Saturday, February 21, 2015

Lugha na Mwamko wa Elimu Tanzania

Katika kuendelea kutekeleza ombi nililopata kutoka kwa mdau wa blogu hii, juu ya sera ya lugha ya kufundishia nchini Tanzania, napenda kuongelea suala la lugha na mwamko wa elimu. Huu ni mwendelezo wa ujumbe nilioandika katika makala yangu, "Tatizo si Lugha ya Kufundishia, ni Uzembe." ambayo niliichapisha katika blogu hii.

Kwanza, nasisitiza mtazamo wangu kuwa tatizo si lugha ya kufundishia, bali uzembe.

Mimi kama mwelimishaji, nimeshuhudia tatizo hili lilivyo katika jamii ya wa-Tanzania. Nitaanza kwa kutoa mfano. Mwaka 1980, nilipokuwa mhadhiri katika idara ya "Literature" ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nilifika kusomea shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, Marekani.

Niliondoka Tanzania wakati jamii ikiwa bado inazingatia mafundisho ya Mwalimu Nyerere kuhusu elimu. Kwa miaka sita niliyokuwa masomoni, nilifanya bidii katika masomo na pia nilinunua vitabu vingi sana, nikijua kuwa ndio nyenzo itakayonifanya nifundishe kwa kiwango cha juu kabisa pindi nitakaporejea tena Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Nilipohitimu masomo, nilirejea nchini nikiwa na shehena yangu ya vitabu. Badala ya kuniulizia kuhusu masomo niliyosomea au elimu niliyoipata, watu waliniuliza kama nimeleta "pick-up." Walinishangaa kwa kuleta vitabu badala ya gari. Haikutegemewa kuwa mtu ukae "majuu" miaka yote ile halafu usirudi na gari.

Hapo nilitambua wazi kabisa kuwa mwamko wa elimu, ambao alikuwa ameuchochea Mwalimu Nyerere, ulikuwa umedidimia. Niliendelea kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam huku nikishuhudia mwamko wa elimu ukiendelea kudidimia nchini.

Jadi ya kuthamini mali na vitu badala ya elimu iliendelea kushamiri. Wasomi wakipata fursa ya kwenda nje, inayojulikana kama "sabbatical," walitegemea na walitegemewa kutumia fursa hiyo kujitafutia vitu, hasa magari. Mwenye kuleta gari au magari alionekana ndiye msomi bora. Ni tofauti kabisa na hapa Marekani, ambapo profesa unathaminiwa kwa ujuzi wako, hata kama unatembelea baiskeli au unapekua kwa miguu. Binafsi, kwa kuwa kipaumbele changu elimu na taaluma nimeridhika kufundisha hapa Marekani, tangu nilipoanza, mwaka 1991.

Tanzania, ilikuwa ni jambo la kawaida kwa walimu kushughulikia shughuli zao za kujipatia pesa hata kama walipaswa wawe darasani wakifundisha. Jambo hili limekuwa likitajwa na wanafunzi wetu wa ki-Marekani tunaowapeleka kusoma Tanzania, kwani katika vyuo vyao hapa Marekani, profesa hawezi kukosa kuingia darasani bila sababu ya maana kama vile kuumwa. Na akikosa kipindi, hufanya mpango wa kukifidia.

Katika jamii ya wa-Tanzania, nilishuhudia kushamiri utamaduni wa kutafuta vyeti kwa njia yoyote, badala ya kutafuta elimu. Nilishuhudia jinsi watu walivyokuwa tayari kutafuta hata vyeti feki. Hata baadhi ya wale wanaoitwa viongozi wamejipatia hivyo vyeti feki, kutoka  vyuo ambavyo havina hadhi itambulikanayo katika ulimwengu wa taaluma.

Kama ambavyo nimekuwa nikilalamika tena na tena katika blogu hii, utamaduni wa kununua na kusoma vitabu umekosekana katika jamii ya wa-Tanzania. Wazazi, ambao wangetegemewa kuwa wanunuaji wa kuaminika wa vitabu na wawe wanawasomea vitabu watoto wao, kama wafanyavyo wa-Marekani, hawafanyi hivyo.

