Friday, April 29, 2011

Neno Kuhusu Ualimu

Picha hii ilipigwa Dar es Salaam, Septemba 2004,kwenye viwanja vya makumbusho ya Taifa, wakati wa tamasha la vitabu. Naonekana nikiwa na walimu kutoka Kunduchi Girls Islamic High School. Walikuja na hao watoto kwenye meza ambapo nilikuwa nimeweka vitabu vyangu.

Tulizungumza na kushauriana mambo ya manufaa kuhusu elimu na kadhalika, nao walinialika kutembelea shule yao. Haya ndio mambo tunayohitaji katika nchi yetu. Na hao watoto katika picha wanasikia tunachoongea sisi watu wazima. Tuwaleavyo ndivyo wakuavyo.

Ninapowakumbuka na kuwaangalia watoto, kama hao waliomo katika picha, hisia zangu za kiualimu zinaibuka. Kwa upande mmoja, nafurahi na kushukuru kuwa nimejaliwa uwezo na fursa ya kuwaelimisha watoto hao. Ninawapenda. Soma, kwa mfano, makala yangu hii hapa.

Papo hapo, ninapowawazia watoto wa Taifa letu, najiwa na wasi wasi kwa jinsi baadhi ya watu wanavyoeneza mitazamo na mawazo kama udini, ubaguzi na uhasama baina ya makundi mbali mbali ya jamii. Hizo ni sumu, nami nahofia athari zake kwa watoto wetu.

Ualimu ni wito, nami nilisikia wito huu wakati nikiwa bado mdogo, sijaanza hata shule. Ni wito wa kuwa mtafuta elimu muda wote, wito wa kuwalea wanafunzi wawe wanaothamini na kutafuta elimu; wawe watu wema kwa mujibu wa maadili ya jamii yao. Elimu haina mwisho. Mimi ni mwalimu wa madarasa ya chuo kikuu, kuanzia mwaka 1976, lakini ningefurahi kama ningekuwa pia na utaalam wa kuweza kufundisha shule ya msingi. Nimeelezea hayo katika kitabu cha CHANGAMOTO.

Wednesday, April 27, 2011

Maktaba ya Lushoto

Kila ninapokuwa Tanzania, najitahidi kutembelea taasisi za elimu kama vile shule na maktaba. Mwaka jana, wakati nipo mjini Lushoto, nilipata dukuduku ya kujua kama kuna maktaba hapo, na iko wapi. Nimeshaona maktaba za hata miji midogo kama Mbinga na Mbulu.

Niliulizia mitaani, na watoto wa shule ya msingi wakanionyesha maktaba ilipo. Hiyo ilikuwa ni tarehe 5 Agosti. Niliingia ndani nikaona vitabu vya aina aina, vya taaluma mbali mbali, kuanzia fasihi, hadi masuala ya jamii na maendeleo. Niliona hata vitabu viwili vitatu vya Karl Marx, Kwame Nkrumah, na Issa Shivji.

Ingawa maktaba hii haina vitabu maelfu na maelfu, nilipata hisia kuwa mtu anayeishi katika mji huu akiamua anaweza kujielimisha kiasi cha kueleweka kwa kusoma vitabu vilivyomo katika maktaba hii.

Niliongea na mama mhudumu wa maktaba. Alinieleza mazingira magumu ya maktaba hii, nami nilijionea mwenyewe. Niliona jinsi yanavyohitajika makabati bora, kwa mfano. Nilimwambia kuwa nami kama mwalimu naguswa na moyo wa kujitolea wa watu wa aina yake, kwani sote tuko katika kusukuma gurudumu la elimu kwa jamii. Alifurahi kusikia hivyo.

Jambo la msingi ni kuwa nawasifu walioanzisha maktaba hii, na wale wanaoiendesha. Changamoto iliyopo ni kwa jamii yetu kuboresha taasisi kama hii maktaba. Pesa tunazo. Tatizo ni vipaumbele. Tukiangalia bajeti ya ulabu, kwa mfano, kwa wiki, mwezi au mwaka, ni wazi kuwa tungeweza kuwa na maktaba nzuri katika kila mji.

Tuesday, April 26, 2011

Rais Obama Awasomea Watoto Hadithi


Leo, katika kuvinjari kwenye mtandao wa Facebook, nimeona video ya Rais Obama na familia yake. Wako bustanini wakiwasomea watoto hadithi.

Nimeguswa sana na video hii. Niliwahi kuandika makala kuhusu kuwasomea watoto vitabu. Katika makala hii nilielezea jinsi wenzetu huku Marekani wanavyojali suala hili, kuanzia watu wa kawaida hadi viongozi wa juu kabisa. Hata dakika ile Marekani iliposhambuliwa, tarehe 11 Septemba, 2001, Rais Bush alikuwa darasani na watoto wakisoma kitabu.

Makala yangu ile niliipanua na kuiboresha na imechapishwa katika kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Katika makala hiyo, na kila mara ninapoongelea masuala ya aina hii ya kutokuwa na utamaduni huo kama wenzetu.

Lakini haingekuwa vigumu kuuanzisha na kuujenga utamaduni huo. Ni faraja kuona kuwa wako wengine wenye mawazo hayo hayo, na hapo napenda kumtaja Dada Sophie Kagambo Becker, ambaye ameelezea hayo katika blogu yake.

