Sunday, February 15, 2015

Hadithi za Wa-Matengo Chuoni Montana

Leo nimepata ujumbe wa barua pepe kutoka kwa mwalimu mmoja wa Chuo Kikuu cha Montana.Ananiambia kuwa muhula huu anafundisha kozi ya Mythologies, na kati ya nyenzo anazotumia ni kitabu changu cha Matengo Folktales. Ananiulizia kama nitaweza kuongea na wanafunzi wake kwani itawafaidia sana kuweza kuongea na mtafiti aliyeandaa kitabu, akatoa maelezo kuhusu mambo kadha wa kadha, kama vile mchakato wa utafiti. Amependekeza kuwa ikiwezekana, tupange siku waweze kuongea nami kwa njia ya Skype.

Nimemjibu kuwa niko tayari kutoa mchango wangu, na kuwa ninafurahi kusikia kuwa anafundisha masimulizi ya wa-Matengo, sambamba na yale ya wa-Griki wa kale na wengine. Ingawa binti yangu Zawadi alishanionyesha namna ya kutumia Skype na akanisajili, sijawahi kutumia tekinolojia hii. Wengi wa rika langu au wale wanaotuzidi umri, tumezoea mambo ya zamani. Lakini dunia inavyobadilika, hasa tekinolojia, tunalazimika kukiri mazoea yana taabu.

Ujumbe niliopata leo umenifanya niwazie mambo kadhaa. Kwanza, ni kwamba nilifanya utafiti na kuandaa kitabu hiki kwa miaka yapata 23. Wakati nachapisha kitabu hiki, nilikuwa tayari ninafundisha huku Marekani, baada ya kufundisha Chuo Kukuu Cha Dar es Salaam. Nilikuwa na hamu kuwa kitabu kiwe mchango wangu kwa elimu Tanzania, kwa ufundishaji wa chuo kikuu, kwani hapakuwa na kitabu cha aina ile nchini, kilichofaa kufundishia somo hili la hadithi za mapokeo ("folktales"). Nilijua hayo, kwa vile mimi ndiye nilikuwa mhadhiri wa somo la fasihi simulizi, sambamba na somo la nadharia ya fasihi.

Kilichotokea ni kuwa kitabu hiki kinatumika au kimetumika katika vyuo vikuu vya Marekani. Vyuo ninavyovifahamu ni Wichita State University, University of California San Diego, St. Olaf College, Colorado College, na College of St. Benedict/St. John's University. Niliwahi kualikwa na hicho chuo cha St. Benedict/St. John's kutoa mhadhara katika darasa la "fairy tales," ambalo lilikuwa linasoma kitabu cha Matengo Folktales, kama nilivyoripoti katika blogu yangu, na nilitoa pia mhadhara kwa jumuia ya chuo kuhusu kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Hayo ni baadhi ya mawazo yaliyomo akilini mwangu, wakati huu ninapofikiria ujumbe niliopata leo. Ingawa kwa upande mmoja ninafurahi, sijawahi kuridhika na hali hii ya vitabu vyangu kuwa vinawafaidia wa-Marekani, lakini sio wa-Tanzania. Hata hivi, kosa si langu. Mimi natimiza wajibu wangu wa kufanya utafiti, kuandika, na kuchapisha maandishi. Baada ya hapo, mwenye macho haambiwi tazama.

4 comments:

Anonymous said...

Prof Mbele. Pole na kazi za kila siku.
Ningependa kujua nini maoni yako kuhusu kutumia kiswahili kama lugha kuu ya kufundishia mpaka chuo kikuu. Je unalionaje hili, unaona kutakuwa na athari zozote kutokana na elimu?. Je ni kweli tutakuwa tumejitenga na dunia?.

Ningeomba kama ungepata nafasi basi ukaliandika hili kama post katika blog na wala si comment. Nakutakia siku njema

Mbele said...

Ndugu Anonymous, shukrani sana kwa ujumbe wako. Kwa heshima na taadhima, nitaandika maoni yangu katika blogu hii, kama unavyoelekeza, pamoja na kuelewa kwangu kuwa mawazo yangu sio bora kuliko ya wengine. Insh'Allah, nitafanya hivyo wiki hii hii.

Yasinta Ngonyani said...

Ni kitabu chenye mafunzo mengi ninacho hapa nyumbani na nimekisoma . Hongera kwa hilo.

Mbele said...

Dada Yasinta, shukrani kwa ujumbe wako. Nilijua kuwa unacho kitabu hiki, na kwamba unakipenda, kama ulivyowaeleza walimwengu katika blogu ya "Jielewe."

Kama nilivyogusia katika makala yangu, nilikiaandaa kitabu hiki kwa miaka mingi, miaka yapata 23, ili kuhakikisha kuwa kinafaa kufundishia hadi kiwango cha chuo kikuu. Nami nikiwa ni mhadhiri wa somo hili pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nilijua ninachofanya.

Insha za maelezo nilizoweka baada ya kila hadithi, na insha niliyoweka mwishoni kujumlisha mambo muhimu ya fani hii ya hadithi za mapokeo, ni changamoto kwa taaluma sio tu kwa hadithi ya ki-Matengo, bali kwa hadithi za Afrika na ulimwengu.

Hii ndio maana kimeingia katika madarasa ya maprofesa kadhaa hapa Marekani wanaofundisha masomo kama "folklore," "fairy tales," au "mythology."

Lakini kinafaa kwa yeyote anayetaka kujua au kutafakari maana na umuhimu wa hizi hadithi za mapokeo, ambazo mara nyingi watu hawaelewi kuwa zina masuala mengi na falsafa.

Miaka 23 ya kutafiti, kutafakari na kuandika, hasa kutafakari, sio michache. Ingekuwa ni kulipwa, kwa kazi yote niliyofanya, na taabu niliyopata, ningekuwa tajiri sana.

Lakini, kwa kuandika kitabu cha aina hii, lengo lako haliwezi kuwa hela bali kuchangia elimu, na hizo pesa unazoweza kupata hazitoshi hata kugharamia utafiti, tafakari na uandishi niliofanya. Lengo ni kuchangia elimu, na ndio furaha yangu.

Ninapangia kuendelea na utafiti wa hadithi za wa-Matengo, kwa sababu lugha ninaifahamu na utamaduni wake. Hilo ni jambo muhimu sana. Nikipata hela na likizo ya utafiti, nitaenda kuendeleza utafiti huo.

Wakati nangojea fursa hiyo, ninaendelea na kufundisha na kutafakari. Kwa mfano, zao moja la tafakari niliyofanya miaka ya karibuni ni makala hii hapa.