Friday, April 29, 2016

Ninajiandaa Kushiriki Tamasha Rochester

Jioni hii, ninajiandaa kwenda Rochester, Minnesota, kushiriki tamasha la kimataifa kesho. Nitaondoka asubuhi sana ili nikawahi kabla ya saa nne litakapoanza tamasha. Nimeshalipia meza. Nitapeleka vitabu vyangu kama kawaida.

Meza ya vitabu katika tamasha ni kivutio kwa watu, sawa na meza za bidhaa na vitu vingine mbali mbali vinavyokuwepo. Watu wanapenda kuangalia vitabu, kuuliza masuali juu ya vitabu hivi, na wengine kuvinunua. Mimi mwenyewe ninapenda kuongelea mambo yanayonisukuma kuandika, hasa fasihi, tamaduni, na changamoto zitokanazo na tofauti za tamaduni.

Nitabeba pia bendera ya Tanzania. Nilishawahi kuelezea katika blogu hii namna nilivyofikia uamuzi wa kununua bendera hii, kwa ajili ya matamasha na maonesho mbali mbali. Huku ughaibuni, bendera ya Taifa ina mguso wa pekee moyoni. Kwa vile tamasha la kesho ni la kimataifa, bendera hii itakuwa mahali inapohitajika.

Tamasha la kimataifa hufanyika kila mwaka mjini Rochester. Mji huu una wakaazi kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kufanyika kwa tamasha la kimataifa katika mji huu ni jambo lenye mantiki bora. Watu wanaonesha tamaduni za nchi zao, na wote wanajifunza kutoka kwa wenzao.

Mwaka jana nilihudhuria tamasha la Rochester kwa mara ya kwanza, na niliandika habari zake hapa, na hapa. Ninangojea kwa hamu kukutana tena kesho na baadhi ya watu niliokutana na kufahamiana mwaka jana.

Kwangu mimi mwalimu, matamasha ya aina hii ni kama darasa. Kila ninapohudhuria, ninajikuta nikifundisha na pia kujifunza siku nzima. Nategemea kuandika taarifa za tamasha la kesho hapa katika blogu yangu.

Thursday, April 28, 2016

Nimekwama Kutafsiri "Kibwangai."

Jana nilichapisha katika blogu hii shairi la Haji Gora Haji liitwalo "Kibwangai," nikasema kuwa ninataka kulitafsiri kwa ki-Ingereza. Niliamini kabisa kuwa ningeweza kulitafsiri kwa kiwango cha kuniridhisha.

Baada ya kulichapisha, nilianza jana hiyo hiyo kujaribu kulitafsiri. Tofauti na mategemeo yangu, nilikumbana na hali ngumu tangu mstari wa kwanza. Nilifanya kila juhudi kuutafsiri ubeti wa kwanza, lakini niligonga mwamba. Tafsiri ya kila sentensi katika ubeti huo haikutokea vizuri. Ilikuwa ya ovyo. Nilivunjika moyo, nikaacha kuendelea.

Tatizo liko wapi? Kiswahili ninakijua vizuri. Kiswahili kilichotumika katika shairi la "Kibwangai" nimekielewa vizuri. Ninaamini kuwa shairi nimelielewa vizuri, angalau kwa namna yangu, kuanzia mbinu za kisanaa zilizotumika hadi dhamira zake. Sawa na msomaji mwingine yeyote makini ninaweza kulichambua shairi hili, ingawa, kwa hali yoyote, uchambuzi wangu utakuwa tofauti na ule wa msomaji mwingine yeyote. Hili ni jambo lisilokwepeka katika uchambuzi wa fasihi.

Kwa upande mwingine, ki-Ingereza ninakifahamu vizuri. Ninakifahamu na ninakitumia vizuri kuliko ki-Swahili. Kama kutafsiri ingekuwa ni suala la kujua lugha tu, kwa nini nimekumbana na ugumu nilioelezea? Kwa nini jaribio la kulitafsiri shairi la Kibwangai linaniumiza kichwa, hadi nimeanza kuogopa kuwa nitashindwa kuleta tafsiri ya kuniridhisha mimi mwenyewe au hata wengine?