Hao tunaowaita viongozi Tanzania, na wa-Tanzania wengine wengi, hutembelea nchi za nje. Sijui ni wangapi wanatumia fursa hii kununua vitabu na kurudi navyo Tanzania. Katika miji wanayopita na katika viwanja vya ndege, kuna maduka ya vitabu. Sijui ni wangapi wanapita katika maduka hayo na kununua vitabu. Nimewahi kusafiri mara kwa mara na wa-Tanzania, na nimeona kuwa zawadi wanazonunua ni vitu kama vipodozi, marashi, na mizinga ya vinywaji vikali. Wa-Tanzania hupenda zawadi za aina hiyo. Vitabu je? Jibu mwenyewe.

Sijui ni nyumba zipi katika Tanzania ambazo zina maktaba. Sijui ni nyumba ngapi ambazo zina vitabu angalau 50 au 100, kwa ajili ya watoto na wazazi. Kutegemea kuwa utamwona m-Tanzania amekaa sebuleni, bustanini, ufukweni, ndani ya basi au ndege, anasoma kitabu, ni kama kutegemea kumwona jogoo amevaa suruali.

Niliwahi kuhudhuria tamasha la vitabu Dar es Salaam, mwaka 2004. Watoto walikuwepo, na waalimu, lakini watu wazima walikuwa wachache sana. Hata hao wanaoitwa viongozi, wa ngazi yoyote, hawakuwepo. Watoto walifanya maonesho mbali mbali na waliimba nyimbo. Katika wimbo mmojawapo, waliwasihi wazazi wawe wananunua vitabu na kusoma pamoja na watoto wao majumbani. Wazazi wenyewe hawakuwepo kwenye tamasha. Lakini jioni, nilipokuwa naelekea nyumbani, niliwaona hao watu wazima wamekusanyika kwenye mabaa.

Katika hali hii, tatizo linalohitaji kushughulikiwa ni mwamko wa elimu. Bila mwamko wa elimu, hata lugha ya kufundishia ikibadilishwa mara ngapi, hata tukisema tutumie lugha zetu za ki-Nyaturu, ki-Nyasa, ki-Zaramo, na kadhalika, tusitegemee kuwa tutaleta mapinduzi yatakiwayo. Kinachohitajika ni mwamko wa elimu. Huu ndio msingi, ambao tumeuharibu.

11 comments:

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Kaka Mbele umeongelea jambo muhimu sana hapa. Umenikumbusha miaka ya tisini nilipowatembelea marafiki zangu sehemu mbali mbali jijini na kukuta wamepamba vyombo vya kulia kwenye sebule zao. Walipokuja kwangu walishangaa kukuta nyumba haina lolote la maana zaidi ya seti moja ya runinga na shelves za vitabu tena za mninga kuonyesha ninavyothamini vitabu. Si moja mmoja wa marafiki zangu alikuwa akilalamika kuwa watoto wake hawakupenda kujisomea. Nilimwambia kuwa asipopenda kujisomea anadhani watoto wataiga wapi hiyo tabia? Basi kwa vile watoto wake walikuwa wakiniita uncle na kunizoea, niliamua kuwatembelea na kuwauliza wapi zilikuwa libraries zao. Walishangaa, nilichofanya ni kununua vitabu na kumpa baba yao awapelekee wafungue libraries zao. Na kweli walifanya hivyo na ninapoandika wameishamaliza vyuo wote tena nje ya nchi na wamerejea makwao.
Hii ya kufundishia Kiswahili naona wamenoa. Watapata wapi maprofesa wa fani zote wanaoweza kuzifundisha kwa Kiswahili? Si kujifanya, ukiniamuru nifundishe taaluma yangu kwa Kiswahili umeniua. Hatujawa na vitabu vya kutosha vya kiada vya Kiswahili kuweza kukidhi vyuo, Nadhani wanaoamua huu upuuzi si wana taaluma ya ualimu hata kama wana PhDs.
Kuhusu ukosefu wa motisha, ni dhahiri baada ya jinai kulipa unategemea nini? Imefikia mahali hata wahalifu na hata vyangudoa wanaheshimika kwa vile wana fedha au madaraka. Mara hii mmesahau majambazi wa EPA walivyoishia ikulu na sasa tunalia?

