Friday, November 19, 2010

Wabunge wa CCM Wanakera

Wabunge wa CCM wanakera. Tukianzia na wabunge hao walioapishwa safari hii, sitasahau kuwa hao ndio waheshimiwa waliotoroka midahalo wakati wa kampeni. Wote walitoroka midahalo, kitendo ambacho kimenikera. Mimi kama mwalimu, ninayetambua umuhimu wa midahalo, ninawashutumu hao waheshimiwa. Soma hapa.

Kila nitakapokuwa naona sura za hao waheshimiwa wa CCM, nitakuwa nakumbuka kitendo chao hiki cha kutoroka midahalo. Nitakuwa naangalia kama watajirekebisha au kama kitendo kile ni ishara ya tabia na mwenendo watakaofuata kwa miaka mitano ijayo.

Tukirudi nyuma, kwenye awamu iliyopita, wabunge wa CCM walikera. Ni nani atakayesahau yaliyotokea wakati Dr. Slaa alipoanza kutamka kuwa kuna ufisadi katika nchi yetu? Wabunge wote wa CCM walimpinga vikali na kumtupia shutuma nzito kwamba alikuwa mzushi.

Dr. Slaa hakuyumba, bali aliendelea kutoa madai yake. Hatimaye, ilianza kuthibitika kuwa aliyokuwa anayasema ni kweli, kwamba tuna mafisadi. Baada ya wananchi kuanza kuona ukweli huo, ukawa haupingiki tena, tuliwaona baadhi ya wabunge wa CCM wakijitokeza na kuanza kujinadi kuwa nao ni wapiganaji dhidi ya ufisadi. Sijui kama walikuwa wanaongea kwa dhati au kwa lengo jingine.

Tukirudi nyuma zaidi, tunakumbuka suala la machafuko yaliyotokea Visiwani mwaka 2001. Machafuko yale, yaliyotokana na CCM, chama tawala, kushindwa kutumia haki na busara, yaliiletea Tanzania aibu kubwa duniani. Kwa uthibitisho, soma hapa.

Lakini, pamoja na maovu yote yaliyofanyika Visiwani, pamoja na fedheha yote iliyoiangukia Tanzania, wabunge wa CCM hawakukubali kuwa serikali ya CCM ilikuwa na makosa, wala hawakukubali kuwa Tanzania ilikuwa inafedheheka. Wao waliitetea serikali ya CCM. Maadam palikuwa na suala lililohusu chama cha upinzani, yaani CUF, wabunge wa CCM waliamua kuikingia kifua serikali ya CCM, badala ya kusimamia haki za binadamu na heshima ya Tanzania.

Je, kuna kero kubwa zaidi ya hii ya kutojali maslahi ya Taifa na badala yake kuangalia maslahi ya kikundi fulani?

2 comments:

Mzee wa Changamoto said...

Asante saana Mwalimu kwa maandiko haya. Mimi husikitika kuwaona wabunge wanaojiita wameshinda kwa kishindo ilhali WAKIENDESHWA NA MAHITAJI YA LUMUMBA (zilipo ofisi kuu za chama) NA SIO MAHITAJI YA WANANCHI WALIOWACHAGUA.
Hata watu kama Dr Faustine ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa matendo ya serikali na chama, alipoingia kwenye kinyang'anyiro cha Ubunge akaamua kuifunga blogu ambayo aliitumia kuanika uozo wa "WENZAKE WA SASA." (Jaribu www.drfaustine.blogspot.com) uone ilivyowekewa KUFULI. Na kisha yeye aliyekuwa akizungumzia mambo ya uwazi, ukweli na uwajibikaji akakacha mdahalo kwa AMRI YA WAKUBWA WAKE WASIOJUA LOLOTE KUHUSU KIGAMBONI.
Na ndio maana katika makala yangu kuhusu UCHAGUZI WA 2015 nikasema ajenda ya kwanza iwe ni UCHAGUZI 2010 (http://changamotoyetu.blogspot.com/search/label/Uchaguzi%202015)na nikasema "....baadhi ya ajenda za CHANGAMOTOYETU kuelekea uchaguzi 2015 ni.....
1: MIDAHALO KWA WAGOMBEA URAIS NI LAZIMA.
Mwaka huu nilishangazwa, kusikitishwa na kukereka na namna ambavyo chama tawala kilionesha dharau kwa kugoma kufanya mdahalo. Sababu niliyoisikia ikitajwa ni kuwa wagombea watawafuata wananchi huko waliko. Huu ni upungufu wa elimu ya awali ya uraia.
Kuna haja kwa bunge kupitisha SHERIA ya midahalo (japo mitatu) kwa wagombea wote wa nafasi ya uraisi ili kuweza kuwapa uwanja wa kupambana. Mwaka huu tumeona walivyokuwa wakirushiana "ya nguoni" kwa kuwa tu hawakuweza kukabiliana ana kwa ana kupambanisha sera."
Lakini pia nimeeleza katika post yangu nyingine kuwa UJINGA MKUU NI KUWA MJINGA WA UJINGA WAKO (http://changamotoyetu.blogspot.com/2010/11/ujinga-mkuu-ni-kuwa-mjinga-wa-ujinga.html) na naamini ndicho kinachowakumba wanaCCM wengi na nilisema ama kuuliza ama kueleza kuwa "Hivi ni WABUNGE wangapi wanaojua kuwa WAAJIRI WAO NI WANANCHI NA SIO ILANI ZA VYAMA VYAO????
Ni wabunge wangapi wanaojua kuwa katika chaguzi za majimbo yao, wamependwa ama kuchaguliwa wao kwa kuwa ni SULUHISHO la matatizo ya wananchi wao na si kwa kuwa wananchi wengi wa hapo wanapenda chama lichogombea?
Ni wangapi ambao wanatambua kuwa wao ni SAUTI HALISI YA WANANCHI na sio "ujazo' wa kura za kupitisha, kupinga ama kuadhibu kile kionwacho ndivyo ama sivyo na wanachama wa chama awakilishacho?
Ni wangapi ambao wanaamini kuwa HAWALAZIMIKI KUUNGANA NA CHAMA CHAO katika maamuzi, kama maamuzi hayo yanawakandamiza ama kutowanufaisha wananchi wao?
Ni wangapi ambao wanajua kuwa hapo ni kama SHULE na wamalizapo muhula wanatakiwa kurejea NYUMBANI walikochaguliwa wakiwa na ripoti ya matokeo ya mtihani wao wa uwakilishi?"

NI WAJINGA WA UJINGA WAO NA NDIO MAANA NAWAONA NI WAJINGA WAKUU

Mbele said...

Shukrani sana kwa mchango wako. Ni jambo jema sana kwamba unatupeleka kwenye makala zilizotangulia, na hivi kutupa upeo mpana wa suala zima. Huku ndiko kuelimishana. Tuendelee namna hiyo hiyo.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...