Posts

Showing posts from October, 2011

Wa-Islamu Vyuoni Marekani

Image
Leo tulikuwa na mjadala mjini Faribault, Minnesota, kuhusu wa-Islam vyuoni Marekani. Walioandaa mjadala ni Anna na Rachel, wanafunzi wa Chuo Cha Carleton. Walengwa walikuwa ni wazazi na vijana wa ki-Somali, ambao ndio jamii ya ki-Islam inayofahamika hapa Minnesota ya Kusini Mashariki. Hapa kushoto tunaonekana wanajopo tukiwa mzigoni. Rachel amejishughulisha na wa-Somali kwa kitambo. Aliwahi kufanya mahojiano nami miezi kadhaa iliyopita kuhusu changamoto zinazowakabili wa-Islam Marekani. Rachel na Anna waliniomba nikawe mwanajopo katika mjadala wa leo, kwa vile wanafahamu ninafahamika na kukubalika katika jamii ile. Mjadala ulilenga kuwapa fursa wazazi na vijana kufahamu hali halisi, faida na changamoto za vyuo kwa wa-Islam ambao pia ni wahamiaji kutoka Afrika. Wazazi na vijana walipata fursa sawa ya kuelezea mawazo yao, mitazamo, mategemeo, wasi wasi na mapendekezo. Zilijadiliwa changamoto wanazokabiliana nazo vijana wa kiIslam wanapowazia au kujiandaa kupeleka maombi ya kujiu

Katuni: Sisiem Haing'oki, Labda Mlete NATO

Image

Mwandishi Nuruddin Farah Katutembelea

Image
Jana jioni, mwandishi maarufu Nuruddin Farah, mzaliwa wa Somalia, alikuja chuoni Carleton , hapa Northfield, kuongea na wadau kuhusu riwaya yake mpya, Crossbones , ambayo imechapishwa mwaka huu. Nilienda kumsikiliza. Kama ilivyo kawaida katika shughuli za aina hii, vitabu vyake vilikuwepo, vinauzwa. Kwa vile ninavyo vitabu vyake vingine, nilinunua hiki kipya. Hapa pichani mwandishi anasaini nakala yangu. Bei yake ni dola 27.95, yapata shilingi 50,000 za Tanzania. Hiki ni kiasi kidogo sana ukifananisha na hela tunazotumia wa-Tanzania kwenye ulabu na makamuzi mengine. Bora kununua kitabu. Ingawa bado sijaisoma riwaya ya Crossbones , kwa kufuatilia mazungumzo ya jana na kuiangalia kijuu juu, ni riwaya inayohusu Somalia kabla tu na baada ya uvamizi wa kijeshi uliofanywa na Ethipia miaka michache iliyopita. Ni riwaya inayoelezea athari za matukio hayo katika maisha ya wahusika. Kwa bahati, nimeshamwona Nuruddin Farah mara kadhaa akihutubia, hapa Marekani. Vile vil

Vitabu Vyangu Vinapatikana Bagamoyo

Image
Ukiwa Bagamoyo, kwenye barabara itokayo kwenye makumbusho ya historia, Caravan Serai, kuelekea kwenye mgahawa wa Top Life, utaona duka upande wa kushoto liitwalo Sanaa Sana Art Shop. Mmiliki ni Dada Neema, mjasiriamali anayeuza vitu mbali mbali, kuanzia vinyago, vikapu, na nguo za ki-Tanzania, hadi picha na postikadi za ki-Tanzania. Nilionana naye hapa Bagamoyo mwaka jana, na ndipo alipofahamu habari za vitabu vyangu, akaamua awe anaviuza, kama wanavyofanya wajasiriamali wengine wawili watatu nchini Tanzania. Mimi si mfanyabiashara bali mwalimu na mwandishi. Ila niko tayari muda wote kuwawezesha wajasiriamali kuvipata vitabu vyangu. Namba ya simu ya duka la Dada Neema ni 0754 445 956.

Taswira za Mjini Songea

Image
Nchi yetu ya Tanzania ni kubwa sana. Ina mikoa, wilaya na vijiji vingi, na siamini kama yuko m-Tanzania atakayeweza kupita kila sehemu. Mimi mwenyewe nimebahatika kutembelea sehemu nyingi katika mikoa mbali mbali. Hata hivyo, kuna sehemu ambazo sijafika, kama vile Bukoba, Mpanda, Sumbawanga, na Singida. Kutokana na ukweli huo, ninawashukuru wanablogu ambao wamekuwa mstari wa mbele kutuletea habari na taarifa za sehemu mbali mbali za nchi yetu. Blogu ya Mwenyekiti Mjengwa ilinigusa kwa namna ya pekee tangu mwanzo, kwa jinsi alivyokuwa anatembelea vijiji ambavyo wengi wetu hatutavifikia. Kutokana na jinsi nilivyofaidika na jambo hilo, nami najaribu kuleta picha za sehemu mbali mbali, ili wa-Tanzania wengine wapate kuzifahamu sehemu ambako nimefika. Leo naleta baadhi ya picha nilizopiga mjini Songea mwaka huu. Nimeshaleta taarifa kadhaa za Songea katika blogu hii, kama vile hii hapa . Napangia kuleta taarifa na picha zaidi. Wale ambao hawajafika Songea watapata fununu kidogo kuhusu mah

Ukiwa na Siri, Iweke Kitabuni

Image
Hapa kuna picha nilizopiga kwenye tamasha la vitabu mjini Minneapolis, Oktoba 15, mwaka huu. Habari za tamasha hilo niliziandika hapa . Picha zote hizi nilizipiga kwa muda wa dakika mbili hivi, nikiwa nimesimama sehemu moja. Niliangalia jinsi watu walivyokuwa wanavichangamkia vitabu. Nilikumbuka ule usemi kuwa ukiwa na siri, iweke kitabuni. Hapo watu makini na wasio makini watajipambanua wenyewe. Kwa uzoefu wangu, kama ninavyosema tena na tena katika blogu na sehemu zingine, wa-Marekani ni kati ya hao watu makini. Ukiweka siri kitabuni, wataiona.

Sehemu za Kupumzikia, Mbamba Bay

Image
Mbamba Bay ni mji mdogo, kando kando ya Ziwa Nyasa, upande wa Tanzania. Ingawa umaarufu wa mji huu tangu zamani ni bandari, hapo ni mahali pazuri kwa mapumziko. Picha ninazoleta hapa nilipiga mwanzoni mwa Agosti, mwaka huu. Unaweza kusogea hapo ufukweni, ukawa unapunga upepo na kuangalia shughuli za wavuvi, wauzaji wa samaki, akina mama wakifua nguo, na watoto wakicheza majini. Kama unajua kuogelea, mahali hapo utafafurahia. Ukija siku ambapo meli inakuja, utajionea ujio wa meli na kuondoka kwake. Kama unapenda kukaa kwenye mwinuko, uangalie mji na Ziwa kwa chini yako, hoteli ya masista panafaa. Habari zake niliandika hapa . Ukipata chumba kinachoangalia upande wa Ziwa, huko nyuma ya hoteli, utafaidi mandhari ya Ziwa na sehemu kadhaa za Mbamba Bay. Ukitoka nje ukaingia bustanini, utapanda mawe na kuliona Ziwa vizuri sana. Hapo kwenye paa la blue ni baa ya Four Ways, ambayo picha zake niliwahi kuziweka hapa . Mwaka huu, nilipokuwa Mbamba Bay sikupata fursa ya kuingia ndani.

Ziara ya Uyole Kufuatilia Chuo Kikuu Kipya

Image
Mwaka huu, nilipokuwa Tanzania na wanafunzi katika programu ya LCCT , tulipata fursa ya kutembelea Uyole, mkoani Mbeya. Hiyo ilikuwa ni tarehe 19 Agosti. Hapo tulienda kuangalia mipango ya uanzishwaji wa Chuo Kikuu ambao ni mradi wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania. Kabla ya yote, napenda kuwashukuru wachungaji Dr. Mwalilino na Dr. Stephen Kimondo kwa kuandaa mawasiliano yaliyotuwezesha kufanya ziara hii. Mwenyeji wetu alikuwa Mchungaji Dr. Gwamaka Mwankenja, ambaye ndiye mratibu wa mpango huu wa kuanzisha chuo kikuu. Alitukaribisha vizuri na tuliongea kirefu. Alituelezea mpango mzima na changamoto zake, akatutembeza maeneo ya chuo. Kama mwanataaluma na mwalimu, nafuatilia sana hali na maendeleo ya elimu Tanzania, sio tu kwa kusikia au kusoma taarifa, bali kwa kutembelea shule na vyuo kila ninapokuwa nchini. Napenda kufuatilia vyuo vikuu vipya. Kwa mfano, nilishazuru Chuo Kikuu cha Sebastian Kolowa kilichoko Lushoto. Niliangalia ukarabati wa majengo ya shule ya zama

JK na Pinda Wakiwapagawisha Wadau

Image
Kati ya kali zote nilizoziona mwaka huu, hii ya JK na Pinda ni kiboko. Imenivunja mbavu kabisa. Wako mzigoni kikweli kweli, wala si utani. Halafu nikizingatia kuwa wote wawili ni watani wangu, naishiwa nguvu kabisa. Niliiona hapa .

Tamasha la Vitabu, Minneapolis

Image
Leo, mjini Minneapolis lilifanyika tamasha la vitabu, ambalo hufanyika kila mwaka, mwezi Oktoba. Tamasha hili huandaliwa na jarida la Rain Taxi . Ingawa kila mwaka, kwa miaka kadhaa sasa, nimeshiriki tamasha hili, kwa maana ya kupeleka vitabu vyangu, mwaka huu nilighilibika kidogo. Nilidhani nimefanya mpango wa kulipia meza, halafu nikaenda Tanzania. Niliporudi kutoka Tanzania, nikagundua kuwa hapakuwa na meza iliyobaki. Mwakani, Insh'Allah, nitakuwa makini zaidi. Kutokana na kughafirika huko, vitabu vyangu havikuwepo mwaka huu. Hata hivi, nilifunga safari, maili 45, kwenda kuangalia tamasha hili. Pamoja hali ya uchumi wa Marekani kuwa mbaya miaka hii, na watu wengi kukosa ajira au kuishi katika wasi wasi mkubwa kuhusu hali yao ya uchumi kwa siku za usoni, inashangaza jinsi tamasha la vitabu linavyowavutia. Wanafahamu umuhimu wa vitabu kiasi kwamba wako tayari kusamehe mengi mengine ili hela walizo nazo waje kuzitumia hapa. Nilifurahi kumwona huyu ma

Ni Msimu Mwingine kwa Wanafiki Kumkumbuka Nyerere Kinafiki!

Image
Tafakuri Jadidi Chanzo Raia Mwema Ni msimu mwingine kwa wanafiki kumkumbuka Nyerere kinafiki! Johnson Mbwambo 12 Oct 2011 KESHOKUTWA, Ijumaa, Oktoba 14, Taifa litatimiza miaka 12 kamili tangu kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, kilichotokea kule London, Uingereza katika hospitali ya Mtakatifu Thomas. Kama ambavyo imekuwa kwa miaka 11 iliyopita, Watanzania wataitumia pia keshokutwa kumkumbuka mpendwa wao huyo; huku wakitafakari, kama Taifa, zile “t” tatu maarufu : Tulikotoka, tulipo na tunakokwenda. Na kama ilivyokuwa kwa miaka 11 iliyopita, Taifa litaiadhimisha siku hiyo ya Ijumaa, Oktoba 14, kwa makongamano, semina na matamasha yenye mahusiano na maisha ya Baba wa Taifa. Kama ilivyokuwa kwa miaka 11 iliyopita, maadhimisho hayo ya kumbukumbu ya Nyerere yatapambwa na kauli nzito kuhusu mchango wake katika kujenga Taifa letu, mawazo yake na visheni yake. Wengi wataonyesha kwa dhati hisia zao za mapenzi waliyokuwanayo kwa mtu huyo ambaye, kwa jinsi alivyoipenda Tanzania, mim

