Darasa Chuo Kikuu Dar es Salaam
Leo nilikwenda Chuo Kikuu Dar es Salaam kuongea na wanafunzi wa shahada ya juu katika ki-Swahili. Profesa Mugyabuso Mulokozi, aliyeketi hapo juu mstari wa mbele kushoto, alikuwa amenialika kuongea na wanafunzi wake hao katika somo la tendi. Walikuwa wakijadili utendi wa Hamziya , nami nilikaribishwa kuongelea tendi kwa ujumla. Niliongelea dhana kadhaa zihusuzo tendi, hasa dhana ya ushujaa, nikitoa mifano ya tendi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kama vile Illiad , Gilgamesh , Sundiata , Kalevala , Ozidi , na Liongo . Msimamo wangu kama nilivyoulezea katika maandishi kadhaa, ni kwamba dhana ya ushujaa ndio msingi wa tendi. Niliwaeleza kuwa tendi zinahitaji kuangaliwa kwa uyakinifu, kwa kuzingatia mabadiliko yake, na jinsi zinavyojitokeza katika sura mbali mbali. Kwa mfano, shujaa katika masimulizi ya utendi fulani anaweza asiwe shujaa katika masimulizi hayo hayo katika jamii tofauti. Wazo moja ambalo lilionekana kuwasisimua wanafunzi ni mchango wa wanawake katika ten