonekana nao katika picha hapa kushoto, wamefika Iringa kujitolea katika Kwanza Jamii, kampuni inayoendesha gazeti na redio. Maggid hakutuambia watakaa muda gani hapo Iringa, lakini nilijibu ujumbe wake "Facebook" namna hii:

"Safi sana. Ninapoona au kusikia mambo ya aina hii, wazo linalonijia akilini ni kuwa muhimu wageni wapate mtu wa kuwaelezea angalau yale ya msingi kuhusu tofauti kati ya utamaduni wa-Marekani na ule wa wa-Bongo, na wa-Bongo pia waelezwe kuhusu tofauti kati ya utamaduni wao na ule wa wa-Marekani. Hii ni kwa ajili ya kurahisisha shughuli na maisha kwa pande zote mbili. Kila la heri."

Suala hili nililoongelea ni muhimu hasa katika dunia ya utandawazi wa leo. Hao wageni wanapokuja kwetu na sisi tunapoenda kwenye nchi zao, ni mihumu kulizingatia, ili kufanikisha shughuli na mahusiano baina yetu. Nimeandika kuhusu tofauti baina ya utamaduni wa wa-Marekani na wa-Afrika katika kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho nashukuru kwa jinsi kinavyowasaidia watu wanaokisoma, kama ilivyoelezwa hapa na hapa.

Hilo ni suala ninalolishughulikia sana katika utafiti, mihadhara na warsha. Hiyo picha hapa juu tayari inanipa vidokezo muhimu. Ninaona jinsi hao wasichana walivyomwangalia Maggid usoni, na yeye ameangalia chini. Hapo Mjengwa anaonyesha heshima kwao, kwa mujibu wa utamaduni wetu wa ki-Tanzania na ki-Afrika kwa ujumla.

Nao hao wasichana, kwa mujibu wa utamaduni wa Marekani, wanaonysha heshima kwa kumwangalia Maggid usoni. Huenda wanashangaa kwa nini hawaangalii usoni. Hilo suala la kuangaliana usoni ni moja ya yale ninayoyaongelea katika kitabu changu:

Kama hii picha ingekuwa ni video, ingenipa fursa ya kusema mengi zaidi.

Sunday, February 1, 2015

Uandishi ni Kazi ya Upweke

Waandishi kadhaa maarufu wametamka kuwa uandishi ni kazi ya upweke. Mmoja wa waandishi hao ni Ernest Hemingway, ambaye picha yake inaonekana hapa kushoto.

Katika hotuba yake ya kupokea tuzo ya Nobel, alisema:

Writing, at its best, is a lonely life. Organizations for writers palliate the writer's loneliness but I doubt if they improve his writing. He grows in public stature as he sheds his loneliness and often his work deteriorates.

Najaribu kuitafsiri kauli hii:

Uandishi, katika hali yake bora kabisa, ni maisha ya upweke. Vyama vya waandishi hupunguza upweke wa mwandishi lakini sidhani kama vinaboresha uandishi wake. Hadhi yake katika jamii hukua kwa kadiri anavyoupunguza upweke wake na aghalabu ubora wa kazi yake hudorora.

Hemingway alilitafakari na kuliongelea sana suala la uandishi. Alifanya hivyo katika riwaya, insha na barua zake na pia katika mahojiano na maongezi mengine. Nami ninajifunza mengi kutoka kwake.

Katika makala yangu ya juzi nilitamka kwamba ninapoandika katika blogu yangu hii, ninajiandikia mwenyewe. Sijui na sijali kama kuna atakayesoma ninachoandika. Lengo langu la msingi ni kutimiza haja yangu ya kuutua mzigo uliokuwepo mawazoni mwangu.

Ni wazi kuwa fikra yangu hii inahusiana na yale ninayojifunza kutoka kwa Hemingway. Siko tayari kusukumwa na imani kwamba ninaiandikia jamii. Ningependa kuzingatia kauli ya Hemingway kwamba, "Writing, at its best, is a lonely life."