Tuesday, November 30, 2010

Asante, Joseph Mbele

Jioni hii, katika kuzurura mtandaoni, mitaa ya Google, nimekumbana na makala kwenye blogu fulani, ambayo inanitaja. Soma hapa.

Sikuwa nimeiona makala hii ambayo inataja ziara niliyofanya College of St. Benedict/St. John's University mwaka jana. Nilialikwa kutoa mihadhara. Katika darasa la Profesa Lisa Ohm, niliongelea hadithi na utamaduni, kufuatia maelezo yaliyomo katika kitabu cha Matengo Folktales, ambacho walikuwa wanakitumia. Soma hapa.

Mhadhara wa pili niliutoa kwa wanafunzi na walimu waliokuwa wanajiandaa kwenda Tanzania na Afrika ya Kusini, lakini ulihudhuriwa na wengi wengine. Lengo lilikuwa kuwaarifu kuhusu tofauti za msingi baina ya tamaduni wa mw-Afrika na ule wa m-Marekani, kama nilivyoeleza katika kitabu cha Africans and Americans.

Nakumbuka jinsi ukumbi ulivyojaa watu kwenye mhadhara huu, na kwenye meza nyuma ya umati walikuwa wameweka nakala nyingi za vitabu hivi viwili, kama ilivyo desturi hapa Marekani, wanapowaita waandishi kuzungumzia vitabu na uandishi. Soma hapa.

Nimefurahi kuona kuwa mazungumzo yangu kwa hao wa-Marekani yameelezwa kama ilivyoelezwa na mwandishi huyu. Nimefurahi jinsi anavyokiri kuwa yale niliyowaambia ndiyo aliyoyakuta Afrika Kusini. Huwa nakutana na wa-Marekani wengi wanaosema hivyo hivyo, wanaporudi kutoka Afrika. Nami nafanya juhudi nijielimishe zaidi kuhusu tofauti za tamaduni hizi, ili niweze kuboresha mafunzo na mawaidha ninayotoa.

Thursday, November 25, 2010

Kuendesha Blogu Mbili

Nina blogu mbili: ya ki-Swahili na ya ki-Ingereza. Kuendesha blogu moja ni kazi, blogu mbili ni zaidi. Kwa nini naendesha blogu mbili?

Nimewahi kuelezea kwa nini ninablogu. Labda nisisitize tu kuwa blogu yangu ya ki-Swahili inanipa fursa ya kujiongezea uzoefu wa kuandika kwa ki-Swahili, na pia kuwasiliana na wa-Tanzania wengi, wakiwemo wale wasiojua ki-Ingereza. Ninafahamu pia kuwa wako wasomaji wa blogu hii ambao si wa-Tanzania. Kuna hata wa-Marekani ambao wameniambia kuwa wanaisoma. Wanajikumbusha mambo ya Tanzania na pia lugha ya ki-Swahili.

Katika blogu yangu ya ki-Ingereza siandiki sana masuala ya Tanzania. Kadiri siku zinavyozidi kwenda, napata hisia kuwa ninaandika kwa ajili ya walimwengu kwa ujumla. Naona jinsi ninavyozingatia masuala ya taaluma, hasa fasihi. Naamini natoa mchango kwa wale wapendao fasihi au wenye duku duku ya kuifahamu. Hapo nawafikiria sana wa-Tanzania.

Katika kuongelea kazi za fasihi, siandiki makala ndefu, bali nagusia vipengele muhimu, na pia natoa dokezo ambazo ni changamoto kwa yeyote, aweze kuzifanyia utafiti na tafakari. Naamini kuwa kwa namna hii, yeyote atajiongezea ufahamu wa fasihi.

Labda nijieleze zaidi kwa wa-Tanzania wenzangu: siandiki kwa ajili ya wale ambao lengo lao kuu ni kupasi mtihani. Naandika kwa ajili ya wale wenye kupenda fasihi au wenye duku duku ya kujifunza fasihi. Pia kama nilivyosema kabla, naandika kwa ki-Ingereza ili kutoa mfano wa uandishi bora wa ki-Ingereza, jambo ambalo linahitajika katika jamii yangu ya wa-Tanzania.

