Tuesday, May 30, 2017

Likizo Inaanza: Ni Kujisomea Vitabu na Kuandika

Tumemaliza muhula wa mwisho wa mwaka wa masomo hapa chuoni St. Olaf. Tunamalizia kusahihisha mitihani na matokeo yatakuwa yamekamilika tarehe 5 Juni. Kuanzia pale tutakuwa na miezi mitatu ya likizo. Lakini kwetu waalimu, likizo si likizo, bali fursa ya kujisomea, kufanya utafiti, na kuandika, bila kuhusika na ufundishaji darasani.

Mpango wangu kwa likizo hii ni kutumia wiki sita za mwanzo katika kujisomea vitabu na kuandika, halafu wiki sita zitakazofuata nitafundisha kozi ya fasihi ya Afrika. Kufundisha kipindi hiki cha likizo ni jambo la hiari. Mwalimu anatangaza kozi anayotaka kufundisha na wanafunzi wanaohitaji wanajisajili. Wanafunzi huwa wachache. Ni fursa nzuri kwa mwalimu kujaribisha mambo mapya.

Wakati huu ninavyoandika ujumbe huu, ninafadhaika katika kuamua nisome vitabu vipi. Maktaba yangu ina vitabu vingi ambavyo sijavisoma. Kwa likizo hii, nimewazia nisome tamthilia za William Shakespeare, au George Bernard Shaw, au Sean O'Casey, au Anton Chekhov, au riwaya za Orhan Pamuk ili niweze kupata mwanga juu ya huyu mwandishi maarufu aliyejipatia tuzo ya Nobel mwaka 2006 na ambaye nimekuwa nikimtaja katika blogu hii. Nimewazia pia kusoma hadithi fupi na riwaya za Ernest Hemingway, zile ambazo sijazisoma.

Ningependa kuonja uandishi wa Svetlana Alexievich, ambaye nimemgundua wiki iliyopita. Nilijipatia kitabu chake, Secondhand Time: The Last of the Soviets, cha bure, hapa chuoni. Sikuwa ninamfahamu mwandishi huyu mwanamke m-Rusi, ambaye alipata tuzo ya Nobel mwaka 2015, "for her polyphonic writings, a monument to suffering and courage in our time," kwa mujibu wa kamati ya tuzo.

Wafuatiliaji wa nadharia ya fasihi wanafahamu kuwa dhana ya "polyphony" katika fasihi ilifafanuliwa vizuri na mwanafalsafa na mhakiki m-Rusi Mikhail Bakhtin akimaanisha sauti na mitazamo mbali mbali inayounda kazi ya fasihi. Nimefurahi kumfahamu mwandishi huyu mwanamke kutoka u-Rusi. Amenifanya nimkumbuke mwandishi mwanamke m-Rusi, Anna Akhmatova, mshairi maarufu. Nina dukuduku ya kujua kama waandishi hao wawili wanaweza kulinganishwa.

Hakuna kazi ya fasihi inayozuka katika ombwe. Inatokana na jadi fulani na mfumo mpana wa kazi za fasihi, na kazi yoyote mpya inachangia jadi na mfumo wa fasihi. Dhana hiyo ilielezwa vizuri na T.S. Eliot, mshairi na mwanafasihi maarufu, katika insha yake, "Tradition and the Individual Talent."

Ninapowazia waandishi wa fasihi wanawake waliopata tuzo ya Nobel, majina yanayonijia akilini hima ni Sigrid Undset wa Norway, Nadine Gordimer wa Afrika Kusini, Toni Morrison wa Marekani, Alice Munro wa Canada, na Doris Lessing wa Zimbabwe na Uingereza. Ninashawishika na wazo la kutunga na kufundisha kozi juu ya maandishi ya wanawake waliopata tuzo ya Nobel katika fasihi.

Papo hapo, katika likizo hii ninataka kuendelea kuandika makala ambayo nilianza kuiandika miezi kadhaa iliyopita, "Folkloric Discourse in Ama Ata Aidoo's The Dilemma of a Ghost." Azma ya kuendelea kuandika makala hii ni kubwa, kwani ninaamini kuwa hii itakuwa makala bora kabisa.

Hizi ndizo ndoto zangu. Ni ajenda kubwa, kielelezo cha namna akili yangu inavyohangaika kutokana na kutambua kuwa vitu vy kusoma na kuandika ni vingi kuliko muda unavyoruhusu. Sitaweza kufanya yote ninayowazia kwa likizo hii, lakini si neno. Nitatumia muda wangu vizuri na kufanya nitakachoweza.

6 comments:

mwanammuni said...

Natumaini u mzima!
Kama nilivyojieleza kabla ya kwamba napita pita maeneo haya. Mimi nakuunga mkono katika maombi yako ya kutaka kufanikisha Yale uliyojiandalia kuyafanya ktk likizo yako. Likizo njema

Mbele said...

Shukrani, mwanammuni, kwa ujumbe wako. Nilivyoona tu jina lako, nimekumbuka kuwa ulishawahi kuandika jambo hapa ukumbini pangu. Nakushukuru kwa kunitembelea. Ninakuhesabu kama jirani mwema. Nashukuru kwa kunitakia mafanikio katika maazimio yangu, nawe nakutakia kila la heri.

Francis Daudi said...

Hongera sana kwa kuwa na mpango mzuri kabisa wakati huu wa likizo, nami ninaisubiri likizo yangu mwezi ujao(Julai) niweze kupata nafasi ya kusafiri na kusoma pia vitabu vyangu nilivyojipangia. Nategemea pia kumalizia mswaada wangu wa kitabu WANAWAKE MASHUHURI KATIKA HISTORIA YA TANZANIA. Lengo likiwa ni kuweka mchango wa wanawake katika kurasa za historia, usisahauliwe hata kwa vizazi vijavyo. Nitahitaji sana usaidizi wako Profesa wangu.

Mbele said...

Ndugu Daudi Francis, shukrani kwa ujumbe wako. Hongera kwa kujiwekea malengo hayo murua. Kuhusu mada ya kitabu chako juu ya wanawake mashuhuri katika historia ya Tanzania unanikumbusha utafiti wa Profesa Susan Geiger (marehemu sasa) ambaye alikuwa anafundisha katika Chuo Kikuu cha Minnesota. Alihitimu shahada ya uzamifu (Ph.D.) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1973, katika somo la historia ya Afrika. Kati ya machapisho yake ni kitabu kiitwacho "TANU Women: Gender and Culture in the Making of Tanganyikan Nationalism, 1955-1965."

Kama kuna jambo ninalolifahamu, nitakueleza bila kipingamizi, kwani nchi yetu inahitaji mchango wa sisi sote kufuatana na uwezo wetu. Kila la heri.

mwanammuni said...

Asante nakushukuru!

mwanammuni said...

Wanawake wanasiasa au hata watendaji na wataalamu katika fani mbalimbali?

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...