Kitabu Kimeingia Barnes and Noble

Kwa wasomaji wa vitabu hapa Marekani, jina la Barnes and Noble si geni, kwani ni jina la kampuni inayomiliki maduka mengi ya vitabu yaliyoko nchi nzima. Maduka ya Barnes and Noble ni maarufu kiasi kwamba watu wanapoongelea maduka ya vitabu, huwazia kwanza Amazon na Barnes and Noble.

Leo nimepata ujumbe kutoka kwa mhudumu wa duka la Barnes and Noble Burnsville, mwendo wa nusu saa kutoka hapa ninapoishi. Ameandika:

Hi Joseph. Just letting you know I put your book on the staff recommendation display at the Barnes and Noble Burnsville where I work. The book about cultural differences between Africans and Americans. I really enjoyed it!

Tafsiri yangu:

Jambo Joseph. Nakufahamisha tu kwamba nimeweka kitabu chako sehemu vinapoonyeshwa vitabu vilivyopendekezwa na wahudumu wa duka la Barnes and Noble Burnsville ambapo ninafanya kazi. Kile kitabu juu ya tofauti za tamaduni baina ya wa-Afrika na wa-Marekani. Nilikifurahia sana!


Bwana huyu aliyeniandikia ujumbe alikuwa mhudumu wa duka la vitabu la hapa Chuo cha St. Olaf,  na ndipo alipokisoma kitabu changu. Yeye na wahudumu wenzake tulikuwa tukipenda kuongea. Kwa kuwa walikuwa wamesoma kitabu changu, walipokuwa wanaenda kujisaidia walipenda kusema, "kuchimba dawa," usemi waliouona kitabuni. Tulikuwa tukicheka. Nilikuwa nikivunjika mbavu na kujisikia raha kuwasikia hao wazungu wakiwa wa-Swahili namna hiyo. Niliona kitabu changu kimewagusa.

Nimefurahi kusikia kuwa kitabu changu kimeingia Barnes and Noble namna hiyo. Nasema ”namna hiyo” kwa maana ya kitabu kuwemo dukani, kwani, kwa miaka, kimekuwepo kwenye mtandao wa Barnes and Noble. Sitaki kusema mengi, nisije nikawa nahesabu vifaranga kabla havijaanguliwa, kama isemavyo methali ya ki-Ingereza. Nitasubiri nione.

Comments

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini