Jana nilinunua vitabu vitatu katika duka la vitabu la chuoni St. Olaf. Viwili, Two Years Eight Months and Twenty-Eight Nights cha Salman Rushdie na A Strangeness in my Mind cha Orhan Pamuk, niliviona juzi. Cha tatu, Why Homer Matters, kilichotungwa na Adam Nicolson, nilikiona hiyo hiyo jana.
Nilipoingia dukani, nilikumbuka makala niliyoisoma juzi usiku, kuhusu vitabu halisi na vitabu pepe. Makala hii, sawa na nyingine nyingi, inatafakari iwapo vitabu vya jadi vitasalimika katika himaya hii ya vitabu pepe. Lakini inahitimisha kuwa hakuna ushahidi kuwa vitabu vya jadi vitapoteza mvuto au kufifia.
Mimi ni mmoja wa wale ambao hatujabadilika. Bado tumezoea vitabu halisi, yaani vitabu vya jadi, na ndio maana sisiti kuvinunua, wala sisiti kuelezea tabia yangu hiyo. Hapa nitaelezea kifupi kwa nini nimenunua vitabu hivi vitatu.
Kitabu cha Salman Rushdie kilinivutia kwa sababu ya umaarufu wa mwandishi huyu. Bila shaka wengi watakumbuka kitabu chake, Satanic Verses, ambacho kilipigwa marufuku katika nchi nyingi kwa madai kuwa kinaukashifu u-Islam. Ayatollah Khomeini wa Iran alitangaza fatwa kuwa Salman Rushdie anapaswa kuuawa.
Duniani kote, na hata miongoni mwa wa-Islam wenyewe hukumu hii ilizua mjadala. Baadhi walisema kuwa fatwa haikupaswa kutolewa kabla ya Salman Rushdie kupewa fursa ya kujieleza na kukiri kosa lake. Watu wengine walisema kuwa zogo hili lilimpa Salman Rushdie umaarufu ambao hakustahili kwa kigezo cha ubora wa uandishi wake.
Ninavyo baadhi vitabu vya Salman Rushdie, kikiwemo hiki cha Satanic Verses. Nimemewahi kufundisha riwaya yake maarufu, Midnight's Children. Ninavutiwa na ubunifu wake katika kuelezea mambo, na uhodari wake wa kutumia lugha. Uandishi wake unasisimua na kufikirisha.
Orhan Pamuk ni mwandishi ambaye nimewahi kumtaja katika blogu hii. Nina vitabu vyake kadhaa, na nimekuwa na hamu ya kuvisoma, ila bado sijapata wasaa. Huyu amenivutia si tu kwa kuwa alipata tuzo ya Nobel, bali pia kwa sababu ninafahamu kiasi fulani kuhusu fasihi simulizi ya Uturuki, kama vile hadithi za Nasreddin Hodja na Dede Korkut.
Why Homer Matters nimekipenda kwa kuwa taaluma ya tendi nimeipenda na kuishughulikia kwa miaka mingi. Homer, ingawa taarifa zake hazijulikani vizuri, ndiye anayehusishwa na tendi maarufu za u-Griki ya kale, The Iliad na The Odyssey. Kwa kuangalia juu juu, niliona kuwa mwandishi wa Why Homer Matters ana uwezo mkubwa wa kuelezea masuala ya Homer na hizi tendi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
5 comments:
Hongera sana. Nazifuatilia nukuu zako na ni msaada mkubwa kwangu. Kila la kheri
Shukrani, ndugu mwanammuni, kwa ujumbe wako. Ninaandika sana kuhusu vitabu na masuala ya aina hiyo ili kujiwekea kumbukumbu, lakini pia ili kuwahamasisha wengine. Uwekezaji katika vitabu na elimu kwa ujumla ndio uwekezaji ambao nimeutambua kuwa ni muhimu kabisa katika maisha yangu.
Manufaa ya kuzingatia vitabu na elimu tangu nilipokuwa kijana mdogo kijijini ninayaona, na ninataka vijana wafuatilie taarifa zangu, ili nao wajijengee msingi bora wa maisha yao ya baadaye. Nikifanikiwa kuwashawishi vijana wetu kwa hilo, nitajipongeza daima.
Narudia shukrani zangu kwako, na ninakutakia kila la kheri pia.
Ndugu Mbele napenda sana mapenzi yako kwa maarifa na vitabu. Kwangu mimi binafsi hakuna mali niliyo nayo na ninayoithamini kama hazina yangu ya vitabu hapa na nyumbani. Hakika umewamotisha wengi kuanza kuenda vitabu. Ushahidi ni maoni niyaonayo unapoongelea vitabu. Siku moja nitakutumia zawadi ya kitabu lau kimoja.
Shukrani kwa ujumbe, ndugu NN Mhango. Juhudi yako ya kuandika vitabu inavutia, na hizi blogu zetu ninazipenda kwa kuwa haziendekezi udaku. Kila la heri.
Ndugu NN Mhango, shukrani sana, kwa vitabu. Nimevipata asubuhi hii. Nikimaliza tu kusahihisha mitihani, nitavisoma kwa makini na kuandika mawili matatu. Kila la heri.
Post a Comment