Posts

Showing posts from 2011

Mahojiano na Profesa Mbele, "Kombolela Show"

Nimeona niwaletee wadau mahojiano niliyofanyiwa katika "Kombolela Show," Oktoba 2, 2010. Mwendesha mahojiano alikuwa Metty Nyang'oro. Kwa jinsi mtandaoni kunavyofurika taarifa, nimeona si vibaya kuyaleta tena mahojiano haya, ili wadau wayasikie na kuyatafakari na kuchangia, endapo watajisikia kufanya hivyo, kwani elimu haina mwisho, wala haina mwenyewe.

Hadithi za wa-Matengo Zatamba Ughaibuni

Image
Hivi karibuni, nilipata ujumbe kutoka kwa Profesa Paschal Kyoore wa Chuo cha Gustavus Adolphus kuwa anatunga kozi mpya, "The African Trickster," akaomba ushauri wangu, kwani mada hiyo ya "trickster" nimeifanyia utafiti na kuandika makala kwa miaka mingi. Hatimaye, Profesa Kyoore ameniletea ujumbe kuwa ameshaagiza nakala za kitabu cha Matengo Folktales kwa ajili ya darasa hilo. Kisha angependa siku moja niende kuongea na wanafunzi wake, nami nimekubali. Ninafurahi sana ninapoona watu wa ughaibuni wakipata fursa ya kujifunza mambo ya kwetu, na hadithi za jadi ni hazina mojawapo kubwa, kama nilivyoelezea hapa . Ni fursa kwetu na kwa walimwengu kutambua mchango wa wahenga wetu kwa utamaduni wa dunia, kwani katika hadithi zao, wahenga waliongelea na kutafakari kila aina ya suala linalomkabili binadamu, sawa na watu walivyofanya watu wa mataifa mengine. Hadithi za wa-Matengo zinatumika katika vyuo mbali mbali hapa Marekani, kama nilivyoelezea hapa . Yapata miaka

Maongezi na Wanafunzi Waendao Tanzania

Image
Profesa Barbara Zust , wa Chuo cha Gustavus Adolphus , amenialika kwenda kuongea na wanafunzi anaowaandaa kwa safari ya Tanzania. Anafundisha masomo ya uuguzi, na mwezi Januari anawapeleka wanafunzi Tanzania kujifunza masuala ya afya na matibabu katika utamaduni tofauti na ule wa Marekani. Profesa Zust ameshawapeleka wanafunzi Tanzania mara kadhaa. Katika kuwaandaa, hutumia kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences na pia hunialika nikaongee nao. Anajisikia vizuri sana ninapokutana na wanafunzi wake kujibu masuali yao na kuwapa maelezo mbali mbali, nami huwa nafurahi kukutana na wanafunzi hao wanaosomea taaluma ambayo sikusomea, ila ni wazi kuwa wanafaidika na mawazo yangu kuhusu jinsi tofauti za tamaduni zinavyohusika katika taaluma yao. Hapa kushoto ni picha tuliyopiga na wanafunzi waliokuwa wanaenda Tanzania mwaka 2009. Tulikuwa kwenye chumba cha mkutano cha kanisa la Shepherd of the Valley, mjini Apple Valley. Habari za mkutano wetu niliziandika hapa .

Mdau Mwingine, Mwanafunzi, Kaja

Image
Mara kwa mara naandika habari za wasomaji wa maandishi yangu wanaonitembelea, au ninaokutana nao sehemu mbali mbali. Jana, baada ya kumaliza kufanya mtihani wa mwisho wa somo langu la fasihi ya Afrika Kusini, kaja ofisini mwanafunzi Logan. Alikuja na nakala ya kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences , ili nikisaini. Nilisaini, tukaendelea na michapo. Logan alisoma somo langu jingine mwaka jana. Chuo Cha St. Olaf kinaamini kuwa ni muhimu wanafunzi waufahamu ulimwengu nje ya Marekani. Kilinileta hapa, mwaka 1991, kuanzisha masomo katika idara ya ki-Ingereza juu ya uandishi wa ki-Ingereza kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Wanafunzi wanavutiwa na fursa hii ya kupanua upeo wao, kuzifahamu jamii na tamaduni mbali mbali.

Makari Hodari

Image
Kwa sisi tuliosoma shule ya msingi zamani, Makari Hodari ni jina tunalolikumbuka sana. Tulisoma habari zake zilizotungwa na Padri Alfons Loogman, mwandishi wa vitabu vya Someni Bila Shida na Someni Kwa Furaha . Kwa kweli, padri huyu aliziteka nyoyo zetu watoto, akatufanya tupende kusoma. Aliandika vitabu kadhaa vya masomo ya ki-Swahili na hata mwongozo kwa walimu kuhusu kufundisha kusoma. Nakumbuka kuwa katika shule yangu ya msingi ya Litembo , tulikuwa tunasoma hadithi ya Makari Hodari kwa kuiimba. Watoto wote darasani tulikuwa tunaimba kwa pamoja, kwa furaha. Hadi leo naweza kuimba tulivyoimba. Na mwalimu alikuwa akiimba nasi. Pamoja na utamu wa hadithi, tulivutiwa na picha. Nikiitafakari hadithi ya Makari Hodari, naona kuwa ilijengeka katika mfumo wa zile hadithi za kale za mashujaa, ambazo zinasimuliwa katika tamaduni mbali mbali. Kwa mfano, Wa-Haya wana hadithi za mashujaa kama Mugasha, Rukiza, na Kilenzi. Wa-Chagga wana hadithi ya Mrile, wa-Swahili hadithi ya Liongo Fumo. Had

Wanafunzi Wangu Wameondoka Tanzania

Image
Mapema leo, wanafunzi niliowaleta Tanzania mwaka huu wameondoka nchini, baada ya kumaliza masomo ya miezi kadhaa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam . Wanafunzi hao nami tunaonekana katika picha hapa kushoto, tuliyopiga kwenye hoteli ya Wilolesi , mjini Iringa, tarehe 10 Agosti. Kama nilivyoelezea mara kadhaa katika blogu zangu, tulizunguka sehemu mbali mbali, kama vile Kalenga , Matema Beach , Lyulilo na Bagamoyo . Baada ya mizunguko hiyo niliwafikisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam , nami nikarejea Marekani kwani muhula wa masomo ulikuwa unaanza. Ni faraja kuona wameondoka salama, kwani nilikuwa na wasi wasi kutokana na taarifa za migomo, vurugu na mabomu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam . Kwa miaka yote niliyofundisha hapa Marekani nimekuwa mshauri katika programu kadhaa zinazopeleka wanafunzi Tanzania na nchi zingine za Afrika, kama nilivoelezea hapa . Huwa tunawaambia hao wanafunzi kuwa wasishiriki maandamano au migomo katika nchi husika. Kwa upande wa Tanzania, nimekuwa mwepesi kuwaeleza j

Vitabu Kama Zawadi ya Idd el Fitr na Krismasi

Hebu fikiria: sikukuu ya Idd el Fitr au Krismasi imewadia na unataka kuwapa zawadi ndugu na marafiki zako, wa-Tanzania wenzako. Unaamua kwenda kwenye duka la vitabu, na unawanunulia nakala za kitabu kama Kufikirika cha Shaaban Robert, au Binadamu na Maendeleo cha Mwalimu Nyerere, au kwa wanaojua ki-Ingereza, The Tempest cha Shakespeare. Unawafungia vizuri, kisha unawapelekea. Je, watajisikiaje hao wa-Islam na wa-Kristu wa Tanzania? Miaka ya tisini na kitu, katika jumuia ya mawasiliano ya mtandaoni iitwayo Tanzanet, ambayo wanachama wake ni wa-Tanzania na marafiki wa Tanzania, niliwahi kuandika, kiutani, kwamba siku za usoni huenda nikaamua kwamba, kwenye mialiko ya arusi nisipeleke kreti ya bia, bali kreti ya vitabu. Ingawa ulikuwa ni mchapo, nilikuwa na jambo muhimu kichwani, kwani ni kweli kuwa vitabu ni hazina, na ni bora kuliko bia. Hapa Marekani, ni kawaida watu kutoa au kupokea zawadi ya vitabu. Msimu kama huu wa Krismasi, watu wengi wananunua vitabu ili kuwapa zawadi wenzao

Hatimaye Itabidi Nielezee Nilivyotoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam

Mwaka 1991 niliondoka Chuo Kikuu Dar es Salaam , nikaja kufundisha Chuo cha St. Olaf hapa Marekani. Kulikuwa na mlolongo wa masuala yaliyonifanya nikaondoka, baada ya kuwa mwalimu pale kuanzia mwaka 1976. Sijaelezea masuala hayo, ingawa yamo katika maandishi kwenye makabrasha, ambayo yalikuwa mawasiliano rasmi baina ya wahusika. Mwaka jana, nikiwa maeneo ya Mwenge, Dar es Salaam, na marafiki zangu, nilikutana na Profesa Sam Maghimbi wa Chuo cha Elimu cha Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam . Nilishangaa alivyokumbushia nilivyotoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam , na marafiki zangu wakasikia. Nilifarijika kuona kuwa kumbukumbu bado zipo kiasi hiki. Wako wengi wanaokumbuka nilivyofundisha Chuo Kikuu Dar es Salaam , na jinsi nilivyoondoka. Lakini, kwa jinsi miaka inavyopita, wanafikia umri wa kustaafu, na wengine wamefariki. Nami natatizwa na fikra ya wa-Tanzania wengi za kudhani kila m-Tanzania anayeenda kufanya kazi nje hana sababu nyingine bali kufuata maslahi binafsi. Hata mafisadi walioza

Leo Nimekuwa Marley Katika Hadithi ya Charles Dickens

Image
Leo katika idara yetu ya ki-Ingereza tulifanya onesho la tamthilia kutokana na hadithi ya A Christmas Carol iliyotungwa na mwandishi maarufu Charles Dickens. Watu tuliosoma shule zamani tunakumbuka sana vitabu vya Charles Dickens, hasa Oliver Twist . Ni nani asiyekumbuka wahusika wa hadithi hii, kama vile Oliver Twist mwenyewe, The Artful Dodger, na Fagin m-Yahudi? Ilikuwa raha kusoma miaka ile, na tulikuwa tunapenda hata kukariri baadhi ya kauli za hao wahusika. Basi katika kipindi hiki cha kuelekea Krismasi, idara yetu ina jadi ya kufanya jambo la kumbukumbu na burudani. Kwa miaka kadhaa, tumekuwa tukiigiza mchezo huu unaotokana na riwaya hii ya Dickens. Katika A Christmas Carol kuna wahusika wakuu kadhaa, na Scrooge ndio kinara. Huyu ni mfanyabiashara bahili, ambaye zamani alikuwa na mshiriki wake wa kibiashara aliyeitwa Jacob Marley. Wakati hadithi inapotokea, tunaambiwa kuwa Jacob Marley alifariki miaka saba iliyopita. Tunachoona ni mzimu tu wa Marley, ambao unamtokea Scroo

Posho za Wabunge Hazitoshi

Yapata mwaka 1997 nilipokuwa katika utafiti Mwanza, mimi na washiriki wa utafiti tulikutana na mbunge katika hoteli ya Ramada. Sikumbuki alikuwa ni mbunge wa sehemu gani nchini. Katika maongezi yetu, alilalamika kwa masikitiko kuwa wa-Tanzania wanaamini kuwa mbunge ni mtu mwenye hela sana. Akatoa mfano wa maisha yake mwenyewe, kwamba nyumbani kwake, watu wamejaa kwenye makochi muda wote. Mchana wako hapo, na usiku wanalala hapo. Na yeye anawajibika kuwalisha na kuwanywesha siku zote. Wakati huu ambapo wa-Tanzania wanalumbana kuhusu kuongeza posho za wabunge, mimi nakumbuka kilio cha yule mbunge. Nasita kuwalaumu wabunge wanapodai kuongezewa posho. Naamini kuwa posho zao hazitoshi. Tatizo ni sisi wa-Tanzania, sio wabunge. Mtu akishapata ubunge, tunamtegemea atufanyie mambo mengi sana yanayohitaji hela. Mbunge akiingia baa, tunategemea ofa zake, tena za uhakika, sio soda za reja reja. Tunamtegemea achangie hela nyingi kwenye vikao vya "send-off," kipaimara, arusi, na kadhalik

Miaka 50 Baada ya Uhuru, Mtoto Albino Anaogopa Kwenda Shule

Image
Jana ilikuwa ni kumbukumbu ya miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika. Nilijaribu sana kuandaa makala kuhusu siku hiyo ya jana, lakini nilipata kigugumizi. Kwa upande moja, ninafahamu kuwa ndoto ya uhuru aliyokuwa nayo Mwalimu Nyerere, ya kuleta ukombozi wa kweli katika nyanja mbali mbali na kujenga taifa linalojitegemea, imezimishwa na sera zilizopo, ambazo zinaimarisha ukoloni mamboleo. Kama ningeandika makala jana kuhusu kumbukumbu za uhuru wa Tanganyika, pangekuwa hapatoshi. Lakini jambo jingine lililonipa kigugumizi ni kuwa mawazo yangu yalikuwa yanarudi tena na tena kwenye taarifa niliyosoma wiki kadhaa zilizopita, kuhusu mtoto albino wa Ludewa ambaye anaogopa kwenda shule asije akauawa na watu wenye imani za kishirikina. Habari hii niliiweka hapa . Siku nzima ya jana nilikuwa najiuliza, inakuwaje miaka 50 baada ya uhuru, mtoto huyu anaishi katika hofu ya kuuawa? Tumepiga hatua mbele au nyuma? Enzi za Mwalimu Nyerere, mtoto huyu angekuwa anaenda shule sawa na watoto wengine. Ndoto ya M

Hifadhi za Historia Bagamoyo

Image
Bagamoyo ni mji maarufu katika historia ya nchi yetu na dunia. Kwa mtu anayetaka kujifunza historia hiyo, napendekeza ziara Bagamoyo kuangalia hifadhi zilizopo. Mwaka huu, nilitembelea Bagamoyo, na wanafunzi kutoka Marekani, kama nilivyoelezea hapa . Mahali pamoja tulipotembelea ni Caravan Serai, hifadhi mojawapo ya historia. Hapa kushoto ninaonekana mbele ya mlango wa kuingilia Caravan Serai. Kuna sanamu ya mtumwa aliyebeba pembe ya ndovu. Hapa kushoto tunaonekana katika eneo la Caravan Serai, tukiwa na mfanyakazi wa hifadhi hiyo, ambaye alikuwa anatuonyesha na kutuelezea yaliyomo. Hapa anaonekana mtaalam wetu akitoa maelezo ya historia ya Caravan Serai. Humo ndani kuna nyaraka, picha na vitu mbali mbali, kama vile vyombo vya nyumbani, na maelezo kuhusu vitu hivyo. Hapa kushoto, katika picha ya katikati, anaonekana Tippu Tip. Hapa kushoto ni picha ya watumwa. Hapa kushoto ni picha ya "bangili," kwa mujibu wa bandiko la ma

Barua za Shaaban Robert

Image
Kitabu cha Barua za Shaaban Robert ni mkusanyiko wa barua alizoandika Shaaban Robert kwa mdogo wake Yusuf Ulenge baina ya mwaka 1931 na 1958. Yusuf Ulenge alifanya busara ya kuzihifadhi na sasa zimechapishwa kama kitabu, na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam . Mhariri Profesa Mugyabuso Mulokozi amefanya kazi kubwa na watafiti wenzake katika kuzichapisha na kuziwekea maelezo. Nilikinunua kitabu cha Barua za Shaaban Robert mwaka 2008 katika duka la Taasisi . Nilifurahi na pia kushtuka kugundua kuwa Yusuf Ulenge alikuwa mdogo wa Shaaban Robert. Jina la Yusuf Ulenge nililifahamu tangu kwenye mwaka 1964, nilipokuwa darasa la sita. Nilinunua kitabu kiitwacho Nguzo ya Maji na Hadithi Nyingine , kilichotungwa na Yusuf Ulenge. Miaka yote sikuwa na wazo hata kidogo kuwa huyu alikuwa mdogo wa Shaaban Robert. Sasa, hizi barua zimenifungua macho kabisa, kwani nimejionea jinsi uhusiano wa hao ndugu wawili ulivyokuwa mkubwa na jinsi Yusuf Ulenge naye alivyokuwa mwand

Wadau Wamekuja Ofisini Kwangu

Image
Leo, bila kutegemea, nimetembelewa na akina mama wawili ofisini kwangu. Walijitambulisha, wakasema wamekuja ili nisaini nakala za vitabu vyangu. Anayeonekana kushoto ni Mama Kay wa Lanesboro, Minnesota, na huyu wa kulia ni Mama Sandy wa maeneo ya St. Louis, Missouri. Nimesaini nakala tatu za Matengo Folktales na moja ya Africans and Americans: Embracing Cultural Differences ambazo wamezinunua leo hapa Chuoni St. Olaf . Tumeongelea vitabu hivi na masuala mengine ya aina hiyo. Kumbe, Mama Kay, tulishaonana miaka kadhaa iliyopita hapa St. Olaf , alipokuja na mumewe, ambaye ni marehemu sasa, pamoja na Mchungaji Gabriel Nduye, Mchungaji Mengele (ambaye sasa ni askofu) na mkewe, wote kutoka Njombe. Mama Kay ameshafika Tanzania. Nimewaambia kuwa nimeguswa na ujio wao. Ninaguswa na namna wadau wanavyoyafuatilia maandishi yangu, na falsafa yangu ni kumshukuru Mungu kwa yote. Kama inavyoonekana katika picha, tumefurahi kukutana.

Makafiri

Ingawa watu wengi wanaamini kuwa masuala ya dini ni hatari kujadiliwa, blogu yangu haina kipingamizi kwenye kujadili masuala hayo, kama ilivyo kwa masuala mengine. Kama kuna tatizo, tatizo haliko kwenye mada, bali tatizo ni wahusika, kama nilivyoandika hapa . Leo napenda kuongelea suala ambalo limenikera kwa muda mrefu. Ni suala la watu kuwaita wengine makafiri. Nimeshasoma taarifa kutoka sehemu mbali mbali za Tanzania ambazo zimenifanya niandike ujumbe huu. Leo katika mtandao wa Facebook, nimeona taarifa kutoka Mbeya ambamo mtu analalamika kuwa kuna makafiri sana kule. Miezi kadhaa iliyopita, nilisoma taarifa kutoka Zanzibar, kwamba watu wa kijiji fulani walikuwa hawataki makafiri kwenye eneo lao. Ukipita mtandaoni, utaona kuwa jadi hii ya kuwaita wengine makafiri inajitokeza mara kwa mara miongoni mwa watu wa Visiwani. Sijui hao wanaowaita wengine makafiri walipata wapi uwezo wa kufahamu undani wa watu wengine kiasi hicho. Nilidhani kuwa sote tunaosema tunamwamini Mungu tunafaham

Taarifa ya Ikulu Kuhusu Mkutano wa JK na CHADEMA

Image
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na ujumbe wa Serikali yake leo, Jumapili, Novemba 27, 2011, amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam, yamefanyika katika mazingira ya urafiki na ujumbe wa CHADEMA umewasilisha mapendekezo yake kuhusu mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya Tanzania. Serikali imepokea mapendekezo hayo. Hata hivyo, pande zote mbili zimekubaliana kukutana tena asubuhi ya kesho, Jumatatu, Novemba 28, 2011, ili kuipa nafasi Serikali iweze kutafakari mapendekezo hayo. Lakini pande hizo mbili zimekubaliana kuwa Katiba ya sasa ni Katiba nzuri iliyolilea Taifa kwa miaka 50 iliyopita kwa sababu ni Katiba ya sasa iliyoliwezesha Taifa la Tanzania kuwa na amani, utulivu na kupata maendeleo makubwa ambayo nchi yetu imepata mpaka sasa. Pia pande zote mbili zimekubaliana kuhusu umuhimu wa kutunga Katibu Mpya kama Mheshimiwa Rais Kikwete al

Mahojiano na Profesa Joseph Mbele

Nimefanya mahojiano mara nyingi na watu mbali mbali, wakiwemo wa-Tanzania, kuhusu shughuli zangu katika jamii, kama vile maandishi na mihadhara. Hapa naleta mahojiano yaliyofanyika Septemba 2006, ili wale ambao hawajawahi kusikia sauti yangu au namna yangu ya kujieleza katika mazungumzo ya papo kwa papo, wapate fursa hiyo. (Chanzo: Butiama.podomatic )

Nimekutana na Wadau wa New Hampshire

Leo nimebahatika kukutana na wadau wawili, mtu na mkewe, kutoka New Hampshire, ambako ni waumini wa Kanisa la Holy Trinity. Wamekuja hapa Minnesota kwa masuala ya shirika la Bega kwa Bega , ambalo linashughulikia ushirikiano na maendeleo katika mkoa wa Iringa. Wadau hao, Mama Dot na Mzee Kurt, wanajiandaa kwenda Iringa, ambako wameshaenda mara kadhaa. Katika ujumbe wao wa mwanzo kwangu, walisema kuwa Profesa Joe Lugalla , ambaye wako wote New Hampshire, aliwahamasisha tukutane. Profesa Lugalla, kama mimi, anawasaidia wa-Marekani wanaokwenda Tanzania kwa kuwapa ushauri unaohitajika. Kwa msingi huo, amekuwa mdau mkubwa wa kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences " na amekipigia debe kwa watu hao tangu kilipokuwa mswada tu, mkusanyiko wa dondoo mbali mbali, usio na sura ya kitabu. Wadau hao wawili nami tumeongea kwa karibu saa mbili. Maongezi yetu yalihusu shughuli wanazofanya Iringa katika mpango wa Bega kwa Bega, na hasa maandalizi wanayofanya ya

Wizard of the Crow: Riwaya ya Ngugi wa Thiong'o

Image
Siku hizi, katika darasa langu mojawapo, tunasoma Wizard of the Crow , riwaya ya Ngugi wa Thiong'o. Kama kawaida yake miaka hii, Ngugi huandika riwaya zake kwanza katika lugha ya Kikuyu. Ndivyo alivyofanya kwa riwaya hii, kisha akaitafsiri kama Wizard of the Crow . Hatujamaliza kuisoma, bali tunakaribia katikati. Ni moja kati ya riwaya ndefu kabisa zilizowahi kuandikwa na wa-Afrika. Kwa kigezo hiki, riwaya hii inanikumbusha ile riwaya maarufu ya Bwana Myombekere na Bibi Bugonoka Ntulanalwo na Bulihwali iliyoandikwa na Aniceti Kitereza. Katika riwaya hii, Ngugi si yule Ngugi ambaye tumezoea kumsoma kwa miaka yapata thelathini sasa, ambaye vitabu vyake katika kipindi hiki, tofauti kiasi fulani na miaka ya mwanzo, vimebeba hisia za kupambana na uonevu, unyonyaji, na ukoloni mamboleo bila mzaha. Kwa miaka mingi, Ngugi ameonekana kama mwandishi mwenye hasira, na wasomaji na wahakiki wengi wamekuwa wakilalamika kuwa hasira hizi zimedhoofisha sanaa katika uandishi wake. Lakini Wizard

Wabunge wa CCM Wanakera

Leo unatimia mwaka mmoja tangu nichapishe makala hii hapa chini. Kitu kimoja kilichonifanya niitafute na kuileta tena ni mjadala wa siku chache zilizopita katika Bunge la Tanzania kuhusu suala la Katiba. Niliwaona wabunge wakimjadili mtoa hoja, Mheshimiwa Tundu Lisu, au wakiongelea masuala ya kifamilia ya viongozi wa CHADEMA, badala ya kujadili hoja. Inakera. Na mimi ninayesema hivi ni raia ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa. ------------------------------------------------------- Chanzo: Hapakwetu Wabunge wa CCM wanakera. Tukianzia na wabunge hao walioapishwa safari hii, sitasahau kuwa hao ndio waheshimiwa waliotoroka midahalo wakati wa kampeni. Wote walitoroka midahalo, kitendo ambacho kimenikera. Mimi kama mwalimu, ninayetambua umuhimu wa midahalo, ninawashutumu hao waheshimiwa. Soma hapa . Kila nitakapokuwa naona sura za hao waheshimiwa wa CCM, nitakuwa nakumbuka kitendo chao hiki cha kutoroka midahalo. Nitakuwa naangalia kama watajirekebisha au kama kitendo ki

Mjengwablog Iliibua Kashfa ya Pan African Energy Mapema

Chanzo: Mjengwablog Ndugu zangu, Nafurahi kuwajulisha, kuwa Mjengwablog. com ndio iliyoibua kwa mara ya kwanza kashfa ya mradi wa gesi unaouhusisha kampuni ya Kisweden ya Pan African Energy , Tanesco na Wizara ya Nishati na Madini. Habari kuhusu kashfa hiyo ziliripotiwa kwa mara ya kwanza hapa nchini na blogu hii Ijumaa ya Julai 15, 2011. Ni siku tatu kabla ya Waziri Ngeleja kuwasilisha bajeti ya Wizara ya Nishati Na Madini. Bila shaka yeyote, habari hiyo ilichangia kwenye kuongeza nguvu ya mjadala bungeni. Hapa chini ni habari husika niliyoiposti hapa globuni na kwenye mitandao mingine kama vile Global Publishers, Jamii Forums na Wanabidii. Pichani juu Waziri Ngeleja akipongezwa na wabunge wenzake wa CCM baada ya bajeti ya wizara yake kupitishwa. Ilikwamishwa ilipowasilishwa kwa mara ya kwanza. Mheshimiwa Ngeleja, Sweden Kuna Kashfa Ya Nishati Yetu Ndugu zangu, Waziri wa Nishati na Madini Mheshimiwa William Ngeleja leo anawasilisha bajeti ya wizara yake huku kashfa ya nish

Nimekutana na Mdau Mjini Apple Valley

Image
Leo nimekutana na mdau Dr. Mary Sheedy Kurcinka , mhadhiri na mwandishi maarufu wa masuala ya malezi ya watoto wachanga. Nilishamtaja siku chache zilizopita hapa . Tuliongea kwa saa moja na nusu mjini Apple Valley. Mama huyu alishatembelea Nigeria na Ghana wakati wa ujana wake, akaandika kuhusu malezi ya watoto wachanga katika jamii ya wa-Yoruba. Sasa anapangia kwenda Tanzania, mwanzoni mwa mwaka ujao. Mazungumzo yetu ya leo yalihusu suala hilo analofanyia utafiti. Aliponiandikia ujumbe wa kwanza, wiki kadhaa zilizopita, alisema alisikia habari zangu kutoka kwa muumini wa Shepherd of the Valley Lutheran Church . Leo kaja na nakala ya kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences , ambacho alikinunua hivi karibuni. Amesema amekisoma na amekipenda sana. Kimemkumbusha aliyoyaona alipoishi Nigeria na Ghana. Kama ilivyo kawaida kwa wa-Marekani, aliniomba nisaini nakala yake, nami nikafanya hivyo. Katika kuongea naye, nimepata motisha ya kufuatilia suala la mal

Mhadhara wa Jana Ulivyofanikiwa

Image
Mhadhara wangu wa jana kwenye shule ya Mazingira, Apple Valley, ulifanikiwa sana. Ni umbali wa dakika 45 kutoka hapa ninapoishi. Niliongea kuanzia saa tatu hadi saa sita. Leo Mwalimu Carlson ameniandikia ujumbe huu: I have described the day to many of our faculty.... That was one of the best classroom sessions I have ever been a part of...the kids were buzzing for the rest of the day. Thank you so much . Nitafsiri kwa ki-Swahili: Nimewaeleza walimu wetu wengi shughuli za leo.... Ni kati ya madarasa bora kabisa ambayo nimewahi kushiriki....vijana wamesisimka wakiongelea siku nzima. Asante sana . Nahitimisha kwa kusema kuwa nilishagundua tangu zamani kuwa kuwaneemesha wengine kwa kuwafundisha ninayoyafahamu ni kitu kinachonipa raha mimi mwenyewe. Nafurahi kuwatajirisha vijana kitaaluma na kimtazamo. Mara kwa mara nafanya shughuli hizi kwa kujitolea, lakini sipungukiwi. Ninaamini ule usemi kuwa kadiri unavyotoa ndivyo unavyopewa.

Eti Tuupigie Mlima Kilimanjaro Kura, Kwa Lipi?

Image
(Makala hii imechapishwa katika blogu ya kamalaluta ) eti tuupigie mlima kilimanjaro kura, kwa lipi? sikuupigia kura mlima kilimanjaro na wala sikuwa na mpango wa kuupigia kura na nisingeweza kuupigia kura. ni kweli ungekuwa maajabu ya dunia tungepata pesa nyingi. lakini kwa nini kushiriki kuupigia kura mlima kilimanjaro?? Tanzania hupata pesa nyingi kutokana na utalii, ufadhili na vyanzo vingine.lakini pesa hizo huishia wapi?? tunazidi kukamuliwa kodi na kumasikinishwa. wakulima kama mimi tumekosa mitaji, huku rais wetu akionekana kila siku anawakaribisa matajiri kutoka nje ili wajekuchukua vijishamba vyetu kuwekeza eti. mapato yoote hayo pamoja na utalii huishia wapi? hamna huduma za msingi za jamii, shule alizozijenga nyerere ndo bado zipo zinakaribia kuwaangukia wanafunzi. pesa za kufisidi huwa hazikosi na mafisadi wako huru kuiba watakacho, anasa za watawala nazo hazikosagi pesa. wananunua magariya kitajiri, pinda eti anakataa gari la kitajiri kwa kuwa anaendesha gari la kita

Mhadhara Katika Chuo cha Mazingira, Minnesota

Image
Leo nilikwenda Apple Valley, kuongea na wanafunzi wa Chuo cha Msomo ya Mazingira . Nilialikwa na mwalimu Todd Carlson, na wanafunzi wake hao wamekuwa wakishughulika na mada ya falsafa za jadi. Kwa miaka mingi, mwalimu Carlson amekuwa akinialika kuongea na wanafunzi hao. Katika kuwaandaa, Mwalimu Carlson anawapa sehemu kadhaa za kitabu cha Matengo Folktales wasome. Kutokana na maandalizi hayo, wanafunzi hao wanakuwa na duku duku na masuali mengi ya kuniuliza. Ni wanafunzi makini sana. Wanaulizia kuhusu utafiti wa fasihi simulizi na changamoto za uandishi masimulizi hayo, tafsiri, maana, falsafa na kadhalika, wakizingatia yale niliyoandika katika Matengo Folktales . Kila ninapotembelea Chuo hiki , nawasimulia hadithi angalau moja kutoka katika Matengo Folktale s . Leo niliwasimulia hadithi ya "Jitu Katika Shamba la Mpunga," ambayo ni chemsha bongo ya aina yake, tukatumia muda kuiongelea.

Vitabu Nilivyonunua Leo Apple Valley

Image
Jioni ya leo nilipita kwenye duka la Half Price Books, mjini Apple Valley. Nilikuwa natoka Minneapolis. Nilipoingia ndani, niliwakuta watu wengi humo, wanazunguka huko na huko wakiangalia vitabu. Kwenye sehemu ya kulipia, kulikuwa na foleni. Hii ni jioni ya Jumamosi, wikiendi, na wa-Marekani wamejazana katika duka la vitabu. Je, jambo hili linawezekana nchini mwetu? Baada ya kuangalia vitabu vingi, nilichagua viwili. Kimoja ni The Hottentot Venu s kilichotungwa na Rachel Holmes, na kingine ni The Time and the Place and Other Stories kilichotungwa na Naguib Mahfouz. Hottentot Venus, ni habari ambayo nimeifahamu kwa miaka mingi. Ni jina alilopewa Saartje Baartman , mama mw-Afrika kutoka Afrika Kusini ambaye alipelekwa Ulaya kama kivutio, hasa kwa vile alikuwa na makalio makubwa sana, kutokana na desturi za kwao za kukuza makalio. Huko Ulaya alinyanyasika sana, kwani walimweka kwenye uzio kama mnyama, akitembezwa kwenye miji mbali mbali kwa maonyesho, na kukutana na adha za kila aina

Mbeya Nchi, Raisi Sugu

Image
Kabla ya yote, sherti niseme kuwa nasikitishwa na mambo yaliyotokea Mbeya siku mbili tatu hizi zilizopita na kusababisha uvunjifu wa amani. Natoa pole kwa waathirika. Kwa kuangalia habari zilizopatikana, tatizo limesababishwa na ukosefu wa busara za kiuongozi. Kati ya taswira zilizotolewa kutokana na matukio haya ya Mbeya ni hili bango lisemalo Mbeya Nchi Raisi Sugu. Picha nimeipata kutoka blogu ya Francis Godwin . Bango hili naona lina ujumbe wa kufikirisha. Kwa upande mmoja, mtu anaweza kusema kuiita Mbeya nchi ni makosa na dharau kwa nchi ya Tanzania. Lakini kwa upande mwingine, inakuwa vigumu kuthibitisha kosa liko wapi. Neno nchi limekuwa likitumika kwa namna nyingi katika maisha yetu. Miaka ya zamani na hadi leo, tunaposema u-Gogoni, au u-Sukumani, tunamaanisha nchi ya wa-Gogo na nchi ya wa-Sukuma. Hakuna ubaya wowote hapa. Katika hali hii, inakuwa vigumu kuwakosoa wenye hili bango lisemalo Mbeya Nchi. Kuna wakati tulikuwa na nchi ya Tanganyika. Nchi hiyo ilipata Uhuru mwaka 1

Nitakutana na Mteja Maarufu

Mara kwa mara napata fursa ya kukutana na wateja . Hao ni watu waliosoma vitabu vyangu au wanapangia kufanya hivyo au wamehudhuria mihadhara yangu. Wengine, ambao hatupati fursa ya kukutana uso kwa uso, wanawasiliana nami kwa barua pepe. Kwangu ni jambo la kushukuru, kwamba Mungu kanijalia uwezo na fursa hizo. Siku chache zilizopita, nilipata ujumbe kutoka kwa mama mmoja akisema kuwa alipata taarifa zangu kutoka kwa mama mwingine wa Shepherd of the Valley Lutheran Church . Nilivyoangalia mtandaoni, nimegundua kuwa huyu aliyeniandikia ni mtu maarufu . Wakati anaulizia kama tungeweza kukutana, alisema kuwa amenunua kitabu changu cha Africans and Americans na atakisoma hima. Anapangia kuandika kitabu kingine, na anapenda kusikia mawaidha yangu kuhusu masuala ya utamaduni katika malezi ya watoto. Huyu namhesabu kama mteja maarufu, kwa vile anafahamika sana kutokana na shughuli zake za kuandika na kuelimisha umma. Nangojea siku tuliyopanga kukutana, wiki ijayo, nikizingatia kuwa mteja

Maktaba Kuu ya Taifa, Dar es Salaam

Image
Sijui ni wangapi kati ya mamilioni ya watu wanaoishi Dar es Salaam ambao wameingia katika Maktaba Kuu ya Taifa, au wana mazoea ya kuingia humo. Hapa siongelei wanafunzi, kwani hao wanaingia humo. Naongelea watu wasio wanafunzi. Yawezekana wako ambao wana vijiwe vyao hapa nje ya maktaba, ambavyo wanahudhuria kila siku au kila wiki, lakini hawajawahi kukanyaga ndani ya maktaba hii. Lakini, Mwalimu Nyerere alipofungua maktaba hii, tarehe 9 Desemba, 1967, alitoa ushauri wa maana, na baadhi ya maneno yake ni haya: I am also forced to say that we shall probably not be able to go ahead as quickly as we would like, because even when a library service is run with the utmost economy, it still costs quite a lot of money. For a public library should not just be a place where books can be borrowed. It must also be a center for much wider adult education work of all kinds – ranging from the promotion of the desire for literacy by story telling and discussion, to the erudite lectures of visiting

Hotuba ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Novemba 9

Image
Leo asubuhi, katika kufuatilia habari za mambo yanayotokea Arusha wiki hii, nimesoma kwamba wakati polisi wamewakamata CHADEMA eti kwa kufanya mkutano bila kibali, polisi hao hao hawajawakamata CCM ambao walifanya mkutano bila kibali cha polisi. Mimi kama raia ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa nimeona kwa miaka na miaka jinsi vyombo vya dola Tanzania vinavyofanya umachinga kwa CCM, chama ambacho hatimaye, Mwalimu Nyerere alikiogopa, kama nilivyoelezea hapa .

Maktaba ya Mkoa, Tanga

Image
Maktaba ya mkoa, mjini Tanga, ilifunguliwa mwaka 1958. Wa-Ingereza, ambao walikuwa wanatawala Tanganyika, ndio waliojenga maktaba hii. Ni jengo zuri sana, kama inavyoonekana hapa kushoto. Nimetembelea maktaba hii mara kadhaa. Ni mazoea yangu kutembelea maktaba, kama nilivyoeleza hapa na hapa . Tangu nilipofika hapo maktaba ya Tanga mara ya kwanza, miaka kadhaa iliyopita, nilipata fursa ya kufahamiana na mkurugenzi, ambaye anaonekana nami katika picha hapa kushoto. Nimepata fursa ya kuingia ndani na kuangalia vitabu na machapisho mengine, nikachangia nakala za vitabu vyangu. Maktaba hii ilikuwa nzuri sana tangu ilipofunguliwa. Lakini leo, hali si nzuri, kama ilivyoelezwa hapa . Maktaba inahitaji ukarabati, vitabu vipya, majarida na kadhalika. Kwa nchi tajiri kama Tanzania, ambayo ina rasilimali kuliko nchi nyingi, haieleweki kwa nini isiwezekane kukarabati maktaba kama hii. Jawabu linaeleweka: ni ujinga, ufisadi na ukosefu wa uongozi kitaifa. Uongozi wa maktaba unajitah

Nakunywa Chai na Kahawa ya Tanzania

Image
Ujumbe wangu wa leo ni kuwa wa-Tanzania tunapaswa kutumia bidhaa zinazotengezwa nchini mwetu kila inapowezekana. Iwe tuko Tanzania au nje, tufanye hivyo, kwani manufaa yake ni makubwa. Nimepata wazo la kuandika ujumbe huu kutokana na ukweli kwamba hapa ughaibuni ninakunywa chai na kahawa ya Tanzania. Sibadili. Kila ninapokuwa Tanzania, wakati wa kuondoka nahakikisha kuwa nimenunua chai na kahawa ya kunitosha hadi nitakapokuja tena. Mwaka huu, kwa mfano, wakati naenda kupanda ndege uwanja wa Julius Nyerere Dar es Salaam, nilimwambia dreva wa teksi anipeleke kwanza sehemu wanapouza chai na kahawa ya Tanzania. Ndivyo alivyofanya Faida za kutumia bidhaa za nchini mwetu ni nyingi. Kwanza, tunachangia ajira katika nchi yetu. Kama wa-Tanzania wote, walioko nchini na nje, tungekuwa tunanunua vitu vinavyotengenezwa nchini, kama vile nguo, sabuni, sukari, soda, na viberiti, ajira zingeongezeka mara dufu. Waziri wa mambo ya nchi za nje hivi karibuni aliripotiwa akisema kuwa kuna waTanz

Mwanafunzi Albino Aacha Shule Akihofia Kuuawa

Image
Kila kukicha, zinajitokeza habari za kutia aibu, kusikitisha, na kutisha zinazothibitisha kuwa Tanzania ni kichwa cha mwendawazimu. Hapa ni habari mojawapo kutoka blogu ya Francis Godwin kuhusu mtoto albino. Taarifa hizi za uhayawani zinapojitokeza huwa najiuliza kama Tanzania ni nchi kweli, au imeshakuwa jehenam. &&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&& Mtoto Albino aliyeacha masomo akifanya mahojiano na waandishi wa habari MWANAFUNZI wa darasa la pili shule ya msingi Bulongwa wilaya ya makete mkoani Iringa Emeliana Chaula (9)mwenye ulemavu wa ngozi (albino) ambeye pia ni yatima anayelelewa katika kituo cha watoto yatima cha ELCT Bulonga Wilayani Makete ameacha masomo yake kwa kuogopa kuuwawa . Mwandishi wa mtandao

Wa-Islamu Vyuoni Marekani

Image
Leo tulikuwa na mjadala mjini Faribault, Minnesota, kuhusu wa-Islam vyuoni Marekani. Walioandaa mjadala ni Anna na Rachel, wanafunzi wa Chuo Cha Carleton. Walengwa walikuwa ni wazazi na vijana wa ki-Somali, ambao ndio jamii ya ki-Islam inayofahamika hapa Minnesota ya Kusini Mashariki. Hapa kushoto tunaonekana wanajopo tukiwa mzigoni. Rachel amejishughulisha na wa-Somali kwa kitambo. Aliwahi kufanya mahojiano nami miezi kadhaa iliyopita kuhusu changamoto zinazowakabili wa-Islam Marekani. Rachel na Anna waliniomba nikawe mwanajopo katika mjadala wa leo, kwa vile wanafahamu ninafahamika na kukubalika katika jamii ile. Mjadala ulilenga kuwapa fursa wazazi na vijana kufahamu hali halisi, faida na changamoto za vyuo kwa wa-Islam ambao pia ni wahamiaji kutoka Afrika. Wazazi na vijana walipata fursa sawa ya kuelezea mawazo yao, mitazamo, mategemeo, wasi wasi na mapendekezo. Zilijadiliwa changamoto wanazokabiliana nazo vijana wa kiIslam wanapowazia au kujiandaa kupeleka maombi ya kujiu