Monday, April 25, 2011

Msamvu, Morogoro

Blogu yangu hii ni sehemu ya mambo mengi binafsi, zikiwemo kumbukumbu. Leo najikumbusha kuhusu Msamvu, kitongoji cha mji wa Morogoro. Ni kumbukumbu ya ziara yangu ya mwaka jana, ambayo nilishaielezea kidogo katika blogu hii.

Morogoro ina vitongoji vingi, ambavyo sivijui kabisa au sivijui vizuri. Ila nimepata fursa ya kuifahamu Msamvu, maarufu kwa sababu ni kituo kikubwa cha mabasi.


Msamvu ni sehemu ya biashara. Kuna migahawa na vijiduka. Kwa wafanyabiashara ndogo ndogo, wasafiri ni wateja muhimu. Wageni kutoka ughaibuni wanapofika kwetu wanashangaa kuwa basi linaposimama, ghafla linavamiwa na wachuuzi wa kila aina ya bidhaa, ambazo hupitishwa madirishani, kuanzia matunda na biskuti hadi kadi za simu.

Kule mbele, kwenye miti, kuna hoteli na baa nzuri. Nimewahi kutua hapo mara mbili tatu, wakati nikingojea usafiri wa kwenda Dar es Salaam. Ni sehemu nzuri ya kupumzikia.

Thursday, April 21, 2011

Ziara Yangu Shanghai

Mwaka 2003 nilipata bahati ya kutembelea China. Hii ni kati ya ziara ambazo nazikumbuka sana. Nilialikwa kwenda kutoa mihadhara East China Normal University, mjini Shanghai.Mihadhara ilikuwa kama ifuatavyo:

25 Novemba, "My Folklore Research Experience,"
25 Novemba "American Folklore Studies Today,"
26 Novemba, "My Folklore Research Experience"
1 Desemba, "African Folklore Research."

Picha zinazoonekana hapa ni za wanafunzi wa shahada ya juu. Mwalimu wao, ambaye amevaa jaketi jekundu, alinialika niongee na hao wanafunzi darasani kwao kuhusu "My Folklore Research Experience" na vile vile "Women in African Folklore" hiyo tarehe 26Novemba.

Nilifurahi kupata fursa hii ya kubadilishana mawazo na watafiti wa China. Walikuwa na masuali mengi. Huyu bwana aliyesimama pembeni alikuwa katika ngazi ya juu kuliko hao wanafunzi wengine. Wao walikuwa wanasomea shahada ya uzamili, wakati yeye alikuwa katika shahada ya udaktari. Alivyokuwa na masuali mengi magumu na niliongea naye muda mrefu.

Tarehe 27 Novemba, wenyeji wangu, wakiongozwa na huyu mwalimu mwenye jaketi jekundu, walinitembeza hadi kwenye mji wa Suzhou, ambao ni maarufu kwa historia na utalii. Tulifikia Sheraton Suzhou. Kuna vivutio vingi vya utalii Suzhou, kama vile bustani za kale.

Tarehe I Desemba alifika hapo Chuoni mwandishi wa gazeti la "Oriental Morning Post," akiwa na mpiga picha Zhang Dong, akanifanyia mahojiano ya saa nzima kuhusu utafiti wa Folklore, fasihi, na uhusiano baina ya taaluma hizo. Baada ya mahojiano hayo, walihudhuria mhadhara wangu kuhusu "African Folklore Research." Kisha tukafanya tena mahojiano ya saa nzima na nusu. Mwandishi huyu alikuwa makini kwa masuali na nakumbuka aliniulizia hata kuhusu mwandishi J.M. Coetzee wa Afrika Kusini, ambaye alikuwa amepata tuzo ya Nobel wiki chache tu zilizotangulia, mwanzoni mwa mwezi Oktoba. J.M. Coetzee amehamia Australia.

Fursa ya kutembelea China ilikuwa ni jambo la pekee sana kwangu, kutokana na historia ya urafiki baina ya Tanzania na China. Nami nilianza mihadhara yangu yote kwa kukumbushia urafiki huo, ambao ulianza miaka ya mwanzo baada ya Uhuru wa Tanganyika.

Wakati naandaa safari ya China, nilipewa jina la Mchina ambaye anaifahamu Tanzania na Zambia. Aliyenipa jina hili ni profesa katika Chuo cha St. Olaf ambapo nafundisha. Ni profesa wa lugha na fasihi ya China, ambaye ana uzoefu sana na China. Alinielezea habari za huyu Mchina, kuwa alikuwepo Tanzania miaka ile ya ujenzi wa reli baina ya Tanzania na Zambia.

Nilipelekwa nyumbani kwake mjini Shanghai na tuliongea sana. Alikuwa na vinyago vya ki-Makonde nyumbani mwake, na vitu vingine vya aina hiyo. Ni mtu ambaye anaisifu Tanzania na Zambia kwa mambo mengi. Kwa kifupi, ziara yangu ilikuwa nzuri sana, na nitakumbuka daima ukarimu wa wenyeji wangu.

Tuesday, April 19, 2011

Mawaidha ya Mwakilishi Keith Ellison

Leo hapa Chuoni St. Olaf tulitembelewa na mgeni maarufu, Keith Ellison, ambaye ni mwakilishi kutoka Minnesota katika Congress, ambalo ni bunge la Marekani. Keith Ellison ni mu-Islam wa kwanza kuwa mjumbe katika Congress.