Mbele said...

Ndugu Mhango, shukrani kwa mchango wako. Haya tunayoyasema ni lazima yasemwe. Watu waache kuukwepa ukweli.

Hao tunaowaita viongozi, kwa mfano, hawaonyeshi mfano wowote katika masuala haya ya vitabu. Ni vipofu. Sasa vipofu watawezaje kuwa viongozi?

CCM, chama tawala, ni kinara wa vipofu. Hakuna hata siku moja wameandaa warsha kuhusu fikra za Mwalimu Nyerere, ambamo kungekuwa na mijadala na tathmini ya maandishi yake.

Ningependa kujua ni nani kati ya hao vigogo wa CCM anaweza kukutajia majina ya vitabu vinne tu vya Mwalimu Nyerere. Ataje tu, wala siongelei suala la kuvisoma, maana ukiuliza hilo suali, unaweza kukamatwa kwa madai ya uchochezi.

Nawataja vigogo wa CCM kwa sababu, ingekuwa wanasoma maandishi ya Mwalimu Nyerere, kama vile "Azimio la Arusha" na "Mwongozo," hawangethubutu kukiita chama chao chama cha mapinduzi. Wangethubutu vipi hali chama chenyewe kimejikita katika kuhujumu mapinduzi?

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Kaka Mbele umenichekesha. Hata kweli hawawezi kutaja Ujamaa au Julius Kaisari! Rais Kikwete ataingia kwenye vitabu vya historia kama rais aliyehudhuria misiba mingi kuliko matamasha vyuoni na mashuleni. Ataingia vitabuni kama rais aliyepiga picha na wasanii wengi kuliko wasomi. Anyways, nitaiandikia makala hii.

Mbele said...

Ndugu Mhango, we angalia hata kwenye mikutano mikubwa ya CCM. Wanaleta watumbuizaji wa bongo fleva na taarab. Tangu Mwalimu Nyerere aondoke, hakuna kitabu kimeandikwa na CCM kufafanua malengo yake watu tukasoma kama tunavyosoma maandishi ya Mwalimu Nyerere.

Wakati alipokuwa anajiandaa kung'atuka, Mwalimu Nyerere alizunguka nchini kukagua kile kilichoitwa uhai wa chama.

Inavyoonekana, alishuhudia umbumbumbu ulivyokuwa umekithiri ndani ya CCM, kwani ilifika mahali alisema kuwa wako watu ndani ya CCM ambao hata mtihani juu ya "Azimio la Arusha" hawawezi kupasi.

Hayo situngi mimi. Yalisemwa na Mwalimu Nyerere mwenyewe, tukayasoma katika magazeti.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Kaka Mbele usemayo ni kweli. Kikwete anaingia kwenye historia kama rais aliyewakingia kifua mawaziri waliotuhumiwa kughushi. Hakutaka hata kuwasimamisha kwa muda lau wajitete hata kama utetezi wenyewe hauingii akilini.
CCM imebakikuwa chama cha mabazazi, mafisadi na matwahuti ambacho hakina watu wa kuonyesha dira. Nashangaa hata akina January Makamba wanaojinasibu wamesoma wanatungiwa vitabu utadhani marehemu! Inashangaza kuona nchi inaongozwa na profesa Kikwete kama waramba makalio yake wanavyopenda kumuita lakini inafanya mchezo na elimu. Tuomboleze na tuendelee kutoa maoni yetu hata kama watayadharau lakini wanayasoma. Usiku mwema kaka.

babumbwa said...

Prof. Mbele, ukienda kwenye shule za sekondari za Tanzania ukaangalia ufundishaji na ujifunzaji unaofanyika huko hakika utatoa machozi! kwani hakuna kitabu kinachosomwa huko, walimu na wanafunzi wamejikita kukariri miongozo(marking schemes) ya usahihishaji ya baraza la mitihani! Hata mpango wa "Big Results Now" tuliouiga kwa wenzetu nao unahimiza kukariri majibu ya maswali ya mitihani iliyopita! Maarifa mapya tutayapataje bila kusoma vitabu?

