Saturday, February 21, 2009

Nchi Zinazoendelea: Ni Zipi Hizo?

Dhana ya "nchi zinazoendelea" imejengeka vichwani mwa watu, tangu zamani. Pamoja na dhana hiyo, kuna pia dhana ya "nchi zilizoendelea." Je, dhana hizo zina mantiki yoyote?

Binafsi, ingawa zamani nilikuwa na mawazo kama wengine, kwamba kuna nchi zilizoendelea na zile zisizoendelea au zinazoendelea, miaka hii nimegundua kuwa dhana hizi hazina mantiki, na ni ushahidi wa kasumba vichwani mwa watu, au elimu duni.

Kwa mujibu wa dhana hizo, nchi kama Marekani, Uingereza, Sweden, Ujerumani, na Japani zinahesabiwa kuwa zimeendelea. Lakini nchi kama Tanzania, Kenya, na Uganda zinahesabiwa kuwa nchi zinazoendelea.

Kwa nini nasema dhana hizi ni duni? Kwanza, hakuna nchi duniani ambayo imesimama tu. Kila nchi iko katika mchakato na mabadiliko katika uchumi, siasa, utamaduni, na kadhalika. Marekani ya mwaka juzi ni tofauti na Marekani ya leo, na Marekani ya miaka mitano ijayo itakuwa tofauti na hii ya leo. Na ndivyo ilivyo kwa nchi zote. Kama ni tekinolojia, kwa mfano, tekinolojia inabadilika muda wote katika nchi kama Marekani. Kama ni utamaduni, ni hivyo hivyo. Na ndivyo ilivyo kwa nchi zote. Mabadiliko hayaishi, iwe ni katika Tanzania au Uingereza.

Kama huu mchakato na mabadiliko ndio maendeleo, basi kila nchi duniani ni nchi inayoendelea. Ni upuuzi kuziona baadhi ya nchi kama nchi zilizoendelea, wakati nazo ziko katika kubadilika muda wote.

Lakini, jambo la msingi zaidi ni dhana ya maendeleo. Maendeleo ni nini, na nani anayeweka vigezo vya kupima haya maendeleo? Hili ni suali la msingi.

Kwa ujumla, baadhi ya nchi, hasa zile ambazo zilikuwa zimetutawala wakati wa ukoloni, na zile zenye nguvu katika dunia ya leo, ndizo zinazoweka vigezo. Na wengi wamefundishwa kukubali hayo mawazo ya kikoloni na kikoloni mamboleo, bila kufikiri. Kwa vile Ulaya inajitapa kwamba imeendelea, Waafrika na wengine sehemu mbali mbali za dunia nao wanakubali hivyo na kuziona nchi zao kuwa ni nchi zinazoendelea au zisizoendelea. Hii ni kasumba.

Ingekuwa tunavyo vichwa timamu na tunavitumia ipasavyo, tungetafakari mambo sisi wenyewe, na tungetathmini dhana ya maendeleo. Tungejiuliza, maendeleo ni nini? Tungejiuliza iwapo dhana ya maendeleo ya watu wa Ulaya ni sherti tuipokee na kuikubali. Tungechukua jukumu na wajibu wa kujitungia vigezo vyetu na kuvitumia.

Kwa vile hatufanyi hivyo, tumebaki kuwa kasuku. Chochote kinachotoka Ulaya au Marekani tunakiona ni maendeleo. Papo hapo, watu wa Ulaya hawaoni chochote cha kwetu kuwa ni maendeleo. Ni pale tu tunapoiga mambo yao ndipo tunahesabiwa kuwa tunaendelea.

Hata kama jambo halina maana, maadam linatoka Ulaya au Marekani, watu katika nchi zetu wanaliona ni maendeleo. Hata kama ni mambo yasiyoendana na utu, maadam yametoka Ulaya, watu wetu wanayaona ni maendeleo. Kwa mfano, nchi zinazoitwa zimeendelea zimefanikiwa kuharibu mazingira kwa ujenzi wa viwanda na miundombinu mbali mbali, kiasi kwamba hewa katika nchi hizo sio safi, maji sio salama, mahusiano ya jamii ni ya wasi wasi.

Cha kushangaza ni kuwa watu wetu nao wanataka tufanye kama wanavyofanya Ulaya au Marekani, na miji yetu iwe kama ya huko Ulaya na Marekani, na viwanda na miundombino iwe kama ilivyo Ulaya na Marekani. Wanatamani nchi zetu ziwe na kila kitu ambacho kiko Ulaya na Marekani, ili tuonekane tumeendelea. Je, hayo ndio maendeleo?

