Friday, April 27, 2018

Madaktari Wanafundishia Kitabu Hiki

Nilivyoandika kitabu changu Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, sikuwazia kingetumika kwa namna nyingi kama ilivyotokea baadaye. Kilichonishtua zaidi ni pale waalimu wa uuguzi wa chuo cha Gustavus Adolphus walipoamua kukitumia kufundishia, wakaanza, kila wanapofundisha kozi hiyo, kunialika kuongea na wanafunzi.

Baada ya muda si mrefu, Dr. Randy Hurley mwanzilishi na mhusika mkuu wa  na programu ya hospitali ya Ilula, mkoani Iringa, alinialika kuhutubia mkutano wa mwaka wa wadau wa hospitali hiyo. Ulikuwa ni mkutano wa kuchangisha fedha za kuendelezea programu. Hapo ndipo nikajua kuhusu programu ya kuelimisha wauguzi ambayo inafanyika Ilula, ikiwahusisha wa-Marekani na wa-Tanzania.

Nilijua kuwa wanatumia kitabu changu, bali sikuwa na taarifa zaidi. Lakini siku chache zilizopita nimeona jinsi kitabu hicho kinavyotajwa katika silabasi mpya ya kozi yao. Wanafunzi wanahimizwa kukisoma. Kwa kuwa mimi si mtaalam wa masuala ya uuguzi na matibabu, nilijiuliza masuali, kwa sababu baadhi ya mambo niliyoandika kitabuni ni tofauti na taaluma ya uuguzi na matibabu. Dukuduku yangu hii niliigusia katika blogu hii.

Hatimaye, nilikuja kuelewa vizuri mantiki ya madkatari na waalimu wa uuguzi kukitumia kitabu hiki. Ni kwa sababu kinaelezea utamaduni hauwezi kutenganishwa na masuala ya matibabu ba uuguzi. Madaktari na wauguzi wanatakiwa kuwafahamu wale wanaowahudumia, katika vipengele kama jadi, tabia, matarajio, miiko, imani, na hisia. Ni muhimu kwa muuguzi au daktari kuyafahamu na kuyazingatia wakati anatoa huduma. Kwa hivyo, sasa ninavyosikia kitabu kinatumiwa na watu katika taaluma hizo, sina masuali bali ninashukuru kwamba nimeweza kutoa mchango fulani wa manufaa.

Saturday, April 21, 2018

Mdau Amechagua Kitabu

Jana nimeona taarifa iliyonigusa kwa namna ya pekee. Mdau ameweka mtandaoni picha inayoonekana kushoto, akiwa ameambatanisha ujumbe: "Decided to bring some required reading with me." yaani anasema ameamua kubeba vitabu muhimu vya kujisomea. Hakusema kama anasafiri, lakini ujumbe wake unaashiria hivyo.

Niliguswa kuona kitabu changu Africans and Americans: Embracing Cultural Differences ni kimojawapo alichochagua, nikaandika "I am humbled that you have my "Africans and Americans" book on your list," yaani "nimeishiwa nguvu kuona kuwa umetaja kitabu changu katika orodha yako." Jibu aliloandika ni "Yes! I'm learning a lot. It's funny too. Thanks for the enlightenment," yaani "Ndio! Ninajifunza mengi. Kitabu kinachekesha pia. Asante kwa uelimishaji."

Nimeguswa kwa namna ya pekee kwa sababu mdau huyu, ambaye anaonekana nami pichani hapa kushoto, ni mtu mwenye ushawishi katika jamii, kama nilivyowahi kuelezea katika blogu hii. Ninafarijika kuwa kitabu changu ambacho nilikichapisha mwaka 2005 bado kinafanikisha malengo niliyokuwa nayo wakati nilipokuwa ninakiandaa na kukiandika. Lengo kuu lilikuwa ni kuwaelimisha watu, hasa wa-Afrika na wa-Marekani, kuhusu tofauti za tamaduni zao, iwe ni kinga ya kuzuia migongano na kutoelewana. Ila, kama huyu mdau anavyosema, kitabu hiki, pamoja na kuwa kinaelimisha, ni burudani pia.

Ninaweka taarifa hii hapa katika blogu yangu, kwa sababu hapa ni mahali ninapotunzia kumbukumbu zangu, kama nilivyowahi kuelezea.

Monday, April 16, 2018

Tamasha la Kimataifa Rochester Lawadia

Tarehe 28 Aprili, Rochester International Association (RIA) itafanya tamasha la kimataifa. Tamasha hilo hufanyika kila mwaka. Nitashiriki nikiwa na vitabu vyangu na nitaongelea shughuli zangu kama mwalimu na mtoa ushauri wa masuala ya tamaduni.

Ninaona heshima kuwa mwanabodi wa bodi ya RIA, na kushiriki kupanga mipango na matukio yenye maana na umuhimu katika dunia ya leo ambayo inazidi kuwa kijiji.

Sunday, April 15, 2018

Mialiko kwa Mwandishi wa Kitabu

Kutokana na mawasiliano kutoka kwa waandishi chipukizi Tanzania ninafahamu kuwa hao ni miongoni mwa wasomaji wa blogu yangu hii ambamo ninaandika mara kwa mara kuhusu vitabu. Mbali na kuviongelea vitabu, nimekuwa nikiandika kuhusu uandishi, uchapishaji, na uuzaji wa vitabu kutokana na uzoefu wangu.

Leo ninapenda kuongelea kipengele cha mialiko kwa mwandishi wa kitabu, jadi ninayoiona hapa Marekani, mwandishi kualikwa kuzungumza sehemu mbali mbali baada ya kuchapisha kitabu. Mada hii nimeigusia kwa kiasi fulani katika blogu hii Hata hivyo, nimeona niongezee neno.

Kama wewe ni mfuatiliaji wa blogu yangu hii, utakuwa unafahamu kuwa ninapata mialiko mara kwa mara kuongelea mada zinazohusiana na vitabu vyangu: Matengo Folktales na Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Suali ni je, kwa nini watu wanialike badala ya wao kusoma tu nilichoandika? Wananialika nikawasomee?

Jibu ni hapana. Kinachowafanya wanialike ni kutambua kwao, baada ya kusoma kitabu, kwamba wana mambo yatokanayo na yale yaliyomo kitabuni ambayo wangetaka kuyafahamu zaidi. Kitabu changu si kwamba kinajitosheleza, bali kina madokezo muhimu. Ni chachu ya dukuduku kwa wasomaji. Hata kama hakijitoshelezi, wanavutiwa na mwelekeo wa fikra. Hiyo ni sababu muhimu ya kunialika nikazungumze nao.

Wengine wakishasoma kitabu, wanakuwa na imani kwamba ninaweza kuwasaidia mawazo juu ya mipango wanayotaka kutekeleza au mambo yanayowakabili. Kwa mfano, viongozi wa kampuni au taasisi wanaona kwamba ninaweza kuwasaidia katika kuzielewa na kuzitatua changamoto zitokanazo na kuwa na timu ya watu wa tamaduni mbali mbali. Mfano ni nilivyoalikwa RBC Wealth Management.

Kuhusu kitabu cha Matengo Folktales, watu wanataka kufahamu zaidi juu ya utamaduni wa kusimulia hadithi ulivyo Afrika na pia wanataka kusikiliza hadithi zinavyosimuliwa. Ndivyo ilivyokuwa nilipoalikwa chuo kikuu cha St. Benedict/St. John's na pia maktaba ya Redwing.

Kwa upande wa Tanzania, jadi hii ya kuwaalika waandishi kuzungumzia uandishi na vitabu ingekuwa na manufaa kama ilivyo Marekani. Waandishi wangekuwa wanaielimisha jamii uzoefu wao katika vipengele mbali mbali, kama vile jinsi walivyopata wazo la kuandika au walivyoanza kuandika, mchakato wa uandishi, ugumu au urahisi wake, vipingamizi, uchapishaji, uhusiano na wachapishaji, wasomaji, wahakiki, na wauzaji wa vitabu. Waandishi wangetumia fursa hizi kutoa ushauri kwa waandishi chipukizi.

