Posts

Showing posts from January, 2015

Katika Blogu, Sijui Ninamwandikia Nani Zaidi Yangu Mwenyewe

Image
Je, mwandishi wa blogu anamwandikia nani? Kwa mtazamo wangu, hili ni suali gumu. Naliona gumu kulitafakari, achilia mbali kulijibu. Baada ya kuona ugumu wa suali hili, nimeamua kukiri kuwa ninajiandikia mwenyewe. Ndio maana makala ninazoandika aghalabu zinanihusu mimi mwenyewe, shughuli zangu, matatizo na mafanikio yangu, mategemeo yangu na kumbukumbu zangu. Sipendi sana kuwaongelea watu wengine, wala sipendi sana kuongelea mambo kinadharia, bila kujihusisha mwenyewe. Naweza kusema kuwa ndivyo nilivyoandika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Sijajificha nyuma ya pazia la nadharia au taaluma. Nimejiweka wazi kwa namna nilivyoweza. Mwandishi Ernest Hemingway aliongelea suala hili vizuri alipofafanua dhana ya ukweli katika uandishi. Nilivyomwelewa, anasema kuwa ukweli katika uandishi ni kwa mwandishi kuifungua na kuiweka bayana nafsi yake. Ningependa sana niweze kuandika namna hii aliyoongelea Hemingway. Ni ndoto inayovutia, sawa na nyota inayong

Mipango ya Ziara Yangu Mankato Inaendelea

Kama nilivyoandika katika blogu hii , nitakwenda kuongea na wanafunzi wa chuo cha South Central mjini Mankato. Mipango ya ziara hii, ambayo itafanyika tarehe 24 Februari, inaendelea vizuri. Mwenyeji wangu, mwalimu Rebecca Fjelland Davis , amenieleza kuwa shughuli ya kwanza nitakayofanya siku hiyo ni kuongea na wanafunzi katika darasa lake, kuanzia saa nne hadi saa tano na dakika hamsini asubuhi. Hao ni wanafunzi wanaojiandaa kwa safari ya kimasomo Afrika Kusini. Kama sehemu ya maandalizi hayo, wanasoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences , na maongezi yangu nao yatahusu yale niliyoandika kitabuni. Baada ya darasa hilo, kuanzia yapata saa sita, nitatoa mhadhara kwa wanachuo na wana jamii. Mwalimu Fjelland Davis ameniarifu kuwa duka la vitabu la hapo chuoni litakuwa limeandaa nakala za kitabu changu, kwa ajili ya kuuza. Kama ilivyo desturi hapa Marekani, nategemea kuwa baada ya mazungumzo nitasaini nakala za vitabu. Hii sio mara yangu ya kwanza

Wanachuo wa Gustavus Adolphus Wako Tanzania

Image
Wanachuo wa chuo cha Gustavus Adolphus , ambao niliongea nao kabla ya safari yao, walifika salama Tanzania. Wako Tanzania kwa ziara ya kimasomo kwa mwezi moja. Wamekuwa wakiandika kuhusu ziara yao katika tovuti ya chuo chao . Walitua uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro wakatembelea sehemu kama hospitali ya KCMC na shule ya wasichana ya Maasae . Kisha walienda Iringa, ambako wameshatembelea sehemu kama vile Chuo Kikuu cha Iringa , soko kuu, na hospitali ya Ilula . Wamesafiri hadi Tungamalenga, pembeni mwa hifadhi ya Ruaha, ambapo wamepata fursa ya kutembelea hospitali na kuangalia utendaji kazi wake. Kwa ujumla, wanachuo hao, kama ilivyo kwa wa-Marekani wengine wanaotembelea Tanzania, wanaifurahia nchi yetu na watu wake. Wanawasiliana na familia zao na marafiki huku Marekani, na kwa namna hii jina la Tanzania linasambaa kwa namna nzuri. Kwa kawaida, ziara za wanafunzi nazienzi kuliko zile za watalii. Kwa vile wanafunzi wanajumuika na wananchi katika mazingira mbali mbali,

