Saturday, March 16, 2013

Dunia Bila U-Islam

Wiki hii nimenunua vitabu kadhaa. Kimojawapo ni A World without Islam, kilichotungwa na Graham E. Fuller. Na hiki ndicho kitabu ninachotaka kukiongelea hapa.

Nilipokiona kitabu hiki katika duka la vitabu la hapa chuoni St. Olaf, nilivutiwa na jina la kitabu, nikajiwa na duku duku ya kufahamu ni kitabu cha aina gani, na kinaongelea nini. Dhana ya dunia isiyokuwa na u-Islam ilikuwa ngeni kwangu, kwa kuzingatia jinsi dunia ya leo ilivyo na jinsi u-Islam ulivyo na nguvu duniani. Dunia bila u-Islam ingekuwaje?

Ninahisi kuwa hadi hapo, wewe msomaji nawe tayari umeshapata mawazo au hisia fulani. Kama wewe ni mu-Islam, labda umeshaanza kuhisi kuwa kitabu hiki kimeandikwa na adui wa u-Islam. Labda unahisi kuwa kitabu hiki ni mwendelezo wa vita vya Msalaba ("Crusades"). Labda unahisi kuwa ni njama za makafiri dhidi ya u-Islam. Na kama wewe ni mmoja wa wale wanaoitwa wa-Islam wenye msimamo mkali, labda tayari unatamani yafanyike maandamano kulaani kitabu hiki, kama yalivyofanyika maandamano dhidi ya kitabu cha Satanic Verses cha Salman Rushdie.

Kama wewe si mu-Islam, labda ni m-Kristu, huenda una hisia zako pia. Na mimi kama m-Kristu nilikuwa na hisia zangu. Kusema kweli, nilipokiona hiki kitabu, nilihisi kuwa kitakuwa kimeandikwa na mtu ambaye ana ugomvi na u-Islam, na kwamba labda anataka kutueleza kuwa dunia ingekuwa bora endapo u-Islam haungekuwepo.

Hakuna ubaya kuwa na hisia au duku duku, ili mradi mtu uwe na tabia ya kufuatilia ili kujua ukweli. Unapokiona kitabu kama hiki, na hujakisoma, wajibu wako ni kukisoma ili ujue kinasema nini. Sio jambo jema katika taaluma kwa mtu kukumbana na kitu usichokifahamu, halafu ukaendelea na maisha yako bila duku duku ya kujua. Dukuduku hii huitwa "intellectual curiosity" kwa ki-Ingereza.

Duku duku hii ndio inayomtofautisha mtu aliyeelimika na yule asiyeelimika. Mtu aliyeelimika ni yule anayejitambua kuwa upeo wake ni finyu, na kuwa anawajibika kutafuta elimu muda wote. Nimeanza kukisoma kitabu hiki, na tayari nimegundua kuwa anachosema mwandishi si kile nilichodhania, ni tofauti kabisa na kile ambacho labda nawe ulidhania.

Kati ya hoja zake muhimu ni hizi: a) Vita vya Msalaba ("Crusades") vingekuwepo kwa vyo vyote vile, hata bila u-Islam. b) Ukristu wa ki-Orthodox wa Mashariki ungeinukia kuwa na nguvu sana na ungepambana na nchi za Magharibi. c) "Magaidi" wanaojilipua kwa mabomu wangekuwepo, kwani ingawa wengi wanahusisha jambo hili na wa-Islam, ukweli ni kuwa walioanzisha jambo hili ni Tamil Tigers, ambao ni wa-Hindu, kule Sri Lanka.

Inavyoonekana, hiki ni kitabu kimojawapo ambacho kinaelimisha sana. Kinatoa tahadhari mbali mbali kwa wale wanaouwazia u-Islam kwa ubaya.  Kwenye jalada lake, kitabu kimesifiwa sana na maprofesa Akbar S. Ahmed, Reza Aslan, na John L. Esposito, ambao ni wataalam wakubwa wa masuala hayo. Napendekeza tukisome kitabu hiki, kama ninavyopendekeza vitabu vingine katika blogu hii.

1 comment:

emuthree said...

Wakati mwingine vichwa vya habari huwekwa kwa minajili y akuvutia hisia za watu, maana kiukweli hicho kichwa cha habari tu, kinaweka hisia ya kujiuliza, na kama umdadidi na unataka kuelewa, utakisoma hicho kitabu.
Kiujumla lengo la dini zote ni `nia njema' ya kumjua mungu, japokuwa huyo mungu katafsiriwa kwa kila mtu na imani yake.
Lakini sio kumjua tu, hapana, ni kujua kwanini katuumba, na kama yeye ni muumbaji ina maana yeye ni mwenye mamlaka, kwahiyo atakuwa katuagiza tuishije.
Mimi nilichogundua ni kuwa `tafsiri' na `utashi' wa watu ndio umekuja kuharibu maana halisi na nia njema ya dini.
Mtu anaangalia vipi atalichafua shati la mwenzake ambalo kaliona ni safi,...huenda akalirushia matope, ili liharibike na kuanza kutangaza mitaani, `unaona lile shati sio jeupe, lina mdoa, ni chafu...
Profesa tunashukuru kwa juhudi zako za kuiweka jamii,katika mstari kwa kupitia kwenye vitabu, tatizo, siku hizi wasomaji wanapungua.
Siku hizi watu wanapenda sana kuangalia, na kusikiliza, kuliko kusoma na kuchanganua bongo zao, na madhara ya hizi hisia mbili(kuangalia na kusikiliza tu) tunayajua.
Ni hayo kwa leo Profesa

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...