Katika mkutano na mwandishi, vitabu vya mwandishi vinaweza kuwepo, ili wahudhuriaji wanunue. Huu ni utaratibu unaofanyika sana hapa Marekani. Ni njia nzuri ya vitabu kuifikia jamii. Vile vile, kwa uzoefu wangu hapa Marekani, uwepo wa mwandishi na jinsi anavyojieleza, kunawavutia watu kununua kitabu. Kitu kingine kinachovutia ni kusainiwa kitabu na mwandishi, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii, katika kubadilishana mawazo na mwanablogu Christian Bwaya.

Friday, April 13, 2018

Taarifa Tatu Kuhusu Kitabu Changu

Blogu hii ni mahali ambapo ninajiwekea kumbukumbu zangu, sambamba na mambo mengine. Jana na leo zimekuwa siku za pekee, kwani nimefikiwa na taarifa tatu kuhusu kitabu changu Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Jana jioni, nilikutana na bwana moja mwenye asili ya ki-Somali aliyejitambulisha kama kiongozi mojawapo wa shule za Minneapolis. Tulipotambulishwa, alianza kunielezea kuwa alishasoma kitabu changu, akagusia jambo mojawapo analolikumbuka kuhusu dhana ya uzuri wa maumbile yetu. Huo ulikuwa ni ujumbe moja kuhusu kitabu changu.

Ujumbe mwingine nimepata leo kutoka Nairobi kwa muasisi na mkurugenzi wa taasisi iitwayo IIHT Tulifahamiana alipokuwa anafanya kazi jimboni Illinois hapa Marekani baada ya kuhitimu shahada ya uzamifu. Aliwahi kuendesha semina kwa washiriki yapata 100. Alikuwa ameagiza nakala za kitabu changu kwa washiriki wote wa semina na alinialika kuhutubia. Baada ya kupoteana kwa miaka yapata kumi, nilimtafuta mtandaoni. Nilimwandikia kumsalimia, naye ameandika kuwa ananikumbuka na kuwa anatumia kitabu changu kuwafundishia wakufunzi kutoka India.

Leo pia nimepata ujumbe kutoka kwa profesa mwenzangu wa hapa chuoni St. Olaf ambaye aliwahi kuniambia kuwa atapeleka wanafunzi Tanzania mwaka ujao. Alisema kuwa angependa nimpe ushauri. Leo katika ujumbe wake amesema anasoma kitabu changu na anakifurhia. Tumekubaliana kuwa niongee na wanafunzi wake tarehe 27 mwezi huu.

Kumbukumbu zangu hizi zitanisaidia siku za usoni endapo nitapenda kuandika kitabu kuhusu uzoefu wangu kama mwandisho wa vitabu. Akitokea mtu mwingine akataka kuandika, naye atakuwa na taarifa za kutumia.

Thursday, April 12, 2018

Mhadhara Wangu Chuo Kikuu cha Minnesota

Tarehe 9 mwezi huu, nilienda Chuo Kikuu cha Minnesota kutoa mhadhara. Mada niliyoombwa kuongelea ni "Embracing African and African American Culture." Hiyo ilikuwa ni fursa nyingine kwangu kuelezea mtazamo wangu juu ya mahusiano baina ya wa-Marekani Weusi na wa-Afrika. Nilikuwa na mambo manne ya kuelezea: umuhimu wa mada ya mahusiano baina ya wa-Marekani Weusi na wa-Afrika, umuhimu wa kutambua utata na matatizo ya uhusiano huo, umuhimu wa kuelewa tulifikaje hapa tulipo, na umuhimu wa kutafakari namna ya kusonga mbele.