Aliongelea changamoto zinazoikabili Marekani na dunia katika mkabala wa kuwepo kwa tofauti za dini.

Kwa kutumia mifano ya Marekani, alisisitiza kuwa watu wa dini mbali mbali tuna uchaguzi wa kufanya. Tunaweza kuchagua kuheshimiana, kuelewana na kujenga dunia ya amani, upendo na mshikamano, au tunaweza kuchagua kuwa na uhasama, ubaguzi, chuki, mfarakano, na migogoro.

Alisema kuwa wahubiri wa dini wana wadhifa mzito. Wanapopanda kwenye mimbari au sehemu nyingine ya kuhubiria, wana ushawishi mkubwa mioyoni mwa waumini. Wana wajibu wa kujua hilo, kwani wanao uwezo wa kujenga umoja na maelewano katika jamii au wanaweza kujenga uhasama na chuki katika jamii.

Alisisitiza wajibu wetu wa kuwaheshimu watu wa dini mbali mbali, na watu wasio na dini. Wote wanastahili heshima, na wala hakuna mwenye haki ya kumshinikiza mwenzake kwenye masuala ya imani za dini.

Hotuba yake iliwagusa sana watu. Kitu kimoja kilichonivutia zaidi ni hoja yake kuwa mtu ukifanya juhudi ya kuifahamu dini kwa kusoma na kutafakari, utagundua kuwa inakupeleka kwenye mtazamo wa maelewano, upendo, kuwaheshimu wanadamu wengine, wawe wana dini au hawana dini.

Aliyoongelea yanatugusa sote. Nilitamani angekuja Tanzania kutoa mawaidha hayo. Hotuba yake HII HAPA.

Monday, April 18, 2011

Twahir Hussein: Wanaharakati Waislam Mmekosea

Blogu hii inatoa fursa ya mawazo ya aina mbali mbali kusikika, sio mawazo yangu tu, bali ya wengine pia. Leo nimeona niweke makala ya Twahir Hussein, ambayo ilichapishwa katika twahirhussein.blog.

Hii sio mara ya kwanza kwa blogu hii kuchapisha maoni ya wa-Islam. Mfano ni huu hapa.

Utafiti na mijadala huru ni njia muafaka ya kuelimishana na kutafuta ukweli. Blogu hii inaheshimu mijadala, kama nilivyosema hapa. Basi tumsikilize Twahir Hussein, msomi mu-Islam na mhadhiri katika chuo kikuu.

----------------------------------------------------------

Wanaharakati waislamu mmekosea

Na Twahir Hussein

Majuma kadhaa yaliyopita uliwasilishwa muongozo wa waislam kuelekea uchaguzi mkuu 2010. Muongozo huo, pamoja na mambo mengine kwa kiasi kikubwa umejikita katika kuwakumbusha waislam yale ambayo wamekuwa wakiyakabili tangu baada ya uhuru mpaka miaka ya hivi karibuni katika nyanja mbalimbali za kimaisha kama vile siasa, elimu, uchumi na kadhalika.

Aidha, kwa undani zaidi, muongozo huo umesadifu kinaga ubaga katika kuwasilisha hisia,fikra na utashi binafsi wa waandishi.

Kilichotustaajabisha waumini wengi wa dini ya kiislam ni ule ukiritimba wa mitazamo ya kisekula iliyowatawala waandishi wa muongozo huo katika jambo la dini. Waandishi wameshindwa kabisa kuzitambua tunu na fanaka za maangalizo na mafunzo ya vitabu vitakatifu vya dini yao katika medani za kijamii.

Binafsi, nimeusoma muongozo huo kwa zaidi ya masaa 360. Kwa wazi kabisa muongozo huo umejenga taswira ya uchochezi miongoni mwa waislamu na jamii ya watanzania kwa ujumla.

Nikaona si jambo jema kunyamazia sampuli hii ya ufisadi wa maandishi. Mimi ni muumini wa dhati wa dini ya kiislamu. Kwa dhati kabisa sijapata kuona wala kusikia kwamba uislamu unafundisha uchochezi utakaoleta aina Fulani ya machafuko au kutokuwa na maelewano miongoni mwa wanajamii katika jamii yoyote ile iwayo.

Na sababu kuu ya uchochezi huu ni kukosekana kwa nuru ya demokrasia katika nyoyo za waandishi wa muongozo huo. Kwamba muongozo umekuwa ni mkusanyiko fikra za kikundi cha watu wachache ambao wanabainika kuwa na ajenda binafsi za siri. Jambo ambalo si la busara hata kidogo mbele ya uislamu na jamii kwa ujumla. Dini ya kiislamu imezuia na inaendelea kuonya viakali kabisa mtu au watu fulani kuchukua dhima ya kufikiri kwa niaba ya wengine. Kwamba, waandishi wa muongozo huo wameonyesha dhamira ya wazi ya kuwadharau waislamu kwa kuwaona ni wavivu wa kufikiri na kutoa mawazo.

Kimsingi, muongozo huo kabla ya kuandikwa ulipaswa kukusanya mawazo ya waislamu kitaifa. Kwamba, waandishi wa muongozo walipaswa kutumia njia za utafiti katika kukusanya maoni kuanzia ngazi ya kata,wilaya hadi mkoa.

Njia za maswali katika vikaratasi, usaili, na vikundi-mjadala(focus group discussion) zilipaswa kutumika katika kukusanya mawazo ya waislamu kuhusu dira yao katika kuelekea uchaguzi mkuu 2010.

Mawazo hayo ndiyo yangeweza kuunda kitu ambacho kinaitwa muongozo. Zoezi hili lingekuwa gumu sana lakini ndio msingi wa haki na uwakilishi huru. Hii ni kwasababu kila muislamu ana maono,fikra,utashi na upembuzi wake binafsi katika kuyaangalia na kuyaendea mambo mbalimbali katika duru za kijamii.

Waislamu wa Tanzania bado hawalazimiki kujifungamanisha na mrengo wa siasa za aina fulani ili kukidhi mahitaji yao kama ambavyo waandishi wa muongozo wanainisha. Badala yake watabakia kuwa watu wa kundi maslahi.

Waandishi wa muongozo wanatiririsha maelezo kwamba CCM imelikumbatia kanisa katoliki ili kuwahujumu waislamu kupitia serikali. Hapa waandishi wanajaribu kuifitinisha serikali na waislamu, na kuwafitinisha waislamu na wakatoliki. Jambo hili ndugu zangu waislamu mlioandika muongozo si zuri. Huu ni uchochezi. Mnawaongoza waislam katika vita kali sana ambayo hamtoweza kuizima.

Na hatari zaidi waandishi wa muongozo wamelemazwa kabisa akili na maneno ya kilaghai ya kitabu cha padri aliyefukuzwa na kanisa katoliki,bwana Sivalon. Ukweli ni kwamba maelezo ya sivalon yalikuwa na utashi binafsi,hayakutafitiwa na yamepitwa na wakati. Ilikuwa ni presha tu. Ukweli wa hili unathibitishwa na kifungu kifuatacho cha muongozo huo kilichopewa anuani ya “mapinduzi ya kanisa” ambacho kinanukuu melezo ya Sivalon kama ifuatavyo:

“Padri sivalon anafafanua kuwa viongozi wa kanisa katoliki walikuwa katika nafasi nzuri ya kuelekeza ujamaa na viongozi wa serikali waliwatambua hivyo. Kwa kutumia mapinduzi haya ya kimya kimya kanisa limefanikiwa kuitumia mno serikali kwa maslahi yake, kiasi cha kufunga mikataba mikubwa na ya kudhulumu raia wa jamii ya wengine wasiokuwa wakristo. Mfano hai wa hili ni ule makataba wa mwaka 1992 ujlikanao kama memorandum of understanding between Christian council of Tanzania and Tanzania Episcopal conference and the united republic of Tanzania (MoU)”

Kifungu hiki kimenukuliwa kwa dhamira na dhana ileile ya uchochezi ya waandishi wa muongozo. Msingi wa kifungu hiki si wa kweli. Kwanini? Kwasababu: mkataba wa MoU uliwanufaisha na unaendelea kuwanufaisha watanzania wa dini zote.

Ukweli ambao waandishi wa muongozo wa waislamu walipaswa kuuainisha kuhusu mkataba wa MoU ni kwamba kwa wakati ule tayari makanisa kupitia wazungu ambao ni wafadhili wao waliweza kujenga hospitali kubwa kama vile KCMC, Bugando na nyinginezo.

Hospitali hizi dhahiri zimekuwa zikihudumia jamii kubwa ya watazania. Ili kukidhi gharama za uendeshaji zilihitaji msaada wa serikali. Na kiutaratbu serikali haiwezi kutoa msaada kama raia mwema anavyotoa msaada kwa kwa ombaomba barabarani. Lazima pawe na mkataba. Hii ndio kusema baada ya mkataba wa MoU haspitali hizi zikaidhinishwa kuwa za rufaa.

Waislamu ni miongoni mwa watu wanaopata huduma na ajira katika hospitali za KCMC,BUGANDO na hospitali nyinginezo za misheni. Hili hakuna muislamu atakayethubutu kulipinga.labda asiyemuogopa Allah.

Lakini waandishi wa muongozo huo wameficha kabisa kuainisha hili! Ni ajenda gani hii kama si uchochezi? Ajenda hii inajenga mustakabali gani wa waislamu na Taifa?

Rejea pia kifungu hiki “waislamu wengi hunyimwa huduma stahiki na kuzuiliwa fursa muhimu kwa sababu tu ya uislamu wao. Ubaguzi huu umepelekea taasisi nyingi za umma, kwa mfano wizara ya elimu, baraza la mitihani, bodi ya shirika la taifa la utangazaji(TBC) na TRA kuwa na twaswira ya parokia. Katika maofisi ya serikali waislamu hunyimwa uhuru wa ibada na hasa swala, ikiwemo ijumaa na kuvaa mavazi ya stara”

Kifungu hiki pia ni cha kichochezi. Waandishi wameficha kuweka wazi orodha ya majina ya watumishi yanayounda taswira hiyo ya kiparokia. Pili, mheshimiwa rais Jakaya Kikwete aliepuka uteuzi wa aina hiyo. Kwa mfano, wizara ya elimu inaundwa na waziri(muislamu), manaibu waziri wawili(mkristo na muislam), Katibu mkuu(muislam) na naibu katibu mkuu(mkristo). Parokia inajengwaje hapo? Halikadhalika, baraza la mitihani, bodi ya shirika la taifa la utangazaji(TBC) na TRA muundo ni wa aina hiyo.