Kwa Anayewazia Kuchapisha Kitabu

Wazo la kuchapisha kitabu linawavutia watu wengi. Ni wazo lenye ndoto za mafanikio.Wako wanaoamini kuwa kuchapisha kitabu kutawapa umaarufu. Kuna wanaoamini kuwa kuchapisha kitabu kutawaletea fedha nyingi. Wengi, labda wote, wanaamini kuwa wakisha chapisha kitabu, kazi yao inakuwa imemalizika; kinachobaki ni kungojea matokeo, kama vile umaarufu na fedha. Ni bora mtu anayewazia kuchapisha kitabu ajielimishe zaidi kuhusu jambo hili, nami hupenda kuchangia yale ninayoyafahamu, kwa kadiri ya uwezo wangu. Vipengele ni vingi, lakini hapa nitaongelea vichache tu. Mtu uandike kitabu kutokana na kujua kuwa una jambo la kusema kimaandishi. Uwe una jambo ambalo linakuelemea akilini mwako na kukusukuma uandike. Msukumo utoke ndani ya nafsi yako. Ukishaandika kitabu kwa msingi huo, utajisikia una raha sawa na mtu aliyetua mzigo. Kuridhika kwako ndilo jambo mihimu. Mengine yanafuata baadaye. Huenda kitabu chako kitawavutia watu wakakinunua na kukisoma, au huenda kisiwavutie. Lakini sidhani kam

Mihadhara Nisiyolipwa

Image
Nimewahi kuongelea suala la kulipwa ninapotoa mihadhara . Nilisema kuwa wa-Marekani wanapokualika kutoa mhadhara huuliza malipo yako ni kiasi gani. Nilitamka kuwa huwa sitaji kiasi ninachotaka kulipwa, bali nawaachia wanaonialika waamue kufuatana na uwezo wao. Hata kama hawana uwezo, niko tayari kuwatimizia ombi lao. Napenda kufafanua kidogo kuhusu utoaji wa mihadhara bila kulipwa. Labda wako watu ambao watashangaa kwa nini ninaridhika kutoa mihadhara ya aina hiyo. Labda wako watakaosema ninapoteza muda wangu. Huenda wengine wataniona nimechanganyikiwa. Ni jambo la kawaida kwetu wanadamu kuwa na fikra na mitazamo inayotofautiana. Nina sababu zangu kwa kuwa na huu msimamo wangu. Kwanza ninatanguliza ubinadamu na utu, sio hela. Kuwasaidia wengine ni jambo jema sana, ambalo lina maana kuliko hela. Unaweza kuwa na hela nyingi ukazifuja, zisikuletee faida yoyote maishani, lakini, kama walivyosema wahenga, wema hauozi. Kuna usemi mwingine, "Tenda wema nenda zako; usingoje shukrani

Rakesh Rajani, Muasisi wa TWAWEZA, Aaga Tanzania

"Leading Beyond the Walls:" Kitabu Murua

Image
Kwa siku kadhaa sasa, nimekuwa nikisoma Leading Beyond the Walls: How High-Performing Organizations Collaborate for Shared Success , kitabu kilichohaririwa na Frances Hesselbein, Marshall Goldsmith, na Iain Somerville. Ni mkusanyo wa makala 23 zilizoandikwa na wataalam mbali mbali katika tasnia ya uongozi, wakizingatia hali halisi ya utandawazi wa leo, na umuhimu wa kwenda na wakati. Kwenda na wakati kunahitaji wepesi wa kubadilika kifikra, kimwenendo, kimfumo na hali zingine, ili kumudu mahitaji na hali halisi ya mabadiliko yanayotokea ulimwenguni, ambayo hayakwepeki. Mafanikio ya shirika, taasisi, au kampuni yanategemea utayari wa kujibadili. Mazoea ni kipingamizi kikubwa cha mafanikio; ni kama kuta ambazo tumejizungushia. Jukumu letu, ambalo halikwepeki, ni kuvunja hizo kuta, tuwe na uwanja na upeo usio na mipaka. Wengi wa watunzi wa makala zilizomo kitabuni humu nilikuwa sijawahi hata kuwasikia, isipokuwa Joseph S. Nye, Jr., Stephen R. Covey, na Peter F. Drucker, ambaye niliwa