Ingawa kuendesha hizi blogu mbili si kazi rahisi, nitajitahidi kuzimudu kwa kadiri ya uwezo wangu. Kazi ya kuendesha blogu hizi inaniwekea aina ya nidhamu katika maisha yangu. Kuandika katika blogu hizi mara kwa mara imeshakuwa kama deni na wajibu, lakini naona manufaa yake kwangu, kwa jinsi ninavyotumia muda wangu na akili yangu kwenye shughuli ya maana.

Wednesday, November 24, 2010

Kitendo cha CHADEMA Kususia Hotuba ya JK

Kitendo cha wabunge wa CHADEMA kususia hotuba ya JK Bungeni kimeibua mjadala mkubwa miongoni mwa wa-Tanzania. Wakati mjadala huu ukiendelea, nami nina la kusema.

CHADEMA imesema kuwa, mapema kabisa, ilipeleka malalamiko kwenye tume ya uchaguzi (NEC) kuhusu mchakato wa utangazaji wa matokeo ya urais, na kuomba utangazaji ule usimamishwe ili kuchunguza dosari ambazo CHADEMA ilikuwa na taarifa nazo.

Kwa msingi huu, ningependa kusikia taarifa ya NEC, niweze kufahamu kama kweli ililetewa malalamiko hayo. Kama iliyapata, napenda kujua iliyashughulikia vipi. CHADEMA inasema kuwa NEC haikuyajibu wala kuyashughulikia malalamiko yale.

Kama hii ni kweli, basi naitupia NEC lawama nzito. CHADEMA imesema kwamba kutokana na kuupuziwa malalamiko yao na NEC, na kutokana na kwamba sheria inasema kuwa tangazo la NEC la mshindi wa urais haliwezi kupingwa mahakamani au penginepo, walilazimika kutafuta hatua zingine za kuelezea malalamiko yao. CHADEMA wanasema kuwa kususia hotuba ya JK ni njia waliyoamua kuchukua kwa msingi huo.

Kama hali ndio hiyo inayoelezwa na CHADEMA, na kama NEC haitatoa maelezo ya kuthibitisha vingine, msimamo wangu ni kuwa CHADEMA walikuwa na haki ya kususia hotuba ya JK kama walivyofanya. Kama raia ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa, bali ni mpenda haki, uwazi, na ukweli, nawaunga mkono CHADEMA kwa suala hilo.

Nchi lazima iwe na kiongozi muda wote. Kwa msingi huu, JK ni rais, na CHADEMA hawajakataa hilo, ingawa kuna watu ambao, kwa sababu wanazozijua wao, wanaizushia CHADEMA uwongo kuwa haimtambui rais na serikali yake. Najiuliza kama watu hao wana akili timamu au kama wanaitakia mema nchi yetu.

Monday, November 22, 2010

Kitabu Kilivyopokelewa Ubalozi wa Kenya

Mwaka 2007 mwanzoni, jumuia ya wa-Kenya wanaoishi Minnesota waliandaa mkutano kuhusu uwekezaji nchini kwao. Walihudhuria wa-Kenya wengi sana, wakiwemo maofisa wa serikali na taasisi mbali mbali waliofika kutoka Nairobi. Nilishiriki, nikiwa na meza ambapo niliweka vitabu vyangu na machapisho mengine.

Nilikutana na wa-Kenya wengi, baadhi ambao tulifahamiana kabla na wengine kwa mara ya kwanza. Mmoja wa hao tuliofahamiana kabla alikuwa Julia Opoti, ambaye ni mwanahabari anayeendelea kujipatia umaarufu, na ni shabiki wa siku nyingi wa maandishi yangu. Alikuja kwenye meza yangu akiwa na bwana mmoja, akatutambulisha.

Yule bwana alikuwa afisa katika ubalozi wa Kenya, Washington DC. Julia alikuwa amemwambia kuhusu kitabu cha Africans and Americans naye akakinunua. Tarehe 17 Aprili, yule afisa aliniandikia ujumbe huu:

Kuhusu kitabu chako, hivi sasa nafikiri kimesomwa na watu kadri ya watano hapa ubalozi wetu na kimependwa sana. Ni matumaini yangu kuwa ukipata wasaa mzuri utaandika vitabu zaidi katika fani hii ili upate kunufaisha watu juu ya swali hili muhimu la tafauti ya mila na utamaduni.


Ujumbe huu, ingawa ulinifurahisha, haukunishangaza, kwa sababu ninafahamu jinsi wa-Kenya wanavyothamini vitabu na elimu kwa ujumla. Nimefahamu jambo hilo tangu nilipoanza kutembelea Kenya, mwaka 1989, na katika kuwaona huku ughaibuni. Nimeshasema hivyo hata katika kitabu changu cha CHANGAMOTO. Jambo la pili ni kuwa nilivutiwa na wito kuwa niendelee kuandika, wito ambao nimeupata kutoka kwa wasomaji wengine pia. Naendelea kuandika.

Friday, November 19, 2010

Wabunge wa CCM Wanakera

Wabunge wa CCM wanakera. Tukianzia na wabunge hao walioapishwa safari hii, sitasahau kuwa hao ndio waheshimiwa waliotoroka midahalo wakati wa kampeni. Wote walitoroka midahalo, kitendo ambacho kimenikera. Mimi kama mwalimu, ninayetambua umuhimu wa midahalo, ninawashutumu hao waheshimiwa. Soma hapa.

Kila nitakapokuwa naona sura za hao waheshimiwa wa CCM, nitakuwa nakumbuka kitendo chao hiki cha kutoroka midahalo. Nitakuwa naangalia kama watajirekebisha au kama kitendo kile ni ishara ya tabia na mwenendo watakaofuata kwa miaka mitano ijayo.

Tukirudi nyuma, kwenye awamu iliyopita, wabunge wa CCM walikera. Ni nani atakayesahau yaliyotokea wakati Dr. Slaa alipoanza kutamka kuwa kuna ufisadi katika nchi yetu? Wabunge wote wa CCM walimpinga vikali na kumtupia shutuma nzito kwamba alikuwa mzushi.

Dr. Slaa hakuyumba, bali aliendelea kutoa madai yake. Hatimaye, ilianza kuthibitika kuwa aliyokuwa anayasema ni kweli, kwamba tuna mafisadi. Baada ya wananchi kuanza kuona ukweli huo, ukawa haupingiki tena, tuliwaona baadhi ya wabunge wa CCM wakijitokeza na kuanza kujinadi kuwa nao ni wapiganaji dhidi ya ufisadi. Sijui kama walikuwa wanaongea kwa dhati au kwa lengo jingine.

Tukirudi nyuma zaidi, tunakumbuka suala la machafuko yaliyotokea Visiwani mwaka 2001. Machafuko yale, yaliyotokana na CCM, chama tawala, kushindwa kutumia haki na busara, yaliiletea Tanzania aibu kubwa duniani. Kwa uthibitisho, soma hapa.

Lakini, pamoja na maovu yote yaliyofanyika Visiwani, pamoja na fedheha yote iliyoiangukia Tanzania, wabunge wa CCM hawakukubali kuwa serikali ya CCM ilikuwa na makosa, wala hawakukubali kuwa Tanzania ilikuwa inafedheheka. Wao waliitetea serikali ya CCM. Maadam palikuwa na suala lililohusu chama cha upinzani, yaani CUF, wabunge wa CCM waliamua kuikingia kifua serikali ya CCM, badala ya kusimamia haki za binadamu na heshima ya Tanzania.

Je, kuna kero kubwa zaidi ya hii ya kutojali maslahi ya Taifa na badala yake kuangalia maslahi ya kikundi fulani?

Thursday, November 18, 2010

Kwa Nini Wabunge wa CHADEMA Wamesusia Hotuba ya JK

Leo, Novemba 18, katika ukurasa wake katika mtandao wa Facebook, Dr. Slaa ameelezea kwa nini wabunge wa CHADEMA wamesusia hotuba ya JK Bungeni. Mimi ni raia ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa. Nina ugomvi wangu na CCM, kama ninavyoeleza mara kwa mara katika blogu hii na blogu zingine, katika makala mbali mbali, na hata katika kitabu cha CHANGAMOTO. Papo hapo, ninaheshimu midahalo, na nimeshaishutumu CCM kwa kukimbia midahalo wakati wa kampeni zilizopita. Naweka hapa kauli hii ya Dr. Slaa kwa vile ninawaheshimu watu wanaojitokeza na kujieleza kwa hoja:
------------------------------------------------------------------------

Wabunge wetu wamechukua uamuzi mgumu sana, uamuzi ambao unataka ujasiri na uthubutu wa vitendo. Ni lazima tuelewe kuwa mgogoro uliopo siyo na Kikwete kama Kikwete, la hasha bali na mfumo uliomuingiza madarakani safari hii, mfumo ambao tunautuhumu kuwa haukuwa huru na wa haki. Uamuzi huu haukuwa wa chuki binafsi au kisirani dhidi ya Kikwete kama Kikwete, bali dhidi ya mfumo ulioundwa na kulelewa na CCM na ambao umetuonesha kuwa hauwezi na haupaswi kulelewa kwa muda mwingine wowote ujao.


