Showing posts with label Salman Rushdie. Show all posts
Showing posts with label Salman Rushdie. Show all posts

Thursday, May 18, 2017

Vitabu Nilivyonunua Jana

Jana nilinunua vitabu vitatu katika duka la vitabu la chuoni St. Olaf. Viwili, Two Years Eight Months and Twenty-Eight Nights cha Salman Rushdie na A Strangeness in my Mind cha Orhan Pamuk, niliviona juzi. Cha tatu, Why Homer Matters, kilichotungwa na Adam Nicolson, nilikiona hiyo hiyo jana.

Nilipoingia dukani, nilikumbuka makala niliyoisoma juzi usiku, kuhusu vitabu halisi na vitabu pepe. Makala hii, sawa na nyingine nyingi, inatafakari iwapo vitabu vya jadi vitasalimika katika himaya hii ya vitabu pepe. Lakini inahitimisha kuwa hakuna ushahidi kuwa vitabu vya jadi vitapoteza mvuto au kufifia.

Mimi ni mmoja wa wale ambao hatujabadilika. Bado tumezoea vitabu halisi, yaani vitabu vya jadi, na ndio maana sisiti kuvinunua, wala sisiti kuelezea tabia yangu hiyo. Hapa nitaelezea kifupi kwa nini nimenunua vitabu hivi vitatu.

Kitabu cha Salman Rushdie kilinivutia kwa sababu ya umaarufu wa mwandishi huyu. Bila shaka wengi watakumbuka kitabu chake, Satanic Verses, ambacho kilipigwa marufuku katika nchi nyingi kwa madai kuwa kinaukashifu u-Islam. Ayatollah Khomeini wa Iran alitangaza fatwa kuwa Salman Rushdie anapaswa kuuawa.

Duniani kote, na hata miongoni mwa wa-Islam wenyewe hukumu hii ilizua mjadala. Baadhi walisema kuwa fatwa haikupaswa kutolewa kabla ya Salman Rushdie kupewa fursa ya kujieleza na kukiri kosa lake. Watu wengine walisema kuwa zogo hili lilimpa Salman Rushdie umaarufu ambao hakustahili kwa kigezo cha ubora wa uandishi wake.

Ninavyo baadhi vitabu vya Salman Rushdie, kikiwemo hiki cha Satanic Verses. Nimemewahi kufundisha riwaya yake maarufu, Midnight's Children. Ninavutiwa na ubunifu wake katika kuelezea mambo, na uhodari wake wa kutumia lugha. Uandishi wake unasisimua na kufikirisha.

Orhan Pamuk ni mwandishi ambaye nimewahi kumtaja katika blogu hii. Nina vitabu vyake kadhaa, na nimekuwa na hamu ya kuvisoma, ila bado sijapata wasaa. Huyu amenivutia si tu kwa kuwa alipata tuzo ya Nobel, bali pia kwa sababu ninafahamu kiasi fulani kuhusu fasihi simulizi ya Uturuki, kama vile hadithi za Nasreddin Hodja na Dede Korkut.

Why Homer Matters nimekipenda kwa kuwa taaluma ya tendi nimeipenda na kuishughulikia kwa miaka mingi. Homer, ingawa taarifa zake hazijulikani vizuri, ndiye anayehusishwa na tendi maarufu za u-Griki ya kale, The Iliad na The Odyssey. Kwa kuangalia juu juu, niliona kuwa mwandishi wa Why Homer Matters ana uwezo mkubwa wa kuelezea masuala ya Homer na hizi tendi.

Sunday, September 7, 2014

Ninasoma "Shalimar the Clown," Riwaya ya Salman Rushdie.

Salman Rushdie ni mmoja wa waandishi maarufu kabisa wanaoandika katika ki-Ingereza. Kwa uandishi wake, amepata tuzo zinazoheshimika sana, kama vile "Booker Prize."

Mimi ni mwalimu wa fasihi ya ki-Ingereza. Mara moja moja ninafundisha kozi ya "South Asian Literature," yaani fasihi ya Asia ya Kusini. Katika kozi hii, ninafundisha maandishi ya watu kama Rabindranath Tagore, R. K. Narayan, Raja Rao, Mulk Raj Anand, Anita Desai, Michael Ondaatje, na Salman Rushdie.

Haiwezekani kusoma au kufundisha maandishi yote. Vile vile, kazi mpya za fasihi zinaendelea kuchapishwa. Kwa hivi, kila ninapofundisha kozi ya namna hii, najua kuwa katika orodha yangu kuna waandishi ambao hawamo. Kuna kazi muhimu za fasihi ambazo hazimo. Huu ndio ukweli, ingawa haupendezi.

Uchaguzi wowote wa waandishi au maandishi ambao ninafanya kwa kufundishia katika muhula fulani wa masomo una utata na unazua masuali. Nilipofundisha kozi ya "South Asian Literature" kwa mara ya kwanza, Salman Rushdie hakuwemo. Nilijiuliza kama hii ni sahihi.

Hatimaye, nilianza kutumia maandishi ya Rushdie. Nilianzia na riwaya yake maarufu ya Midnight's Children. Hii sio riwaya rahisi kuisoma, lakini wanafunzi wangu nami tulifanya bidii tukaimaliza. Salman Rushdie anaandika ki-Ingereza ambacho kina mvuto wa pekee, ingawa sio rahisi, kwa mbinu za kila aina. Anadhihirisha ufahamu mkubwa wa ki-Ingereza, falsafa, fasihi, dini, siasa, na tamaduni mbali mbali. Msomaji unajikuta katika kazi kubwa ya kufikiri na kukabiliana na chemsha bongo mbali mbali.

Midnight's Children ilinipa hamasa ya kutumia maandishi ya Rushdie. Muhula huu wa masomo ambao ulianza wiki iliyopita, nitatumia riwaya yake ya Shalimar The Clown. Sikuwa nimeisoma riwaya hii, bali nimeanza, katika kujiandaa kuifundisha. Panapo majaliwa, hapo tutakapokuwa tumemaliza kuisoma na kuijadili, nitaandika habari zake katika blogu hii. Ila napenda kutoa tahadhari kuwa dhana ya kumaliza kusoma kazi yoyote ya fasihi sio dhana yenye ukweli. Ingawa tunaitumia dhana hii, tunajidanganya.


Thursday, July 18, 2013

Kiu ya Kusoma Vitabu

Daima nina kiu ya kusoma vitabu.  Sio rahisi unikute sina kitabu. Hii sio tu kwa vile mimi ni mwalimu. Ni tabia ambayo nilijengeka nayo tangu nikiwa kijana mdogo.

Kuwa mwalimu kumenipa motisha zaidi ya kusoma sana vitabu. Wakati huu ninapoandika, wanafunzi wangu na mimi tumemaliza kusoma Half of a Yellow Sun kilichoandikwa na Chimamanda Ngozi Adichie. Sote tumekifurahia sana. Lakini, mwandishi huyu amechapisha hivi karibuni na kitabu kingine kiitwacho Americanah, ambacho tayari kinazungumziwa sana miongoni mwa wapenda vitabu. Kwa hivi, nami najipanga kujipatia kitabu hiki, nikisome.

Kitabu kingine ambacho tumekimaliza katika darasa tofauti siku chache zilizopita ni Midnight's Children cha Salman Rushdie.  Kitabu hiki ni kama chemsha bongo, kwa jinsi kilivyotumia mbinu mbali mbali za kuelezea maisha ya mhusika mkuu Saleem Sinai. Maisha hayo yamefungamana na historia ya India, tangu dakika ile India ilipopata uhuru, usiku wa manane, mwaka 1947. Rushdie amechanganya matukio ya historia na ubunifu wake wa ajabu katika kitabu hiki.

Midnight's Children ni kitabu kinachokutegemea msomaji uwe na ufahamu fulani wa mila, desturi na dini za India, hasa u-Hindu, u-Islam, u-Kristu, na u-Parsi. Uwe na ufahamu fulani wa historia ya India hasa katika karne ya ishirini, inayojumlisha viongozi maarufu kama Mahatma Gandhi, Jawaharlal Nehru, Muhammad Ali Jinnah, na Indira Gandhi. Ujue mazingira yaliysababisha kuzaliwa kwa nchi mbili za India na Pakistan, na mgogoro wa Kashmir, ambao bado unaendelea. Kwa bahati nzuri, katika miaka niliyofundisha hapa chuoni St. Olaf, nimefundisha sana fasihi ya India na hayo yote niliyoyataja.

Tulipofikia ukurasa wa mwisho wa kitabu hiki, tulijisikia kama washindi wa mashindano magumu. Kwa upande wangu, baada ya kupambana na Midnight's Children hadi mwisho, nimejawa na hamasa ya kusoma kitabu kingine cha Rushdie Satanic Verses, ambacho nilikinunua zamani, nikajaribu kukisoma, bila kufika mbali. Ninahisi kuwa kwa kusoma Midnight's Children nimejiandaa vilivyo kukabiliana na Satanic Verses. Au labda nianzie na kitabu chake kiitwacho The Enchantress of Florence, ambacho nimekuwa nacho kwa miaka kadhaa, bila kukisoma.

Ni jambo jema kujaribu kusoma maandishi mbali mbali ya mwandishi yeyote, sio kitabu kimoja tu. Kwa mfano, kwa upande wa Tanzania, utawakuta watu wakitaja kitabu cha Hamza Njozi kuhusu mauaji ya Mwembechai lakini hawajui kuwa mwandishi huyu amechapisha vitabu vingine pia, na makala nyingi, kuhusu u-Islam na fasihi.

Vile vile, wengi wakisikia jina la Salman Rushdie, wanalihusisha na kitabu cha Satanic Verses tu. Huu nao ni uzembe, kwani mwandishi huyu amechapisha vitabu vingi, kuanzia riwaya hadi insha kuhusu masuala mbali mbali ya sanaa, siasa na utamaduni. Kumtendea haki Rushdie ni lazima tusome maandishi yake mbali mbali.

Akili zetu zinapaswa ziwe na duku duku isiyoisha ya kujua mambo. Njia moja kuu ya kujaribu kukidhi kiu hii ni kusoma sana vitabu. Hapo utaona kwamba, tofauti na imani ya jamii yetu ya Tanzania, wajibu wa kusoma vitabu ni wa watu wote, sio wanafunzi tu.

Saturday, March 16, 2013

Dunia Bila U-Islam

Wiki hii nimenunua vitabu kadhaa. Kimojawapo ni A World without Islam, kilichotungwa na Graham E. Fuller. Na hiki ndicho kitabu ninachotaka kukiongelea hapa.

Nilipokiona kitabu hiki katika duka la vitabu la hapa chuoni St. Olaf, nilivutiwa na jina la kitabu, nikajiwa na duku duku ya kufahamu ni kitabu cha aina gani, na kinaongelea nini. Dhana ya dunia isiyokuwa na u-Islam ilikuwa ngeni kwangu, kwa kuzingatia jinsi dunia ya leo ilivyo na jinsi u-Islam ulivyo na nguvu duniani. Dunia bila u-Islam ingekuwaje?

Ninahisi kuwa hadi hapo, wewe msomaji nawe tayari umeshapata mawazo au hisia fulani. Kama wewe ni mu-Islam, labda umeshaanza kuhisi kuwa kitabu hiki kimeandikwa na adui wa u-Islam. Labda unahisi kuwa kitabu hiki ni mwendelezo wa vita vya Msalaba ("Crusades"). Labda unahisi kuwa ni njama za makafiri dhidi ya u-Islam. Na kama wewe ni mmoja wa wale wanaoitwa wa-Islam wenye msimamo mkali, labda tayari unatamani yafanyike maandamano kulaani kitabu hiki, kama yalivyofanyika maandamano dhidi ya kitabu cha Satanic Verses cha Salman Rushdie.

Kama wewe si mu-Islam, labda ni m-Kristu, huenda una hisia zako pia. Na mimi kama m-Kristu nilikuwa na hisia zangu. Kusema kweli, nilipokiona hiki kitabu, nilihisi kuwa kitakuwa kimeandikwa na mtu ambaye ana ugomvi na u-Islam, na kwamba labda anataka kutueleza kuwa dunia ingekuwa bora endapo u-Islam haungekuwepo.

Hakuna ubaya kuwa na hisia au duku duku, ili mradi mtu uwe na tabia ya kufuatilia ili kujua ukweli. Unapokiona kitabu kama hiki, na hujakisoma, wajibu wako ni kukisoma ili ujue kinasema nini. Sio jambo jema katika taaluma kwa mtu kukumbana na kitu usichokifahamu, halafu ukaendelea na maisha yako bila duku duku ya kujua. Dukuduku hii huitwa "intellectual curiosity" kwa ki-Ingereza.

Duku duku hii ndio inayomtofautisha mtu aliyeelimika na yule asiyeelimika. Mtu aliyeelimika ni yule anayejitambua kuwa upeo wake ni finyu, na kuwa anawajibika kutafuta elimu muda wote. Nimeanza kukisoma kitabu hiki, na tayari nimegundua kuwa anachosema mwandishi si kile nilichodhania, ni tofauti kabisa na kile ambacho labda nawe ulidhania.

Kati ya hoja zake muhimu ni hizi: a) Vita vya Msalaba ("Crusades") vingekuwepo kwa vyo vyote vile, hata bila u-Islam. b) Ukristu wa ki-Orthodox wa Mashariki ungeinukia kuwa na nguvu sana na ungepambana na nchi za Magharibi. c) "Magaidi" wanaojilipua kwa mabomu wangekuwepo, kwani ingawa wengi wanahusisha jambo hili na wa-Islam, ukweli ni kuwa walioanzisha jambo hili ni Tamil Tigers, ambao ni wa-Hindu, kule Sri Lanka.

Inavyoonekana, hiki ni kitabu kimojawapo ambacho kinaelimisha sana. Kinatoa tahadhari mbali mbali kwa wale wanaouwazia u-Islam kwa ubaya.  Kwenye jalada lake, kitabu kimesifiwa sana na maprofesa Akbar S. Ahmed, Reza Aslan, na John L. Esposito, ambao ni wataalam wakubwa wa masuala hayo. Napendekeza tukisome kitabu hiki, kama ninavyopendekeza vitabu vingine katika blogu hii.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...