Aidha kuhusu kunyimwa uhuru wa kuvaa hijabu, waadishi wa muongozo wa waislam wanazidi kutia petroli moto wa uchochezi. Hebu ndugu yangu muislamu na mtanzania mwingine yeyote mtazame waziri Hawa Ghasia;havai hijab? Waziri Mwantum Mahiza havai hijab? Waziri Batilda Buriani havai hijab; halikadhalika wanafunzi waislamu vyuoni na mashuleni hawavai hijab? Labda ni idara za serikali ipi ambazo waandishi wa muongozo wanazikusudia?

Uchochezi si jambo jema hata kidogo. Kwa nini waandishi wa muongozo wanathubutu kupandikiza mbegu hiyo kwa jamii ya waislamu? Rejeeni kwa Mola wenu. Kaeni chini mtubu dhambi hiyo. Dhambi yenu italitafuna Taifa.

Mwisho niseme tu hakuna haja ya kutumia mbinu ya uchochezi ili kuwachota waislamu na kuwamimina katika chama fulani cha upinzani. Hii si mbinu muafaka. Waacheni wanasiasa wapige kampeni na kunadi sera na ilani za vyama vyao kisha waislamu na watanzania wengine waamue.

Mimi nimesikitika sana kuona waandishi wa muongozo wa waislamu wananakili vvipengele vya ilani ya chama Fulani cha siasa kuwa vipengele vya muongozo wa waislamu. Ni kufilisika gani huku!

Mathalan, katika muongozo huo, vipengele vya taswira ya uchaguzi mkuu uliopita, dhana ya uchaguzi, uhuru wa kutoa maoni, tumefikaje hapa tulipo,maadili, elimu, afya,kilimo, fedha na uwezeshaji, maisha bora, sheria, umoja na amani, muungano wa Tanganyika na Zanzibar, uwakilishi wa umma, hadaa za uchaguzi na dira ya uchaguzi, waandishi wa muongozo wamenakili bila woga sera zilizoainishwa katika ilani na katiba ya chama Fulani cha siasa! Dhamira hasa ni kuwalazimisha waislam waamini tu CCM ni mbaya na badala yake wawe chama Fulani cha upinzani. Huu si mkakati mwema wa kutamalaki maslahi ya waislamu na Taifa, na wala si mtindo huru wa kupiga kampeni.

Ningewashauri waandishi wa muongozo kwa waislam waitishe mkutano na waandishi wa habari watangaze kuufuta muongozo huo na badala yake watangaze kuandaa muongozo mwingine mpya ambao utakuwa wa kidemokrasia, huru na wenye kujenga mustakabali mwema wa waislamu na watanzania wengine .

Mwandishi wa makala haya ni muumini wa dini ya kiislam, mwalimu wa chuo kikuu na pia ni msomaji wa gazeti la Tanzania Daima. Anapatikana katika simu nambari 0713 111058

Friday, April 15, 2011

Hatimaye, Bia Zitazinduliwa Ikulu

Ni juzi tu hapo niliandika makala kuhusu jinsi wa-Tanzania wanavyowajibika katika unywaji wa ulabu. Makala hiyo ni "Kazi ya Kunywa". Katika kuhitimisha, nilitamka kuwa, kwa mwendo tunaokwenda, huko mbele ya safari ulabu utakuwepo hadi shuleni na Bungeni.

Ni kama vile niliota. Wiki hii wabunge wa Tanzania wameweka historia kwa kuzindua vinywaji vikali huko Dodoma. Soma hapa.

Nchi yetu ni ya pekee. Tunauenzi ulabu kiasi hiki, ingawa unasababisha au kuchangia matatizo mengi, kuanzia ajali barabarani zinazosababisha vifo vingi na watu wengi kuumia, uharibifu wa mali, magomvi katika jamii, kuharibika akili na matatizo ya kisaikolojia.

Tunakwenda kwa kasi na ari kiasi kwamba siku si nyingi kuanzia sasa, bia zitakuwa zinazinduliwa Ikulu. Na siku ya kuzindua bia itakuwa ni ya kukumbukwa ki-Taifa.

Enzi za uongozi wa Mwalimu Nyerere, wabunge wangekuwa wanazindua maktaba, si ulabu. Hakuna mtu aliyethubutu kufanya mambo yanayofanyika leo. Lakini mambo ndio hayo: akiondoka paka, panya hutawala.

Monday, April 11, 2011

Ugumu wa Kusoma Vitabu vya Dini Isiyo Yako

Hapo juzi, niliandika kuwa nasoma vitabu vya dini mbali mbali. Lakini jambo moja ambalo sikuongelea ni kuwa inaweza kuwa vigumu kufikia uamuzi wa kusoma vitabu hivyo. Napenda kuongelea uzoefu wangu.

Nilizaliwa katika familia na jamii ya wa-Katoliki. Dini pekee iliyokuweko katika eneo langu, kwa maili nyingi kuzungukia eneo hilo, ilikuwa ni u-Kristo, madhehebu ya Katoliki. Watu pekee ambao hawakuwa wa-Katoliki ni wale wachache ambao walikuwa hawajabatizwa.

Sikumbuki kama niliwahi kusoma kitabu cha dini nyingine yoyote au dhehebu jingine lolote zaidi ya u-Katoliki. Hata niliposoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuanzia mwaka 1973, nikaanza kufundisha hapo mwaka 1976, katika idara ya "Literature," sikumbuki kama nilisoma kitabu cha dini nyingine.

Lakini nilipokuwa nasomea shahada ya juu katika Chuo Kikuu Cha Wisconsin-Madison, 1980-86, nilipata fursa ya kufahamiana vizuri na mwanafunzi mwenzangu mu-Islam kutoka Sudan. Huyu alikuwa mmoja wa marafiki zangu.

Alipoona nina hamu ya kufahamu kuhusu u-Islam, alifanya mpango akanitafutia nakala ya Quran ambayo ni tafsiri ya Abdullah Yusuf Ali. Aliniambia kuwa hiyo ndio tafsiri inayotambuliwa na kuheshimiwa zaidi.

Hiyo ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuishika Quran. Kabla ya hapo, Quran ni kitabu nilichokuwa nakisikia tu, na hata kukiogopa. Tuna umbumbumbu sana nchini mwetu, hata kufikia kuwa na hofu za namna hiyo. Sikutegemea ningethubuku kuishika Quran. Lakini baada ya kupewa namna hii, tena na mu-Islam niliyemfahamu kuwa amebobea katika dini yake, hofu ilitoweka.

Nilianza kuisoma. Kitu kilichonishangaza tangu kurasa za mwanzo, ni jinsi masimulizi yake yanavyofanana na yale ya "Agano la Kale" katika Biblia. Nilishtuka. Suali lililokuwa linazunguka kichwani mwangu ni je, kwa nini watu tunaamini kuwa vitabu hivi ni tofauti sana, kama mchana na giza? Hilo limebakia suali ambalo natafuta jibu lake, na labda hatimaye nitapata jibu lake.

Baada ya kuja huku Marekani, mwaka 1991, kufundisha masomo ya fasihi, nimejikuta nikifundisha maandishi kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Mengi yamekuwa ni maandishi ya wa-Islam kutoka nchi kama Misri, Senegal, Mali, Somalia, Pakistan, na India.

Mara kwa mara, katika hadithi zao, mambo ya u-Islam yanajitokeza. Kwa hivi, ili niweze kuyaelezea vizuri katika ufundishaji wangu, imenibidi nijifunze zaidi kuhusu u-Islam. Mfano ni riwaya ya Twilight in Delhi, kama nilivyoelezea hapa.

Katika kufundisha somo hilo hilo la fasihi, nimejikuta nikifundisha fasihi ya nchi kama India, ambako dini kuu ni u-Hindu. Katika maandishi hayo, na hata baadhi ya maandishi kutoka sehemu kama visiwa vya Caribbean, dini hii inajitokeza mara kwa mara. Kwa hivyo, imenibidi kusoma kuhusu dini hii ili niweze kuelezea yale yaliyomo katika fasihi.

Kwa kifupi, nafurahi jinsi mambo yalivyotokea katika maisha yangu, hadi kunifikisha hapa nilipo, katika hali ambayo nina motisha na pia fursa ya kusoma maandishi ya dini mbali mbali.

Lakini, bila mazingira hayo, huenda ningekuwa bado nimejifungia katika dini yangu tu. Huenda ningekuwa bado naogopa kuvigusa vitabu vya dini nyingine. Huenda ningekuwa naogopa kukiuka au labda "kuchafua" imani ya dini yangu.

Naamini hofu za namna hii wanazo wengine pia. Lakini, nashukuru kuwa sioni tatizo lolote katika hayo ninayofanya, wala imani yangu katika dini yangu haijawahi kutetereka. Badala yake, naona nimejifunza kuziheshimu dini za wengine.

Sunday, April 10, 2011

Kuwalea Watoto Katika Usomaji Vitabu

Huwa natafakari sana suala la kuwalea watoto katika usomaji vitabu. Mtoto huyu hapa kushoto alikuwa anaangalia vitabu vyangu katika maonesho ya elimu na ajira yaliyofanyika mwaka jana Diamond Jubilee Hall, Dar es Salaam. Hiki kitabu alichoshika kinaitwa CHANGAMOTO.

Katika matamasha ya aina hiyo, hasa ya vitabu, navutiwa ninapowaona wazazi wamekuja na watoto wao. Huku Marekani ni jambo la kawaida.

Katika tamasha hilo la elimu na ajira Dar es Salaam, nilimwona mama mmoja amekuja na mtoto wake. Mama huyu, anayeonekana katika picha hii, alikuja kwenye kibanda changu, ambapo nilikuwa nimeweka vitabu vyangu, akaniuliza masuali kadhaa, huku mwanawe akisikiliza. Niliongelea masuali yake, kuhusu shughuli zangu katika elimu na uandishi, na kadhalika. Ilikuwa ni fursa kwangu pia ya kumhamasisha mtoto wake. Sitasahau mfano alioonyesha mama huyu. Wahenga walisema, mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.