Kuhusu umuhimu wa mada, nilisisitiza kwamba watu weusi ulimwenguni wanakabiliana na matatizo ya pekee, tofauti na watu wengine. Nilisema kwamba waasisi wa "Pan-Africanism" walitambua jambo hilo vizuri. Kuhusu kipengele cha pili, nilitoa mifano na kufafanua migogoro na kutoelewana baina ya wa-Marekani Weusi na Wa-Afrika. Kuhusu tulivyofika hapa tulipo, niliongelea historia ya Afrika, tangu mwanzo, ambako tulikuwa jumuia moja, hadi pale watu wa Ulaya, kwa msukumo wa ubepari, walipofika na kuwachukua wa-Afrika kwa mamilioni kuwapeleka utumwani mbali na Afrika na papo hapo, kwa msukumo huo huo wa ubepari, wakavamia bara la Afrika na kulifanya makoloni.

Hapo ndipo wa-Afrika waliopelekwa Marekani wakaanza kuwa na historia tofauti na ile ya wa-Afrika waliobaki Afrika, kwani Marekani kulikuwa na mfumo wa utumwa na ubaguzi wa rangi na ukandamizwaji wa aina ya pekee. Hapo ndipo tofauti kubwa lilijengeka katika pande hizo mbili katika tamaduni, mitazamo, hisia, na mambo mengi mengine. Chimbuko la misuguano baina ya wa-Afrika na wa-Marekani Weusi ni hilo, kwani walipitia njia tofauti. Jukumu lililopo ni kujielimisha. Wa-Afrika wajielimishe kuhusu historia ya wa-Marekani Weusi. Wajielimishe kwa dhati. Wa-Marekani Weusi wajielimishe kuhusu historia ya wa-Afrika. Wajielimishe kwa dhati. Mimi kama mwanafasihi ninafahamu kuwa fasihi ina mchango mkubwa katika elimu hiyo.

Kwa kiasi kikubwa, mhadhara huo ulifuata mwelekeo wa mhadhara niliotoa mwezi Januari katika mkusanyiko wa Nu Skool. Imekuwa ni bahati kupata fursa mbili kuelezea mawazo yangu na kusikiliza na kujadili masuali na maoni mbali mbali.

Sunday, April 8, 2018

Nimenunua Kitabu cha Grimm Brothers

Leo, nilikwenda Apple Valley kumpelekea mama mmoja Mmarekani Mweusi nakala ya kitabu changu Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kama zawadi, kwa kuwa alikuwa ameniambia anapenda kujifunza kuhusu utamaduni wa Afrika.

Baada ya kukutana naye, nilikwenda katika duka la Half Price Books. Nilipita upesi sehemu yenye vitabu vya Hemingway, halafu nikaenda kwenye sehemu yenye vitabu vvya bei ya chini kabisa, yaani "clearance" kwa ki-Ingereza cha Marekani.

Hapo ingawa nilishawishika kununua kitabu hiki au kile, kikiwemo The Inheritance of Loss cha cha Kiran Desai,sikununua. Nilishawishika kuhusu hiki kitabu cha Desai kwa sababu muhula huu ninafundisha kitabu chake kingine, Hullabaloo in the Guava Orchard.

Badala ya vitabu hivyo, nilinunua The Complete Illustrated Stories of the Brothers Grimm. Kitabu hiki nimekifahamu kwa miaka mingi, kwani hao ndudu wawili, Wajerumani, Jacob na Wilhelm Grimm ndio wanaotambulika kama waasisi wa taaluma ya ukusanyaji na uchambuzi wa hadithi za jadi.

Walirekodi hadithi sehemu mbali mbali katika nchi yao wakaanza kuzichapisha mwaka 1812. Walifanya kazi hiyo kwa miaka mingi, wakaanza vile vile kutafakari mambo yanayojitokeza katika hadithi za jadi. Kwa namna hiyo waliasisi taaluma ambayo nami ninashughulika nayo.

Kuna mjadala wa tangu zamani kuhusu kama ndugu hao wawili walichapisha hadithi kama walivyosimuliwa au walizihariri ili kuondoka vipengele walivyoona havifai kimaadili na vinginevyo. Hili ni suala tata hadi leo, katika jamii kadhaa, kama vile Marekani.

Ninazo hadithi mbali mbali zilizorekodiwa na hao ndugu wawili, lakini kitabu hiki ni muhimu kwa sababu kina hadithi zote kwa pamoja.