Maazimio ya Mwaka Mpya, 2015

Image
Kila unapoanza mwaka mpya, ni kawaida kwa watu kujipangia au kuweka bayana mambo ya kufanya katika mwaka unaoanza. Nami nina yangu, lakini kwanza namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuuvuka mwaka uliopita na kuingia katika mwaka huu mpya. Jambo la msingi ninalopangia ni kuendelea kufanya bidii katika kazi ambayo naamini Mungu mwenyewe alinipangia, kazi ya ualimu. Kazi hii inajumlisha mambo kadhaa hasa kujielimisha na kuwa tayari muda wote kuwapa wengine yale ninayoyajua. Elimu yangu si yangu pekee, bali ni dhamana kwa manufaa ya wanadamu. Nitaendelea kusoma vitabu na makala za kitaaluma kwa bidii. Hii ni njia muhimu ya kujielimisha, ili niweze kufundisha kwa ufanisi zaidi. Nitaendelea kutoa ushauri kwa jumuia na taasisi yoyote au kwa watu binafsi. Hii sio tu kwa faida yao, bali kwa faida yangu, kwani kwa kufanya hivyo ninapata fursa ya kupima ni kiasi gani ninafahamu jambo fulani. Nitaendelea kufanya utafiti na kuandika. Kuandika ni aina ya ufundishaji. Mwalimu wa kiwango cha

Tumefanya Kikao cha Bodi ya "Africa Network"

Leo tulikuwa na kikao cha bodi ya Africa Network . Hii jumuia ya vyuo vya Marekani ambavyo vinataka kushirikiana katika ufundishaji na utafiti kuhusu Afrika. Mwanzilishi wake ni Profesa Tom Benson. Kikao chetu cha leo kilikuwa cha kutumia simu ("teleconferencing"). Hii ni tekinolojia ambayo haihitaji watu kusafiri na kukutana uso kwa uso. Nimeshiriki mikutano ya aina hii mara nyingi katika nyadhifa zangu kama mwanabodi wa Africa Network  na  Afrifest. Leo tumeongelea zaidi masuala ya kutafuta fedha, kuboresha tovuti yetu, na kupata wanachama wengine. Mbali na suala la tovuti yetu, tumeongelea pia suala pana zaidi la kujiingiza katika mitandao ya kijamii kama Facebook na Twitter. Jambo jingine muhimu ambalo tumekubaliana ni kuwa badala ya kuwa na mkutano wa jumuia yote mwaka huu, tufanye kikao cha wanabodi pekee, ili kujinoa katika masuala mbali ya uendeshaji wa Africa Network na kujipanga kwa miaka ijayo. Tutafanya kikao hiki mwezi Aprili, mjini Chicago.

""Till I End My Song:" Tungo za Mwisho za Washairi Maarufu

Image
Kila siku ninapokuwa chuoni St. Olaf , ambapo nafundisha, sikosi kupita katika duka la vitabu. Mbali ya vitabu vilivyomo dukani, wanaweka pia vitabu vingi kwenye meza na makabati nje ya duka. Hapo nje unaweza kuvipata vitabu kwa bei nafuu kuliko kuviagiza wewe mwenyewe sehemu nyingine. Basi, siku moja, katika kuangalia angalia vitabu hapo nje, nilikiona kitabu ambacho rangi za jaladaa lake zilinivutia. Nilivutiwa zaidi nilipoona kimehaririwa na Harold Bloom, na kinauzwa kwa  dola 4.98, ambalo ni punguzo kubwa, kwani bei yake ya halisi ni dola 24.99. Hapo hapo niliamua kukinunua, ingawa nilikuwa na hela kidogo tu, kwani ilikuwa ni mara tu baada ya Krismasi, huku tungiingojea siku kuu ya Mwaka Mpya. Harold Bloom ni bingwa mojawapo duniani katika masomo ya ki-Ingereza na fasihi yake, sio tu kwa upande wa uchambuzi wa maandishi bali pia upande wa nadharia ya fasihi. Ameandika au kuhariri vitabu vingi. Nilipokuwa nasomea shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu Cha Wisconsin-Madison , 1980-