Picha hii ilipigwa Minneapolis, Oktoba 4, 2008, wakati wa sherehe ya kumbukumbu ya Uhuru wa Nigeria. Mama huyu m-Nigeria alikuja kwenye meza yangu ya vitabu na huyu mwanae. Tuliongea, wakaangalia vitabu vyangu na kuvinunua. Kutokana na mfano wa mzazi, mtoto anapata ufahamu kuwa vitabu ni muhimu.

Saturday, April 9, 2011

Hapa Kwetu: Akina "Anonymous" Sasa Ruksa

Tangu nilipoanzisha blogu yangu hii, sikupenda niruhusu akina anonymous kuchangia. Nilielezea duku duku zangu katika makala hii.

Lakini leo nimerekebisha mambo, kufuatia ombi la mdau mmoja ambalo amelitoa kwenye blogu ya Mwenyekiti Mjengwa. Nimeguswa na lugha ya kiungwana aliyotumia huyu anonymous. Kilichobaki sasa ni kuona hali itakavyokuwa.

Friday, April 8, 2011

Nasoma Vitabu vya Dini Mbali Mbali

Kati ya mambo ya manufaa kabisa maishani ni kujielimisha. Nami husoma vitabu kila siku kama njia mojawapo ya kujielimisha. Pamoja na vitabu vya taaluma mbali mbali, hadithi, mashairi, na kadhalika, hupenda kusoma vitabu vya dini.

Nina vitabu vya dini mbali mbali, hasa u-Hindu, u-Islam, na u-Kristu. Nina vitabu kama vile Bhagavad-Gita, Upanishads, Quran, na Biblia. Nina vitabu kuhusu watu muhimu wa dini hizo, kama vile Yesu Kristu, Muhammad na Swami Vivekananda. Vyote hivyo ninavipitia, angalau mara moja moja.

Mimi ni m-Katoliki; habari ndio hiyo. Kwa msingi wa dini yangu, nawajibika kuwajali na kuwapenda wanadamu wote. Yesu alifafanua amri kuu kuliko zote kuwa ni kumpenda Mungu kwa uwezo wetu wote, akili yetu yote, na nafsi yetu yote; kumpenda jirani yetu vile vile, na kuwapenda maadui zetu vile vile. Huu ndio mtihani aliotuachia Yesu.

Sasa kwa vile ukweli ndio huo, ninajiuliza ni njia ipi ya kufuata ili niweze kufaulu mtihani huo. Nimeamua kuwa ni wajibu kujielimisha: kuwafahamu wanadamu, maisha yao, fikra zao, na imani zao. Ni wajibu kuzifahamu dini zao. Naamini tungechangia kujenga mahusiano mema duniani iwapo tungekuwa na utamaduni huu wa kuviheshimu na kuvisoma vitabu vya dini zetu na vile vya dini za wenzetu. Ni muhimu vile vile kusoma vitabu vya wale wasioamini dini, na kuwaheshimu.

Wednesday, April 6, 2011

Mijadala ya Dini ni Muhimu

Watu wengi katika jamii yetu wanasema kuwa tusiendekeze mijadala ya dini. Wanasema kuwa ni tishio kwa amani na maelewano. Ninapenda kutafakari suala hilo.

Binafsi, naamini kuwa watu wenye akili timamu wanaweza kujadili mada yoyote bila matatizo. Watu wa aina hiyo wanajua kuwa katika mjadala wanachopaswa kufanya ni kutoa hoja, kusikiliza hoja, na kupinga hoja kwa hoja.

Watu wenye akili timamu wanafahamu kuwa, katika mjadala, kila mtu ana uhuru wa kuelezea fikra zake na mtazamo wake, na ana haki ya kusikilizwa. Na kila mtu ana wajibu wa kusikiliza hoja na mtazamo wa wengine.

Suala la mijadala, kwa watu wenye akili timamu, ni suala lililojengeka katika haki, uhuru, na wajibu, kama nilivyoelezea hapo juu. Wajibu huo ni pamoja na wajibu wa kuheshimiana katika hiyo mijadala. Kwa maana hiyo, mada yoyote inaweza kujadiliwa na watu wenye akili timamu, iwe ni siasa, uchumi, au dini.

Kuna pia wajibu wa kujielimisha. Mbali ya kwenda shule, au kusoma vitabu, mijadala ni njia mojawapo muhimu ya kuelimishana. Siamini kama dini zetu zinatutegemea tuwe waumini mbumbumbu. Naamini kuwa Muumba mwenyewe anatutegemea tuwe waumini tunaojibidisha kuzifahamu dini zetu. Kwa hivi, kusoma kuhusu dini na kushiriki mijadala kuhusu dini ni wajibu.

Sasa tatizo liko wapi, inapokuja kwenye dini, hadi watu waseme kuwa tusiendekeze mijadala ya dini? Tatizo si mada, bali vichwa vya wahusika. Labda ni wajinga au walevi. Hili ndilo tatizo. Wajinga au walevi wakipewa mada yoyote, uwezekano wa kushikana mashati ni mkubwa. Hata kama mada ni kuhusu umuhimu wa kujenga hospitali au kupeleka watoto shule, wajinga au walevi wanaweza kushikana mashati.

