Posts

Showing posts from May, 2016

"The Snows of Kilimanjaro" Yatimiza Miaka 80

Image
Mwaka huu 2016, The Snows of Kilimanjaro , hadithi maarufu ya Ernest Hemingway, inatimiza miaka 80 tangu ichapishwe kwa mara ya kwanza. Ilichapishwa katika jarida la Esquire, toleo la Agosti, 1936. Sidhani kama kuna hadithi fupi katika fasihi ya ki-Ingereza inayofahamika na ni maarufu kuzidi The Snows of Kilimanjaro . Hemingway aliandika utangulizi mfupi wa hadithi yake, ambao unaamsha hisia zinazoendelezwa katika hadithi nzima, ikiwemo hisia ya masuali yasiyojibika: "Kilimanjaro is a snow covered mountain 19,710 feet high, and it is said to be the biggest mountain in Africa. Its western summit is called the Masai "Ngáje Ngái," the House of God. Close to the western summit there is the dried and frozen carcass of a leopard. No one has explained what the leopard was seeking at that altitude."  The Snows of Kilimanjaro inamhusu mtu aitwaye Harry, mzungu. Tunamwona akiwa mgonjwa kutokana na kidonda alichopata baada ya kuchomwa na mwiba porini. Kilichosababisha

Uandishi wa ki-Ingereza Bora

Ninafundisha katika idara ya ki-Ingereza katika Chuo cha St. Olaf, hapa Marekani. Moja ya masomo ninayofundisha ni uandishi bora wa ki-Ingereza, yaani ki-Ingereza sanifu. Ninawajengea wanafunzi nidhamu ya kuboresha uandishi wao wa insha. Wakishaandika insha, ninawashinikiza waiboreshe, kwa kuangalia na kutafakari kila neno, na kila sentensi, mara nyingi iwezekanavyo. Hii ni kazi ngumu kwa yeyote, wakiwemo wanafunzi wangu, pamoja na kwamba ki-Ingereza ni lugha mama yao. Moja ya kazi ninazowapa ni kuiboresha insha yangu iitwayo "Do You Have an Accent?" ambayo niliandika miaka iliyopita, ikachapishwa hapa Minnesota. Nilikuwa nimeandika mswada wake, nikaurekebisha tena na tena, hadi kufikia kiwango cha kuweza kuchapishwa. Lakini, hata baada ya kuchapishwa, niliendelea kuiangalia makala hii kwa jicho kali, tena na tena. Katika jitihada hii, niligundua vipengele visivyopungua nane ambavyo vinaweza kurekebishwa na insha ikawa bora zaidi. Ninapowapa wanafunzi wangu zoezi hili,

Hatimaye, Ninatafsiri Shairi la "Kibwangai"

Hivi karibuni, nililalamika katika blogu hii kuwa nilikuwa nikijaribu kutafsiri shairi la "Kibwangai" la Haji Gora Haji, lakini nilikwama. Shairi hili lililoandikwa kwa ki-Swahili linaeleweka vizuri kabisa kwangu. Lugha niliyotaka kulitafsiri shairi, yaani ki-Ingereza, ninaifahamu vizuri sana. Sasa tatizo lilikuwa nini? Hili ni suala moja la msingi katika shughuli na taaluma ya tafsiri. Tafsiri sio suala la ufahamu wa lugha tu, bali ufahamu wa mambo mengine pia, ikiwemo lugha ya kifasihi. Unaweza kuwa unakijua ki-Ingereza, kwa mfano, lakini hujui ki-ingereza cha fasihi. Ukitafsiri shairi kama Kibwangai, utaishia kuleta kitu ambacho hakina ladha ya sanaa. Hiyo dhana yenyewe ya ladha ya sanaa inahitaji ufafanuzi. Lugha, iwe ni ki-Swahili, ki-Ingereza, au lugha nyingine, ina matumizi ya kawaida na matumizi ya kisanaa. Kiswahili cha kishairi kinatofautiana na ki-Swahili cha kawaida. Vivyo hivyo ki-Ingereza. Kwa hivi, mtu unapotafsiri shairi kutoka lugha moja kwenda lugha n

Leo Nimemwandikia Mzee Patrick Hemingway

Image
Leo nimemwandikia barua pepe Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee aliye hai wa mwandishi maarufu Ernest Hemingway. Nilipiga naye picha inayoonekana hapa kushoto tarehe 27 Aprili, 2013, nyumbani pake mjini Craig, katika jimbo la Montana. Nilifahamu habari zake kwa miaka mingi kabla ya kufahamiana naye na halafu tukakutana. Ni mzee mwenye maongezi ya kusisimua kuhusu baba yake Ernest Hemingway na waandishi wengine wa wakati wake. Pia ana kumbukumbu nyingi za Tanganyika, na kisha Tanzania, ambako aliishi kwa miaka yapata 25 kabla ya uhuru na baada ya uhuru, akiendesha kampuni ya utalii, na hatimaye akiwa mkufunzi katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori cha Mwika. Tangu tulipoanza kufahamiana, ameguswa na ari yangu ya kutafiti maandishi, falsafa, na maisha ya Ernest Hemingway, na amevutiwa na msimamo wangu kuwa Ernest Hemingway ni mwandishi aliyetuenzi sana sisi watu wa Afrika Mashariki, na tunapaswa kujielimisha kuhusu mchango wake, na kisha kuutumia katika kujitangaza kama alivyot

Nimenunua "Good Prose," Kitabu Kuhusu Uandishi

Image
Siku chache zilizopita, katika duka la vitabu la hapa chuoni St. Olaf, nilikiona kitabu kiitwacho Good Prose: The Art of Nonfiction . Jina hilo lilinivutia, nikapata duku duku ya kukiangalia. Nilivyoona kuwa mwandishi mojawapo, Tracy Kidder alikuwa amepata tuzo ya Pulitzer, nilivutiwa kabisa. Hii ni tuzo ya uandishi yenye hadhi kuliko zote zinazotolewa hapa Marekani. Nilivyochungulia kurasa zake, niliona kina mawaidha mazuri kuhusu uandishi bora. Si uandishi wa kazi za fasihi, bali uandishi kama wa insha. Huu ndio uandishi wangu, na ndio uandishi ninaofundisha. Nilivutiwa pia nilipoona waandishi maarufu wamenukuliwa katika kitabu hiki, kama vile Norman Mailer,  Ernest Hemingway, Vladimir Nabokov, na William Strunk, Jr. Kwa bahati mbaya sikuwa na hela, nikaondoka bila kukinunua, kwa shingo upande. Leo nilikwenda tena dukani, nikakuta kitabu bado kipo. Nilikinunua hapo hapo. Pamoja na kwamba nina uzoefu wa miaka mingi wa kufundisha uandishi bora wa ki-Ingereza, na pamoja kwamba n

Muhula Unaisha; Umebaki Utafiti

Jana tumemaliza muhula wa masomo hapa chuoni St. Olaf. Nilikuwa ninafundisha "Folklore," Muslim Women Writers, na "First Year Writing." Kwa utaratibu wa chuo hiki, masomo matatu kwa muhula ndio kiwango cha juu kabisa. Hatufundishi zaidi ya masomo matatu. Kwa hivi, nilitegemea ningekuwa nimechoka, lakini sisikii uchovu. Alhamdulillah. Kwa wiki nzima inayokuja, tutakuwa na mitihani. Baada ya hapo tutaanza likizo ndefu ya miezi mitatu na kidogo. Inaitwa likizo, lakini maprofesa tunaona ni wakati muafaka wa kufanya shughuli za kitaaluma kama utafiti na uandishi. Nami nimeamua kwenda Boston kwa siku chache kufanya utafiti juu ya Ernest Hemingway katika maktaba ya John F. Kennedy. Humo kuna hifadhi kubwa kuliko zote duniani ya vitabu, miswada, picha na  kumbukumbu zingine zinazomhusu Hemingway. Ingawa nimefika Boston mara kadhaa, sijawahi kwenda katika maktaba hiyo maarufu. Nina bahati kuwa ninafahamiana na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee wa Ernest Hemingway

Dini ya Kweli

Leo ni Jumapili, nami nimerejea kutoka kanisani kusali. Nilipokuwa njiani, nilijikuta nikiwazia suala la dini, nikajiuliza kuhusu dhana ya dini ya kweli. Nini maana ya dini ya kweli? Kuna dini ya kweli? Kama ipo, ni ipi? Hili ni suala tata, nami napenda kuthibitisha angalau kidogo utata huo. Ninategemea kuwa wasomaji wangu watachangia mawazo. Kwa mtazamo mmoja, tunaweza kusema kuwa kila dini ni dini ya kweli, kwa maana kwamba iko. Ni sawa na kitu chochote kinginecho kilichopo. Kila kilichopo ni kitu cha kweli, iwe ni chakula, bangi, au kifo. Vyote hivyo ni vitu vya kweli, kwa maana kwamba vipo. Na dini ni hivyo hivyo. Dini ziko. Kila dini ni dini ya kweli. Kwa mtazamo mwingine, watu wanapoongelea dini ya kweli, wanamaanisha dini inayokubalika kwa Mungu. Wanamaanisha dini itakayomfikisha binadamu kwenye uokovu. Hapo pana utata mkubwa, kwani waumini wa dini mbali mbali wana tabia ya mwamba ngoma, ambaye huvutia ngozi upande wake. Matokeo yake katika historia ya binadamu yamekuwa maba

