Saturday, December 30, 2017

Tutasoma Visa vya Iceland

Muhula ujao, katika kozi yangu ya Folklore, nitafundisha fasihi simulizi kutoka nchi mbali mbali, kama kawaida. Lakini kwa mara ya kwanza, nitafundisha fasihi simulizi kutoka Urusi na Iceland. Hapo pichani ninaonekana nikiwa nimeshika kitabu kiitwacho Hrafnkel's Saga and Other Icelandic Stories.

Wanataaluma wa fasihi simulizi wanaelewa kuwa haya masimulizi yaitwayo saga ni ya nchi za ulaya Kaskazini, kama Iceland na Ireland. Ni sawa na tendi za kale katika utamaduni wa wa-Swahili.

Nilivutiwa na wazo la kuhusisha fasihi simulizi ya Iceland katika kozi yangu ya Folklore, kutokana na kufundisha utungo wa Kalevala kutoka Finland. Utungo huu , ambao umetafsiriwa katika lugha nyingi, ikiwemo ki-Swahili, iulinifungua macho kuhusu fasihi simulizi ya Ulaya ya kaskazini. Mvuto wa usimuliaji wa hadithi, mila na imani zilizomo zilinigusa kwa namna ya pekee.

Kuhusu hizi saga, kwa miaka mingi nilikuwa ninafahamu uwepo wake, na nilifahamu majina ya baadhi ya hizi saga. Wakati ninasoma katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, 1980-86, profesa Harold Scheub alitufundisha kuhusu Njal's Saga, ambayo inafahamika sana.

Baada ya kuamua kuhusisha fasihi simulizi ya Iceland katika kozi yangu, na baada ya kuamua kuwa nitumie saga, nilianza kutafakari ipi nitumie saga ipi. Mwanafunzi wangu mmoja hapa chuoni St. Olaf aliniambia kuwa mama yake alifanya utafiti na kuhitimu shahada ya uzamifu juu ya saga za Iceland. Tulikubaliana awasiliane naye, na ndiye aliyependekeza nitumie Hrafnkel's Saga.

Baada ya kupata pendekezo hilo, nilifanya utafiti kidogo, nikagundua kwamba Hrafnkel's Saga inazua malumbano miongoni mwa wanataaluma. Suali mojawapo ni iwapo kisa hiki asili yake ni fasihi simulizi au andishi. Baada ya kuona huo utata, niliona kuwa kisa hiki kitafaa katika kozi yangu kama changamoto ya kusisimua akili.

Sunday, December 17, 2017

Tumetoka Darasani

Picha hii ilipigwa tarehe 29 Novemba. Niko na wanafunzi wangu, tukiwa tumetoka darasani. katika somo la "First Year Writing." Hili ni somo la uandishi bora wa ki-Ingereza. Ninalipenda somo hili kama ninavyoyapenda masomo yangu mengine. Darasa letu lina wanafunzi 19.

Baada ya kumaliza kipindi tulitawanyika, lakini dakika chache baadaye nilikutana na hao wawili katika jengo la Buntrock Commons karibu na maktaba, tukapiga picha. Huyu wa katikati anatoka Norway, na huyu mwenzake ni wa hapa Marekani.

Nina bahati na ninafurahi kuwa mwalimu, kushughulika na wanafunzi na vitabu muda wote. Ni kazi ambayo niliitamani tangu nilipokuwa kijana mdogo. Nilipofundishwa ualimu katika chuo kikuu cha Dar es Salaam, ambapo nilisomea Literature, English, na Education, nilifundishwa kuwa mwalimu anashika nafasi ya wazazi, in loco parentis, kwa ki-Latini. Ninawaona wanafunzi kama watoto wangu.

Ninachukulia jukumu langu la kuwaelimisha na kuwalea wanafunzi kwa dhati. Tangu nilipoanza kufundisha, chuo kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1973, nimezingatia wajibu na maadili ya ualimu, ambayo ni kujielimisha kwa bidii, kufundisha kwa uwezo wangu wote, na kuwatendea haki wnafunzi wote bila upendeleo.

Ninafurahi kufundisha hapa chuoni St. Olaf. Walimu wanachapa kazi na uongozi wa chuo unawaheshimu. Wanafunzi wanajua wajibu wao. Wana heshima, na ni wasikivu, wenye dukuduku ya kuhoji na kujua mambo. Ninawapenda. Pamoja na kuwafundisha kwa moyo wote, ninapenda kuwatania. Popote tunapokutana, tunafurahi kama inavyoonekana pichani.

Saturday, December 16, 2017

Vitabu Kama Zawadi ya Krismasi

Niliwahi kuandika makala katika blogu hii kuhusu vitabu kama zawadi ya sikukuu. Kwa wenzetu huku ughaibuni, hili ni jambo la kawaida. Watu wanafurahi kununua vitabu na kuwapelekea ndugu na marafiki wakati wa sikukuu. Watu hufurahi kupata zawadi ya vitabu.

Leo nimeviangalia baadhi ya vitabu nilivyonunua mwezi huu nikajiwa na mawazo kwamba vitabu hivi ni kama zawadi ya Krismasi ambayo nimejinunulia mwenyewe. Watu wengi wanajitayarisha kwa sikukuu kwa kujinunulia mavazi na siku ambayo ndio sikukuu wanajizawadia kwa vyakula maalum na vinywaji. Wanywaji wa bia wananunua bia.

Katika kufikiria hivyo, nimejiaminisha kwamba sijakosea katika kujiaminisha kuwa vitabu nilivyonunua katika katika kipindi hiki cha kuelekea Krismasi ni zawadi yangu. Tofauti na bia, vitabu hivi nitavifurahia kwa miaka yote ya maisha yangu, na vitabaki hata baada ya mimi kuondoka duniani.

Pichani hapa kushoto kuna vitabu vinne. Cha kwanza ni Behold the Dreamers, cha Imbolo Mbue. Huyu ni dada kutoka Kamerun. Nilikuwa nimesikia jina lake kijuu juu, lakini sikuzingatia. Nilipoona kitabu chake hicho katika duka la vitabu la hapa chuoni St. Olaf niliamua kukinunua. Nilivyoangalia ndani nimeona kimepata sifa nyingi sana kutoka kwa wahakiki. Bila shaka nitakiweka katika kozi yangu mojawapo.

Kitabu cha pili ni Shot All to Hell: Jesse James, the Northfield Raid, and the Wild West's Greatest Escape kilichotungwa na Mark Gardner. Hiki ni kimoja kati ya vitabu vingi vilivyowahi kuchapishwa juu ya jambazi Jesse James na washirika wake. Nilishafanya utafiti juu ya Jesse James, kuanzia mwaka 1992 hapa Northfield, ambapo jambazi huyu na genge lake walivamia benki na kujaribu kuiba pesa, lakini wenyeji waliwashtukia na kuzimisha uharamia huo na majambazi wakakimbia. Kitabu hiki nilikinunua kwa sababu kinahusu utafiti wangu na pia kwa kuwa kinahusu mji ambamo ninaishi.

Kitabu cha tatu nilichonunua ni The Essentials of Psychoanalysis, ambacho ni mkusanyo wa insha kadhaa maarufu za Sigmund Freud, ambao umetayarishwa na Anna Freud. Aliyetafsiri insha hizo ni James Strachey. Ninavyo vitabu vyenye insha za Freud, lakini niliona ni vizuri kuwa na insha hizi katika kitabu kimoja.

Kitabu cha nne ni Nana cha Emile Zola. Nilifahamu jina la mwandishi Zola tangu zamani sana, labda wakati ninasoma chuo kikuu cha Dar es Salaam. Nilikuja kumfahamu kama mfano wa waandishi waliofuata mkondo wa "critical realism." Nilifahamu jina la kitabu chake kingine, Germinal. Mimi mwenyewe, ninapofundisha fasihi, mara kwa mara nimekuwa nikimtaja Zola. Nitajitahidi nipate wasaa wa kusoma hizi riwaya za Zola, ingawa ninajua itakuwa baada ya Krismasi

Wednesday, December 13, 2017

Mahojiano Yangu Katika "Wayne Eddy Affair"

Katika wiki chache zilizopita, nimehojiwa mara tatu katika kipindi kiitwacho "Wayne Eddy Affair" cha Kymn Radio hapa Northfield, Minnesota. Mwendeshaji wa kipindi, Wayne Eddy, ambaye anaonekana pichani hapa kushoto, tulikutana kwa bahati tu hapa Northfield, wiki chache zilizopita. Ni mzee mzoefu, ambaye emeendesha vipindi vya redio kwa zaidi ya miaka hamsini, na ni mchangamfu. Kutokana na mahojiano yetu, tumezoeana sana na tumekuwa marafiki.

Mahojiano hayo, ambayo yalikuwa ya papo kwa papo, yalihusu mambo mengi , hasa maisha yangu tangu kijijini kusini magharibi Tanzania, kusoma kwangu, historia na utamaduni wa Tanzania, kuja kwangu Marekani, na shughuli ninazofanya hapa. Katika sehemu ya tatu ya mahojiano haya, ninasikika nikisimulia hadithi ya ki-Matengo na na nyingine kutoka Burkina Faso. Karibu, uyasikilize mahojiano hayo mtandaoni hapa.

Sunday, December 10, 2017

Maonesho ya St. Dominic Boutique, Northfield, Minnesota

Jana, November 9, shule ya St. Dominic ya hapa Northfield, ilikuwa na wageni wengi. Palifanyika maonesho ya vitu mbali mbali vya matumizi na mapambo ya nyumbani na mavazi na urembo, machapisho, kazi za sanaa. Tamasha hilo lililoitwa St. Dominique Boutique lilijumuisha watengenezaji na wauzaji wa vitu hivyo yapata 60, na watu wengi kutoka maeneo mbali mbali walifika kuangalia na kununua. Mimi nilikuwepo, nikapata fursa ya kuongea na watu juu ya maandishi, mihadhara na utoaji ushauri kuhusu masuala ya tamaduni.
Nilipofika maoneshoni na kuelekezwa kwenye sehemu niliyopangiwa, huyu mzee anayeonekana hapa kushoto alisogea hima na kunisaidia kuandaa meza yangu. Alijitambulisha kuwa alihudhuria mhadhara niliotoa katika kanisa mjini Faribault. Hapo nilikumbuka kuwa niliwahi kutoa mihadhara miwili katika kanisa liitwalo First English Lutheran Church kuhusu masuala ya tofauti za tamaduni. Waumini walipata fursa ya kununua nakala za kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Mzee huyu, ambaye alininieleza kuwa ni padri mstaafu, alikuwa na meza yake pembeni yangu. Kwa hiyo, tuliweza kuongea muda wote wa maonesho.


Kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa nane, watu walikuwa wanafika na kuangalia vitu na kununua, na kuongea na sisi tuliokuja kuonesha bidhaa na vitu vyetu vingine.Huyu dada hapa kushoto alifika kwenye meza yangu na dada yake mkubwa. Tuliongea kirefu kuhusu shughuli zangu na kuhusu vitabu vyangu. Hatimaye huyu dada alinunua hivi viwili alivyoshika, tukapiga picha. Kama kawaida, nimejionea mwaka hadi mwaka jinsi wa-Marekani wanavyopenda vitabu. Wakishauliza bei na kutajiwa, wanatoa hela hapo hapo na kununua.
Huyu bwana hapa kushoto sikumwelewa mwanzo alipofika mezani pangu, akaangalia na kuondoka bila kusema kitu, pamoja na kwamba nilimsalimia. Baada ya dakika chache alisogea tena na kuangalia, na hakusema kitu. Kisha akakaa kwenye kiti kilichokuwa pembeni yangu, bila kunisalimia. Akachukua kijidaftari mfukoni mwake, akaanza kuandika sentensi mbili tatu, akanipa. Alikuwa ananiuliza iwapo nimesikia habari za m-Marekani Andrew Foster aliyeanzisha shule Ghana kwa ajili ya wasiosikia. Nilivyosoma na kumwangalia alivyokuwa ananiangalia, nilianza kuhisi kuwa ni mlemavu. Hasikii.

Tuliendelea kuzungumza kwa maandishi, hadi mwisho, na tulipoagana, nilimwandikia ujumbe wa mwisho kumwuliza kama angependa tupige picha, tukapiga. Nitaandika kuhusu tukio hili siku nyingine, katika blogu hii.


Kama nilivyoandika katika blogu hii, kitabu changu cha Matengo Folktales kilitajwa tarehe 23 Novemba katika "Jeopardy," programu  maarufu ya televisheni hapa Marekani. Baada ya kutajwa hivyo na kuleta msisimko hapa Marekani, niliamua kuitumia hiyo kama fursa.

