Monday, February 23, 2015

Mihadhara ya Mankato ni Kesho

Siku zinakwenda kasi. Naona kama ndoto, kwamba safari yangu ya kwenda Chuo cha South Central, mjini Mankato, kutoa mihadhara ni kesho asubuhi.

Ninangojea kwa hamu kutekeleza majukumu yaliyoko mbele yangu, ambayo ni kwanza kuongea na wanafunzi wanaojiandaa kwa safari ya Afrika Kusini kimasomo, na pili ni kutoa mhadhara kwa jumuia ya chuo ambao mada yake itakuwa "Writing About Americans."

Maongezi yote hayo yatahusu masuala ya tofauti za tamaduni na athari zake ulimwenguni. Wanafunzi wanaokwenda Afrika Kusini wanajiandaa kuishi na kushughulika na wa-Afrika, katika utamaduni ambao ni tofauti na ule wa Marekani. Utaratibu huu wa maandalizi, ambao umeshakuwa jambo la kawaida hapa Marekani, ingekuwa bora ufuatwe na wengine, kama nilivyowahi kuwaasa wa-Tanzania wenzangu.

Katika maandalizi hayo, hao wanafunzi wanasoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kitabu ambacho, japo kidogo, kinawagusa watu, tangu nilipokichapisha, tarehe 5 Februari, 2005. Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kukiandika kama nilivyoandika, hadi kimekuwa msingi wa mialiko ya kwenda kuongelea yaliyomo na yatokanayo.

Katika mhadhara wa "Writing About Americans," ninapangia kuelezea mchakato wa kuandika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kuanzia chimbuko la wazo la kukiandika, mchakato wa kukiandika, mambo muhimu niliyojifunza katika kuandika huku, hadi jinsi kitabu kilivyopokelewa na jamii, hasa wa-Marekani, ambao ndio wanaoongoza katika usomaji wake.

Jambo moja kubwa nililojifunza katika kutafakari na kuandika ni kuheshimu tamaduni, pamoja na tofauti zake. Shaaban Robert angeishi miaka mingi zaidi ya ile aliyoishi, angetufundisha mengi kuhusu suala hilo.

Panapo majaliwa, nikikamilisha ziara ya kesho, nitaandika taarifa katika hii blogu yangu.

No comments: