Posts

Showing posts from February, 2016

Nimezuru Nyumba ya Hemingway, Oak Park

Image
Leo nilizuru nyumba ya Hemingway, kitongoji cha Oak Park, karibu na Chicago. Kwa miaka kadhaa, nilikuwa nimewazia kufanya hivyo.  Nyumba hii ambayo ni namba 339 katika mtaa wa Oak Park Avenue, ndimo alimozaliwa Ernest Hemingway na kuishi hadi alipokuwa na miaka sita. Sasa ni nyumba ya hifadhi ya mambo mengi ya familia ya Hemingway. Nimejifunza mengi katika kutembelea nyumba hii.  Nilipoingia, nilijumuika na wageni wengine wanne, tukafanya ziara pamoja, tukiongozwa na dada aliyejitambulisha kwa jina la Michelle ambaye anaonekana pichani. Alitupitisha sehemu zote za nyumba hii, akatuelezea historia yake na habari za vitu vilivyomo. Alituelezea mambo muhimu yaliyomlea Ernest Hemingway katika nyumba hii. Mfano ni namna mama yake alivyotaka kila mtoto na mtu mwingine katika nyumba hii awe na ujuzi wa muziki. Kabla ya ziara hii, nilijua kuwa mama yake Ernest Hemingway alitaka Ernest ajifunze muziki, lakini sikujua kuwa alitaka hivyo kwa kila mtoto na wengine pia. Ziara hii pia imenifung

Jumuia ya Vyuo (ACM) Yakihitaji Kitabu

Image
Leo nimeshinda hapa mjini Chicago nikihudhuria mkutano wa bodi ya programu ya Tanzania ya ACM . ACM ni jumuia ya vyuo vikuu 14 vya hapa Marekani ambayo inaendesha programu za masomo na utafiti sehemu mbali mbali za dunia. Kwa upande wa Afrika, kuna programu ya Tanzania na programu ya Botswana. Mimi ni mjumbe katika bodi za programu hizi mbili. Mkutano kama wa leo tunafanya mara moja kwa mwaka kwa program ya Tanzania na vivyo hivyo kwa programu ya Botswana. Kila mwaka tunapeleka wanafunzi kwenye nchi hizi kwa muhula moja. Tunapokutana tunatathmini mwenendo wa masomo kwa mwaka husika. Tunapitia ripoti mbali mbali na kuzijadili, kubaini mapungufu na mafanikio na mapungufu, kutoa mapendekezo na kujiwekea malengo. Leo, pamoja na yote hayo, limetokea jambo ambalo sikutegemea. Profesa Paul Overvoorde, aliyeambatana na wanafunzi Tanzania muhula uliopita, alianza hima kunieleza kuwa alikuwa ametumia kitabu changu cha Africans and Americans Embracing Cultural Differences na kilimsaidia s

"So Long a Letter" Katika Kozi ya "Muslim Women Writers"

Image
Kozi yangu ya Muslim Women Writers inaendelea vizuri. Tulianzia India, na hadithi ya Sultana's Dream ya Rokeya Sakhawat Hossain. Baada ya hapo tunasoma So Long a Letter , utungo wa Mariama Ba wa Senegal, nchi mojawapo maarufu katika uwanja wa fasihi ya Afrika. Senegal imetoa watunzi kama Leopold Sedar Senghor, Cheikh Hamidou Kane, Birago Diop, na Sembene Ousmane, kwa upande wa wanaume, na kwa upande wa wanawake kuna watunzi kama Aminata Sow Fall na Mariama Ba. So Long a Letter ni utungo ulioandikwa kwa mtindo wa barua, ambayo mhusika mkuu anamwandikia mwanamke mwenzake, rafiki yake. Kwa hali hiyo, utungo huu unafuata jadi ambayo wanafasihi huiita "epistolary." Neno "epistolary" linatokana na neno la ki-Latini ambalo maana yake ni barua. Suala moja muhimu linaloongelewa ni la wake wenza. Ni suala lenye chimbuko lake katika Qur'an, Sura iv aya 3:      If ye fear that ye shall not Bes able to deal justly With the orphans, Marry women of your choic

"Tenzi Tatu za Kale:" Makala Inayosomwa Kuliko Zote

Image
Mara kwa mara, ninaangalia takwimu zinazohusu blogu yangu hii: idadi ya watembeleaji, makala wanazozitembelea, na nchi walimo. Kuanzia wiki kadhaa zilizopita, makala inayotembelewa kuliko zote ni "Tenzi Tatu za Kale." Idadi ya watembeleaji iliongezeka ghafla pale Ndugu Michuzi alipoiweka makala hii katika blogu yake. Ninajiuliza kwa nini makala hii inawavutia wasomaji namna hii. Je, hii ni ishara ya kupendwa kwa somo la fasihi ya ki-Swahili? Siamini kama ni hivyo, kwani ninaandika makala nyingi kuhusu fasihi, ambazo zinagusia tungo mbali mbali. Ingekuwa uwingi wa wasomaji unaonekana kwenye makala hizo pia, ningeamini kuwa kuna msisimko wa kupenda fasihi. Ninapata hisia kwamba labda uhusiano na mahitaji ya shuleni au vyuoni. Ninahisi kuwa labda wanaosoma makala ya "Tenzi Tatu za Kale" ni wanafunzi ambao wanatakiwa kusoma Utenzi wa Al Inkishafi , au Utenzi wa Mwana Kupona , au Utenzi wa Fumo Liyongo : moja, mbili, au zote tatu. Kama ni hivyo, si jambo la kuri

Tumeanza Kujadili "Sultana's Dream" na U-Islam

Image
Katika siku chache zilizopita, nimesoma Sultana's Dream , hadithi iliyotungwa na Rokeya Sakhawat Hossain aliyeishi 1880-1932 nchi ambayo leo ni Bangladesh. Sultana's Dream ni kianzio cha kozi yangu ya Muslim Women Writers. Nilikuwa nimesoma kuhusu hadithi hii mtandaoni, nikaamua kuijumlisha katika kozi yangu. Nimefurahi kuwa nilifanya uamuzi huo. Nimejionea jinsi mwandishi Rokeya Sakhawat Hussain alivyokuwa mwanaharakati aliyepigania ukombozi wa wanawake kutokana na jadi ya wao kufungiwa ndani na kubanwa kimaisha, jadi iliyojengeka katika imani kwamba ni wajibu wa u-Islam. Rokeya alikuwa mwanamama shujaa, ikizingatiwa wakati alioishi. Alibahatika kuwa mumewe alimwachia uhuru na kumsaidia katika uandishi na uhamasishaji wa wanawake. Alichapisha Sultana's Dream mwaka 1905. Ni  hadithi ya kubuniwa, ambayo inaelezea ndoto ya Sultana. Katika ndoto hiyo, Sultana anajikuta katika nchi ambayo inatawaliwa na wanawake, huku wanaume wakiwa ndani katika purdah. Utawala wa hao w

U-Islam ni Dini ya Amani?

Wiki hii, tumeanza muhula mpya wa masomo hapa chuoni St. Olaf. Kozi mojawapo ninayofundisha ni Muslim Women Writers, ambayo nimeshaiongelea katika blogu hii. Nimeshaanza kuwaelezea wanafunzi kuhusu u-Islam. Nimeongelea kuhusu Muhammad, Qur'an, hadith, na nguzo tano za u-Islam: shahadah, salah, zakah, sawm, na hajj. Nimefafanua maana ya kila nguzo. Nimeuelezea u-Islam kwa mtazamo wangu kama mtu ninayeziheshimu dini zote. Kozi yangu hii ni muhimu kwa wanafunzi hao, ambao wengi wao hata msikiti hawajawahi kuuona na hata adhan hawajawahi kuisikia. Ni muhimu katika mazingira ya sasa ya Marekani, ambapo kuna propaganda nyingi dhidi ya u-Islam na wa-Islam. Kwa mfano, siku chache zilizopita, hapa mjini petu, kuna mtu ameandika katika Northfiled News , akiushambulia u-Islam kwamba si dini ya amani. Kwangu ambaye ninatoka Tanzania, nchi ya watu wa dini mbali mbali, makala hii ambayo imezuka hapa ninapofundisha si ya  kuifumbia macho. Nitaipeleka darasani nikaijadili na kisha wanaf

Shairi Linaposomwa kwa Sauti

Image
Jana nilijirekodi katika video nikisoma kwa sauti shairi la W. B. Yeats liitwalo "The Second Coming." Niliweka video hiyo katika mtandao wa Facebook, katika You Tube, na katika blogu hii. Niliiweka katika You Tube baada ya kushindwa kuiweka katika blogu moja kwa moja, na katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo, nilisoma mtandaoni kuwa kwa kuanzia kuiweka You Tube kunaweza kutatua tatizo. Ndivyo ilivyokuwa. Kutokea You Tube, nilifanya "embedding" kwenda kwenye blogu. Napenda kwanza nikiri kuwa nimefurahishwa na jinsi usomaji wangu wa "The Second Coming" ulivyopokelewa na watu wa mataifa mbali mbali. Ni wazi kuwa wameguswa, nami nashukuru. Labda nitaandika zaidi kuhusu hilo. Lengo langu hapa ni kuongelea masuala ya kinadharia na kifalsafa juu ya usomaji wa shairi kwa sauti. Nilidokeza masuala haya katika  ujumbe wa jana. Kwanza, tutafakari dhana ya uandishi. Tuanzie na chimbuko lake, yaani utungaji. Utungaji wa shairi, au kazi yoyote ya sanaa, hufanyika

