Showing posts with label nadharia ya fasihi. Show all posts
Showing posts with label nadharia ya fasihi. Show all posts

Monday, November 13, 2017

Mwongozo wa Riwaya ya "Things Fall Apart"

Mimi mwalimu wa fasihi ya ki-Ingereza. Kati ya mambo ninayofanya ni kuandika miongozo ya fasihi. Nimeshaandika miongozo kadhaa, ikiwemo mwongozo wa Things Fall Apart, riwaya ya Chinua Achebe.

Nimeridhika kuwa mwongozo huu una mawazo muhimu ya kumwezesha mwalimu, mwanafunzi, na msomaji yeyote kuelewa mambo mapya juu ya Things Fall Apart na pia juu ya nadharia ya fasihi. Leo nimezipitia kurasa kadhaa, nikafurahia niliyoandika juu ya mhusika aitwaye Unoka.

Suali ni je, mwongozo huu unawafikia wanafunzi wa waalimu wa Tanzania? Ni wazi kuwa ningependa wafaidike nao, kama wanavyofaidika wanafunzi na wengine nje ya Tanzania, kama vile hapa Marekani. Ningekuwa na uwezo, ningepeleka nakala katika shule na vyuo vyote.

Kwa bahati nzuri, kitabu kinapatikana mtandaoni kama kitabu pepe. Ninafahamu kuwa kuna watu Tanzania ambao wanaweza kuagiza vitabu vya aina hiyo. Ninaamini kuwa kadiri siku zinavyokwenda na tekinolojia kuenea, wengi zaidi watakuwa na uwezo huo. Kwa hivi, nina matumaini makubwa kwa siku za usoni.

Njia nyingine ni kusafirisha vitabu. Mimi mwenyewe, kila ninapokwenda Tanzania, huchukua vitabu na kuvigawa kwenye maktaba na vyuo. Kuna wa-Tanzania wengi huku nje, ambao nao huenda Tanzania. Kama kungekuwa na nia ya kuchangia elimu, ingekuwa rahisi wao pia kuchukua vitabu. Vitu vingine wanachukua, kwa nini washindwe kuchukua vitabu?

Tuesday, May 30, 2017

Likizo Inaanza: Ni Kujisomea Vitabu na Kuandika

Tumemaliza muhula wa mwisho wa mwaka wa masomo hapa chuoni St. Olaf. Tunamalizia kusahihisha mitihani na matokeo yatakuwa yamekamilika tarehe 5 Juni. Kuanzia pale tutakuwa na miezi mitatu ya likizo. Lakini kwetu waalimu, likizo si likizo, bali fursa ya kujisomea, kufanya utafiti, na kuandika, bila kuhusika na ufundishaji darasani.

Mpango wangu kwa likizo hii ni kutumia wiki sita za mwanzo katika kujisomea vitabu na kuandika, halafu wiki sita zitakazofuata nitafundisha kozi ya fasihi ya Afrika. Kufundisha kipindi hiki cha likizo ni jambo la hiari. Mwalimu anatangaza kozi anayotaka kufundisha na wanafunzi wanaohitaji wanajisajili. Wanafunzi huwa wachache. Ni fursa nzuri kwa mwalimu kujaribisha mambo mapya.

Wakati huu ninavyoandika ujumbe huu, ninafadhaika katika kuamua nisome vitabu vipi. Maktaba yangu ina vitabu vingi ambavyo sijavisoma. Kwa likizo hii, nimewazia nisome tamthilia za William Shakespeare, au George Bernard Shaw, au Sean O'Casey, au Anton Chekhov, au riwaya za Orhan Pamuk ili niweze kupata mwanga juu ya huyu mwandishi maarufu aliyejipatia tuzo ya Nobel mwaka 2006 na ambaye nimekuwa nikimtaja katika blogu hii. Nimewazia pia kusoma hadithi fupi na riwaya za Ernest Hemingway, zile ambazo sijazisoma.

Ningependa kuonja uandishi wa Svetlana Alexievich, ambaye nimemgundua wiki iliyopita. Nilijipatia kitabu chake, Secondhand Time: The Last of the Soviets, cha bure, hapa chuoni. Sikuwa ninamfahamu mwandishi huyu mwanamke m-Rusi, ambaye alipata tuzo ya Nobel mwaka 2015, "for her polyphonic writings, a monument to suffering and courage in our time," kwa mujibu wa kamati ya tuzo.

Wafuatiliaji wa nadharia ya fasihi wanafahamu kuwa dhana ya "polyphony" katika fasihi ilifafanuliwa vizuri na mwanafalsafa na mhakiki m-Rusi Mikhail Bakhtin akimaanisha sauti na mitazamo mbali mbali inayounda kazi ya fasihi. Nimefurahi kumfahamu mwandishi huyu mwanamke kutoka u-Rusi. Amenifanya nimkumbuke mwandishi mwanamke m-Rusi, Anna Akhmatova, mshairi maarufu. Nina dukuduku ya kujua kama waandishi hao wawili wanaweza kulinganishwa.

Hakuna kazi ya fasihi inayozuka katika ombwe. Inatokana na jadi fulani na mfumo mpana wa kazi za fasihi, na kazi yoyote mpya inachangia jadi na mfumo wa fasihi. Dhana hiyo ilielezwa vizuri na T.S. Eliot, mshairi na mwanafasihi maarufu, katika insha yake, "Tradition and the Individual Talent."

