Kuanzia mwaka 1966 hadi 1970 nilikuwa mwanafunzi wa sekondari, seminari ya Likonde. Wakati huo riwaya ya Things Fall Apart ilikuwa maarufu. Tulivijua pia vitabu vya watoto ambavyo Achebe alikuwa ameandika. Navikumbuka viwili: The Sacrificial Egg and Other Short Stories na Chike and the River. Shule yetu ilikuwa na maktaba kubwa na nzuri sana. Nidhamu ya kusoma ilikuwa kali, chini ya usimamizi wa mapadri waliokuwa waalimu wetu.
Miaka ile ile, Achebe alichapisha riwaya ya No Longer at Ease na Arrow of God na A Man of the People. Tulikuwa tunamsoma Achebe sambamba na Cyprian Ekwensi. Baadhi ya vitabu vya Ekwensi ambavyo tulivisoma ni Burning Grass, na People of the City na Jagua Nana. Hao wawili walikuwa kama mafahali wawili kutoka Nigeria katika uwanja wa uandishi.
Katika seminari ya Likonde, mwalimu wangu wa ki-Ingereza alikuwa Padri Lambert Doerr OSB, m-Jerumani, ambaye sasa ni askofu mstaafu pale Peramiho. Sidhani kama nimewahi kukutana na mtu anayesoma vitabu kama yeye. Alituwekea amri kwamba tusome angalau kitabu kimoja cha hadithi ya ki-Ingereza kwa wiki. Kitabu kimoja ilikuwa ni kiwango cha chini, lakini usikae wiki bila kumaliza angalau kitabu.
Padri Lambert alikuwa na mtindo wa kugawa daftari kwa kila mwanafunzi ambamo tulipaswa kuelezea kuhusu vitabu tulivyosoma, au ambavyo tulidai tumesoma. Wakati wowote alikuwa anaitisha daftari lako, ili akusikie ukimweleza habari ya kitabu chochote ulichokiorodhesha humo. Kumdanganya ilikuwa haiwezekani, wala huthubutu. Matokeo ya hayo ni kuwa kila mmoja wetu alisoma vitabu vingi sana, na ufahamu wetu wa ki-Ingereza ulikuwa mkubwa kabisa. Achebe, kwa uandishi wake wa kuvutia, alichangia kwa kiasi kikubwa kutufanya tupende kusoma.
No comments:
Post a Comment