Mashairi mengine ya Haji Gora Haji niliyoyatafsiri, ingawa nayo yalikuwa na ugumu, hayakunisumbua namna hiyo. Nilidhani kuwa nilivyoweza kuyatafsiri hadi kuridhika, ingekuwa hivyo hivyo kwa shairi hili la "Kibwangai." Naona kama nilijidanganya. Sasa ninajua kuwa nitahenya sana, bila uhakika wa kufanikiwa.

Halafu, kwa kuwa niliahidi katika ujumbe wangu wa jana kuwa nitalitafsiri shairi la "Kibwangai," dhamiri inanisuta, kwani chambilecho wahenga, ahadi ni deni. Wahenga walisema pia kuwa maji ukiyavulia nguo, huna budi kuyaoga.

Wednesday, April 27, 2016

"Kibwangai:" Shairi la Haji Gora Haji

Ninaleta hapa shairi la Haji Gora Haji liitwalo "Kibwangai," ambalo limechapishwa katika diwani yake iitwayo Kimbunga. Shairi la "Kibwangai" ni chemchemi ya mambo mengi yanayosisimua akili. Mwenye ujuzi wa nadharia za fasihi na uchambuzi wa fasihi atajionea utajiri uliomo katika shairi hili.

Nitalitafsiri shairi hili kwa ki-Ingereza katika siku chache zijazo, ili kuwapa fursa watu wasiojua ki-Swahili fununu ya umahiri wa Haji Gora Haji kama mshairi.

Nimeshatafsiri mashairi yake mawili: "Kimbunga" na "Nyang'au." Kutafsiri shairi au kazi yoyote ya fasihi ni mtihani mgumu. Lakini ni njia ya mtu kupima ufahamu wako wa lugha na ufahamu wa lugha ya kifasihi. Kwa kuwa lugha inabeba hisia na mambo mengine yanayofungamana na tamaduni, kutafsiri ni mtihani ambao unahitaji umakini usio wa kawaida.

KIBWANGAI

1.    Kuna hadithi ya kale, kwa babu nimepokeya
       Kwa manyani zama zile, mkasa ulotokeya
       Nilikuwa mwanakele, hayo nikazingatiya
       Leo nawadokezeya, kwa nilivyoyafahamu

2.    Nyani bada kugundua, watu wanawaviziya
       Sababu yake kwa kuwa, huila yao mimeya
       Na ndipo wakaamuwa, mwenzao kumtumiya
       Ende akawalimiye, mazao yalo muhimu

3.    Kwenye uamuzi huo, baada ya kukusudiya
       Kibwangai jama yao, wakamkata mkiya
       Unyani kwa mbinu zao, kwake ukajitokeya
       Akawa yeye si nyani, bali ni binaadamu

4.    Yalisudi watakayo, nyani wakafurahiya
       Yaliposadifu hayo, wote wakachekeleya
       Walidhani watakayo, atawakamilishiya
       Nyoyo zikategemeya, na nyuso kutabasamu

5.    Pana mmoja kasema, Kibwangai kumwambiya
       Kama tutalokutuma, weza kututimiziya
       Isiwe kurudi nyuma, ewe mwenzetu sikiya
       Wewe tumekuchaguwa, utumikiye kaumu

6.    Kibwangai akasema, hayo nimezingatiya
       Kidete nitasimama, jitijada kutumiya
       Kwa kusia na kulima, mpate jifaidiya
       Sitobadili mawazo, ilipwe yangu kaumu

7.    Kibwangai lipoona, ni mtu kakamiliya
       Akaanza kujivuna, na dharau kuzidiya
       Wala hakujali tena, wenzake walomwambiya
       Akahisi hawi nyani, umbo lile litadumu

8.    Kawa na tabia moja, nyani walipomwendeya
       Akajifunga mkaja, mijiwe kuwarushiya
       Hakujali zao haja, wala kuwahurumiya
       Kapiga na kukemeya, pia na kuwashutumu

9.    Nyani likawakasiri,  ghadhabu wakaingiya
       Wakafanyiza shauri, Kibwangai kumwendeya
       Kwa nguvu au hiyari, kumpa wake mkiya
       Ili awe nyani tena, asiwe binaadamu

10.  Mkia bada kumpa, mambo yakawa mabaya
       Nguo zake kazitupa, unyani kumrudiya
       Kaanza kuchupa chupa, mitini akarukiya
       Akawafata wenzake, akiwa nyani katimu

11. Wenzake wakamcheka, wote na kumzomeya
       Akakosa la kushika, kwa haya kujioneya
       Majuto yakamfika, akabakia kuliya
       Akarudia porini, iliko yake kaumu

Monday, April 25, 2016

Kumbukumbu ya Kifo cha Shakespeare

Wiki hii ni ya kumbukumbu ya kifo cha William Shakespeare. Ingawa siku ya kufariki kwake haijulikani kwa uhakika, mapokeo yameiteua tarehe 23 April, 1616, kuwa ndio siku ya kufariki kwake. Alizikwa tarehe 25 Aprili.

Sisi tuliosoma sekondari miaka ya sitini na kitu tuliweza kusoma maandishi ya Shakespeare na kuyafurahia. Tulisoma tamthilia kama Julius Caesar na The Merchant of Venice. Baada sekondari, sisi tuliokwenda "high school" tulipata fursa ya kusoma na kutafakari tamthilia zake ngumu zaidi, kama vile Hamlet na Othello.

Mwandishi maarufu wa ki-Swahili, Shaaban Robert, alimwenzi Shakespeare. Alisema kwamba akili ya Shakespeare ilikuwa kama bahari ambayo mawimbi yake yalitua kwenye fukwe duniani kote. Laiti kama wa-Tanzania tungefuata nyayo za Shaaban Robert, tukaachana na ufinyu wa fikra kuhusu umuhimu wa lugha mbali mbali na fasihi za ulimwengu, kwa kisingizio cha kukienzi ki-Swahili.

Maandishi ya Shakespeare yana kauli nyingi maarufu. Sijui kama kuna msomaji wa Shakespeare ambaye hakumbuki ile hotuba ya Hamlet inayoanza hivi:

To be, or not to be: that is the question:
Whether 'tis nobler in the mind to suffer
The slings and arrows of outrageous fortune,
Or to take arms against a sea of troubles,
And by opposing end them? To die: to sleep;
No more; and by a sleep to say we end
The heart-ache and the thousand natural shocks
That flesh is heir to, 'tis a consummation
Devoutly to be wish'd.

Sijui kama kuna msomaji wa Shakespeare ambaye hakumbuki ile hotuba ya Mark Antony iliyomo katika Julius Caesar, inayoanza hivi:

Friends, Romans, countrymen, lend me your ears;
I come to bury Caesar, not to praise him.
The evil that men do lives after them;
The good is oft interréd with their bones;
So let it be with Caesar. The noble Brutus
Hath told you Caesar was ambitious:
If it were so, it was a grievous fault,
And grievously hath Caesar answer'd it.

Kuna pia kauli maarufu katika tamthilia ya As You Like It, ambayo ni ya mhusika aitwaye Jaques. Anasema kuwa dunia ni jukwaa, ambapo kila binadamu ni kama mwigizaji:

All the world’s a stage,
And all the men and women merely players;
They have their exits and their entrances,
And one man in his time plays many parts,
His acts being seven ages.

Shakespeare aliona mbali. Kwa mfano, unaposoma The Merchant of Venice, unajionea jinsi Shakespeare alivyokuwa na upeo wa fikra wa kutambua tabia ya ubepari mapema kabisa, wakati ulipokuwa unachimbuka. Haishangazi kwa nini Mwalimu Nyerere, ambaye alikuwa katika harakati za kupambana na ubepari na kujenga ujamaa aliamua kuitafsiri tamthilia hii, akaiita Mabepari wa Venisi.

Shakespeare alizielezea kwa umakini tabia za binadamu, njema au mbaya. Katika tamthilia ya Macbeth, kwa mfano, tunashuhudia jinsi binadamu anavyoweza kuwa mbaya, na kama wewe ni msomaji wa Shaaban Robert utakumbuka jinsi naye alivyoielezea dhamira hii, kwa mfano katika Adili na Nduguze.