"The Second Coming:" Shairi la W. B. Yeats

Image
"The Second Coming," shairi la William Butler Yeats wa Ireland, ni kati ya mashairi maarufu kabisa katika ki-Ingereza. Yeats aliliandika shairi hili baada ya vita kuu ya kwanza ambayo ilisababisha vifo vya mamilioni ya watu na uharibifu mkubwa. Simanzi ilitanda ulimwenguni, na ilikuwa rahisi kukata tamaa kuhusu hatima ya binadamu na ulimwengu. Hisia hizi zinajitokeza kimafumbo katika "The Second Coming." Kinachoshangaza ni jinsi shairi hili lilivyoonekana kubashiri majanga yaliyoikumba dunia miaka iliyofuata. Adolf Hitler aliibuka na himaya yake ya ki-Nazi iliyosababisha mauaji ya mamilioni ya watu na kisha ikaja vita kuu ya pili. "The Second Coming" ni shairi ambalo wengi tulilisoma tulipokuwa sekondari, na wengi wetu tunakumbuka lilivyonukuliwa na Chinua Achebe mwanzoni mwa riwaya yake ya Things Fall Apart. Kati ya mambo mengi, riwaya hii nayo ilielezea mtafaruku uliotokea katika jamii ya asili ya ki-Afrika kufuatia kuingiliwa na wazungu. Kila mt

Ganesha: Mungu Maarufu

Image
Ganesha ni mmoja wa miungu wa dini ya Hindu. Dini hii ilianzia India, miaka zaidi ya elfu tatu iliyopita. Leo ina waumini yapata bilioni sehemu zote za dunia, kuanzia India na nchi za jirani, hadi Afrika Mashariki, visiwa vya Caribbean, na visiwa vya Pacific. Ganesha ni mtoto wa kiume wa Shiva na Parvati. Ni mungu maarufu katika dini zingine pia, kama vile u-Buddha na u-Jaini. Katika michoro na sanamu anatambulika kirahisi, kwa kuwa ana kichwa cha tembo. Kuna masimulizi mbali mbali juu ya asili ya hiki kichwa chake. Ganesha anategemewa kama mungu anayeondoa vikwazo. Anasafisha njia ya mafanikio. Mtu anapoanza safari, biashara, au mradi wowote, huelekeza maombi kwa Ganesha. Lakini pia, Ganesha huwawekea vikwazo wenye kiburi. Ganesha ni mungu mwenye akili sana. Ndiye mlezi wa wanataaluma. Ni mungu wa uandishi pia, na inasemekana alitumia pembe yake kuandika sehemu ya utungo maarufu wa Mahabharata . Washairi na watunzi wa vitabu humtegemea. Aghalabu, katika picha na sanamu, Ganesh

Dini sio Misahafu Pekee

Image
Leo ninapenda kuendelea kuongelea dini, kujenga hoja kwamba dini si misahafu pekee. Ninaongelea mada hii kwa kuwa ninaamini umuhimu wa mijadala ya dini, na kwa kuzingatia tabia ambayo imejengeka Tanzania ya baadhi ya wa-Islam na wa-Kristu kulumbana kuhusu dini zao. Wanaonekana viwanjani wakihubiri dhidi ya dini ya wapinzani wao. Wananukuu misahafu katika kujenga hoja kwamba dini yao ni bora zaidi au ndio dini ya kweli. Binafsi, naona kuwa malumbano haya ni upuuzi mtupu. Dini haiko katika misahafu tu. Ni mfungamano wa nadharia na vitendo. Dini ni mfungamano wa mafundisho ya misahafu na maisha ya kila muumini. Bila mfungamano huo, dhana ya dini inapwaya. Kuna maana gani kwa muumini wa dini kuringia msahafu wa dini yake iwapo maisha yake hayaendani na mafundisho yaliyomo katika msahafu? Badala ya kulumbana kuhusu misahafu, tuangalie maisha ya waumini. Je, tabia za mu-Islam ni bora kuliko za m-Kristu? M-Kristu ni bora kuliko mu-Islam? Jamii ya wa-Islam ni bora kuliko jamii ya wa-Kr