Mbele said...

Ndugu babumbwa, shukrani kwa ujumbe wako. Naona umesema ukweli mtupu. Kwa kuongezea, huwa nafuatilia ziara za wakuu wa CCM, kama vile Abdurahman Kinana, wanavyopita sehemu mbali mbali nchini.

Sijawahi kusikia wametembelea shule, wakajionea hali halisi kama unavyoielezea. Huu kwangu ni ushahidi mwingine wa namna hiki chama tawala kisivyothamini elimu, au jinsi kilivyo usingizini kuhusu suala la elimu, ambalo ni suala la msingi.

Kwa kumalizia, napenda kusisitiza kuwa hii blogu yangu ni ukumbi huru. Inakaribisha hoja zozote.

Anonymous said...

Kwa tathimini ya haraka haraka inaonekana kama kuna mwamko mkubwa sana wa elimu, lakini ukifanya utafiti utagundua kuwa ni mwamko wa kusaka vyeti. Kuna mahali tulikosea(sijui ni wapi?).

Tukumbuke pia mazingira yanachangia sana kuumba tabia na kutokana na kutamalaki wa uzembe, ujinga na uvivu, jamii nzima imekuwa hivyo. Na hivyo ndivyo ilivyo kwa wasomi wa nchii hii. Wasomi wetu wamejikuta ni wasomi baada ya kusaka vyeti.

Wasomi wengi hawasomi vitabu wala hawaandiki. Ni nadra kukuta mwalimu wa chuo ameandika kitu ndani ya mwaka mja. Siku hizi ni kawaida kutumia notsi za mitandao.

Hawana muda wa kutengeneza notsi zao. Yaani kunakatisha tamaa ukiwa mwanafunzi. Ni kama unasoma sekondari. Hakuna changamoto yoyote kusoma chuoni.

Lakini sasa ukisikia takwimu kuhusu elimu ya nchii hii na idadi ya waliomaliza shule na vyuo utadhani kuna mwamko mkubwa sana wa elimu. Kumbe ni vituko tu.
Inasikitisha

Mbele said...

Ndugu Anonymous, shukrani kwa mchango wako. Naona umeimarisha mjadala.

Anonymous said...

Mfumo wa maisha na umaskini vinachangia kwa kiasi kikubwa watu kuthamini vitu kuliko vitabu. Kama mwalimu na msomi au ria yeyote aliye na uwezo na ameajiriwa akiwa hana uhakika wa maisha yake baada ya kustaafu, itamlazimu kujijenga katika vitu ili awe na uhakika wa kujitegemea.

Huu ufisadi uliokithiri unachangiwa kwa kiasi kikubwa na hili.Tumeshuhuda maisha magumu wayoishi wastaafu walio kuwa waadilifu. Nakumbuka mwaka jana nilisoma habari za aliyekuwwa katibu mkuu wizarani akihangaikia mafao yake miaka sasa bila bila. Kama mimi ni mtoto wake nitajifunza nini kutoka kwake?

Ni ulize swali rahisi tu, hivi ukiwa na shs 2000 tu kati ya mkate na kitabu utanunua nini?.

Ni mtazamo tu. Msinishambulie.

Mbele said...

Ndugu Anonymous uliyeandika February 25, 2015 at 6:11 PM, binafsi, kama mmiliki wa blogu hii ya hapakwetu, napenda kwanza kukushukuru kwa dhati kwa mchango wako.

Pili, napenda kukuhakikishia kuwa blogu hii inakaribisha mijadala, na hoja yoyote ni ruksa, tena sio tu ruksa, bali inahitajika, kwani elimu haina mwisho wala haiwezi kuwekewa mipaka.

Mawazo uliyotoa nayaona ni mihimu sana katika kutajirisha mjadala huu. Umesema sawa kabisa kwamba hali ya jaamii yetu ni kipingamizi.

Kutokana hilo, naamini tunatakiwa kuielimisha jamii kuwa ulimwengu wa utandawazi wa leo unahitaji elimu, maarifa, na ujuzi. Kwa hivi, anayewekeza katika vitabu anajijengea fursa nzuri na madhubuti katika dunia hii ya leo na kesho.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...