Saturday, April 23, 2016

Ujumbe Mzuri Kutoka kwa Mwanafunzi

Leo nimepata ujumbe mzuri kutoka kwa m-Tanzania ambaye simfahamu. Amejitambulisha kwamba alipokuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari ya Namtumbo, alisoma mwongozo wangu juu ya Things Fall Apart na Song of Lawino. Nimefurahi kusikia habari hii ya kusomwa maandishi yangu sehemu ya mbali kama Namtumbo ambayo iko njiani baina ya Songea na Tunduru.

Inawezekana kuwa huyu mtu alimaanisha kijitabu changu ambacho kilikuwa na mwongozo wa Things Fall Apart na The African Child, ambao niliuelezea katika blogu hii. Ni hivi karibuni tu nimechapisha mwongozo wa Song of Lawino. Si hoja, ili mradi watu wasome ninayoandika.

Mimi ni mwalimu, na dhana yangu ya ufundishaji ni pana. Inajumlisha ninavyofundisha darasani, ninavyoandika na kuchapisha vitabu na makala, ninavyoblogu, ninavyoshiriki matamasha ya vitabu na utamaduni, ninavyoongea na watu ana kwa ana, kama vile mitaani, ninavyoendesha warsha, ninavyoshiriki mijadala mitandaoni, na kadhalika.

Mwalimu si mtu wa kuficha mawazo na mitazamo yake. Hachelei kujieleza. Ni wajibu wake. Mwalimu wa Chuo kikuu ana wajibu wa pekee wa  kufanya utafiti na kuandika vitabu na makala ili kuchangia taaluma. Anawajibika kwa wanataaluma wenzake na pia kwa jamii. Huu wajibu mpana ndio unanifanya nijishughulishe na jamii katika nyanja kama magazeti, blogu, mitandao. Miongozo ninayoandika juu ya kazi za fasihi ni sehemu ya azma hii ya kuisogeza taaluma katika jamii.

Mwongozo wangu wa Things Fall Apart alioongelea huyu mtu inaonekana ni wa mwanzo mwanzo. Nilifanya juhudi kuuboresha. Uthibitisho wa ubora wake ni kwamba unapendekezwa kwa wanafunzi hapa Marekani wanaosoma Things Fall Apart, kama ilivyofanywa na Chuo Kikuu cha Cornell. Ninafurahi kwamba ninatoa mchango wangu kwa namna hiyo, kuanzia Marekani hadi Namtumbo.

No comments: