Saturday, July 25, 2009

Taifa la Kesho

Wahenga walisema, mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Picha hii inatueleza mengi kuhusu malezi ya watoto katika jamii yetu. Ni kawaida kwa watoto katika Tanzania kuonekana kwenye baa, na kwenye miziki, hata usiku wa manane. Humo mitaani wanashuhudia mambo ya ajabu mengi, kuanzia ulevi, matusi, na hata watu kuumizwa au kuuawa kwa tuhuma za wizi. Kuwapiga au kuwaua wezi imeshakuwa kivutio kikubwa mitaani, kama vile burudani. Haya ndio malezi ya watoto wa leo. Watakapokuwa watu wazima, itakuwaje?

Picha hapo juu niliiona kwenye blogu fulani, ila nimesahau. Nitapenda kutafuta chanzo ili niweke taarifa kikamilifu.

Wednesday, July 22, 2009

Picha kutoka Tamasha la Utalii (KTTF) 2009

Tarehe 5-7 Juni, kulifanyika tamasha la utalii Arusha, Tanzania. Tamasha hili hufanyika kila mwaka mwanzoni mwa mwezi Juni.

Wahusika wa Programu ya Utalii Mto wa Mbu walishiriki tamasha hilo. Leo wameniletea picha za kumbukumbu.


Wednesday, July 15, 2009

Mafanikio ya Mradi wa Utalii: Mto wa Mbu

Nimesoma taarifa ya kufurahisha katika Arusha Times kuwa mradi wa utalii Mto wa Mbu, umeteuliwa kuwa mfano wa kuigwa nchini Tanzania. Ni heshima kubwa, nami natoa pongezi kwa vijana wanaoendesha mradi huu.

Nimewafahamu vijana hao kwa miaka kadhaa, tukizungumzia masuala mbali mbali muhimu. Katika kupita kwangu Mto wa Mbu na wanafunzi wa kiMarekani, vijana hao wamekuwa wenyeji wetu wa kutueleza masuala ya tamaduni za mji ule.

Nimeandika habari zao kwenye blogu yangu. Nao katika blogu yao wameandika habari ya ushirikiano wetu.

Ni jambo la kufurahisha kuwaona vijana wakijituma katika shughuli za maendeleo namna hii, na nawatakia mafanikio makubwa zaidi siku za usoni.

Friday, July 10, 2009

Lugha za asili ni muhimu sana zisiachwe zikatoweka


(Picha: Mkurugenzi wa Mradi wa Lugha za Tanzania (LOT) katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Profesa Josephat Rugemalira)

Wadau mbalimbali wa lugha walikutana katika warsha iliyoandaliwa na Mradi wa Lugha Tanzania(LOT) na kujadiliana kuhusu lugha za asili Tanzania. Makala hii ya Mwandishi Wetu, aliyehudhuria warsha hiyo yaeleza.

Lugha za asili zimebeba maarifa mengi yaliyolimbikizwa na jamii ambapo kama jitihada za makusudi hazitachukuliwa sasa kuzidumisha,kuzififisha na kuzibeza zitakufa taratibu katika kipindi cha miaka 20 ijayo.

Mkurugenzi wa Mradi wa Lugha za Tanzania (LOT) katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Profesa Josephat Rugemalira anasema, iwapo raia wamenyang'anywa fursa ya kutumia lugha yao kujadili sera ziletwazo kwao au kuhoji sheria zinazotungwa ili kuwadhibiti, raia hawa ni kama wanyama waliohasiwa wasiweze kujiamulia mambo yahusuyo maisha yao wala kurithisha raslimali zao kwa watoto na wajukuu.

“Lugha hizi , lazima zifunguliwe milango katika sekta ya habari na mawasiliano, katika elimu na katika siasa. Kuthamini lugha zetu kutatupa msukumo mkubwa katika kujiletea maendeleo, kujenga demokrasia na kuhifadhi utamaduni wetu,” anasema.