Kwa hali ilivyo, hali ya nchi kadhaa kujiona kuwa zimeendelea, nchi zetu hazitafikia wakati wa kuwa sawa na hizo zingine. Mfumo huu uliopo hautaisha. Watu wa Ulaya na Marekani wataendelea kuyaona mabadiliko ya nchini kwao kuwa ndio maendeleo, na sisi tutakuwa daima watu wa kufuata hayo ya kwao. Kwa mtindo huu, hatutaweza kuwa mbele yao au sambamba nao.

Nchi zote ziko katika hali ya mabadiliko ya kila aina, katika nyanja mbali mbali. Hakuna nchi iliyomaliza mchakato huu na kuwa nchi ambayo imesimama na haibadiliki tena. Pasipo kuwa na vigezo vinavyozingatia haki ya kila watu duniani kuchangia katika kutunga tafsiri na viwango vya maendeleo, si sahihi kuendelea kutumia dhana ya nchi zilizoendelea na nchi zinazoendelea au zisizoendelea. Inatubidi tubadili fikra; tukatae huu mkondo uliopo sasa wa kuitwa au kujiita nchi zinazoendelea. Ni fikra tegemezi, za kikasuku, na kikoloni mamboleo, fikra zinazothibitisha kuwa tunahitaji elimu.

Wednesday, February 4, 2009

Kuwasomea Watoto Vitabu

Enzi za mababu na mabibi zetu, ilikuwa ni kawaida kwa wazee kukaa na watoto jioni na kuwasimulia hadithi. Utamaduni huu ulikuwa sehemu ya maisha. Ilikuwa ni sehemu ya elimu waliyopewa hao watoto. Hapakuwa na shule tulizo nazo leo, wala vitabu, lakini wazee walikuwa walimu bora, waliotumia mbinu mbali mbali, kama hizi hadithi, katika kuwaelimisha watoto.

Siku hizi, kutokana na kuwepo kwa vitabu, tunayo fursa ya kutumia vitabu kuendeleza elimu ya watoto. Kama hatuna uwezo wa kuwasimulia hadithi kwa mtindo wa mababu na mabibi zetu, tunayo fursa ya kuwasomea vitabu. Wenzetu katika nchi kama Marekani wanaendeleza utamaduni huu kwa kuwasomea watoto hadithi za vitabuni. Watoto wa kiMarekani wanategemea mzazi awasomee vitabu. Ni kawaida kwa mzazi kumsomea mtoto kitabu kabla hajalala.

Mashuleni na kwenye maktaba za Marekani, kuna utaratibu wa kuwa na vipindi vya kuwasomea watoto vitabu. Watu wanajitolea kwenda maktabani au mashuleni kufanya kazi hiyo, wawe ni wafanyakazi maofisini, madaktari, wanajeshi au polisi, wanasiasa au viongozi.

Kila mtu atakumbuka, kwa mfano, kwamba siku ile ya Septemba 11, 2001, ambapo mji wa New York ulishambuliwa na magaidi, Rais Bush alikuwa darasani akijumuika na watoto waliokuwa wakisoma. Rais mpya Obama, pamoja na shughuli zake nyingi, anafuata utamaduni huo, kama ilivyoandikwa hapa.

Kuwasomea watoto vitabu kunawajengea mazoea ya kusoma na kuwapanua mawazo. Ni fursa ya kujenga na kuimarisha uhusiano baina ya watoto na watu wazima. Wataalam wa elimu ya watoto wanasema kuwa kumsomea mtoto vitabu tangu anapokuwa mdogo ni njia moja ya kumjengea msingi wa mafanikio maishani.

Watanzania tuko wapi katika suala hili? Je, wazazi wanaendeleza utamaduni wa mababu na mabibi wa kuwasimulia watoto hadithi? Na kwa vile tuko katika utamaduni wa vitabu, tunavyo vitabu majumbani? Tunawasomea watoto wetu?

Watu wazima katika Tanzania wanatumia muda mwingi kwenye sehemu zinazoitwa vijiweni. Wangeweza kutumia muda huu kwenda shuleni kusaidiana na walimu kwa namna moja au nyingine, kama wanavyofanya Wamarekani, kwa kujitolea. Wakati walimu wanasahihisha daftari, kwa mfano, wazazi wangeweza kusimamia shughuli za nje ya darasa, kama vile usafi, kilimo, au ufugaji, au wangeweza kusaidia somo moja au jingine.

Kuna watu wazima wengi Tanzania ambao wamesoma vya kutosha, na wangeweza kutoa mchango mkubwa mashuleni, kwa msingi wa kujitolea. Kama wabunge, wafanyabiashara, viongozi wa mitaa, watafiti na wengine wangefanya hivyo, watoto wangefaidika, na Taifa lingepiga hatua nzuri.