Shakespeare alikuwa mtunzi wa tamthilia na mashairi. Alitunga mashairi mengi, na baadhi ya hayo yako katika tamthilia zake. Haiwezekani kumtendea haki Shakespeare kwa kuelezea mchango wake katika makala ndogo kama hii. Kuna makala nyingi na vitabu juu yake na kazi zake, na maandishi yanaendelea kuchapishwa katika lugha nyingi. 

Kama Shaaban Robert alivyosema, akili ya Shakespeare ni kama bahari, ambayo mawimbi yake yanatua kwenye fukwe duniani kote. Ni miaka mia nne imepita tangu Shakespeare afariki, lakini mawimbi ya akili yake yataendelea kumwagika duniani kote.

Saturday, April 23, 2016

Ujumbe Mzuri Kutoka kwa Mwanafunzi

Leo nimepata ujumbe mzuri kutoka kwa m-Tanzania ambaye simfahamu. Amejitambulisha kwamba alipokuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari ya Namtumbo, alisoma mwongozo wangu juu ya Things Fall Apart na Song of Lawino. Nimefurahi kusikia habari hii ya kusomwa maandishi yangu sehemu ya mbali kama Namtumbo ambayo iko njiani baina ya Songea na Tunduru.

Inawezekana kuwa huyu mtu alimaanisha kijitabu changu ambacho kilikuwa na mwongozo wa Things Fall Apart na The African Child, ambao niliuelezea katika blogu hii. Ni hivi karibuni tu nimechapisha mwongozo wa Song of Lawino. Si hoja, ili mradi watu wasome ninayoandika.

Mimi ni mwalimu, na dhana yangu ya ufundishaji ni pana. Inajumlisha ninavyofundisha darasani, ninavyoandika na kuchapisha vitabu na makala, ninavyoblogu, ninavyoshiriki matamasha ya vitabu na utamaduni, ninavyoongea na watu ana kwa ana, kama vile mitaani, ninavyoendesha warsha, ninavyoshiriki mijadala mitandaoni, na kadhalika.

Mwalimu si mtu wa kuficha mawazo na mitazamo yake. Hachelei kujieleza. Ni wajibu wake. Mwalimu wa Chuo kikuu ana wajibu wa pekee wa  kufanya utafiti na kuandika vitabu na makala ili kuchangia taaluma. Anawajibika kwa wanataaluma wenzake na pia kwa jamii. Huu wajibu mpana ndio unanifanya nijishughulishe na jamii katika nyanja kama magazeti, blogu, mitandao. Miongozo ninayoandika juu ya kazi za fasihi ni sehemu ya azma hii ya kuisogeza taaluma katika jamii.

Mwongozo wangu wa Things Fall Apart alioongelea huyu mtu inaonekana ni wa mwanzo mwanzo. Nilifanya juhudi kuuboresha. Uthibitisho wa ubora wake ni kwamba unapendekezwa kwa wanafunzi hapa Marekani wanaosoma Things Fall Apart, kama ilivyofanywa na Chuo Kikuu cha Cornell. Ninafurahi kwamba ninatoa mchango wangu kwa namna hiyo, kuanzia Marekani hadi Namtumbo.

Wednesday, April 13, 2016

Nawazia Mwongozo wa "The African Child"

Tangu miaka ya sabini na kitu, nilivutiwa na wazo la kuandika miongozo ya kazi maarufu za fasihi ya Afrika. Nilianza kujijengea uzoefu kwa kuandika mwongozo wa tamthilia ya Arthur Miller, A View From the Bridge. Niliandika mwongozo ule, ambao niliutaja katika blogu hii, kwa kuombwa na mwalimu Egino Chale, ambaye alikuwa mratibu katika Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Tanzania.

Baadaye, kutokana na mashauriano na ndugu A.S. Muwanga wa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, niliandaa mwongozo wa Things Fall Apart na The African Child. Hiyo miongozo miwili ilichapishwa kama kitabu kimoja.

Hatimaye, niliamua kuushughulikia upya mwongozo wa Things Fall Apart, na kuuchapisha peke yake, kama nilivyoelezea katika blogu hii. Wazo langu lilikuwa kwamba hatimaye niushughulikie pia mwongozo wa The African Child na kuuchapisha peke yake.