Mwandishi wa habari na vitabu wa siku nyingi nchini, Ndimara Tegambwage, akizungumzia mtazamo wake kuhusu lugha hizo katika warsha ya Wadau wa lugha za asili Tanzania, hivi karibuni jijini Dar es salaam, anasema kuzuia matumizi ya lugha hizo ni kumnyima mtu uhuru wa kufikiri.

“ Anayetaka kukuza lugha za jamii (asili) si mhaini na mchochezi. Kamwe lugha za asili haziwezi kuwagawa watu kama wengi wanavyodhani, haya ni mawazo potofu.” alisema na kutoa mifano ya nchi zinazotumia lugha moja, lakini hakuna umoja katika nchi hizo.

Kimsingi alisema kuwa, lengo la kukuza na kushawishi watawala, watunga sera ni muhimu ili kuwafikia wanahabari/wadau,wabunge na watu wenye mamlaka makubwa katika nchi hii watazame hoja hiyo.

Profesa Amandina Lihamba wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, akichangia mtazamo wake, alisema upo umuhimu wa kuendelea kuzitumia na kuzihifadhi lugha hizo, kwa njia mbalimbali, ikiwemo kuandika hadithi kwa kutumia lugha za asili.

“ Huu ni utamaduni ambao inabidi tuuenzi na kuutunza,” alisema na kutoa changamoto ya kuandikwa kwa kamusi nyingi za lugha za asili.

Dk Azaveli Lwaitama, akichangia katika warsha hiyo, alisema kuwa katika kijiji kimoja sio rahisi kuwa na wazungumzaji wa kabila moja tu na kwamba kuna baadhi ya shule watoto wanakwenda shule wakiwa hawajui Kiswahili kabisa.

“Kuna ubaya gani Mwalimu asiwafundishe kwa lugha yao? Ifike mahali kuzitumia lugha hizi isionekane ni kosa kuzitumia. Kuna ubaya gani Mwalimu akitumia lugha ya Kimasai au Kimatengo na nyinginezo kama wanafunzi waliomo darasani wanaielewa vyema lugha hiyo. Hatusemi lugha hizi zikitumika Kiswahili kisitumike,” anasema.

Kwa upande wa demokrasia, alisema kuwa hatuwezi kuwalazimisha watu kutumia lugha zao na kwamba wataalamu kinachotakiwa ni kuwaelimisha tu, kisha wao waamue kutumia lugha zao au la.

“Ireland kuna wakati walikataa lugha yao isitumike, lakini sasa wanahoji kwa nini isitumike lugha hiyo. ,” alisema.

Kimsingi madai kuwa lugha za kikabila zinaweza kuchochea mapigano, basi zipigwe marufuku sio sahihi kwa sababu nchini Kenya hakuna uhakika kama kuna sera ya kuendeleza na kuchochea chuki za kikabila au kidini, lakini wanasiasa ndio wanaochochea na kusababisha watu wapigane.

“Jumuia ya Ulaya wanaweza wakaungana, lakini kila taifa likawa na lugha yake na haiwakatazi kuungana. Mtu anaweza kuchochea watu wapigane kwa sababu ya imani zao za dini, lakini haijawahi kutolewa tamko au msimamo kuwa dini zipigwe marufuku.” ilisemwa.

Dk H.R.T.Muzale kwa upande wake anasema kuwa, lugha na wazungumzaji wake hazikai sehemu moja zilipozaliwa na kwamba huenea na kuelekea sehemu nyingine na kwamba tafsiri ya lugha na lugha kuu ya kwanza ni ile ya mtu alipozaliwa na kwamba ni muhimu sana kujiepusha kuwa yatima wa lugha ambao hawana lugha nyingine za asili.

Profesa Fikeni Senkoro pia wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, alisema jitihada za kukusanya maneno na misamiati ya lugha za asili pekee haitoshi na kushauri kuwa, ni muhimu kufanya utafiti wa kukusanya hadithi ambazo zinaweza kuchangia kupatikana mambo mengi zaidi na kutoa mwanga wa fani na maudhui ili kuibua mjadala mpana zaidi ikiwa pamoja na falsafa za jamii husika.

