Posts

Showing posts from May, 2017

Likizo Inaanza: Ni Kujisomea Vitabu na Kuandika

Image
Tumemaliza muhula wa mwisho wa mwaka wa masomo hapa chuoni St. Olaf.  Tunamalizia kusahihisha mitihani na matokeo yatakuwa yamekamilika tarehe 5 Juni. Kuanzia pale tutakuwa na miezi mitatu ya likizo. Lakini kwetu waalimu, likizo si likizo, bali fursa ya kujisomea, kufanya utafiti, na kuandika, bila kuhusika na ufundishaji darasani. Mpango wangu kwa likizo hii ni kutumia wiki sita za mwanzo katika kujisomea vitabu na kuandika, halafu wiki sita zitakazofuata nitafundisha kozi ya fasihi ya Afrika. Kufundisha kipindi hiki cha likizo ni jambo la hiari. Mwalimu anatangaza kozi anayotaka kufundisha na wanafunzi wanaohitaji wanajisajili. Wanafunzi huwa wachache. Ni fursa nzuri kwa mwalimu kujaribisha mambo mapya. Wakati huu ninavyoandika ujumbe huu, ninafadhaika katika kuamua nisome vitabu vipi. Maktaba yangu ina vitabu vingi ambavyo sijavisoma. Kwa likizo hii, nimewazia nisome tamthilia za William Shakespeare, au George Bernard Shaw, au Sean O'Casey, au Anton Chekhov, au riwaya za Orh

"Witchcraft by a Picture" (John Donne)

Image
Juzi, nilinunua kitabu cha mashairi kiitwacho  The Works of John Donne, kama nilivyosema katika blogu hii. John Donne aliishi Uingereza, hasa London, miaka ya 1572-1631. Katika kuyasoma mashairi yake, nimeona kuwa yanahitaji utulivu wa pekee, na tafakari, kwani matumizi yake ya lugha yanaonyesha uangalifu mkubwa. Ki-Ingereza chake ni cha miaka ile, ambayo ni miaka ya William Shakespeare, si cha leo. Hapa naleta shairi mojawapo, "Witchcraft by a Picture." Labda siku moja nitapata ujasiri wa kujaribu kulitafsiri kwa ki-Swahili.          Witchcraft by a Picture I fixe mine eye on thine, and there      Pitty my picture burning in thine eye, My picture drown'd in a transparent teare,      When I looke lower I espie;           Hadst thou the wicked skill By pictures made and mard, to kill, How many wayes mightst thou performe thy will? But now I have drunke thy sweet salt teares,      And though thou poure more I'll depart; My picture vanish'd, van

Vitabu Nilivyonunua Leo

Image
Leo nikitokea Minneapolis, nilipita Apple Valley, katika duka la vitabu la Half Price Books. Nilikuwa nimepania kununua kitabu juu ya Hemingway, Hemingway's Boat: Everything He Loved in Life, And Lost , kilichotungwa na Paul Hendrickson, ambacho nilikifahamu kwa miezi, na hivi karibuni nilikiona katika duka hilo, kama nilivyoripoti katika blogu hii. Kwa hivi, leo niliombea nikikute hiki kitabu, na kwa bahati nzuri nilikikuta. Baada ya kukichukua mahali kilipokuwepo, nilienda sehemu panapouzwa vitabu kwa bei ndogo zaidi. Bila kuhangaika sana, niliona kitabu kiitwacho F. Scott Fitzgerald , kilichotungwa na Arthur Mizener.  Nilifungua kurasa mbili tatu, nikakichukua. Nilifahamu kwa muda mrefu kuwa Fitzgerald alizaliwa St. Paul, Minnesota, mji ninaoutembelea mara kwa mara. Nilishasoma riwaya yake maarufu, The Great Gatsby . Halafu, miaka hii ambapo nimekuwa nikisoma sana maandishi na habari za Ernest Hemingway, nimeelewa kuwa haiwezekani kumtenganisha Hemingway na Fitzgerald.