Lakini badala ya kuushughulikia mwongozo wa The African Child, niliamua kuandika mwongozo wa Song of Lawino. Taarifa za shughuli hiyo nimeandika siku chache zilizopita katika blogu hii. Sasa maadam nimeshachapisha mwongozo huo, nitaelekeza mawazo yangu katika kuandaa mwongozo wa The African Child.

Kitabu hiki ambacho kinasimulia maisha ya Camara Laye ni kati ya vitabu vilivyotuvutia sana tulipokuwa vijana tukisoma sekondari. Ingawa ni tafsiri kutoka ki-Faransa, kitabu hiki kina mvuto wa pekee kwa yale kinachoelezea na pia kwa upande wa namna yanavyoelezwa. Ninategemea kubainisha hayo katika mwongozo wangu ambao siwezi kusema nitaukamilisha lini, kwa sababu, kama ilivyo kawaida yangu, ninaandika vitu mbali mbali wakati wote.

Wednesday, April 6, 2016

"Song of Lawino" Yatimiza Miaka 50

Mwaka huu, Song of Lawino, utungo maarufu wa Okot p'Bitek wa Uganda, unatimiza miaka hamsini tangu uchapishwe. Utungo huu, ambao unafahamika kama wimbo, ulichapishwa na East African Publishing House mwaka 1966 ukapata umaarufu tangu mwanzo.

Ulisomwa mashuleni na katika jamii kote Afrika Mashariki na sehemu zingine. Ulileta msisimko na upeo mpya katika dhana ya ushairi katika ki-Ingereza, na ulichochea washairi wengine kutunga kwa mtindo aliotumia Okot p'Bitek, ambao ulijaa athari za ushairi wa jadi wa ki-Afrika.

Siku chache zilizopita, niliandika katika blogu hii kuwa nimechapisha mwongozo wa Song of Lawino. Kitu ambacho sikusema ni kuwa nilikuwa na sababu ya kuchapisha mwongozo huu wakati huu, na sababu yenyewe ni hayo maadhimisho ya miaka 50.

Nilisoma taarifa, zaidi ya mwaka mmoja uliopita, kwamba idara ya "Literature" ya Chuo Kikuu cha Makerere ilikuwa inaandaa maadhimisho ya kumbukumbu hii, ambayo yangehusisha mihadhara na shughuli zingine. Ingekuwa niko Afrika Mashariki, ningeshiriki. Kwangu ingekuwa fursa sio tu ya kushiriki maadhimisho, bali pia kujikumbusha ziara ambazo niliwahi kufanya katika Chuo Kikuu cha Makerere.

Mara ya kwanza, mwaka 1978, nilienda kuhudhuria mkutano wa waalimu wa "Literature" kutoka vyuo vikuu vya Afrika Mashariki, na mara ya pili, mwaka 1990, nilikwenda kama mtahini wa nje katika idara ya "Literature and Mass Communications."

Kwa vile nilijua kuwa nisingeweza kuhudhuria maadhimisho, niliamua kuendelea kurekebisha mswada wa mwongozo wa Song of Lawino ambao nilikuwa nimeanza kuuandika miaka yapata ishirini iliyopita. Nilijiwekea lengo la kuchapisha mwongozo huu wakati huu wa maadhimisho ya miaka 50. Nafurahi kuwa nimefanikisha azma yangu.

Kwa mujibu wa taarifa nilizozisoma, maadhimisho yalifana. Ingawa shughuli rasmi zilifanyika katika Chuo Kikuu cha Makerere, taarifa za maadhimisho haya zilizagaa katika vyombo vya habari nchini Uganda. Mifano ni taarifa hii hapa na hii hapa.

Shughuli moja iliyonivutia katika maadhimisho haya ni kuzinduliwa kwa tafsiri ya Luganda ya Song of Lawino. Wanafasihi tunafahamu kuwa utungo huu una historia ndefu ya kutafsiriwa. Nimegusia suala hilo katika mwongozo wangu. Hadi leo, kuna tafsiri katika lugha zaidi ya thelathini. Kwa njia hii, umaarufu wake unaendelea kuenea ulimwenguni.


Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...