Tuesday, November 30, 2010

Asante, Joseph Mbele

Jioni hii, katika kuzurura mtandaoni, mitaa ya Google, nimekumbana na makala kwenye blogu fulani, ambayo inanitaja. Soma hapa.

Sikuwa nimeiona makala hii ambayo inataja ziara niliyofanya College of St. Benedict/St. John's University mwaka jana. Nilialikwa kutoa mihadhara. Katika darasa la Profesa Lisa Ohm, niliongelea hadithi na utamaduni, kufuatia maelezo yaliyomo katika kitabu cha Matengo Folktales, ambacho walikuwa wanakitumia. Soma hapa.

Mhadhara wa pili niliutoa kwa wanafunzi na walimu waliokuwa wanajiandaa kwenda Tanzania na Afrika ya Kusini, lakini ulihudhuriwa na wengi wengine. Lengo lilikuwa kuwaarifu kuhusu tofauti za msingi baina ya tamaduni wa mw-Afrika na ule wa m-Marekani, kama nilivyoeleza katika kitabu cha Africans and Americans.

Nakumbuka jinsi ukumbi ulivyojaa watu kwenye mhadhara huu, na kwenye meza nyuma ya umati walikuwa wameweka nakala nyingi za vitabu hivi viwili, kama ilivyo desturi hapa Marekani, wanapowaita waandishi kuzungumzia vitabu na uandishi. Soma hapa.

Nimefurahi kuona kuwa mazungumzo yangu kwa hao wa-Marekani yameelezwa kama ilivyoelezwa na mwandishi huyu. Nimefurahi jinsi anavyokiri kuwa yale niliyowaambia ndiyo aliyoyakuta Afrika Kusini. Huwa nakutana na wa-Marekani wengi wanaosema hivyo hivyo, wanaporudi kutoka Afrika. Nami nafanya juhudi nijielimishe zaidi kuhusu tofauti za tamaduni hizi, ili niweze kuboresha mafunzo na mawaidha ninayotoa.

6 comments:

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Mwalimu, unagusa maisha ya watu wengi kichanya, si katika shughuli zako za kitaaluma tu bali katika mambo ya jumla katika maisha kama hili la utangamano wa kitamaduni.

Ijumaa hii katika mfululizo wa Fikra ya Ijumaa katika blogu yangu kuna makala mafupi yanayokuhusu. Makala haya yanaitwa "Kama Tungemsikiliza na Kumwelewa Profesa Mbele". Usiyakose!

Mbele said...

Mwalimu Matondo, shukrani kwa ujumbe. Niseme tu kifupi kuwa namshukuru Muumba kwa kunipa uwezo na fursa ya kufanya shughuli hizi. Natambua nina wajibu wa kufanya hayo yote kwa kadiri ya uwezo alionipa, bila kuzembea.

Napata furaha ya kweli ninapotambua kuwa nimefanikiwa kumwepushia binadamu matatizo ambayo yangempata katika kuishi katika utamaduni tofauti. Nafurahi ninapofanikiwa kumpa mawaidha ambayo ni nyenzo ya mafanikio kwake.

Matokeo ya msimamo wangu huu ni kuwa nazidi kupata baraka maishani na furaha moyoni. Ujumbe kama huu alioandika huyu jamaa ni kama ameniombea dua njema kwa Muumba, nami matokeo yake nayaona.

emuthree said...

Mimi niseme tu hongera sana, kwani wewe waonyesha kwa vitendo, na sio mchoyo kwa kile ukijuacho, na hii ni dalili ya watu wenye hekima

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Hongera mwalimu Mbele. Maana kwa mwandishi hakuna kitu cha maana kama kuona wengine wanavyoichukulia kazi yake. Inakuwa faraja zaidi unapogundua kuwa kumbe unaweza kubadili maisha ya wenzako jambo ambalo ni tunu kubwa tu kuliko hata hiyo pesa.Keep it up and indeed God will reward you abundantly.

Simon Kitururu said...

Na kuna la kujifunza kwa akumbukaye angalau KUSHUKURU!

@Mtakatifu NN Mhango:Sijasahau kuhusu ahadi ya CRITIQUE ya kile kitabu chako Nguli!Utastukia ni kwanini imechelewa kidogo ndude Mkuu nikiwakilisha ambapo niseme TUKIWAKILISHA maana watu kadhaa kazi yako imetudaka kiaina na kuna wasikitikao KITABU CHAKO kipya kinazinguliwa na wasiotaka usikike!:-(

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Mtkatifu Kiturur,
Sijakata tamaa kupata CRITIQUE yako. Kwani najua kusoma si mchezo. Ila nimefarijika kusikia kuwa kumbe na kazi yangu ni nguli! Hiki cha pili naamini kitatoka maana mafisadi si Mungu na Mungu si binadamu. Tuombeane dua tu.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...