"Contagious Success," Kitabu Muhimu

Image
Nina furaha wakati huu kwa kuwa ninasoma kitabu kiitwacho Contagious Success: Spreading High Performance Throughout Your Organization . Nilinunua kitabu hiki siku chache zilizopita, kama nilivyoripoti katika blogu hii. Sikupoteza fedha zangu. Mwandishi wa kitabu hiki, mwenyekiti wa Hudson Highland Center for High Performance, ni mwenye ujuzi na uzoefu mkubwa. Kitabu chake hiki ni matokeo ya utafiti ulioshirikisha watu wa sehemu mbali mbali ulimwenguni, ambao ni wafanyakazi katika sekta zinazotegemea na kuendeshwa na ujuzi na maarifa. Kwa ki-Ingereza, watu hao huitwa "knowledge workers." Hii ni dhana muhimu katika dunia ya leo na kesho, ambayo inaendelea kuwa dunia ya "knowledge economy." Tangu mwanzo, kitabu hiki kina mafundisho muhimu kwa viongozi, mameneja, wamiliki wa biashara, watoa huduma na kadhalika. Ujumbe mahsusi ni namna ya kuyaeneza mafanikio katika shirika, kampuni, taasisi, au jamii. Mwandishi anasema: "Every company has high-performing work

Vitabu Nilivyonunua Jana

Image
Jana nilinunua vitabu vitatu katika duka la vitabu la chuoni St. Olaf. Viwili, Two Years Eight Months and Twenty-Eight Nights cha Salman Rushdie na A Strangeness in my Mind cha Orhan Pamuk, niliviona juzi. Cha tatu, Why Homer Matters , kilichotungwa na Adam Nicolson, nilikiona hiyo hiyo jana. Nilipoingia dukani, nilikumbuka makala niliyoisoma juzi usiku, kuhusu vitabu halisi na vitabu pepe.  Makala hii, sawa na nyingine nyingi, inatafakari iwapo vitabu vya jadi vitasalimika katika himaya hii ya vitabu pepe. Lakini inahitimisha kuwa hakuna ushahidi kuwa vitabu vya jadi vitapoteza mvuto au kufifia. Mimi ni mmoja wa wale ambao hatujabadilika. Bado tumezoea vitabu halisi, yaani vitabu vya jadi, na ndio maana sisiti kuvinunua, wala sisiti kuelezea tabia yangu hiyo. Hapa nitaelezea kifupi kwa nini nimenunua vitabu hivi vitatu. Kitabu cha Salman Rushdie kilinivutia kwa sababu ya umaarufu wa mwandishi huyu. Bila shaka wengi watakumbuka kitabu chake, Satanic Verses , ambacho kilipigw

Vitabu Nilivyonunua Leo

Image
Leo nilikwenda tena Apple Valley, kwa muda mfupi, nikaingia katika duka la Half Price Books. Niliangalia kwanza sehemu vinapowekwa vitabu vya Hemingway au juu ya Hemingway. Kitabu cha pekee nilichokiona, ambacho nimekifahamu kwa miezi kadhaa ila sijakinunua, ni Hemingway's Boat: Everything He Loved in Life, And Lost , kilichotungwa na Paul Hendrickson. Nilielekea sehemu ambapo huwekwa vitabu vya bei rahisi kabisa. Kwa kuwa sikuwa na muda mwingi, niliangalia haraka haraka, nikaona kitabu cha Matigari cha Ngugi wa Thiong'o, kilichotafsiriwa kwa ki-Ingereza na Wangui wa Goro. Ngugi alikuwa amekiandika kwa Kikuyu. Nilivutiwa kuona kuwa ni nakala ya jalada gumu, iliyochapishwa na Africa World Press. Nilichukua. Wasomaji wa Ngugi wanakumbuka kuwa tafsiri hii ilichapishwa kwanza na Heinemann. Kisha, sehemu hiyo hiyo, katika kuchungulia chungulia, niliona kitabu Contagious Success: Spreading High Performance Throughout Your Organization , kilichoandikwa na Susan Lucia Annunzio

Msikilize Raia wa Marekani Anavyomrarua Kiongozi

Image
Jambo moja linalonivutia kuhusu Marekani ni uhuru wa kujieleza. Katiba ya Marekani inalinda uhuru huo kikamilifu. Kwa mfano, kulikuwa na kesi dhidi ya mtu aliyechoma moto bendera ya Taifa, lakini mahakama kuu iliamua na imeendelea kusisitiza kuwa kuchoma moto bendera ya Taifa ni sehemu ya uhuru wa kujieleza, ambao unalindwa na katiba. Mahakama kuu inasisitiza kuwa kauli tata, za kukera, au za kuwakosoa watawala ndizo hasa katiba ilikusudiwa kuzilinda. Serikali ya Marekani inafahamu kuwa raia ana uhuru na haki kamili ya kuikosoa. Viongozi wa Marekani wanajua hilo. Ninaleta video hapa, inayomwonyesha mwananchi akimfokea kiongozi bila kumung'unya maneno. Mwone kiongozi huyu kutoka chama tawala cha Rais Donald Trump alivyonywea, wakati kipigo kinaendelea.

Shukrani kwa Msomaji

Image
Msomaji mwingine wa kitabu cha Africans and Americans; Embracing Cultural Differences amejitokeza na kuandika maoni yake kuhusu kitabu hiki. Ameandika maneno matatu tu, "Short and sweet," katika mtandao wa Goodreads , ambao ni maarufu miongoni mwa wasoma vitabu. Humo wanaweka maoni yao kuhusu vitabu walivyosoma au vitabu wanavyopangia kusoma. Kama ilivyo kawaida yangu katika blogu hii, ninamshukuru kwa kujipatia kitabu hiki, kukisoma, na kuwajuza walimwengu maoni yake. Amefanya hivyo kwa hiari yake, akijua kwamba kauli yake itasomwa na watu wengi. Namshukuru kwa hisani yake; amenifanyia kazi bila malipo wala kutegemea shukrani. Maoni ya wasomaji yana manufaa makubwa. Kwanza yananiwezesha kufahamu kama ninafikisha ujumbe wangu na unaeleweka vipi. Kila msomaji anapotoa maoni, hutaja jambo fulani au mambo fulani yaliyomgusa kwa namna ya pekee. Wasomaji wanaweza kuwa wamekipenda kitabu hicho hicho, lakini kwa misingi au namna mbali mbali. Pili, kuwepo kwa maoni ya waso

Mwanahabari Amy Goodman Amehutubia Hapa Kwetu

Image
Leo, mwanahabari na mwanaharakati maarufu Amy Goodman amehutubia chuoni Carleton hapa Northfield. Mada yake ilihusu "threats to freedom of the press and the importance of independent media," yaani mambo yanayotishia uhuru wa vyombo vya habari na umuhimu wa media zisizo chini ya mamlaka yoyote. Ninaamini tafsiri yangu inaweza kuboreshwa. Amy Goodman ni maarufu kama mwendesha kipindi kiitwacho Democracy Now!, ambacho kinachambua masuala kwa mtazamo tofauti na ule wa watawala wakandamizi na propaganda zao za kurubuni watu na kuhalalisha hali iliyopo. Mtazamo wa Amy Goodman ni wa kichochezi kwa maslahi ya walalahoi, wavuja jasho, na wale wanaoonewa na kudhulumiwa. Ni mwana harakati ambaye hasiti kujitosa sehemu ambapo watu wanadhulumiwa ili kuwaunga mkono na kuwezesha sauti zao kusikika ulimwenguni. Katika mhadhara wake wa leo, ameongelea zaidi hali ya Marekani, akiainisha madhaifu ya vyombo vya habari na media kwa ujumla. Alianza hotuba yake kwa kauli ya kusisimua na kufi