Wednesday, March 20, 2013

Tamko la CCM Mkoa wa Vyuo Vikuu

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mkoa maalum wa vyuo vikuu, kanda ya Dar es salaam, umefanya kikao cha kujadili mipango na mikakati mbalimbali ya kuimarisha Mkoa huo na Chama kwa ujumla. Pamoja na Ajenda hiyo, pia kikao hicho:-

· Kimelaani vikali matukio ya kuvamiwa, kudhuru mwili na kuuawa kwa baadhi ya viongozi wa Dini na wanahabari. Mkoa umesikitishwa sana na tukio la kushambuliwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF) na Mhariri Mtendaji wa New Habari 2006 Ndugu Absalom Kibanda.

· Lakini pia, kimevitaka vyombo vya Dola kuwakamata, kuwashikilia na kuwachukulia hatua za kisheria wote waliothibitika kuhusika na matukio ya namna hiyo bila kuangalia Itikadi za Kivyama, Cheo ama Kundi. Na pia kuyataka makundi ya kijamii, wanaharakati na wanasiasa kuacha kuingilia/kuvuruga kwa namna yeyote taratibu za kisheria na kiusalama.

· Pia, kuwataka wanausalama kumhoji kwa kina Dr Slaa juu ya tuhuma zake dhidi ya Kurugenzi ya Usalama wa Taifa (TISS) na kumtaka kuthibitisha madai yake kuwa baadhi ya watendaji wa taasisi hiyo muhimu na nyeti wanaripoti kwake kinyume cha utaratibu, kanuni na maadili ya taasisi hiyo.

Kwani tuhuma hizo ambazo Dr Slaa amekuwa akizisema mara kwa mara tangu kipindi cha Kampeni za Urais Mwaka 2010 zimeanza kuaminika, lakini pia zimepelekea wananchi sasa kukosa imani na Taasisi hiyo na zaidi kupoteza imani juu ya uwezo wa serikali kuwalinda na kuwahakikishia Usalama wa maisha yao, ambapo ni jukumu la kikatiba la serikali.

Imetolewa na:- Daniel Zenda.

Katibu wa Wilaya Dar es salaam.

-----------------------------------------------------------------

Hili hapa juu ndilo tamko la CCM mkoa wa vyuo vikuu. Nami kwa mtindo wa majibizano ya blogu, nimejibu hivi:

Wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2010, mheshimiwa mmoja wa ngazi ya juu kabisa katika CCM alitamka kwamba CHADEMA wamepeleka vijana wao nje kwa mafunzo ya kuhujumu amani na kwamba vijana hao wameshaingia nchini baada ya mafunzo hayo.

Kauli hii ya mheshimiwa wa CCM ilinishtua, kwa maana mbali mbali, hasa kwa vile ilikuwa inajenga hisia kuwa Tanzania haina ulinzi wa kufaa, na kwamba kama kuna idara ya usalama wa Taifa, basi idara hiyo haiko makini.

Je, nyinyi CCM wa vyuo vikuu mlimsikia mheshimiwa huyu, na je, hamkutambua kuwa amewaambia walimwengu, wakiwemo maadui, kwamba nchi yetu haina ulinzi imara?

Je, mlitoa tamko la kutaka mheshimiwa huyu akamatwe na ahojiwe? Leo mnasema Dr. Slaa ahojiwe, kwa nini msimwunganishe na huyu mheshimiwa wa CCM?

Nyinyi CCM wa vyuo vikuu mnanitia kichefuchefu kwa jinsi mlivyokosa umakini. Mimi nilikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu Dar kuanzia 1973 na wakati ule nilikuwa katika Umoja wa Vijana wa TANU (TANU Youth League)

TANU Youth League hatukuwa vikaragosi wa TANU. Tulikuwa makini katika kudumisha fikra za mapinduzi, na mara kwa mara tulikuwa tunawapinga wazee wa TANU. TANU yenyewe haikuwa ina msimamo kama wetu, na Nyerere alikiri hivyo. Lakini alituachia tufanya tulivyoamini.

Kwa mfano, tulikuwa tunaendesha jarida liitwalo "Maji Maji," na nendeni maktaba mkaone. Mtaona kuwa hatukuwa vikaragosi wa TANU, kama vile nyinyi mlivyo vikaragosi wa CCM. Wala hamjaonyesha uwezo wowote wa kutafakari masuala ya mwelekeo wa nchi.

Kwa mfano, mnashindwa hata kutafakari suali la msingi la, Je, CCM ni chama cha mapinduzi?

Ingekuwa nyinyi ni wasomi, angalau mngepitia "Azimio la Arusha," "Mwongozo," na maandishi mengine, mkafahamu dhana ya Mapinduzi ambayo wa-Tanzania tulianza nayo enzi za Nyerere, halafu mfananishe na sera za CCM, ambazo ni sera za kuhujumu Mapinduzi.

Kwa kweli, nyinyi CCM wa vyuo vikuu ni mfano hai wa jinsi viwango vya elimu vilivyoporomoka.

Mkitaka kujibizana nami, mjitokeze kwa majina yenu, sio "anonymous," kwani itakuwa ni fedheha ya ziada iwapo wasomi mnajificha namna hiyo. Kwenye mijadala, wasomi tunajitokeza wazi wazi. Nawasubirini.1 comment:

Steven Ludovick said...

Vijana wa CCM sio vikaragosi wa CCM bali ni vijana makini wa chama hiche wenye nia ya dhati ya kuendelea kupigania chama cha mapinduzi na kukiendeleza kukiimaarisha.