Saturday, November 24, 2018

Kumbukumbu ya Matengo Folktales Kutajwa Katika "Jeopardy."

Kipindi kama hiki, mwaka jana, kitabu cha Matengo Folktales kilitajwa katika kipindi maarufu cha televisheni kiitwacho Jeopardy." Ilikuwa tarehe 23 Novemba, nami niliandika taarifa katika blogu hii.

Tukio hili la kushtukiza lilinifungua macho nikatambua kuwa "Jeopardy" ni maarufu sana hapa Marekani. Bado sijui taarifa za kitabu changu zilifikaje kule, ila ninafurahia kuwaambia waMarekani taarifa hizo kila ninaposhiriki matamasha ya vitabu.

Thursday, November 22, 2018

Vitabu Kama Zawadi ya Sikukuu

Kwa watu wengi, huu ni wakati wa maandalizi ya sikukuu ya Krismasi. Pamoja na mengine, ni kununua zawadi kwa ajili ya ndugu, marafiki na kadhalika. Hapa Marekani, vitabu ni zawadi mojawapo inayothaminiwa.

Hapa kushoto ni picha niliyopiga tarehe 16 Novemba katika duka la vitabu la Barnes and Nobel mjini Burnsville. Inaonyesha kabati la vitabu vilivyopendekezwa na wahudumu wa duka. Nilipiga picha hiyo kwa sababu kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kipo hapo. Kimekuwepo kwa wiki nyingi. Bila shaka kuna wateja wanaoingi na kuchungulia kwenye kabati hilo ili kupata wazo juu ya kitabu cha kununua, kwani tayari kimependekezwa na watu wazoefu wa vitabu.

Utamaduni wa kuvihesabu vitabu kama zawadi muafaka kwa sikukuu au mazingira yeyote mengine unanivutia, kama nilivyowahi kueleza katika blogu hii. Ninatamani utamaduni huu uote mizizi katika nchi yangu. Nawazia furaha watakayokuwa nayo watoto kwa kupewa vitabu kama zawadi, kwa sababu ninajua kuwa watoto wanapenda vitabu, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii.  Nawazia namna ambavyo mitazamo na fikra za watu zingeboreka kwa kuwa na utamaduni wa kuthamini na kusoma vitabu vya aina mbali mbali.

Saturday, November 10, 2018

Nimeongea na Lumen Christi Book Club

Miezi kadhaa iliyopita, nilipata mwaliko wa kwenda Lumen Christi Catholic Community kuongelea kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Aliyenialika ni Jackie ambaye alikuwa amekisoma kitabu hicho. Alisema kwamba jumuia ya waumini hao wana klabu yao ya usomaji vitabu, na kwa sasa wamejikita katika vitabu vinavyohusu Afrika.

Nilipoingia ukumbini, niliona meza imepangwa vizuri karibu na mlandoni, yenye vitabu vyangu na vya waandishi wawili ambao tunafahamiana: Maria Nhambu ambaye alizaliwa Tanzania, na Afeworki Ghorghis, jaji mstaafu wa mahakama kuu ya Eritrea.

Baada ya Jackie kunitambulisha, nilielezea kifupi nilivyokulia Tanzania, katika utamaduni wa wa-Matengo, na hatimaye nilivyokutana na utamaduni wa Marekani, nilipokuwa masomoni katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, na kufikia kuwa mshauri kwa vyuo vinavyopeleka wanafunzi Afrika, kama nilivyoandika katika utangulizi wa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Katika kuelezea uandishi wangu juu ya masuala ya utamaduni, nilianza na kitabu cha Matengo Folktales.

Baada ya hapo, Jackie alitaja vipengele vilivyomo kitabuni ili nielezee, na wengine waliniuliza masuali yao. Kati ya masuala tuliyoongelea ni "gifts" (sio kwa maana ya zawadi), uzee, na "African time." Nilielezea nilivyoandika kitabuni kuhusu masuala hayo. Klabu hii ya vitabu ni ya aina yake, kwa maana kwamba watu wanahudhuria hata bila kusoma kitabu kinachojadiliwa.

Mkutano ulikuwa mzuri na wenye manufaa. Binafsi, nilitoa shukrani kwa fursa ya kufahamiana na watu wapya, kwani inatajirisha maisha yangu. Nilifurahi kuweza kuwaelezea shughuli zangu kama mtoa ushauri chini ya mwavuli wa Africonexion.  Baada ya mimi kurejea nyumbani, Jackie aliniletea ujumbe kwamba atanitambulisha kwa mkurugenzi wa East Side Freedom Liabrary ambaye wakati huu anaandaa programu kuhusu Afrika. Sikuwa ninajua kuhusu maktaba hiyo. Ninasubiri.