Ninapowazia waandishi wa fasihi wanawake waliopata tuzo ya Nobel, majina yanayonijia akilini hima ni Sigrid Undset wa Norway, Nadine Gordimer wa Afrika Kusini, Toni Morrison wa Marekani, Alice Munro wa Canada, na Doris Lessing wa Zimbabwe na Uingereza. Ninashawishika na wazo la kutunga na kufundisha kozi juu ya maandishi ya wanawake waliopata tuzo ya Nobel katika fasihi.

Papo hapo, katika likizo hii ninataka kuendelea kuandika makala ambayo nilianza kuiandika miezi kadhaa iliyopita, "Folkloric Discourse in Ama Ata Aidoo's The Dilemma of a Ghost." Azma ya kuendelea kuandika makala hii ni kubwa, kwani ninaamini kuwa hii itakuwa makala bora kabisa.

Hizi ndizo ndoto zangu. Ni ajenda kubwa, kielelezo cha namna akili yangu inavyohangaika kutokana na kutambua kuwa vitu vy kusoma na kuandika ni vingi kuliko muda unavyoruhusu. Sitaweza kufanya yote ninayowazia kwa likizo hii, lakini si neno. Nitatumia muda wangu vizuri na kufanya nitakachoweza.

Monday, June 8, 2015

Nimerekebisha Kitabu Changu

Kwa zaidi ya wiki moja, nimekuwa nikikipitia kitabu changu cha Matengo Folktales kwa ajili ya kukiboresha. Rekebisho moja nililofanya ni kuongeza ukubwa wa herufi ili kitabu kisomeke kwa urahisi zaidi. Nilikuwa pia naangalia kama kuna kosa lolote katika uandishi wa maneno. Nimerekebisha dosari zilizoziona katika maneno yapata matano

Ingawa nimetumia masaa mengi katika shughuli hiyo, kwangu si kitu, nikifananisha na kazi niliyofanya kwa miaka yapata ishirini na tatu katika kukiandaa kitabu hiki, tangu kuzitafuta na kuzirekodi hadithi, kuziandika kwa kuzitafsiri kwa ki-Swahili, kuzitafsiri kwa ki-Ingereza, kuzichambua, kusoma nadharia mbali mbali ili kutajirisha uchambuzi, na kurekebisha tafsiri na uchambuzi tena na tena.

Bahati ni kwamba miaka ya sabini na kitu, nilianza pia kufundisha somo la fasihi simulizi ("Oral Literature") na nadharia ya fasihi (Theory of Literature") katika idara ya "Literature" ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Katika kufundisha nilijionea mwenyewe kuwa hapakuwa na kitabu nilichoona kinafaa kwa somo la fasihi simulizi kwa wanafunzi wa kiwango cha chuo kikuu. Kuna usemi kuwa kama kitabu unachosoma huridhiki nacho, andika hicho kitabu unachokitaka.

Hali hiyo ya kukosekana kitabu kilichofaa katika ufundishaji wangu ilinihamasisha kutafakari masuala niliyokuwa nakumbaba nayo katika kuandika kitabu changu. Nilipania kuwa kiwe kinafaa kwa kufundishia. Miaka ilipita, nami nikawa natafiti, natafakari, na kuandika kiasi nilivyoweza. Wakati huo huo, nilikuwa nahangaika kuziboresha tafsiri za hadithi katika muswada. Shughuli hii ilinifundisha mengi kuhusu tafsiri, kama nilivyogusia katika makala iliyochapishwa katika jarida la Metamorphoses.

Historia ya kitabu hiki ni ndefu, na labda nitaweza kuiandika kiasi fulani siku za usoni. Ninakumbuka, kwa mfano, kwamba nilipokuwa nasomea masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Wisconsin, 1980-86, nilichukua somo la nadharia ya fasihi katika idara ya "Comparative Literature" lililofundishwa na Professor Keith Cohen. Kati ya nadharia tulizojifunza ni "Structuralism." Professor Cohen alitupa "homework" ya kuchambua hadithi yoyote kwa kutumia nadharia ya "Structuralism."

Nilitumia fursa hii kuichambua hadithi ya "The Tale of Two Women," ambayo imo katika Matengo Folktales. Mtu anayefahamu angalau kidogo nadharia ya "Structuralism" ataona athari zake, japo kidogo,  katika uchambuzi wangu.

Baada ya harakati za aina aina kwa miaka mingi, nilichapisha kitabu hiki mwaka 1999. Ndoto yangu ya kuandika kitabu cha kutumiwa katika ufundishaji wangu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam haikutimia nilivyotarajia. Niliondoka Tanzania mwaka 1991, nikaja kufundisha katika idara ya ki-Ingereza Chuoni St. Olaf, huku  nikiwa bado naufanyia kazi mswada wangu. Kwa hivi kitabu kilichapishwa huku Marekani, na wanaokisoma ni wa-Marekani, kuanzia katika jamii hadi vyuoni, kama nilivyoelezea hapa na  hapa.

Masimulizi ni mengi, na kama nilivyogusia, labda nitafute wasaa miaka ijayo niandike kumbukumbu zangu za historia ya kitabu hiki.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...