Thursday, April 28, 2016

Nimekwama Kutafsiri "Kibwangai."

Jana nilichapisha katika blogu hii shairi la Haji Gora Haji liitwalo "Kibwangai," nikasema kuwa ninataka kulitafsiri kwa ki-Ingereza. Niliamini kabisa kuwa ningeweza kulitafsiri kwa kiwango cha kuniridhisha.

Baada ya kulichapisha, nilianza jana hiyo hiyo kujaribu kulitafsiri. Tofauti na mategemeo yangu, nilikumbana na hali ngumu tangu mstari wa kwanza. Nilifanya kila juhudi kuutafsiri ubeti wa kwanza, lakini niligonga mwamba. Tafsiri ya kila sentensi katika ubeti huo haikutokea vizuri. Ilikuwa ya ovyo. Nilivunjika moyo, nikaacha kuendelea.

Tatizo liko wapi? Kiswahili ninakijua vizuri. Kiswahili kilichotumika katika shairi la "Kibwangai" nimekielewa vizuri. Ninaamini kuwa shairi nimelielewa vizuri, angalau kwa namna yangu, kuanzia mbinu za kisanaa zilizotumika hadi dhamira zake. Sawa na msomaji mwingine yeyote makini ninaweza kulichambua shairi hili, ingawa, kwa hali yoyote, uchambuzi wangu utakuwa tofauti na ule wa msomaji mwingine yeyote. Hili ni jambo lisilokwepeka katika uchambuzi wa fasihi.

Kwa upande mwingine, ki-Ingereza ninakifahamu vizuri. Ninakifahamu na ninakitumia vizuri kuliko ki-Swahili. Kama kutafsiri ingekuwa ni suala la kujua lugha tu, kwa nini nimekumbana na ugumu nilioelezea? Kwa nini jaribio la kulitafsiri shairi la Kibwangai linaniumiza kichwa, hadi nimeanza kuogopa kuwa nitashindwa kuleta tafsiri ya kuniridhisha mimi mwenyewe au hata wengine?

Mashairi mengine ya Haji Gora Haji niliyoyatafsiri, ingawa nayo yalikuwa na ugumu, hayakunisumbua namna hiyo. Nilidhani kuwa nilivyoweza kuyatafsiri hadi kuridhika, ingekuwa hivyo hivyo kwa shairi hili la "Kibwangai." Naona kama nilijidanganya. Sasa ninajua kuwa nitahenya sana, bila uhakika wa kufanikiwa.

Halafu, kwa kuwa niliahidi katika ujumbe wangu wa jana kuwa nitalitafsiri shairi la "Kibwangai," dhamiri inanisuta, kwani chambilecho wahenga, ahadi ni deni. Wahenga walisema pia kuwa maji ukiyavulia nguo, huna budi kuyaoga.

No comments: