Monday, December 23, 2013

Nimepata Zawadi Murua ya Krismasi Leo

Wafuatiliaji wa fasihi ya ki-Ingereza wanafahamu kuwa juzuu la pili la barua za Hemingway, limechapishwa mwaka huu. Sawa na juzuu la kwanza, hili ni buku kubwa, kurasa 519.

Leo nimepokea kifurushi kutoka Amazon.com. Binti yangu Zawadi aliponiletea nilishangaa, maana sijaagiza kitabu kutoka Amazon kwa miezi kadhaa. Nilipofungua kifurushi sikuamini macho yangu. Ni juzuu hilo nililolitaja. Nimefurahi sana. Nilikuwa natamani kufanya mkakati wa kununua. Lakini Mungu mkubwa, kamwongoza huyu bwana aninunulie hiki hiki ambacho roho yangu ilikuwa inatamani.

Bwana aliyeniletea ni David Cooper, mzazi wa mwanafunzi mmojawapo wa wale waliokuja Tanzania mwezi Januari mwaka huu kwenye kozi ya Hemingway. Baba huyu ni msomaji makini wa Hemingway na waandishi wengine.

Ni huyu bwana, anayeishi Ohio, alipoambiwa na kijana wake kwamba natamani siku moja kwenda Montana kuongea na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee wa Ernest Hemingway aliebaki, alisema atatusafirisha kwa ndege yake.

Siku ilipofika, yeye na rubani wake walifika Minnesota, wakatuchukua, mimi na wanafunzi wawili, akiwemo yule kijana wake.

Bwana huyu ni kama tumejenga urafiki. Namshukuru sana.
 

Wednesday, December 18, 2013

Mama Kutoka Togo Kawahi Kununua Zawadi za Krismasi

Mama mmoja kutoka Togo ambaye ni rafiki ya familia yangu, alitutembelea wiki kama tatu zilizopita. Kati ya mambo mengine, alsema anataka kununua nakala mbili za kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Alisema ni zawadi ya Krismasi kwa marafiki zake waliopo hapa hapa Marekani.

Huyu mama ni kati ya wasomaji wa mwanzo kabisa wa kitabu hiki mara kilipochapishwa, mwanzoni mwa mwaka 2005. Alikipenda sana na kuanzia pale akawa anakipigia debe kwa watu mbali mbali. Hata kuna wakati ndugu yake alikuja kutoka Togo, akamtafutia nakala, ambayo alienda nayo Togo.

Namshukuru mama huyu. Nanatafakari suala hilo. Kuna vitabu vingi sana hapa Marekani ambavyo vinafaa kama zawadi kwa ndugu na marafiki. Lakini mama huyu kachagua kitabu changu. Halafu huyu mama hana kibarua au kipato cha ajabu: anafanya kazi ya kutunza wazee hospitalini.

Lakini, mama huyu, pamoja na ugumu wa kupata hela hapa Marekani, pamoja na ugumu wa matumizi kwa ujumla, kabana hela akaamua kununua vitabu hivi. Halafu, mteja anapokurudia tena, kwa hiari yake, ni jambo la kushukuru, kwamba aliridhika au alifurahishwa na kile alichokipata mwanzo kutoka kwako. Kwa vile mama huyu ni mpiga debe wangu makini, nilimpa punguzo zuri la bei.

Nimeona tabia hii ya kununua vitabu miongoni mwa wa-Afrika wa nchi zingine, ila sio Tanzania. Kwa mtazamo wangu, hao wenzetu wanatoka nchi ambazo zimewaelimisha.

Niliwahi kuandika makala katika blogu hii kuhusu suala la kumpa mtu kitabu kama zawadi ya Krismasi au Idd El Fitr. Mawazo niliyotoa bado ninayo vile vile vile.

Tuesday, December 10, 2013

Kwa Wapumbavu wa Kigoma Wanaoleta Vurugu Kwenye Mikutano ya Dr. Slaa

Huu ni ujumbe kwenu wapumbavu wa sehemu mbalimbali za Kigoma ambao mmekuwa mkileta vurugu kwenye mikutano ya Dr. Slaa, katibu mkuu wa CHADEMA.

Ni moja ya haki za binadamu kutafuta, kupata, au kusambaza taarifa na mitazamo katika masuala mbali mbali yanayoihusu jamii. Someni tangazo la kimataifa la haki za binadamu. Taarifa hizo hupatikana kwa namna mbalimbali, kuanzia vyombo vya habari hadi mikutano.

Nimeona picha za makundi ya watu wakiwa wamekusanyika kumsikiliza Dr. Slaa. Hiyo ni haki yao, mojawapo ya haki za binadamu. Lakini nimeona pia taarifa za wapumbavu wachache, kama vile Kasulu, wakija kuvuruga au kujaribu kuvuruga mikutano hiyo. Hao ni wapumbavu. Kenge wakubwa.

