Thursday, October 29, 2015

Shairi la "Kimbunga" (Haji Gora Haji)

Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasihi. Tofauti na inavyoeleweka katika jamii, kutafsiri ni suala pana kuliko kuwasilisha ujumbe kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine, bali ni kutunga upya kazi ya fasihi inayotafsiriwa. Hili suala linajadiliwa sana na wataalam wa lugha, fasihi, na falsafa.

Pamoja na matatizo yote, ninapenda kuchemsha akili yangu kwa kutafsiri kazi za fasihi. Kwa mfano, nimetafsiri hadithi za ki-Matengo, na shairi la Mama Mkatoliki.

Hapa naleta shairi la Haji Gora Haji, mshairi maarufu wa Zanzibar, ambaye niliwahi kukutana naye. Shairi hilo ni "Kimbunga" ambalo limo katika kitabu chake kiitwacho Kimbunga. Jisomee shairi hilo na ujionee nilivyopambana na lugha katika kutafsiri. Ni mapambano, na kuna wakati unajikuta umepigwa butwaa au mwereka.
-----------------------------------------------------------------------------------------------------------------

                               Kimbunga

1.     Kimbunga mji wa Siyu, kilichowahi kufika
       Si kwa yule wala huyu, ilikuwa patashika
       Kimeing'owa mibuyu, minazi kunusurika
       Nyoyo zilifadhaika.

2.     Yalizuka majabali, yakabirukabiruka
       Zikadidimia meli, ngarawa zikaokoka
       Kimbunga hicho kikali, mavumbi hayakuruka
       Nyoyo zilifadhaika.

3.     Nyumba kubwa za ghorofa, siku hiyo zimeruka
       Zikenenda kwa masafa, kufikia kwa kufika
       Vibanda vyao malofa, vyote vikasalimika
       Nyoyo zikafadhaika.

4.     Chura kakausha mto, maji yakamalizika
       Pwani kulikuwa moto, mawimbi yaliyowaka
       Usufi nusu kipeto, rikwama limevunjika
       Nyoyo zikafadhaika.

5.     Kuna kikongwe ajuza, viumbe kimewateka
       Hicho kinamiujiza, kila rangi hugeuka
       Wataokiendekeza, hilaki zitawafika
       Nyoyo zikafadhaika.


                                 A Hurricane

1.     A hurricane once arrived in Siyu town
       Sparing neither that one nor this one, it was sheer mayhem
       It uprooted babobab trees, the coconut trees surviving
       Hearts went panicking.

2.     Big rocks turned up, tumbling over and over
       Ships were sinking, while mere boats survived
       Fearsome as the hurricane was, it raised no dust
       Hearts went panicking

3.     Great storied houses were blown away that day
       They flew quite a distance, landing wherever they landed
       The huts of the lowly, all survived intact
       And hearts went panicking

4.     The frog drained the river, the water all dried up
       On the shore was conflagration, of the waves flaming
       Half a container of kapok, broke the coolie's cart
       And hearts went panicking

5.     A wizened hag there was, who held beings captive
       She is given to magical powers, changing hues at will
       Those who let her be, perdition will be their lot
       And hearts will go panicking.

7 comments:

Pascal Bacuez said...

Asante mzee Mbele kwa kutukumbusha kwamba Tanzania pamejaaliwa malenga wazuri kama Haji Gora. Lakini sidhani kwamba Kimbunga ndilo shairi litakalofaa endapo tunataka kuelewa kinachoendelea siki hizi huko kwenu, kuhusu sijui Magufuli, sijui Lowasa… Uchaguzi wa kawaida sio mapinduzi yale ya zamani ! Nakumbuka nilipokwenda Tumbatu huku nikifuatana na Haji Gora — kwa kuwa ndiko alikozaliwa — nami nilitaka kuchambua mashairi yake kwa « kupiga mbizi » kabisa ndani ya « ghibu » zake, na wakati huo nilijua fika kwamba kitanda usichokilalia… Basi Haji alinifahamisha vizuri jinsi alivyoanza kutunga mashairi kwa kuunda chama cha vijana kilichoitwa « Zigezaga » nacho kilikuwa na azimio zuri sana la kuponda vijana wengine waliokuwa wanachama wa kikundi kingine kiitwacho « Ngwamba » nao walikuwa na tabia mbaya ya kuchunguza mambo ya wenzake badala ya kujijali mwenyewe. Nadhani kwamba mtindo huo wa kuvutana na kunyanyuana vizuri kupitia ngoma hizo za kishairi na malumbano ya nyimbo umekufa kabisa. Ni hasara kubwa sana na jambo la kusikitisha pia kuona kwamba demokrasia hiyo ya kikale imerukwa na domokasia ya kihola holela ya kisasa.

Mbele said...

Ndugu Pascal Bacuez, Shukrani kwa ujumbe wako. Nilipoamua kulitafsiri shairi hili, sikuwa nawazia siasa za Tanzania. Nilikuwa narejea tu katika shughuli hii ya kutafsiri tungo, ambayo nimekuwa nikifanya kwa miaka mingi. Shairi hili limo katika kitabu ambacho kilichapishwa mwaka 1994. Lilitungwa miaka mingi kabla ya haya matukio ya kisiasa ya wakati huu.

Shairi hili ni mwendelezo wa jadi ya tungo za ki-Swahili, jadi ambayo imekuwepo kwa karne nyingi. Haji Gora Haji anataja Siyu, mji wa kale wa u-Swahilini, mwambao wa Kenya, sambamba na miji kama Pate na Lamu. Huko ndiko chimbuko la ki-Swahili, na tungo zinazosifika tangu zamani sana.

Shairi la "Kimbunga" ni fumbo. Hakuna mtu anayeweza kutueleza maana yake, ikawa ndio kikomo cha ukweli. Kama kazi zote za fasihi, shairi hili linaelezeka kwa namna mbali mbali, likaleta maana tofauti kwa kila mtu, kila jamii. Kwa mfano, kwa watu wa Pemba, Tumbatu, na Mafia, ambao wanakumbana na vimbunga, na wanaijua minazi na ngarawa, shairi hili linaleta hisia fulani.

Baada ya kutafsiriwa kwa ki-Ingereza, shairi litasomwa hata na watu wa visiwa vya mbali kama Fiji na Jamaica, ambao wanaijua bahari, ngarawa, minazi, na vimbunga, na watalielewa kwa hisia zinazotokana na mazingira yao hayo.

Lakini hapo yanakuja masuala tata. Kwa mfano, hao wanaosoma tafsiri yangu wanasoma shairi la Haji Gora Haji, au wanasoma nini? Je, wale ambao hawaijui minazi au mibuyu, wala hawajawahi kusafiri kwa ngarawa na kukumbana na kimbunga, wanaelewa nini au kwa namna gani?

Nilivyotafsiri shairi hili jana, nilipangia kuliweka shairi na tafsiri yangu pia katika blogu yangu ya ki-Ingereza, pamoja na dondoo chache za uchambuzi. Insh'Allah, nitafanya hivyo leo au kesho.

Pascal Bacuez said...

Asante ndugu Mbele kwa ufafanuzi wako mzuri sana ambao kwa kweli unatuelezea pia msimamo wako kuhusu swala hilo gumu la kuchambua mashairi. La kushangaza kwangu ni kwamba umeweka mbele swala la hisia, kitu ambacho ni kinyume kabisa na mkabala ninaofuata wakati ninapofundisha tanzu hii ya fasihi darasani. Shairi lolote duniani kwanza ni umbo kwa sababu limeundwa kwa kutumia mbinu kadhaa (vina, beti, n.k.) ; pili ni maana : kama ulivyosema katika shairi la kimbunga Haji Gora anataja vitu halisi ambavyo havipo katika kanda nyingine za dunia. Hakuna ngarawa Kilimanjaro. Na ngarawa si mashua, wala jahazi, wala dingi. Na ukijua kwamba mashua ina gadi wakati ngarawa ina mirengu, hapo kweli mtu atajisogeza mbele zaidi katika kuelewa maana ya shairi hilo. Na hali kadhalika, kimbunga si tofani, wala chanchera, wala mboji, wala umande, n.k. Nadhani kwamba kutoa maelezo hayo katika darasa ni wajibu wetu sisi walimu ili kusudi wanafunzi wetu wasije wakasadifu kuhisi hisia fulani kwa kubahatisha tu. Tatu shairi (la aina hii) ni nia au kusudio. Na hapo mwanafunzi akiwa amebahatika kusomeshwa vizuri kuhusu wasifu wa Haji Gora, nadhani kwamba itakuwa si vigumu kuelewa kilichokusudiwa katika shairi hilo hata kama hana « utamaduni » wa mswahili. Aidha kusema ni fumbo si kusema kwamba shairi halina maana au kwamba kila mtu atajenga maana yake kufuatana na hisia alizo nazo. Relativism hii ni msimamo ulioenea sana katika dunia yetu ya siku hizi, jambo ambalo linaua fasihi. Haji Gora mwenyewe alikusudia maana fulani alipoandika Kimbunga na sababu yake tunaijua, mwenyewe hakupenda (au hapendi ?) mashairi ya mipasho. Fumbo lina maana na kusema (kwa mfano) kwamba Kimbunga ni shairi linalonisaidia mimi mzungu kuelewa machafuko yanayokumba Ulaya siku hizi ni kama kutoa maana mpya ambayo msanii mwenyewe hakunuia wakati alipotunga shairi lake. Lakini maana hiyo itaingia katika ikisiri ya shairi hilo, jambo ambalo linazidi kupanua uelewa wake (na umbuji wake) kwa « kulitoa » katika jamii yake asiliya na kufanya lifahamike katika jamii nyingine. Na tafsiri hapo ni mbinu inayofaa sana katika kujenga maelewano baina ya watu wasiokuwa na lugha moja kwa kuwa inachangia tujenge ubinadamu wetu. Hongera sana kwa tafsiri yako !

Mbele said...

Ndugu Pascal Bacuez, Ni sawa kabisa kuwa na mitazamo tofauti katika kuchambua kazi ya fasihi. Ni hali halisi isiyopingika. Hata nadharia za fasihi ni nyingi, na zinatofautiana, lakini kila nadharia inatoa mchango wake katika juhudi zetu za kuufahamu uwanja huu mpana, wenye sura mbali mbali, unaobadilika daima, na wa kusisimua, unaoitwa fasihi.

Binafsi, navutiwa na kila nadharia, na ninapofundisha najaribu kuwaeleza wanafunzi nadharia mbali mbali na tofauti zilizomo. Wanajua kwamba tunapojadili kazi ya fasihi, tutakuwa na fursa ya kuiangalia kwa mitazamo mbali mbali.

Kwa mtazamo wangu, kila nadharia ina ubora na umuhimu, lakini haitoshelezi kwa kila hali, kuijadili kazi ya fasihi. Tunahitaji mitazamo mingi iwezekanavyo. Hata hili wazo la kuangalia mwandishi alikusudia nini limeleta mgogoro. Kuna watu wanaosema kwamba kazi ya fasihi inajieleza yenyewe, na hatuhitaji kumwona mwandishi kuwa ndiye mwenye mamlaka ya mwisho ya kusema kazi aliyoandika ieleweke vipi.

Mwandishi akishaandika kazi yake ya fasihi na kuiweka Mbele yetu wasomaji, yeye anakuwa ni mmoja tu wa wasomaji, na huenda wasomaji tukamweleza mambo kuhusu kazi yake ambayo yeye hakuwazia wakati anaandika. Kwa mfano, shairi hili la "Kimbunga" mimi kama mwanafasihi linanikumbusha shairi la W.B. Yeats liitwalo "The Second Coming," kwa kiasi fulani, ingawa Haji Gora Haji hakukusudia kuwa shairi lake lionwe namna hiyo.

Tatizo jingine la nadharia ya kuzingatia makusudio ya mwandishi ni kuwa waandishi wengi hatuwezi kuwasikia wakitueleza walikusudia nini. Akina Cervantes, Shakespeare, Balzac, Tolstoy, Shaaban Robert, na kadhalika walishakufa. Tumebaki na tungo zao, na tungo zinajieleza zenyewe.


Anonymous said...

http://mandelapallangyo.com/prof-joseph-mbele-alivyotafasiri-shairi-la-nyangau/

Mbele said...

Ndugu Mandela Pallangyo,

Nimefurahi kuona umeweka shairi la "Nyang'au" la Haji Gora Haji, pamoja na tafsiri yangu, katika blogu yako. Tunao watunzi maarufu katika ki-Swahili, kwa karne yapata tatu, ambao tunapaswa kutafiti maisha yao na tungo zao, tuzisome tungo zao kwa makini, tuzichambue kwa makini, na pia tuzitafsiri kwa lugha mbali mbali, ili zifahamike ulimwenguni kama mchango wetu katika ustaarabu wa binadamu.

Katika mijadala miongoni mwa wanataaluma kuhusu suala la kutafsiri kazi za fasihi za ki-Afrika, hawazungumzii tu kutafsiri kutoka lugha za ki-Afrika kwenda lugha za ki-zungu, bali pia kutoka lugha za kiafrika kwenda katika lugha zingine za ki-Afrika.

Hebu fikiria, kwa mfano, utamu utakavyokolea iwapo shairi kama hili la "Nyang'au" likitafsiriwa katika ki-Zulu, ki-Hausa, au ki-Wolof. Hebu fikiria iwapo tungo za ki-Hausa, ki-Zulu, au ki-Shona, zikitafsiriwa katika ki-Swahili.

Unknown said...

I need poems

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...