Posts

Showing posts from May, 2012

Warembo Wengine Hawa Hapa

Image
Siku chache zilizopita, niliweka makala kuhusu mrembo hapa katika blogu yangu . Lengo langu lilikuwa kuchochea mjadala kuhusu suala la urembo, ambalo, kama nilivyogusia, nimelijadili katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Nimeona picha nyingine ya warembo katika mtandao wa Facebook, ambayo naileta hapa. Sisi tuliokulia vijijini Afrika tunaweza kusema kuwa ingekuwa bora kama hao warembo wangejisitiri vizuri zaidi kimavazi. Lakini huenda hao si wa-Afrika. Hapa Marekani, kwa mfano, wakati wa joto, watu wengi huvaa vivazi ambavyo kwetu tunaviona si vya heshima, lakini hapa wanaona ni sawa.

Tamko la Askofu Mkuu Kufuatia Vurugu za Zanzibar

Image
TAMKO LA ASKOFU MKUU WA TANZANIA ASSEMBLIES OF GOD, DK.BARNABAS MTOKAMBALI, KUHUSU MATUKIO YANAYOASHIRIA UVUNJIFU WA AMANI NCHINI. Kwa kipindi kirefu sasa kumekuwa na mfululizo wa matukio yanayoashiria uvunjifu wa amani, umoja na utengamano wa taifa letu la Tanzania, haya ndiyo yanayonisukuma kutoa tamko hili leo ili kuonya na kushauri. Katika siku za karibu kiumeibuka makundi mbalimbali ya kidini ambayo yalianza kutoa matamko yenye kuchochea ghasia za kidini Tanzania, na pengine kauli hizo ndizo zinazotimizwa kwa vitendo hivi sasa. Miongoni mwa matukio hayo ni: Januari sita mwaka huu, kikundi kimoja kinachoitwa JUAKATA, kiliitisha kongamano la kujadili katiba mpya Tanzania, kwa upande wa Waislam. Katika kongamano hilo lililofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam kauli zifuatazo: 1. Lazima Rais ajaye atoke Zanzibar 2. Kukabiliana na ukuaji wa kasi wa dini ya Kikristo 3. Kupinga Muungano ili kuupa nguvu Uislamu 4. Kupigana kufa na kupona kutetea masla

Uamsho (Zanzibar): Taarifa kwa Vyombo vya Habari

Image
Jumuia ya Uamsho (Zanzibar) imetoa taarifa kufuatia maandamano na kisha vurugu zilizotokea Zanzibar wiki hii. Nimezipata picha na taarifa kutoka Zanzibar Yetu . Inatia moyo kuona jinsi taarifa hiyo inavyoanza kwa kumtaja Allah na Mtume Muhammad na kisha kusisitiza suala la amani na kuheshimu haki za watu wote. Inatia moyo kuona jinsi taarifa hii inavyotaja wazi kuwa tunawajibika kuheshimiana, kutunza amani, kuheshimu mali na haki za kila mtu, ikiwemo kuheshimu dini na nyumba za ibada. Hayo ni mawaidha mema kabisa. Ingekuwa mawaidha hayo yanatolewa na kusisitizwa kila wakati, katika mihadhara yote na mahubiri mengine, nje na ndani ya nyumba za ibada, nina imani amani ingedumu katika jamii. Lakini je, mawaidha hayo ndiyo yanayotolewa na kusisitizwa katika mihadhara na mahubiri yote? Hapa kushoto ni picha mojawapo ya uharibifu uliofanyika wakati wa vurugu za wiki hii, ambapo kanisa lilichomwa moto , sambamba na hilo gari. Waumini wa dini zote tunaweza kunukuu misahafu na kuthibi

Wa-Tanzania Katika Shughuli za Kila Siku

Image
Ninawawazia watu ninaowaona mitaani, kila mtu akiwa na harakati zake, mategemeo yake, na bila shaka wasi wasi na shida pia. Laiti ingewezekana kuongea na kila mtu na kuzipata habari zake. Hapa ni Ubungo. Nilipiga picha hii nikiwa ndani ya basi kutokea mikoani. Nilivutiwa na huyu kijana mwenye mkokoteni, akiwa katika kujitafutia riziki. Barabara inavyopinda kushoto inaelekea Chuo Kikuu na Mwenge. Hapa ni mjini Moshi. Hapa ni kituo cha mabasi cha Msamvu, Morogoro. Hapa ni Lyulilo, karibu na Matema Beach, Ziwa Nyasa. Ni siku ya soko, kama nilivyoelezea hapa .

Mbunge Mnyika Ashinda Kesi

Image
Mimi kama raia wa Ubungo nimevutiwa na picha hii, inayowaonyesha wananchi wakiwa wamembeba mbunge wetu, Mheshimiwa John Mnyika baada ya kushinda kesi ya uchaguzi iliyokuwa inamkabili. Tuko pamoja.  (Chanzo: Matukio-Michuzi )

Makaa Yetu ya Mawe Yanakwenda Wapi?

Image
Hapa ni Bandari ya Ndumbi iliyopo mwambao mwa ziwa Nyasa.Bandari hii inatumika kusafirishia makaa ya mawe ambayo yanachimbwa katika kijiji cha Ngaka wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.Takwimu zinaonesha kuwa kila wiki zaidi ya tani 600 za makaa ya makaa ya mawe zinasafirishwa kupitia bandari hii kupelekwa sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi.Hata hivyo hakuna anayefahamu ukweli kuhusu kile ambacho kinasafirishwa kupitia bandari hiyo ambayo haina ofisi muhimu za serikali.  (Picha na maelezo na Albano Midelo, Maendeleo ni Vita )

Mnadani Karatu

Image
Tanzania ni nchi kubwa, yenye mengi ya kuvutia. Mwaka 2008, kwa mfano, nilishuhudia mnada katika mji wa Karatu. Watu walijaa hapo kwenye viwanja vya mnada. Walikuwepo wauzaji na wateja wa bidhaa na huduma mbali mbali. Wengine, kama mimi, tulienda kuangalia. Kulikuwa na mengi ya kuyaona na hata kustaajabia. Mnada hufanyika Karatu kila mwezi, tarehe 7. Katika pitapita zangu katika sehemu kama Mbulu, Karatu na Arusha, nimeona kuwa utamaduni huu wa minada umejengeka sana. Siku ya mnada ni siku muhimu katika maisha ya watu wa sehemu hizo. Nami nikiwa maeneo hayo, sitakosa kuhudhuria.

Mteja Anaporudi Tena

Image
Niliwahi kuandika habari ya hao akina mama wanaoonekana nami katika hii picha, jinsi walivyonitembelea ofisini . Huyu aliyesimama kulia kanipigia simu wiki hii akiulizia upatikanaji wa nakala za kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences " . Nakala aliyokuwa nayo imeazimwa na rafiki yake. Anataka nakala nyingine kwa ajili yake na kwa marafiki zake wengine. Mmoja wao anaenda Ghana, aende akifahamu atakayokumbana nayo kule, niliyoelezea kitabuni. Basi, kwa kuzingatia yale ninayojifunza na kuwahubiria wengine kuhusu huduma kwa mteja , nimelitekeleza ombi hilo haraka na kumpelekea vitabu. Mteja anapokuja tena, kwa hiari yake mwenyewe, ni dalili nzuri. Inamaanisha karidhika au kafurahia huduma. Nawashangaa wanaoamini kuwa wateja huvutwa kwa mitishamba.

Safari ya Afrika Kusini

Nimepata mwaliko kutoka mamlaka inayojumuisha vyama vya taaluma hapa Marekani, ACLS . Ni mwaliko wa kwenda kushiriki mkutano wa wanataaluma utakaofanyika katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand , Afrika Kusini, Juni 15-17. Tutakutana katika kitengo cha utafiti kiitwacho WISER . Ni fursa ya wanataaluma mbali mbali kubadilishana mawazo na kutathmini hali na mwelekeo wa taaluma katika Afrika na ulimwenguni. Sijawahi kukanyaga Afrika Kusini. Kwa hivi ninaingojea safari hii kwa hamu. Chuo Kikuu cha Witwatersrand ni maarufu. Kwa upande wangu, ninaposikia jina la Witwatersrand, au Johannesburg kwa ujumla, huwa nakumbuka mengi. Mbali ya harakati za ukombozi kama zile zilizoibuka Soweto, na mbali ya maandishi mbali mbali ambayo nimesoma na kufundisha katika masomo ya fasihi, jambo jingine muhimu kwangu ni kwamba baadhi ya vitabu vya Shaaban Robert vilichapishwa na Witwatersrand University Press. Hii ni kumbukumbu muhimu sana kwangu, na ningependa kuitembelea taasisi hiyo, ikiwezekana. Kama kawa

Burudani Longido

Image
Hapa kushoto ni mpiga gitaa tuliyemkuta Longido mwaka 2008. Longido ni mji mdogo kwenye barabara itokayo Arusha kwenda Namanga. Ni karibu na Namanga. Nilikuwa hapo na wanafunzi katika kozi kuhusu mwandishi Hemingway . Tulikaa hapo siku mbili, tukifuatilia habari za Hemingway, ambaye alikuwa Kenya na Tanganyika miaka ya 1933-34 na 1953-54, akaandika mambo kadhaa kutokana na kuwepo kwake pande hizi. Hapo Longido tulikuwa wageni wa programu ya utalii inayoendeshwa na wenyeji wa hapo. Akina mama walitupikia vizuri na baada ya chakula cha jioni ilifuata burudani ya muziki. Huyu ndugu alikuwa anapiga gitaa na kuimba nyimbo mbali mbali, zikiwemo "zilipendwa" za Afrika Mashariki na za Marekani. Tulifurahi sana kwa burudani hiyo.

Mrembo

Image
Katika kitabu changu kiitwacho Africans and Americans: Embracing Cultural Differences , pamoja na masuala mengine, nimeongelea suala la urembo. Nimesema kuwa dhana ya urembo ni tofauti katika tamaduni mbali mbali na katika mazingira mbali mbali. Kwa mfano, nimenukuu hadithi ya mapokezi ya kabila la Efik-Ibibio, Nigeria, inayoelezea unene kama kigezo cha urembo: There was once a very fat woman who was made of oil. She was very beautiful and many young men applied to her parents for permission to marry her and offered a dowry; but the mother always refused. Kifungu hiki nimekinukuu katika ukurasa 54 wa kitabu changu, na naweza kutoa tafsiri hii: Alikuwepo mwanamke mnene sana aliyeumbwa kwa mafuta. Alikuwa mzuri sana na vijana wengi waliwaomba wazazi wake ruhusa ya kumwoa wakatoa mahari, lakini mama mtu daima alikataa . Katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii , kuna sehemu ambayo inaongelea mashindano ya urembo, kukumbushia kuwa kila jamii inayojitambua na kujiheshimu i

Kibonzo cha Mpangala

Image
Kwa kibonzo hiki, shukrani kwa Nathan Mpangala .

Kituoni Mbamba Bay

Image
Hapa ni eneo la kituo cha mabasi Mbamba Bay. Kama hakuna basi, unachoona ni huu uwanja na maduka pembeni, Nilikuwepo Mbamba Bay mwaka jana, kama nilivyoelezea hapa . Picha zinazoonekana hapa nilipiga wakati huo. Upande wa kulia wa mlima unaoonekana ndipo ziwani. Maduka yameuzunguka uwanja huu, kama nilivyogusia hapa . Nyumba inayoonekana kulia katika picha hii hapa ndio ofisi ya kukatia tiketi. Kwa vile mji ni mdogo sana, na mabasi ni labda mawili tu kwa siku, ofisi haina kazi nyingi kama ilivyo katika miji mikubwa. Basi likishafika, uwanja huu unapata uhai, kwa maana ya kuwepo na watu wengi, wakiwemo wasafiri wanaoshuka na wengine wanaopanda basi. Basi hili lilikuwa linatoka Liuli, likiwa njiani kwenda Songea.

Mama Mjasiriamali, Baina ya Matema Beach na Tukuyu

Image
Mwaka jana, nilifika hadi mkoani Mbeya, nikiwa na wanafunzi kutoka Marekani, kama nilivyoelezea hapa . Tukiwa njiani kutoka Matema Beach kuelekea Tukuyu, tulimkuta mama anauza soda na bidhaa zingine katika kibanda kando ya barabara. Mama huyu anaonekana hapa kushoto kabisa. Tulisimama hapo na kununua vitu viwili vitatu. Kila ninapomkumbuka mama yule najiwa na mawazo ambayo yalinijia siku ile. Ni kuhusu wajasiriamali wanawake. Nimesoma taarifa kuwa akina mama hao wenye kipato hafifu wakiwezeshwa, huwa wajasiriamali makini. Mama kama huyu akipata mtaji mkubwa anaweza kufanya mambo makubwa.

The Snows of Kilimanjaro

Image
Wiki hii, nimesoma tena "The Snows of Kilimanjaro," hadithi maarufu ya Ernest Hemingway mwandishi m-Marekani aliyezaliwa mwaka 1899 akajiua kwa risasi mwaka 1960. Baada ya kusoma hadithi kwa makini, nimeangalia tena DVD iliyotokana na hadithi hii, ambamo waigizaji wakuu ni Gregory Peck na Ava Gardner. Nimefuatilia maandishi na maisha ya Hemingway kwa muda mrefu. Hakuna siku inayopita bila mimi kusoma, kuwazia, au kuongelea habari za Hemingway. Ni mwandishi ambaye amenigusa kwa namna mbali mbali, kuanzia kipaji cha uandishi hadi falsafa yake kuhusu mambo mengi. Nimeunda hata kozi kuhusu mwandishi huyu, kama nilivyoelezea hapa na hapa . "The Snows of Kilimanjaro" ni hadithi mojawapo maarufu kuliko zote katika lugha ya ki-Ingereza. Inamhusu mwandishi aitwaye Harry, ambaye tunamwona mbugani karibu na Kilimanjaro, akiwa anauguza kidonda mguuni, kilichotokana na kuchomwa mwiba wakati akiwinda. Ni kidonda kibaya, ambacho kinaonekana kutishia maisha ya Harry. Tunamwo

Nkrumah Hall, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Image
Ukumbi wa Nkrumah ni moja ya sehemu muhimu sana katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Tangu nilipojiunga na Chuo hiki kama mwanafunzi, mwaka 1973, nilishuhudia umuhimu wa ukumbi huu wa mikutano. Kwanza, napenda kusema kuwa ni jambo la heshima kuwa ukumbi huu ulipewa jina la Nkrumah, kiongozi maarufu wa harakati za ukombozi Afrika na duniani. Watu maarufu walihutubia katika ukumbi huu. Miaka niliyosoma na kufundisha pale, tuliwasikiliza watu kama Mwalimu Nyerere, William Tolbert, Gatsha Buthelezi, Robert Mugabe, Agostino Neto, Gora Ibrahim, Ali Mazrui, na Samir Amin. Ukumbi huu ulikuwa ni sehemu ya mijadala baina ya watafiti na walimu maarufu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kama vile Walter Rodney, Wadada Nabudere, Yash Tandon, Mahmoud Mamdani, na Issa Shivji. Kila aliyesoma au kufundisha hapa chuoni atakuwa na kumbukumbu za mambo au matukio ya ukumbi wa Nkrumah. Nami nina kumbukumbu zinazonihusu moja kwa moja. Kwa mfano, nilipokuwa mhadhiri msaidizi, bado kijana, jumuia ya wali