Nilitengeneza bango lenye tamko lililokuwepo kwenye kipindi cha Jeopardy."  Ilikuwa ni burudani kuwaonyesha wa-Marekani hili bango na kitabu, huku nikifanya utani kuhusu kitabu changu kuonekana "Jeopardy."Ninaipongeza shule ya St. Dominic kwa kuandaa maonesho hayo. Ingawa ilikuwa ni mara yao ya kwanza kufanya hivyo, shughuli ilifanikiwa sana. Watu wa aina mbali mbali walifika. Ingawa shule ni ya madhehebu ya Katoliki, hapo kwenye meza yangu pekee niliweza kuongea na watu wa imani mbali mbali. Kwa kadiri nilivyoona, itakuwa vizuri iwapo maonesho haya yatakuwa endelevu kwa siku zijazo. 

Thursday, December 7, 2017

Kitabu "Matengo Folktales" Chaendelea Kuwa Gumzo

Kama nilivyoeleza katika blogu hii, kitabu changu, Matengo Folktales, kilitajwa tarehe 23 November, 2017, katika programu ya televisheni iitwayo Jeopardy ambayo ni maarufu hapa Marekani. Kwa kuwa sikuwa na mazoea ya kuangalia program hii, wala nyingine yoyote, sikufahamu umaarufu wake. Kumbe sasa, baada ya kitabu changu kutajwa, nimeshuhudia na ninaendelea kushuhudia msisimko miongoni mwa wa-Marekani wa kina aina.

Mbali na watu ninaokutana nao mitaani, maprofesa wenzangu hapa chuoni St. Olaf nao wamekuwa wakinipongeza sana. Siku kadhaa nilizopita, kwenye mkutano mjini St. Paul, profesa moja wa chuo cha Macalester naye aliniambia kutajwa katika Jeopardy ni kwamba nimefikia kilele cha "popular culture" hapa Marekani.

Note hayo badi hayajaniingia sawa sawa kichwani, kwa sabbat, kama nilivyosema, sikuwa na mazoea wala ufahamu wa kipindi cha Jeopardy. Ninaanza kuelewa, ila sitaweza kuelewa kama wa-Marekani wenyewe wanavyoelewa, kwani ni suala la tofauti za tamaduni. Kama hukukulia katika utamaduni fulani, ni vigumu sana kuyafahamu mambo ya utamaduni ule sawa na wanavyofahamu wenye utamaduni ule. Ni hivyo kwa Wa-Afrika walioko hapa Marekani, na kwa wa-Marekani walioko Afrika.

Leo hapa chuoni tulikuwa na mkutano wa maprofesa, ambao tunafanya mara moja kila mwezi. Mkutano ulihusu masuala mbali mbali, na ulipokaribia kwisha, ilikuja zamu ya afire taaluma wa chuo kusema machache. Baadhi ya mambo aliyosema ni kutangaza mania ya watu waliochapisha vitabu katika siku za karibuni, na majina ya watu waliojipatia tuzo au heshima kwa namna nyingine. Kati ya watu has, alitaja tukio la kitabu changu kutajwa katika Jeopardy. Alianza kwa kuuliza, nani kati yetu anategemea itakuja siku atajwe katika Jeopardy?

Baada ya kusema hivyo, alionyesha kwenye skrini kubwa picha hii hapa kushoto kama iliyoonekana katika Jeopardy. Mkutano ulipoisha, watu waliendelea kuongea nami kwa furaha kuhusu maana ya tukio hili katika utamaduni wa Marekani. Kwangu hii ni elimu ya ziada, nikiwa kama mtafiti wa tamaduni, mada ambayo ninaitolea mihadhara katika taasisi na jumuia mbali mbali na nimeiandikia makala na pia kitabu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Kwa kuwa ninafanya juhudi kujielimisha na kuelimisha wengine, nina kila sababu ya kujiwekea kumbukumbu ya mambo hayo, kama ninavyofanya hapa katika blogu yangu. Ni muhimu nijiwekee kumbukumbu hizi, ili angalau watoto wangu na vizazi vijavyo waweze kujua nilikuwa ninafanya nini wakati wa uhai wangu.