
Ulisomwa mashuleni na katika jamii kote Afrika Mashariki na sehemu zingine. Ulileta msisimko na upeo mpya katika dhana ya ushairi katika ki-Ingereza, na ulichochea washairi wengine kutunga kwa mtindo aliotumia Okot p'Bitek, ambao ulijaa athari za ushairi wa jadi wa ki-Afrika.
Siku chache zilizopita, niliandika katika blogu hii kuwa nimechapisha mwongozo wa Song of Lawino. Kitu ambacho sikusema ni kuwa nilikuwa na sababu ya kuchapisha mwongozo huu wakati huu, na sababu yenyewe ni hayo maadhimisho ya miaka 50.
Nilisoma taarifa, zaidi ya mwaka mmoja uliopita, kwamba idara ya "Literature" ya Chuo Kikuu cha Makerere ilikuwa inaandaa maadhimisho ya kumbukumbu hii, ambayo yangehusisha mihadhara na shughuli zingine. Ingekuwa niko Afrika Mashariki, ningeshiriki. Kwangu ingekuwa fursa sio tu ya kushiriki maadhimisho, bali pia kujikumbusha ziara ambazo niliwahi kufanya katika Chuo Kikuu cha Makerere.
Mara ya kwanza, mwaka 1978, nilienda kuhudhuria mkutano wa waalimu wa "Literature" kutoka vyuo vikuu vya Afrika Mashariki, na mara ya pili, mwaka 1990, nilikwenda kama mtahini wa nje katika idara ya "Literature and Mass Communications."

Kwa mujibu wa taarifa nilizozisoma, maadhimisho yalifana. Ingawa shughuli rasmi zilifanyika katika Chuo Kikuu cha Makerere, taarifa za maadhimisho haya zilizagaa katika vyombo vya habari nchini Uganda. Mifano ni taarifa hii hapa na hii hapa.
Shughuli moja iliyonivutia katika maadhimisho haya ni kuzinduliwa kwa tafsiri ya Luganda ya Song of Lawino. Wanafasihi tunafahamu kuwa utungo huu una historia ndefu ya kutafsiriwa. Nimegusia suala hilo katika mwongozo wangu. Hadi leo, kuna tafsiri katika lugha zaidi ya thelathini. Kwa njia hii, umaarufu wake unaendelea kuenea ulimwenguni.
No comments:
Post a Comment