Hapa ni ndani ya kituo cha utamaduni cha jiji la Arusha |
Na Albano
Midelo
UTALII wa kiutamaduni bado ni nadharia changa katika nchi za ulimwengu wa tatu ikiwemo Tanzania,kutokana na ukweli kuwa katika nchi hizo wamezoea kuona utalii wa asili wa kutembelea mbuga za wanyama.
Utalii wa kiutamaduni ni nadharia mpya hapa nchini ambapo serikali imeanza kuutambua utalii wa kiutamaduni na kuupa nguvu kubwa aina hiyo ya utalii miaka ya hivi karibuni,zamani vivutio vya utalii wa kiutamduni kama majengo ya kale,maeneo ya kihistoria na makumbusho hayakupewa mtazamo wa kiuchumi zaidi.
Maeneo hayo yalipewa mtazamo wa kielimu zaidi na kuundwa idara za mambo ya kale na idara ya makumbusho ambazo zote awali zilikuwa katika wizara ya elimu na utamaduni ambavyo viliwekwa kama vyanzo vya elimu zaidi kuliko vyanzo vya utalii kwa sababu wakati ule watalaamu walifanya tafiti mbalimbali za mambo ya kale wakiwemo wakina Dk.Leakey
Hata hivyo baadaye kulikuwa na
mabadiliko katika ulimwengu mzima hali iliyosukuma kuwepo kwa utalii wa
kiutamduni na nchi zilianza kutoa kipaumbele katika utalii wa kiutamaduni ndiyo
maana hapa nchini idara za mambo ya kale na makumbusho zilihamishwa kutoka
wizara ya elimu na kuingia katika wizara ya utalii na maliasili.
Utalii wa kiutamadini hivi sasa unakuwa na hata mabadiliko ya utalii huo hayawezi
kuonekana kwa haraka badala yake inatakiwa watalaamu kuwahamasisha wananchi kutambua
fursa zilizopo katika aina hiyo ya utalii na kuzitumia ipasavyo fursa zilizopo
ili kujiletea maendeleo wao binafsi na Taifa kwa ujumla wake.
Ni vigumu sana kutenganisha utalii
asili na utalii wa kiutamduni kutokana
na aina hizo mbili za utalii kuwa na mahusiano ya karibu.Watalii wanapoingia
nchini wote wanavutika na utalii wa aina zote mbili .
Mtalii anapokwenda kutembelea utalii
wa asili kama mbuga za wanyama pia anaweza kupita katika maeneo yenye utalii wa
kiutamaduni na kwamba fursa ya utalii wa kiutamaduni ni kubwa kwa wananchi wa
kawaida kuliko aina nyingine za utalii.
Mhadhili msaidizi kutoka idara ya
utalii wa kiutamaduni chuo kikuu kishiriki cha Tumaini Frank Kimaro anabainisha
kuwa utalii wa kiutamaduni unazungumzia
jamii husika na kwamba jamii hiyo inaweza kufaidika kutokana na utalii wa
kiutamaduni ambao unapatikana katika eneo husika hadi kufikia hadi ngazi ya
kitaifa.
“Unaweza kuona aina hii ya utalii ni tofauti na utalii wa asili ambao tunaangalia zaidi mbuga za wanyama na maeneo ambayo yametengwa na serikali ambapo wahusika wakubwa ni serikali yenyewe na siyo watu binafsi,katika utalii wa kiutamaduni wahusika wakuu ni wananchi wenyewe”,anasisitiza na kuongeza
“Wananchi katika utalii wa utamaduni
wanaweza kunufaika kuanzia kiwango cha familia, mtaa, kitongoji,kijiji,wilaya,mkoa
na kitaifa kwa hiyo utalii wa kiutamaduni unatoa fursa kubwa sana ya ukuaji wa
uchumi kuanzia kwa mtu binafsi hadi kwa taifa”
Licha ya utalii wa utamaduni kuonekana
kumlenga zaidi mwananchi wa kawaida ,lakini kipato anachopata mwananchi huyo
kwa kucheza ngoma au kuuza bidhaa za jadi na kazi nyingine za mikono kipato
chake kimekuwa cha chini na kuwakatisha tamaa wananchi.
Kimaro anasema kuwa vitu anavyovifanya
mwananchi katika utalii wa kiutamaduni vina thamani kubwa kuliko mapato
anayopata na kwamba katika hali ya kawaida vitu vya utamaduni vina thamani
kubwa na vikiachwa kupotea haviwezi
kupatikana tena na kwamba hakuna kiwango cha malipo kamili kwa shughuli za
utalii wa kiutamaduni.
Hata hivyo Kimaro anasema kuwa utalii wa kiutamaduni unaweza kubadilisha
kiwango cha maisha ya watu kutokana na kupata kipato kutokana na kazi hiyo kuwa shughuli mbadala ambayo
inawasaidia wao kuwaongezea kipato cha ziada katika mapato yao.
Anabainisha kuwa kabila la wamasai
katika msimu wa utalii wa kiutamaduni wanapata mapato karibu shilingi 30,000
kwa siku kutokana na aina hiyo ya utalii jambo ambalo linaonesha kuwa ni kipato
kikubwa ukilinganisha na vijana wengine mijini ambao wanaingiza kipato kidogo
sana.
Bidhaa zinazotokana na utalii wa
kiutamaduni kama samani zilizotengezewa kwa miti pamoja na sanamu za kuchonga
zimekuwa zinauzwa na watu binafsi kwa watalii na wageni wengine kwa bei za juu
sana kwa mfano kiti kinachotengezwa kwa kutumia miti ya mianzi kinauzwa kati ya
shilingi 200,000 hadi 300,000,
kofia inayotengenezwa kwa ukindu
inauzwa kati ya shilingi 3500 hadi 5000,mkanda unaotengenezwa kwa ngozi yenye shanga unauzwa kati ya shilingi 5000
hadi 10,000,kigoda kilichotengenezwa kwa mti wa kawaida kinauzwa kati ya
shilingi 10,000 hadi 15,000 wakati kinyago cha kuchongwa kinauzwa kuanzia
shilingi 20,000 hadi 500,000 kutegemea na ukubwa wa kinyago hicho.
Hata hivyo amesema bei ya mtengenezaji
ni ndogo ambapo muuzaji wa mwisho ndiyo anayepata faida kubwa kwa kuwa anauza
kwa bei ya juu zaidi na kwamba mnunuzi
wa kati anakwenda kutafuta vitu hivyo sehemu ambazo mzalishaji anauza kwa bei
nafuu ili na yeye aweze kuuza kwa bei ya juu ili kufidia gharama za usafiri, uchukuzi, uhifadhi
na malazi.
Nafasi ya utalii wa kiutamaduni ni
kubwa katika kukuza uchumi wa nchi
kutokana na ukweli kuwa utalii unachangia uchumi wa Tanzania katika
kiwango kikubwa na kuchukua nafasi ya
pili hivyo utalii endelevu una nafasi kubwa katika kuleta maendeleo endelevu.
Kulingana na mhadhili huyo utalii huo
pia una nafasi kubwa ya kuchangia uchumi wa watu binafsi kwa sababu utalii
unatengeneza ajira za moja kwa moja na ajira ambazo sio za moja kwa moja
ambapo watanzania wengi hivi sasa
wamejiajiri katika shughuli za utalii wa kiutamduni ambao wamefungua maduka
ambayo wanauza vitu vya kiutamaduni vyenye bei kubwa zaidi katika soko la
utalii.
“Soko la vitu vya utamaduni wa kitalii vinatoa
ajira kwa watu wengi wakiwemo mwenye duka,mtengenezaji na msambazaji hivyo
kufungua fursa za ajira za moja kwa moja kwa wananchi ambapo watu wengine
wananufaika na utalii wa utamaduni kutoka kwenye migongo ya watu
walioajiriwa moja kwa moja katika sekta
hiyo’’,anasisitiza.
Anawataja watu wanaonufaika katika sekta ya
utalii wa kiutamduni kutoka katika migongo ya watu wengine kuwa ni pamoja na watu wenye hoteli,nyumba za
kulala wageni,watu wanaouza maji na vyakula mbalimbali na kwamba utalii huo unafungua milango ya ajira.
Uchunguzi umebaini kuwa katika
ulimwengu hivi sasa kuna nchi nyingi ambazo zimekuza uchumi wake kwa haraka
kupitia utalii wa kiutamaduni zikiwemo Australia,Ujerumani,Uingereza pamoja na
nchi nyingine nyingi za ulaya ambazo kutokana na ukosefu wa mbuga za wanyama
wengi kama zilivyo katika Afrika wameamua kuendeleza utalii wa kiutamaduni
zaidi kuliko utalii wa asili na kupata maendeleo makubwa kupitia aina hiyo ya
utalii.
Kutokana na hali hiyo watanzania na
wadau wote wa utalii wanatakiwa sasa kubadilika kimawazo na kifkra kutoka katika aina ya utalii wa asili ambao ni
kuangalia wanyamapori na na kuingia katika utalii wa kiutamaduni ambao ni wa
kipekee kwa kuwa hutofautiana kutoka eneo moja kwenda eneo jingine na
watalii kupata vitu vipya hivyo kuvutika zaidi .
CHANZO: Blogu ya Maendeleo ni Vita
No comments:
Post a Comment