CHADEMA: Taarifa kwa Vyombo vya Habari, Machi 14, 2013
CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 14 MACHI, 2013 Ndugu waandishi wa habari,
Tumewaita hapa leo, ili kupitia kwenu tuweze kutoa taarifa inayohusu
kukamatwa kwa mmoja wa viongozi wa chama chetu, Wilfred Lwakatare,
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama, aliyekamatwa jana tarehe 13 Machi 2013,
ofisini kwake makao makuu ya CHADEMA. Jeshi la polisi linasema
limemkamata Lwakatare likimtuhumu kuhusika na mashambulio ya watu
mbalimbali kutokana na ushahidi uliopo kwenye walioita, viedo ambayo pia
imesambazwa kwenye mitandao ya kijamii. Kwanza, tunapenda kuwaambia
umma wa watanzania na watu wote duniani kwamba, CHADEMA hakina nia
yoyote ya kuzuia polisi kutenda kazi zake, iwapo watakuwa wanafanya
hivyo kwa mujibu wa sheria. Bali, tunachoeleza hapa ni jinsi polisi
na vyombo vingine vya dola vinavyoshiriki katika kutengeneza
paropaganda chafu dhidi ya CHADEMA za kuwahusisha viongozi wa CHADEMA na
unyama unaoendelea nchini wa kutesa watu, kupiga, kung’oa kucha na
baadaye kuwatekeleza wakiwa nusu mfu. Mpango huu ulianza katika
tukio la kutekwa kwa Dk. Steven Ulimboka, ukaenda kwa Mwandishi wa
habari, Daudi Mwangosi na baadaye kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri
Absalom Kibanda; na kwa bahati mbaya sana, kwa namna moja au nyingine,
mkakati huu umekuwa ukilihusisha jeshi la polisi katika hatua za
utekelezaji wake. Kuweka kumbukumbu sawa, tunaweza kurejea suala la
kuuawa kinyama kwa Mwangosi, unyama uliosimamiwa na kufanikishwa chini
ya uangalizi wa kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda.
Mara baada ya tukio hilo, jeshi jeshi la polisi kupitia kamishana wake,
Paul Chagonja lilitoa kauli kuwa Mwangosi alilipuliwa na kitu alipokuwa
anawakimbilia polisi kujisalimisha akitokea kwa wafuasi wa CHADEMA,
jambo ambalo limethibitika kuwa halikuwa na ukweli hata kidogo.
Mpaka sasa, jeshi la Polisi halijamchukulia hatua zozote za kisheria
Kamhanda aliyesimamia na kufanikisha kifo cha Mwangosi, pamoja na
ushahidi wa kuhusika kwake kuwepo wazi. Aidha, pamoja na ukweli
uliobainishwa na tume zote zilizotumwa kuchunguza suala la Nyororo
Iringa, kusema Polisi walivunja sheria, walitumia nguvu isiyohitajika,
bado mpaka leo hii wanachama 42 wa CHADEMA wanashikiliwa na polisi
mkoani Iringa kuhusika na vurugu za Nyololo, Mufindi, Iringa. Waandishi
mtakumbuka kuwa Taarifa ya Kamati ya Nchimbi ilitofautiana kabisa na
Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu nay a MCT. Baada ya kazi ya Tume na
Kamati hizo hakuna Taarifa hata mmoja imetolewa na Polisi, walsa hakuna
watu waliohojiwa tena ukiaachawaliokamatwa kabla ya Taarifa za Tume
hizo. Wala sijaona kwa bahati mbaya vyombo vya habari vikichambua
Taaarifa hizo kwa kina, Katika nyakati mbalimbali, CHADEMA
tumefungua jalada Polisi, na nyingine amezifungua Mhe. Lwaklatare
mwenyewe akilalamikia mchezo mchafu tunaofanyiwa ikiwa ni barua
kuandikwa kwa majina yetu, yenye sura ya kutuchafua. Mojawaopo
ikidhaniwa kuandikwa na Rwakatare mwenyewe akiomba Tshs 200 millioni kwa
ajili ya vijana anaodhaniwa kuwaleta toka Tarime kwa ajili ya Igunga.
Hadi leo Polisi hawajamhoji Lwakatare mwenyewe, wala hatujasikia
upepelezi wowte ukifanyika. Aidha tulitoa Taarifa ya mtu aliyepewa
bunduki wakati wa uchaguzi wa Igunga akituhumu kuwa amepewa bastola hiyo
kwa lengo la kudhuru wakati wa Kampeni ya Igunga. Tumetoa mpaka nay a
Bastola husika na mahali ilipotengenezwa. Polisi hadi leo hawajatoa
Tamko lolote kama Bastola hiyo iliyotengenezwa China imesajiliwa kwa
jina la nani, na hivi sasa ipo kwa nani. Lakini kwa tukio tu la
Lwakatare na picha yake kubandikwa kwenye Mtandao, Polisi tayari
wameisha kumkamata. Ni dhahiri kuna mchezo unachezwa dhidi ya CHADEMA,
na Polisi kuiingizwa au kwa kujua au kutokujua katika mtego huo.
Sasa hapo mnaweza kujiuliza, hapo haki ipo wapi? Yaani waliotajwa na
tume yaani polisi – wapo huru, lakini wanaCHADEMA 42 ambao hawakutajwa
popote na tume wanasota gerezani. Hata katika suala la Dk. Ulimboka,
jeshi la Polisi halikutelekeza wajibu wake kikamilifu. Jeshi hilo
limekataa kumhoji Dk. Ulimboka na wala kuwahoji baadhi ya watuhumiwa
wakuu wanaotajwa kuhusika moja kwa moja katika kumteka Dk. Ulimboka,
akiwemo Naibu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Jack Zoka, Afisa wake
Ramadhani Ighondo mwengine anayeitwa Nzowa. Vilevile, kwenye tukio
la kutekwa kwa Kibanda, ambalo linafanana kwa kiasi kikubwa na lile la
Dk. Ulimboka, Afisa Mtendaji Mkuu wa New Habari Corporation, Hussein
Bashe, ametaja kuhusika kwa polisi katika utekaji wa Absalom Kibanda, na
baadaye akamtaja Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe, lakini mpaka sasa, jeshi la Polisi halijachukua hatua
zozote ama kwa waliotajwa au kwa aliyetaja. Lakini katika hili la
Lwakatare CHADEMA kilipata taarifa mapema kuwa upo mkakati unaoratibiwa
na kufanikishwa na Naibu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Jack Zoka na
genge lake lenye wajumbe mashuhuri, Ramadhani Ighondo na Nzowa
linalotaka kukihusisha CHADEMA na njama za kumdhuru Kibanda ili
kukidhoofisha kisiasa. Lilipotokea hili la Lwakatare tukasema, sasa kile
tulichoambiwa ndiyo hicho kimekuja. Bahati njema gazeti la
Mwananchi la leo linasema Lwakatare anatuhumiwa kupanga njama za
kumdhuru Mhariri wa gazeti hilo, Denis Msacky, na kwamba Lwakatare
amekamatwa baada ya kuonekana kwenye video iliyosambazwa kwenye mitandao
ya kijamii haraka inayomuonyesha Lwakatare akipanga njama hizo hatujui
baadhi ya taarifa zingine ingwa kwa hiki kilichopo kwenye mtandao hakuna
popote alipotajwa Msaky. Si nia yangu kuingilia upelelezi wa Polisi,
lakini nimesema CHADEMA tumefurahi kwa kuwa iwapo kwa utaratibu huu au
wowote ule fursa itapatikana na ukweli wote kutolewa hadharani. Ni imani
yangu kuwa zoezi hili litafuata sheria na taratibu zote zilizokwa na
Katiba yetu kulinda haki za mtu. Sasa kutajwa kwa Msacky inawezekana hilo la Kibanda halijaiva, au pengine liko njiani; ama wameona aibu kuliingiza kwa sasa.
Lakini Waandishi wa Habari, mnajua kuwa mara baada ya Kibanda kutekwa,
Ridhiwani Kikwete na Nape Nnauye walivyoshangilia kutekwa kwa Kibanda
katika mtandao huo huo uliotumika kumkamata Lwakatare bila kuwakamata
wahusika hao ambao waliingia kwenye mtandao kwa ID yao wenyewe.
Akiandika katika mtandao wake wa face book Ridhiwani alisema: “Na hili
la Kibanda mtasema ni kazi ya Ramadhani Ighondo, afisa usalama pale
Ikulu?” Kwanza, kauli hii ya Ridhiwani ilikuwa inathibitisha kwamba
aliyepanga njama za kumteka Dk. Ulimboka, ni Ramadhani Ighondo wa
Ikulu. Pili, Ridhiwani alikuwa anataka kuaminisha jamii kwamba
katika hili la Kibanda, yeye na kundi lake hawahusiki, bali wanaohusika
ni CHADEMA; hivyo akawa anachokoza mjadala ambao ulishapangwa ili
baadaye vyombo vya dola viweze kuuchukua, na hivyo ndivyo ilivyotokea.
Tunazo taarifa kutoka vianzio vyetu vya ukakika ndani ya Usalama wa
Taifa kuwa baada ya Ridhiwani kuweka andishi lake kwenye facebook,
aliingia kiwewe sana hasa baada ya Hussein Bashe kuja juu. Ridhiwani
anafahamu nguvu ya Bashe kwenye kufuatilia suala la kutekwa kwa Kibanda
na hivyo amemuomba baba yake kuvitumia vyombo vya dola kumuokoa. CHADEMA
haijawa na haitakuwa, lakini tuliyoambiwa yametimia, na mengine zaidi
yanakuja, kwani kwa Taarifa zetu hiyo yaliyotokea “ni cha mtoto”. Na
wala hatutaki kutabiri mbinu zitakazotumika kumwokoa. Ndugu
waandishi wa habari; katika mlolongo wa kuwakamata viongozi wa CHADEMA,
yumo Mbunge wa Iringa, Mchungaji Msigwa. Mheshimiwa Msigwa tunaambiwa na
watu wetu wamemtafuta kwa muda mrefu sasa. Wanasema sumu anazotema
bungeni na kwengineko dhidi ya idara ya usalama ya taifa juu ya tuhuma
za kuhusishwa na wizi wa nyara za serikali, zinawanyima usingizi na
hivyo wanataka wamnyamazishe. Wanataka kujua kutoka kwa Msigwa ni
nani aliyevujisha na kumpa taarifa zile za ujangiri wa wanyama pori
zinazohusisha CCM, usalama wa taifa, polisi na Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ). Msigwa anaonekana kuwa ni jasiri kusemea udhaifu wa
idara ya usalama, wanaamini anavyo vitu vingi na wao wangependa wajue
ana nini na anapewa na nani. Tayari Mchungaji Msigwa ameondolewa
kwenye kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na kupelekwa
Kamati ya Kilimo ili kulinda uchafu wa serikali, wakati yeye ni waziri
kivuli wa Maliasili na Utalii na Waziri kivuli anatakiwa kuwa Kwenye
Wizara ya Sekta anayoisemea, na wala hajaomba Wizara ya Kilimo.`ni
dhahiri syndicate ya mfumo huu wa kutaka kuisambaratisha CHADEMA.
Huhitaji kwenda chuo Kikuu chochote, kuelewa hili. CHADEMA
kinafahamu kwa undani, kwamba uzushi huu wa Tape ya “Bukoba Boy”.Tunajua
huu umeanzishwa na kuhusisha Usalama wa Taifa, akiwemo Ighondo na
wenziwe pale Ada Estate. Huyu Ighondo ambaye anafahamika pia kwa jina
la “Rama” tunamfahamu vizuri sana. Aliwahi kufanya kazi ya katibu wa
UV-CCM wilaya ya Singida Vijijini, kati ya mwaka 2006 na 2008 na ndiye
aliyekuwa akitumia simu na 0713760473 katika mawawsiliano yake na Dr.
Ulimboka kwa simu na 0713731610 mpaka takriban dakika 3 kabla ya
Ulimboka kutekwa. Gazeti la Mwanahalisi liliandika taarifa ya uchunguzi
ya kina ya Jambo hilo. Rais wetu amenukuliwa na magazeti ya
Serikali Addis Ababa akisema kuwa Mwanahalisi ilifungiwa kwa sababu ya
‘kuchochea uasi katika majeshi yetu’ au maneno Kama hayo. Sitaki
kumwita Rais wetu wwongo leo lakini kwa kuwa Taarifa hiyo haijakanushwa
wala na Rais, wala na Ikulu, tunaamini maneno hayo ni kweli ametamka.