Nimepita Tena Katika Duka la Half Price Books

Image
Leo alasiri nilikwenda eneo la Minneapolis, mwendo wa maili 40, kwa shughuli binafsi. Ilikuwa siku nzuri, ya jua la wastani na hali ya hewa ya kupendeza. Wakati wa kurudi, nilipita mjini Apple Valley, nikaamua kupitia katika duka la Half Price Books. Nilitaka hasa kuangalia kama kuna chochote juu ya mwandishi Ernest Hemingway. Kufuatilia vitabu juu ya Hemingway imeshakuwa mazoea kwangu, wala siwezi kujizuia. Ninajua kuwa sitakikuta kitabu kipya kilichoandikwa na Hemingway. Inafahamika kwamba miswada yote ya vitabu vya Ernest Hemingway imeshachapishwa. Kinachotokea ni kuwa yanachapishwa matoleo mapya ya vitabu vyake, kama vile matoleo yanayohaririwa na mjukuu wake, Sean Hemingway, ambavyo Mzee Patrick Hemingway, mtoto wa Ernest Hemingway, anaviandikia utangulizi. Maandishi mapya kabisa ya Ernest Hemingway yanayochapishwa ni barua zake. Kuna mradi wa kukusanya barua zote za Ernest Hemingway tangu utotoni mwake. Wahariri wa mradi huu ni maprofesa Sandra Spanier na Robert W. Trogdon,

Nimepata Qur'an Mpya

Image
Nimekuwa na kawaida ya kuandika katika blogu hii taarifa za vitabu ninavyonunua, au vitabu ninavyosoma, ingawa siandiki juu ya vyote. Kwa siku nyingi sijafanya hivyo, lakini leo nimeamua kuandika kuhusu Qur'an mpya niliyoipata hivi karibuni, ambayo ni tafsiri ya ki-Ingereza ya Maulana Wahiduddin Khan na Farida Khanam ambaye ni binti yake. Ninayo nakala nyingine ya Qur'an tangu mwaka 1982, ambayo ni tafsiri ya Abdullah Yusuf Ali. Hii ni kubwa kwa kuwa ina maelezo mengi. Hii mpya niliipata tarehe 28 Aprili, mwaka huu, kutoka kwa Dr. Nadia Mohamed, mzaliwa wa Misri. Anaonekana amesimama kulia pichani. Nimefahamiana naye zaidi ya mwaka, tangu tuliposafiri kwenda kwenye semina chuoni Leech Lake, ambapo tulipiga hii picha, pamoja na profesa mwingine wa chuo kile. Dr. Nadia Mohamed ni profesa mwenye shahada ya uzamili katika sheria za ki-Islam na shahada ya uzamifu katika elimu. Nilikuwa nimemwalika kuja kutoa mhadhara katika darasa langu la Muslim Women Writers, na baada

Tamasha la Kimataifa, Rochester, Aprili 30

Image
Tarehe 30 April, nilihudhuria tamasha la kimataifa mjini Rochester ambalo nililizungumzia katika blogu hii. Nilipeleka vitabu vyangu, kwani ninashiriki matamasha kama mwalimu na mwandishi. Nilichukua pia bendera ya Tanzania. Meza yangu ilikuwa inavyoonekana pichani hapa kushoto, picha ambayo ilipigwa na mama mmoja kutoka China, mmoja wa watu walioniambia kuwa walipendezwa na mwonekano wa meza yangu, wakapiga picha. Kwa kuiona bendera yangu, watu kadhaa wa Kenya na Uganda walikuja kuongea nami. Kwa utani na moyo wa ujirani, Wa-Kenya walitumia jina la Bongo muda wote. Pichani hapa kushoto ni jamaa wawili kutoka Guatemala. Niliwapa makala yangu fupi, "Chickens in the Bus," tukaongea kuhusu tamaduni zetu, tukaona jinsi zinavyofanana. Ni kawaida kuwaona watu  Guatemala wakisafiri ndani ya basi wakiwa wamebeba kuku au hata nguruwe. Kwa mujibu wa mama mmoja Mmarekani aliyefika mezani pangu na kuiona makala hiyo, Mexico nako unaweza kuwaona watu ndani ya basi wakiwa na kuku a