Friday, November 12, 2010

Huduma ya Vitabu Gesti

Tarehe 29 Oktoba nilikuwa Chicago, kuhudhuria mkutano wa washauri wa programu ya masomo iitwayo ACM Botswana. Vyuo vingi hapa Marekani vinaendesha programu za kupeleka wanafunzi nchi mbali mbali, nami ni mshauri katika programu kadhaa.

Nilifikia katika hoteli ya Best Western River North. Nimeshalala hapo mara kadhaa, ninapohudhuria mikutano ya ACM Botswana na ACM Tanzania. Safari hii niliona hoteli hii imeanzisha huduma ya vitabu.



Nilivyoingia chumbani, niliona tangazo kwenye meza ndogo ya taa, pembeni mwa kitanda.









Nilipoliangalia karibu zaidi, niliona kuwa ni tangazo la huduma ya vitabu.


























Nilifuatilia. Nikateremka chini, kuelekea sehemu ya mapokezi. Wakati nashuka kwenye lifti, baada ya kufika chini kabisa, nikaona kuwa ukutani pana tangazo kuhusu huduma ya vyakula katika hoteli hii, na pia hii huduma ya vitabu, pamoja na uwepo wa hoteli hii katika mtandao wa Facebook, pia kuwa hoteli ina blogu yake. Hoteli imeanzisha huduma ya vitabu katika kuchangia maendeleo ya jamii.









Halafu karibu na sehemu ya mapokezi ndipo wameweka kabati la hivi vitabu. Nililisogelea nikaona kuna vitabu vya aina aina.








Na utaratibu ni kuwa mgeni anakaribishwa kuvisoma, na hata kuvichukua, na pia kuchangia vitabu.


Jambo hili lilinifurahisha. Nikaanza kuwazia gesti zetu za Tanzania. Kitu cha kwanza nilichokumbuka ni jinsi taa ndani ya gesti za Tanzania zilivyo. Mara nyingi taa katika chumba iko juu sana na mwanga wake ni hafifu. Huwezi kusomea. Mazingira ya kusoma, kwa ujumla hayako. Gesti nyingi ziko pamoja na baa, ambapo muziki na kelele ni mtindo mmoja, na varangati za hapa na pale.

Cha kushangaza pia ni kuwa katika gesti nyingi Tanzania, kuna nakala ya Biblia. Sijui utaratibu huu wa kuweka Biblia ulianzaje. Pia najiuliza kama kuna m-Tanzania yeyote anayesoma Biblia gesti. Sifa na heshima za gesti tunazijua. Hazifanani na sifa na heshima ya Biblia. Nashangaa kwa nini sisi wa-Kristu tunaruhusu kitabu cha dini yetu kuwekwa katika mazingira ya namna hii.

6 comments:

Simon Kitururu said...

Yani inafurahisha sana kuona kuna huduma kama hiyo!

Ila kuwepo kwa BIBLIA gesti pale BONGO mimi naona ni vyema tu kwa kuwa nafikiri BIBLIA ni vizuri iwepo mahali popote hata kule kuonekanapo kama kwa wenye dhambi kwa kuwa naamini hata Yesu mwenyewe alipenda kujichanganya na wenye dhambi na wala sio tu ambao wanamjua na kumfuata Mungu wake tu.
Ingesikitisha kama BIBLIA ingekuwa ni kitabu kitumiwacho MAKANISANI tu au kama zamani ambapo ilikuwa kama wewe sio Padre a, Askofu au mtu fulani KANISANI basi huruhusiwi kujisomea BIBLIA.

Mbele said...

Naafiki kauli yako kuwa Biblia yenyewe haifanyi ubaguzi. Yesu alikuwa anajichanganya na wadau wa aina zote. Alitoa ofa za ulabu pia :-)

Napenda tu kuongezea kuwa hiyo picha ya kitanda niliipiga asubuhi baada ya kuamka hapo. Ndio kusema nilijitahidi kukitandika kama kinavyoonekana :-)

Tukirudi kwenye gesti za Bongo, sijui itakuwaje kama mtu ataanzisha huduma ya vitabu. Mteja wa Bongo aulizwe pale mapokezi kama ana kitabu, au anahitaji kitabu, sijui atajibu vipi :-)

Subi Nukta said...

Nami naungana na Simon kuhusu uwepo wa kitabu cha Biblia kwenye nyumba za wageni.

Historia yake nadhani ilitokana na utaratibu walikuwa nao WaGideoni na Bible Society ambao walikuwa wakitoa matoleo ya chapisho la Biblia na Agano Jipya toleo la Kiswahili mashuleni, hotelini, nyumba za kufikia wageni, sokoni, katika mikutano na mikusanyiko mbalimbali ya watu n.k. kadiri ya vibali wavyopata. Hii ndiyo ikawa kama kanuni.

Zipo nyumba za kufikia wageni zilikuwa na vipeperushi pia mbali ya vya Injili, waliweka vinavyohusu njia za kupata virusi vya UKIMWI na namna ya kujiepusha.

Nadhani umefika wakati ambapo badala ya kuchana vitabu au kuvitumia kama nyenzo za kuhifadhia maandazi, visheti, karanga, mihogo, sembe nk, vingekuwa vinawekkwa katika maeneo hayo (ijapokuwa hata maktaba zetu zinasikitisha kwa kukosa vitabu au kuwa na vitabu vilivyopitwa na wakati mno na vingine kuwa na maelezo potofu kabisa).

Simon Kitururu said...

@Prof Mbele: Dokezeo la kitanda limenikumbusha stori za Mandela na jinsi isemekavyo apendavyo kutandika kitanda tabia iliyomkolea alivyokuwa Jela.:-)

Nahisi Bongo ukiulizia vitabu MAPOKEZI wanaweza kufikiri unahitaji Toilet Paper na labda wafanyakazi wa hapo watawauzia wauza vitumbua hivyo vitabu kama asemavyo NGULI SUBI ,....kwa ajili ya kufungia wateja Maandazi.:-(

@Subi:

Ni kweli vitabu vingi Maktaba za BONGO ni edition za zamani kweli kitu amacho unaweza kujikuta kuhusu maswala ya kileo bado ukitoacho kwenye vitabu hivyo ni kuwa DUNIA iko kama meza (kama elimu ya zamani ilivyodai)na sio almost DUARA (kama elimu ya kisasa idaivyo)

Mbele said...

Dada Subi, umenikumbusha mengi unapoongelea utamaduni wa kuchana vitabu ili kufungia chipsi mayai na mihogo. Ninapokuwa Tanzania, nakutana na watu ambao wakisikia nimeandika kitabu, wanaomba niwape cha bure.

Wakati mwingine watu hao wanasema hivi wakati mkiwa baa na wao wanaagiza kama tulivyo, kama vile bia ni za bure.

Huwa nashangaa kwa nini wanataka kitabu cha bure, wakati hawamwambii meneja wa kiwanda cha bia awape bia za bure. Yaani wanamaanisha kuwa ulabu una maana zaidi kuliko mawazo yaliyomo kitabu mwangu? Niliwahi kuhoji hivyo hapa.

Sasa, baada ya kusikia maelezo yako Dada Subi, nahisi hao jamaa wanataka kitabu cha bure ili wakachane karatasi za kufungia kitimoto na chipsi mayai :-)

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Kwa Bongo usitegemee kukuta huduma ya vitabu guest house zaidi ya salama kondomu na upuuzi mwingine. Otherwise vitabu vyenyewe viwe vya udaku kama yalivyo magazeti yake ya uchafu. Unashangaa kuombwa kitabu cha bure! Mie nshapigwa hata mzinga wa tiketi na mwaliko. Watu wetu kimsingi bado wako karne ya kwanza ambapo kila kitu ni bwerere. Huoni walivyokubaliana na uchakachuaji na ujambazi wa mchana tofauti na wenzetu wa Kenya? Wabongo wameamua kulaza bongo na kuabudia upuuzi badala ya ukombozi. Nakumbuka alipotangazwa mshindi Jakaya Kikwete badala ya kutoa pointi alitoa pumba kuwa tufanye haraka watu waende wakajimwage. Kama rais wao ni zoba hivi unategemea nini toka kwa kina Matonya

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...