Suali ni je, kwa nini mada yoyote iwe ni hatari kujadiliwa? Na tukisema leo tusijadili dini, huenda kesho tutasema tusijadili siasa, na keshokutwa tusijadili elimu, na kadhalika. Kwa nini mada yoyote iwe ni hatari kujadiliwa? Inamaanisha kuwa wa-Tanzania ni wajinga au walevi?

Kama ni walevi, tupunguze ulabu. Kama ni wajinga, kinachopaswa kufanya ni juhudi za kufuta ujinga, ili tufikie mahali wa-Tanzania wawe na akili timamu kama nilivyoelezea hapo juu. Tunahitaji maandalizi ili mada kama dini ziweze kujadiliwa sawa na mada zingine, kuchangia elimu na maelewano.

Tuesday, April 5, 2011

Mwalimu Nyerere Aongelea Uongozi, 1995

Suala la uongozi lilikuwa moja ya vipaumbele vya Mwalimu Nyerere maisha yake yote. Tunasikia, kwa mfano, jinsi alivyolichukulia suala hili alipokuwa kiongozi wa wanafunzi katika shule ya Tabora. Wakati wa kupigania Uhuru na baada ya Uhuru aliliongelea suala hili tena na tena, kama vile katika "Azimio la Arusha" na "Mwongozo."

Mwalimu aliliongelea suala hili tena, kwa masikitiko, katika kitabu chake cha "Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania," akiihofia hatima ya Tanzania kutokana na uongozi mbovu wa CCM. Niligusia suala hilo katika makala hii hapa. Hata baada ya kuandika kitabu hiki, Mwalimu aliendelea kuongelea suala la uongozi. Hebu msikilize katika hotuba yake hii ya mwaka 1995.

Saturday, April 2, 2011

Kitabu Kumhusu Hemingway

Leo nilipita tena katika duka la vitabu la Half Price Books la mjini Apple Valley. Kama kawaida, kutokana na ushabiki wangu wa maandishi ya Ernest Hemingway, nilianza kwa kwenda moja kwa moja kwenye sehemu vinapouzwa vitabu vyake: vile alivyoandika yeye mwenyewe au vilivyoandikwa juu yake.

Hadi sasa nina vitabu vingi vya Hemingway, lakini kila ninapoona kitabu kipya, au ambacho sina, napenda niwe nacho. Leo nimevikuta vitabu kadhaa vya aina hiyo, ila nilivutiwa zaidi ni Hemingway in Cuba, kilichoandikwa na Norberto Fuentes.

Sikuwa nimekiona kitabu hiki kabla. Nilikiangalia, nikaona kina utangulizi ulioandikwa na Gabriel Garcia Marquez. Hapo niliishiwa nguvu, kwani Marquez ni mmoja wa waandishi maarufu kabisa duniani.

Mawazo mengine yakafurika akilini mwangu. Ninajua kuwa Marquez ni rafiki mkubwa wa Fidel Castro, Castro ambaye watu wa kizazi changu tumemwenzi tangu tulipopata Uhuru. Najua pia kuwa Castro ni mshabiki wa maandishi ya Marquez. Cha zaidi ni kuwa najua kuwa Hemingway katika uhai wake alifahamiana na Castro, na pia kuwa Castro amekuwa shabiki wa Hemingway tangu miaka ile.

Pamoja na yote hayo, katika kusoma utangulizi wa Marquez, nimevutiwa kwa namna ya pekee na maelezo yake kuwa Hemingway ni mwandishi ambaye Castro anamsoma kuliko mwandishi mwingine yeyote. Hata anapozunguka nchini kwenye safari rasmi, Castro anakuwa na maandishi ya Hemingway. Marquez anatueleza kuwa Castro anaweza kuelezea maandishi ya Hemingway na kujibu masuali kwa uhodari wa kiwango cha juu.

Mimi kama shabiki mkubwa wa Hemingway najiandaa kukisoma kitabu hiki. Nimekipitia juu juu, nikaona kina mengi mapya kwangu, ingawa kilichapishwa mwaka 1984. Nina vitabu vingine vinavyoelezea maisha ya Hemingway Cuba, lakini hiki cha Fuentes kinazama zaidi katika maelezo yake.

Kwa wale ambao hawajui, Hemingway, ambaye ni m-Marekani aliyezaliwa mwaka 1899 karibu na Chicago, aliishi Cuba miaka 22. Hata alivyosafiri kuja Afrika Mashariki, mwaka 1933 na mwaka 1953, alitokea Cuba, na baada ya safari zake alirejea Cuba. Kuna vitu kadhaa alivyovipata Kenya na Tanganyika, kama vile vichwa vya wanyama aliowawinda, mikuki, na kinyago cha ki-Makonde. Vyote viko katika nyumba yake ya Finca Vigia, ambayo iko nje ya mji wa Havana, ambayo serikali ya Cuba inaihifadhi kwa heshima kubwa na vitu vyote vya Hemingway vilivyokuwamo humo, ingawa yeye alishaondoka na kurejea Marekani, ambako alijiua kwa bunduki mwaka 1961.

Cuba inamwenzi Hemingway kwa namna ambayo ingepaswa sisi wa-Tanzania tuwe tunawaenzi waandishi wetu kama vile Mgeni bin Faqihi wa Bagamoyo, aliyetunga Utendi wa Rasi l'Ghuli, au Shaaban Robert.