CCM, chama ambacho kimeshika hatamu katika nchi hii, chenye wajibu wa kuongoza na kuelimisha jamii, kimekaa kimya. CCM naijumlisha katika kundi hili la wapumbavu. Zito Kabwe, ambaye anatajwa na hao wavurugaji kwamba wanamtambua yeye, naye hajasema kitu. Naye ni mpumbavu.

Kuna haki zingine za binadamu zinazohusika katika suala hili. Moja ni haki ya kila binadamu kukusanyika na kujumika na wengine kwa amani. Nyingine ni haki ya kila raia kwenda popote katika nchi yake. Wapumbavu wa Kigoma mjini waliomtishia Dr. Slaa asikanyage Kigoma wakapimwe akili.

Mimi sio mwanachama wa chama chochote cha siasa. Ila nakerwa na upumbavu nilioelezea.

Monday, December 9, 2013

Wajinga Hunena, CCM Ilileta Uhuru Tanganyika

Kiwango cha ujinga Tanzania kinatisha. Utawasikia wengi wakisema kuwa CCM ilileta Uhuru Tanganyika mwaka 1961. Wajinga wengine, kuanzia wanasiasa hadi watu wa mitaani, husema kuwa CCM imekuwa madarakani kwa miaka 52.

Utamsikia mwanasiasa anaiponda CCM kwa kuuliza, "Miaka yote 52 ya utawala wa CCM, wananchi mmenufaika vipi?" Na utammsikia kada wa CCM akitamba, "CCM ni chama chenye uzoefu wa miaka 52.

Hapakuwa na CCM mwaka 1961. Chama kilicholeta Uhuru Tanganyika ni TANU. Wala CCM haijawa madarakani miaka 52. Kuna mengi katika historia ya Tanganyika na Tanzania ambayo yanasahaulika au kupotoshwa kwa sababu ya uzembe wa wa-Tanzania.

Wajinga wengine wanasema kuwa leo tunasherehekea kumbukumbu ya Uhuru wa Tanzania au Tanzania Bara. Mwaka 1961 hapakuwa na nchi iliyoitwa Tanzania wala Tanzania Bara. Nchi iliyopata Uhuru mwaka ule ni Tanganyika. Inasikitisha.

Monday, December 2, 2013

Ninayo Pia Blogu ya Ki-Ingereza, Jamani

Wadau wa blogu hii ya hapakwetu, samahani kama sikuweka wazi tangu mwanzo kuwa ninayo pia blogu ya ki-Ingereza. Inaitwa "Mbele" na anwani yake ni hii: http://www.josephmbele.blogspot.com.

Niliamua kuanzisha na kuendesha blogu hii ya ki-Kiingereza ili kuchangia elimu hasa katika masuala ya fasihi ya ki-Ingereza. Mimi ni mwalimu wa somo hili mwenye uzoefu tangu miaka ya mwanzoni ya sabini na kitu. Nilifundisha katika idara ya Literature, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuanzia mwaka 1976, nikasomea shahada ya udaktari Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, Marekani, 1980-86, na kuanzia mwaka 1991 nimekuwa nikifundisha katika idara ya ki-Ingereza ya chuo cha St. Olaf hapa Marekani.

Katika blogu hii ya "Mbele" mara kwa mara ninaongelea vitabu, hasa vitabu vya fasihi. Uchambuzi wangu vitabu hivi unasomwa duniani kote. Nimeona kuwa uchambuzi wangu wa riwaya ya The Old Man and the Medal unapitiwa kuliko andiko jingine lolote na watu kutoka duniani kota.

Nina uzoefu na ufahamu mkubwa sana katika masomo hayo, na ndio nikaona niwamegee wanajamii angalau kiasi, kwani blogu si mahala pa kuandika makala ndefu, wala kitabu. Nilivyoanzisha blogu hii ya ki-Ingereza niliwawazia kwa namna ya pekee vijana wa Tanzania.

Nikiongea kwa ujumla kuhusu wa-Tanzania, ni kwamba wale wanaodhani wanajua ki-Ingereza, bado wana safari ndefu. Mimi mwenyewe naendelea kujifunza undani wa ki-Ingereza, ingawa waandishi maarufu hapa Marekani kama vile Mzee Patrick Hemingway na Jim Heynen wanapenda ninavyoandika. Ni jambo baya sana kuridhika na kile unachodhani unajua, na ndio maana nafanya juhudi.

Ninaandika ki-Ingereza sahihi, ipasavyo, na nilitegemea kuwa yoyote anayeisoma blogu ya Mbele kwa makini ataona mfano wa uandishi bora wa ki-Ingereza. Ninafahamu ninachosema, kwani kama nilivyotamka, mimi nafundisha ki-Ingereza katika chuo hapa Marekani. Lakini bado nahangaika kuboresha ujuzi wangu kwa kusoma sana na kuandika sana.

Nimeandika ujumbe huu kwa sababu mbili zinazohusiana. Hutokea mara moja moja mdau akaniuliza blogu yangu nyingine anwani yake ni ipi. Pili, nimegundua kuwa kuitaja tu katika orodha ya blogu niliyoweka hapa kulia, haitoshi. Soma pia makala hii hapa.