Maktaba ya Mkoa, Ruvuma

Image
Nilipiga picha hii ya maktaba ya Mkoa, Ruvuma, tarehe 30 Julai mwaka huu. Niliwahi kuingia katika maktaba hii, ambayo iko mjini Songea, miaka kadhaa iliyopita, lakini safari hii sikupata muda. Nilizunguka maeneo mengine, kama vile Makumbusho ya Maji Maji, ambayo habari zake nategemea kuziandika baadaye. Napenda kuandika habari za maktaba za Tanzania. Nimeshaandika kuhusu maktaba ya Lushoto , Kilimanjaro , na Iringa . Nitaendelea kufanya hivyo.

Kitabu Kinapopigwa Marufuku

Image
Tutafakari suala tata la kupiga marufuku vitabu. Sijui kama wewe mdau unaafiki suala la kitabu kupigwa marufuku. Mimi huwa nakerwa. Kwa kawaida, kitabu kikipigwa marufuku, huwa nakitafuta ili nikisome. Nimeelezea mtazamo wangu kuhusu suala hili kinaganaga katika kitabu cha CHANGAMOTO . Hapa naleta mifano miwili ya vitabu vilivyopigwa marufuku Tanzania. Hapa kushoto ni kitabu cha Hamza Njozi kuhusu mauaji ya Mwembechai . Wako ambao waliona ni muhimu kitabu hiki kupigwa marufuku. Lakini mimi nilikitetea kwa kila namna, hata Njozi mwenyewe amenishukuru katika kitabu chake kilichofuata. Kitabu kingine ni Satanic Verses , cha Salman Rushdie. Wako ambao waliona ni muhimu kitabu hiki kupigwa marufuku. Ayatollah Khomeini wa Iran alitangaza fatwa juu ya Salman Rushdie, kwamba ni ruksa kumwua popote. Tangu mwanzo, watalaam wa dini ya ki-Islam sehemu mbali mbali za dunia walipishana mawazo kuhusu jambo hilo. Wako ambao waliafiki fatwa na wengine walipinga. Chuo Kikuu maarufu cha ki

Mkutano wa wa-Afrika na wa-Marekani Weusi Umefana

Image
Mkutano wa leo wa wa-Afrika na wa-Marekani Weusi umefana mjini Minneapolis. Walihudhuria wa-Afrika kutoka nchi mbali mbali kama vile Kongo, Nigeria, Kameroon, Somalia, Liberia, Ghana na Togo. Wa-Marekani Weusi walikuwa wengi, na nilipata fursa ya kufahamiana pia na dada mmoja kutoka Guyana. Nilifurahi kumweleza jinsi wa-Tanzania tunavyomkumbuka Profesa Walter Rodney. Nilimweleza nilivyomfahamu Profesa Rodney, kuanzia niliposoma Mkwawa High School, 1971-72 hadi Chuo Kikuu Dar. Hapa kushoto ni kiongozi mmojawapo wa Pan African Council, ambayo ndio iliandaa mkutano huu. Anatoka Togo. Katika hotuba yake, aliawasomea wasikilizaji taarifa niliyoandika kuhusu mkutano wa kwanza wa jumuia hii. Nafurahi kwamba tangu mwanzo, viongozi wa jumuia hii wanaitumia taarifa yangu kama kumbukumbu ya mkutano ule. Isome hapa . Niliguswa pale dada huyu aliponiambia baadaye kuwa anaziheshimu sana kazi zangu. Nafahamu anavyo vitabu vyangu. Alivinunua siku zilizopita. Katika picha hii hapa kush