Tunamtaka Rais Kikwete atamke maneno hayo hayo hapa nchini. Kwa njia
yeyote ili ili Watanzana wengi na hasa wasomaji wa Mwanahalisi, na hata
majeshi yetu amba kimsingi ninafahamu walilipenda Gazeti la Mwanahalisi
wamsikie kwa masikio yao wenyewe. Taifa linawekwa pabaya sana Rais
anapofikia kutoa matamko ya upotoshwaji mkubwa kiasi hicho tena nje ya
nchi. Ndiyo maana tunaposema Idara ya Usalama wa Taifa, ni tawi la
CCM, tunaushahidi. Kwa mfano, tunajua jinsi baadhi ya watendaji wajuu wa
idara hiyo kama vile, Zoka na vibaraka wake wadogo akiwamo Ighondo, ni
radical wa CCM, wenye ushabiki uliopitiliza. Hata ukiangalia jinsi
walivyotekeleza mpango wa utekaji wa Dk. Ulimboka, kwamba walifanya
hivyo mbele ya macho ya Dk. Deogratias Michael, haraka utabaini kuwa
utekaji huu ulifanywa kwa ushabiki wa kulinda CCM. Ndugu waandishi
wa habari, kutokana na yote hayo hayo sasa tunasema ifuatavyo: Kwamba
jeshi la polisi lifanye kazi yake bila ushabiki wa kisiasa au shinikizo
la wanasiasa. Ndugu Waandishi,CHADEMA haiko tayari kuruhusu watu
wenye maslahi binafsi kutuchafua mbele ya jamii. Katika hilo,
tutapambana na yoyote bila kujali cheo chake, madaraka yake serikalini,
fedha alizonazo au madaraka mengine. Wakati polisi wakitekeleza
hilo, tunamtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, ajitokoze
hadharani kueleza umma juu ya mgogoro wake na Kibanda. Tunavyofahamu
sisi, Kibanda aliteuliwa kuwa mjumbe katika kamati ya kubuni vazi la
taifa. Lakini alijitoa na kusema aliyemteuwa yaani - Nchimbi - ambaye
wakati huo, alikuwa waziri wa habari, utamaduni na michezo, ndiye
aliyeshinikiza polisi kumfungulia kesi ya uchochezi mahakamani. Hadi
sasa hatujapata taarifa za wazi zinazoonyesha kama uadui wa wawili hawa
uliisha, na kwamba Nchimbi sasa ndiye waziri wa mambo ya ndani, ambapo
polisi wanawajibika kwake. Tuna mashaka kuwa uchunguzi wa tukio
lililomkuta Kibanda unaweza kudhoofika. Kutokana na hayo yote CHADEMA tunasema nini sasa:-
i) CHADEMA katika hatua hii ya awali, tunafuatilia kwa karibu sakata
lote la ukamataji wa Lwakatare na kuona kama sheria za nchi, taratibu
mbalimbali na misingi ya Haki za Binadamu inafuatwa kuikamilifu. ii)
Tunarudia tena madai yaliyotolewa mara nyingi na CHADEMA, kwa Rais
kuandikiwa barua na Mwenyekiti wetu, Iundwe Judicial Commission of
Inquiry (Tume Huru ya Kimahakama kuchunguza vifo vyote vyenye utata na
sura ya kisiasa). Serikali inaogopa nini kuunda Tume hii huru ili ukweli
Ujulikane? Iweje CHADEMA inayotuhumiwa Kupanga njama wanaishinikiza
Serikali kuunda Chombo huru na Serikali ndiyo inayopata kigugumizi?
iii) Kwa wale walioumizwa na kujeruhiwa kama kina Ulimboka Kibanda na
wengine, tunarudia Tamko letu la kuwa hatuna Imani na uchunguzi
unaofanywa na Jeshi la Polisi kwa kuwa viongozi wa Jeshi hilo ni sehemu
ya watu tunaowatuhumu kwa kuhusika kwa njia mbalimbali, na Ushihidi wa
wazi na Taarifa mbili za Serikali kupingana yaani Taarifa ya Kamati yqa
Nchimbi na Tume ya Haki za Binadamu. Tutaiaminije Polisi na Serikali kwa
Taarifa ya Kamati ya Nchimbi? Mwendawazimu tu anaweza kuwa na imani
baada ya Taartifa zile 3. iv) Kuokana na upotoshwaji mkubwa, na
kutokana na uhakika tulionao mkubwa Mwanahalisi ilifungiwa si kwa sababu
yeyote ile, bali kutoka na kukomalia swala la Dr Uliomboka na hasa
uhusika wa Ighondu, Afisa Usalama anayefanya kazi Ikulu chini ya Raisi
mwenyewe. CHADEMA sasa tunaitaka rasmi Serikali ifungulie Gazeti nla
Mwanahali kwa sababu hatuwezi kuendelea kuvumilia uikandamizaji huu wa
uhuru wa Habari, ambao sasa unaelekea kuota mizizi nchini kwetu. Na
kweli ninawaomba na kuwataka waandishi wote msimame imara, bila kujadili
itikadi, au tofauti zetu zozote zile na kusimamia uhuru wa Habari.
Tunataka vivyo hivyo, kwa wanaharakati mbalimbali. Waache hofu, eti
wanaogopa kuhusishwa na vyama vya Siasa! Haki ni haki na haina rangi ya
bendera ya chama chochote. Ndugu Waandishi Nawashukuru sana Imetolewa Makao Makuu ya CHADEMA, na,
No comments:
Post a Comment