Mazungumzo ya Jana na Wanachuo wa Gustavus Adolphus Yalifana

Jana niliandika taarifa fupi kuhusu mazungumzo yangu na wanachuo wa chuo cha Gustavus Adolphus . Ningeweza kuandika kirefu na kuelezea, kwa mfano, masuali niliyulizwa kuhusu yaliyomo na yasiyokuwemo katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Ningeweza kuelezea jinsi wanachuo na wakufunzi wao walivyoyapenda mazungumzo yale, kama walivyoniambia wao wenyewe. Lakini niliona ni bora ningoje watakavyoandika kuhusu mazungumzo yale, wakiwa peke yao bila mimi. Nimeona leo kuwa tayari mmoja wa wanachuo ameshaandika kwenye tovuti ya chuo chao . Sishangai kusikia kauli kama ya mwanafunzi huyu, kwani ninapoalikwa popote kutoa mhadhara, ninalichukulia jukumu langu kwa umakini . Ni namna yangu ya kuwaheshimu wanaonialika na wale watakaohudhuria. Ni kudhihirisha jinsi ninavyoiheshimu taaluma na jinsi ninavyojiheshimu mwenyewe kama mwanataaluma. Kwa jinsi ninavyowafahamu wanafunzi wa Marekani, kuna uwezekano mkubwa kuwa wengine wataandika pia, na nikiona taarifa z

Mkutano na Wanachuo wa Gustavus Adolphus

Image
Leo asubuhi nilikwenda Mount Olivet Conference & Retreat Center , eneo la Farmington, hapa Minnesota, kuongea na wanachuo wa chuo cha Gustavus Adolphus ambao wanaelekea Tanzania kimasomo. Kwa siku hizi mbili tatu kabla ya safari yao, wamekuwa katika maandalizi, nami niliitwa na profesa wao Barbara Zust, kuongea nao kuhusu masuala ya utamaduni ambayo yamo katika kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Nimeshaalikwa mara kadhaa miaka iliyopita, kuongea na wanachuo wa Gustavus Adolphus , katika maandalizi ya kwenda Tanzania, kama nilivyoelezea katika blogu hii . Nilikuwa nimeamua kuwa leo, baada kutoa utangulizi mfupi, nitumie muda karibu wote katika kujibu masuali ya hao wanachuo, kwani nilishafahamishwa kuwa watakuwa wamekisoma kitabu changu. Ilidhihirika wazi, kutokana na masuali yao, kuwa walikuwa wamekisoma kwa makini. Wote tuliyafurahia mazungumzo yetu, ambayo yalidumu kuanzia saa nne hadi saa sita. Baada ya hapo, tulikula chakula cha mcha

Kwa Kina na Prof. Joseph Mbele

Image
Niliwahi kuhojiwa na Jeff Msangi, mwanzilishi na mmiliki wa blogu ya Bongo Celebrity . Yeye, pamoja na Freddy Macha, ambaye ni mwandishi, mwanamuziki, na mwanzilishi wa blogu ya Kitoto , ndio walionihamasisha kuanzisha blogu. Daima ninawashukuru hao ndugu wawili, ambao ni wafuatiliaji makini wa maandishi yangu. Mahojiano yangu na Jeff Msangi yalifanyika mwaka 2008, lakini naona yanastahili kujadiliwa hata leo na siku zijazo. Wadau wengi walichangia maoni yao ambayo unaweza kuyasoma hapa . Mahojiano haya yamechapishwa pia katika kitabu changu cha Changamoto: Insha za Jamii . . ------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------- KWA KINA NA PROF.JOSEPH MBELE     Mbali na kuwa na utajiri wa asili wa aina yake,Tanzania ni nchi ambayo inajivunia kuwa na wasomi maarufu ambao wametapakaa kote ulimwenguni wakifundisha katika mashule na vyuo mbalimbali au kuongoza vitengo nyeti katika idara za kimataifa na zen