Monday, November 27, 2017

Kitabu "Matengo Folktales" Chatajwa Katika "Jeopardy."

Tarehe 23 Novemba, 2017, nitaikumbuka daima. Kwanza, ilikuwa ni sikukuu ya "Thanksgiving" ambayo ni maarufu hapa Marekani.

Jambo la pili liliofanya targhe 23 iwe muhimu kwangu ni kuwa jioni ya siku hiyo, katika kipindi maarufu cha televisheni kiitwacho "Jeopardy," kitabu changu kiitwacho Matengo Folktales kilitajwa. "Jeopardy" ni mchezo kama chemsha bongo. Watu hushindana kujibu masuali ambayo mwendesha kipindi huwauliza, na wanapotoa jibu sahihi hupata fedha. Suali lililoulizwa lilikuwa kuhusu mhusika katika hadithi.
Nilikifahamu kipindi hiki kijuujuu. Lakini baada ya kitabu kutajwa, nimeona wa-Marekani wanaonifahamu wanavyosisimka na kunipongeza. Hata hapa chuoni St. Olaf habari imezagaa hadi kwa wakuu wa chuo. Mkuu wa idara yangu ya ki-Ingereza ameandika ujumbe kwetu waalimu na wanafunzi: Congratulations to Joseph Mbele for an honor that few of us will ever achieve--being mentioned in a clue on Jeopardy! See the image below, referencing Joseph's "Matengo Folktales" book....

Sasa zimepita siku tatu na bado watu wanaendelea kusimulia tukio hili. Ninaendelea kupata taarifa kutoka sehemu mbali mbali za Marekani. Hata hivi, sielewi ni nani aliyepeleka taarifa za kitabu changu kwenye kituo cha "Jeopardy." Unaweza kusikiliza katika video ya YouTube hapa chini. Ukisogeza video ukifikishe kwenye dakika 15:29 ndipo utasikia jina langu na jina la kitabu.

Wednesday, November 22, 2017

Tamasha la Waandishi Minneapolis Lilifana

Tarehe 18 Novemba, tamasha la waandishi, Minnesota Black Authors Expo, lilifanyika mjini Minneapolis, jimboni Minnesota. Walishiriki waandishi 40 wa vitabu, nami nikiwemo. Waandaaji wa tamasha, De'Vonne Pittman na Jasmine Boudah walifanya kazi kubwa kwa miezi minne hadi kufanikisha tamasha hili la aina yake.

Picha hiyo hapa kushoto ni ya jalada la kijitabu walichoandaa chenye taarifa za tamasha, zikiwemo taarifa za waandishi na vitabu vyao. Nimehudhuria matamasha mengi ya vitabu, lakini hii ilikuwa ni mara ya kwanza kuona kimeandaliwa kijitabu cha aina hiyo. Ni jambo zuri sana, kwani mtu unakuwa na fursa ya kufuatilia taarifa ambazo hungeweza kuzipata kikamilifu katika tamasha, kwa sababu ya uwingi wa waandishi.




Hapa pichani anaonekana De'Vonne Pittman akiongea, na pembeni yake anaonekana Jasmine Boudah. Walitugusa kwa uchangamfu na ukarimu wao kipindi chote cha maandalizi ya tamasha na wakati wote wa tamasha ambalo lilidumu kuanzia saa tano asubuhi hadi saa kumi na moja jioni.









Jasmine Boudah naye anaongea.
















Waandishi tulikuwa tumeombwa kuwa tayari ukumbini kabla ya saa nne na nusu. Nilipofika, yapata saa nne na dakika kumi, nilikuta wengi wako tayari.











Wadau nao walianza kuja. Anwani ya ukumbi lilipofanyika tamasha ni 1007 Broadway Avenue West, ambayo ni eneo la kaskazini katika mji wa Minneapolis. Ni eneo linalokaliwa na wa-Marekani Weusi wengi.



Ukisikiliza propaganda za Marekani, utaamini kwamba wa-Marekani Weusi si watu makini katika mambo ya kutafuta elimu. Lakini ukweli ambao hausemwi sana ni kuwa kuna uhaba wa fursa kutokana na mfumo wa kihistoria wa kibaguzi.

Nilivyoshuhuda katika tamasha hili jinsi hao wa-Marekani Weusi wa kila rika, wanaume na wanawake, walivyokuja kwa wingi na ari ya kupata taarifa juu ya vitabu, kuongea na waandishi, na kununua vitabu, nilijiridhisha kuwa propaganda ni tofauti na hali halisi.

Hapa kushoto ninaonekana kwenye meza yangu. Nilipata fursa ya kuongea kwa kina na watu mbali mbali kuhusu vitabu na kazi zangu.

















Hapa kushoto niko na De'Vonna Pittman, mwandaaji wa tamasha. Alikuwa amefika kwenye meza yangu akaniambia kuwa anataka kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Kauli yake ilinipa hisia kuwa alikuwa amenuia tangu kabla kujipatia kitabu hicho.













Huyu mama ni mmoja kati ya wale ambao tuliongea sana. Alitaka kujua kuhusu vitabu vyangu vyote, kisha akanunua hiki alichoshika, Matengo Folktales. Bahati mbaya sikuandika kumbukumbu ya jina lake.














Ingawa nilikuwa kwenye meza yangu karibu muda wote, sawa na waandishi wengine, nilipata pia fursa ya kufahaminana na baadhi ya waandishi. Hapa kushoto, ninaonekana nikiwa na Cavis Adams, ambaye ameshika nakala ya riwaya yake ya kwanza, ambayo aliileta kwenye tamasha, na mimi nimeshika vitabu vyangu.












Hapa kushoto ninaonekana nikiongea na Penny Jones, ambaye meza yake ilikuwa pembeni ya meza yangu, zikiwa zimegusana. Shughuli yake ni kuwapa watu ushauri na elimu juu ya kujiamini katika kukabiliana na masuala ya maisha. Tuliongea sana, tukaona jinsi mawazo yetu yanavyofanana au kukaribiana, kwani sote tunashughulika na masuala ya saikolojia. Nilinunua kitabu chake, Thirty Days of Motivation, A guide to Reaching Your Goals and Staying Focused, naye akanunua kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nitategemea tutaendelea kuwasiliana.









Hapa kushoto ninaonekana na Rita Apaloo, mwenye asili ya Liberia, mwandishi wa kitabu nilichoshika, African Women Connect. Huyu ni mmoja wa wadau na wapiga debe wa vitabu vyangu, hasa Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.
 Binti yangu Zawadi amekuwa akiandamana nami kwenye matamasha na mihadhara yangu tangu alipokuwa mdogo. Anafahamu shughuli zangu, na anaweza kuwaelezea watu hata akiwa peke yake kwenye tamasha.















Hapa kushoto tuko na dada ambaye binti yangu Zawadi alimwona katika umati akamleta kwenye meza yangu kututambulisha. Kumbe anafahamiana na Assumpta, dada mkubwa wa Zawadi. Ni maarufu katika kuandaa shughuli na matukio ya kuwakutanisha watu.

Taarifa yangu ni kielelezo na kumbukumbu ndogo tu ya tamasha ambalo lilifana sana. Waandaaji wanastahili shukrani tele. Wameshatangaza kuwa wanajipanga kuandaa tamasha la mwaka ujao. Nawatakia kila la heri.

Friday, November 17, 2017

Tamasha la Vitabu Minneapolis, 18 Novemba

Kesho nitahudhuria tamasha na vitabu liitwalo Minnesota Black Author's Expo mjini Minneapolis. Waandishi yaapata 40 watashiriki. Nami nitapeleka vitabu vyangu.

Itakuwa ni siku yenye shughuli nyingi za kukutana na wasomaji wa vitabu na kuongelea vitabu na uandishi. Kila mwandishi atapata fursa ya kutoa hotuba fupi kwa wahudhuriaji.

Pia kutakuwa na warsha juu ya uandishi, kwa yeyote atakayependa kujifunza.

Hili ni tamasha la kwanza la aina yake, na limeleta msisimko mkubwa katika jimbo hili la Minnesota. Lilibuniwa na kuandaliwa na waandishi Jasmine Boudah, Tovias Bridgewater Sly, na De'Vonna Pittman.


Monday, November 13, 2017

Mwongozo wa Riwaya ya "Things Fall Apart"

Mimi mwalimu wa fasihi ya ki-Ingereza. Kati ya mambo ninayofanya ni kuandika miongozo ya fasihi. Nimeshaandika miongozo kadhaa, ikiwemo mwongozo wa Things Fall Apart, riwaya ya Chinua Achebe.