Dk Aldin Mutembei wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili anaona kuwa kama kuna una kubishana kwa mawazo ni chanzo kizuri cha mwanafunzi wa uzamivu kuandika tasnifu yake.

Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Rehema Rajabu akichangia katika warsha hiyo, alisema kuwa, lugha za asili zinazozungumziwa ni pamoja na falsafa, utamaduni, mila na desturi zinazowaimarisha wazungumzaji.

Alipingana na mtazamo kuwa, nchi haitaendelea kwa sababu ya matumzi ya lugha za asili na kwamba miongoni mwa maarifa yaliyomo katika mila na desturi za makabila ni pamoja na utamaduini wa kuhifadhi chakula kwa kutumia majani ya asili, tofauti na sasa ambapo zinatumika sumu kwa ajili ya kuhifadhi vyakula.

“Wachaga tulikuwa na utaalamu wa umwagiliaji maji kwa kugawanya nafasi kati ya eneo na eneo na kupata nafasi kubwa ya mafanikio kupitia mfumo huo ambao uliheshimiwa.Tusiache lugha hizi zikafa pamoja na maarifa yaliyomo ya kuendeleza utu. Mijadala hii ya Kiswahili na lugha za asili inaleta joto lakini haileti mwanga” alisema.

Dk Mushumbushi Kibogoyo wa Foreign Language and Linguistics(UDSM),alisema kuwa lugha hizo zinashughulikiwa sio kwa sababu ni mfu, ziko hai ndio maana zinazungumzwa na watu walio hai.

“Kiswahili kinapata wapi haki ya kuua lugha za makabila mengine ili kukikuza. Unapomwambia msukuma aache lugha yake maana ni kwamba unamwambia aache utamaduni wake.Tuyape maana matokeo ya utafiti kwa jamii yetu na si kwa wasomi pekee.” alisema na kuendelea.

“Mfumo wa utawala utambue watu wana lugha zao na lazima ziheshimiwe. Mradi baada ya kwisha muda wake tutakuwa tunafanya ushawishi kiasi gani kisera. Lugha hizi zina nguvu, ndio maana katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Busanda, watu walizungumza kisukuma ili kuwashawishi wapiga kura.Wanaopinga lugha hizi watambue kuwa zinahitajika. Sio lugha mfu ni lugha hai ziheshimike na zinahitajika sio wakati wa uchaguzi tu,” alisema.

Profesa D. Massamba alisema kuwa, utafiti uliofanywa ili kuandika kamusi za makabila mbalimbali umesaidia kupatikana takwimu ambazo zitasaidia kuandika vitabu vya kufundishia na kusogeza mbele taaluma.

Atlasi ya lugha iliyochapishwa itapanua uelewa wa wanafunzi na watu wengine kuhusu jiografia ya nchi.

Profesa Saida Yahya-Othman ambaye amestaafu rasmi kufanya kazi Chuo Kikuu cha Dar es salaam hivi karibuni, akifunga warsha hiyo, alisema kuwa Mradi wa Lugha za Tanzania (LOT, ni wa mafanikio kutokana na matokeo yake na kwamba ni muhimu kufahamu lugha za asili nchini zinatumika kwa kiwango gani ili kuweka uzito.

“Tunahitaji kueleza kwa nini hali iko hivyo ilivyo, kitu gani kimesababisha iwe hivyo, kisiasa na kiuchumi. Hadithi za asili sio hadithi tu kwa kuzitazama sarufi, misamiati, utambaji na mengineyo. Ni muhimu sana kuziangalia zaidi ya hapo, namna gani lugha zinavyotumika, ukosefu wa usawa baina yao na mambo mengine muhimu sana yanayoelezea maisha ya watu, majanga kwa mapana na marefu yake,” alisema.

Profesa Saida alisema kuwa, thamani ya mtu kwa kitu chako ni pale anapokinunua na kwa hiyo ni muhimu kufanya utafiti wa nani anayenunua machapisho yaliyochapishwa kwa lugha za asili na kwa kiwango gani.


Chanzo: Mwandishi maalum, NIPASHE, 7 Julai, 2009.