Nimeridhika kuwa mwongozo huu una mawazo muhimu ya kumwezesha mwalimu, mwanafunzi, na msomaji yeyote kuelewa mambo mapya juu ya Things Fall Apart na pia juu ya nadharia ya fasihi. Leo nimezipitia kurasa kadhaa, nikafurahia niliyoandika juu ya mhusika aitwaye Unoka.

Suali ni je, mwongozo huu unawafikia wanafunzi wa waalimu wa Tanzania? Ni wazi kuwa ningependa wafaidike nao, kama wanavyofaidika wanafunzi na wengine nje ya Tanzania, kama vile hapa Marekani. Ningekuwa na uwezo, ningepeleka nakala katika shule na vyuo vyote.

Kwa bahati nzuri, kitabu kinapatikana mtandaoni kama kitabu pepe. Ninafahamu kuwa kuna watu Tanzania ambao wanaweza kuagiza vitabu vya aina hiyo. Ninaamini kuwa kadiri siku zinavyokwenda na tekinolojia kuenea, wengi zaidi watakuwa na uwezo huo. Kwa hivi, nina matumaini makubwa kwa siku za usoni.

Njia nyingine ni kusafirisha vitabu. Mimi mwenyewe, kila ninapokwenda Tanzania, huchukua vitabu na kuvigawa kwenye maktaba na vyuo. Kuna wa-Tanzania wengi huku nje, ambao nao huenda Tanzania. Kama kungekuwa na nia ya kuchangia elimu, ingekuwa rahisi wao pia kuchukua vitabu. Vitu vingine wanachukua, kwa nini washindwe kuchukua vitabu?

Sunday, November 5, 2017

Hadithi Zetu za Jadi

Hadithi zetu za jadi ni hazina kubwa ya utamaduni wetu. Kila kabila lilikuwa na hadithi nyingi, pamoja na aina nyingine za fasihi simulizi, kama vile nyimbo, na methali. Hadithi zina tafakari juu ya maisha na tabia za binadamu ingawa mara nyingi wahusika wana taswira za wanyama, ndege au viumbe vingine. Zinaelezea masuala ya familia, malezi ya watoto, wajibu wa wazazi na watoto. Zinatoa tahadhari kuhusu tabia mbaya na maelekezo juu tabia njema. Zinafundisha huruma, maelewano, ushiriano na kusaidiana.

Hadith zinaelezea mahangaiko, mategemeo, mafanikio, ubora na udhaifu wa binadamu, Kuna hadithi za kusisimua hisia na fikra, zenye kuibua masuali kuhusu maana ya maisha, kama walivyoibua wanafalsafa wa mkondo uitwao "existentialism," kama nilivyogusia katika kitabu cha Matengo Folktales.

Kitabu hiki ni mkusanyo wa hadithi kumi za ki-Matengo, ambazo nilizitafsiri kwa ki-Ingereza. Niliandika uchambuzi wa kila hadithi na nikaandika pia insha ya jumla kuhusu hadithi, ili kuwapa wasomaji kianzio cha kuzichambua.

Nilipokuwa ninaandaa kitabu hiki, nilikuwa mhadhiri katika Chuo kikuu cha Dar es Salaam. Somo mojawapo nililokuwa ninafundisha ni "Oral Literature" (fasihi simulizi). Hapakuwa na kitabu cha kufaa kufundishia somo hilo kwa wanafunzi wa chuo kikuu. Hapakuwa na kitabu cha kufundishia hadithi za jadi, kama nilivyoelezea katika blogu hii.

Kwa hivyo, lengo langu lilikuwa ni kuziba pengo, kwa kuandika kitabu ambacho nilitaka kiwepo. Hii ni falsafa ambayo imekaa kichwani mwangu: kama hakuna kitabu ambacho ungetaka kiwepo, andika hicho kitabu. Au kama kitabu unachosoma hakikuridhishi, andika hicho ambacho kitakuridhisha.

Ingawa kitabu changu si kikamilifu, angalau kinakidhi mahitaji yangu ya kufundisha somo la hadith i za jadi kwa wanafunzi wa chuo kikuu. Ni faraja kwangu kuwa si mimi peke yangu mwenye wazo hilo. Kuna wengine ambao wanakitumia kama ilivyokuwa katika chuo kikuu cha Montana na chuo cha St. Benedict/St. John's.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...