Kuanzia wakati wa kutangaza matokeo tulitoa malalamiko yetu kwa Tume ya Uchaguzi ili waweze kuyafanyia kazi ili mshindi apatikane katika mazingira ya haki na uwazi. Tume haikusikiliza na ikaendelea na mfumo wake mbovu wa kutangaza matokeo bila kujali malalamiko yetu. Tukazungumza hadharani juu ya kutopatana kwa matokeo ya uchaguzi yanayotangazwa na tume na yale yaliyoko majimboni na kuomba tume wasitishe ili waangalie ushahidi tulio nao, tume haikusikiliza na matokeo yake wakamtangaza Kikwete kuwa Rais licha ya kwamba matokeo majimboni yalikuwa yanaashiria vinginevyo.


Ni muhimu kutambua kuwa ni rahisi kukubali matokeo ya Ubunge kwa sababu yanarasimishwa majimboni na yanaweza kupingwa mahakamani. Katika urais kimsingi ukiangalia Katiba utaona kuwa haijalishi nani kashinda kwenye kura, bali nani katangazwa mshindi. Tunachotuhumu sisi ni kuwa matokeo ya Uchaguzi yangetangazwa kama ilivyoahidiwa na Tume mwezi Machi yangeonesha wazi mshindi ni tofauti na yule aliyetangazwa. Lakini wao tume wakijua kuwa mara wakishatangaza hakuna mahakama inayoweza kuhoji wakafanya hila na haraka ya kutangaza matokeo ya Urais kwa kumtangaza Kikwete kuwa ni Rais.


Kama toka siku ya kwanza tulitoa malalamiko na zikapita siku tano bila kujibiwa wala kusikilizwa na baadaye tunatakiwa tukubali tu kwa vile "keshatangazwa" katika dhamira safi tunaweza vipi kufanya hivyo? Ugomvi wetu wa kisiasa (na siyo chuki wala uhasama binafsi) hauko zaidi na Kikwete bali natume iliyomtangaza. Na kwa vile yeye mwenyewe haoni matatizo katika tume au mfumo wetu wa uchaguzi tunaona kuwa aidha alitoa baraka zake au alikubali kunufaishwa na mfumo huo mbovu.


Hivyo, wabunge wetu kutoka nje ni kutuma ishara mbili: Kwanza, tunapinga mfumo wa kichakachuaji wa tume ya Uchaguzi uliomtangaza Kikwete kuwa Rais, na pili kwa vile Tume imeshindwa kutuonesha uwazi wa ushindi wa Kikwete tunashindwa kukubali kama ni mshindi halali. Ni mpaka pale uchunguzi huru wa kura utakapoonesha kuwa Kikwete kashinda kihalali ndipo tutakuwa tayari kumtambua ukiondoa uwezekano mwingine wa kuelewana.


Tukumbuke kuwa, kama uchaguzi huu ungeendeshwa katika hali ya uwazi, haki na ufanisi tusingefika hapa. CHADEMA siyo wa kulaumiwa katika hili wala wabunge wetu wasibebeshwe mzigo kwa hili; watu waliotufikisha hapa ni Serikali ya CCM na vyombo vyake ikiwemo Tume ya Uchaguzi. Wangeonesha weledi na kutokupendelea kwa wazi tusingefikia mahali pa kutulazimisha kuchukua hatua hizi ambazo kwa kila kipimo ni za wastani sana ukilinganisha na hatua ambazo tungeweza kuzichukua.


Nawasihi tuwaunge mkono wabunge wetu na uongozi wetu kwa kuwatia moyo kwani uamuzi waliouchukua ni uamuzi wa kijasiri lakini ulioweka historia katika Tanzania kuwa hatuwezi tena kusukumwa na kuburuzwa kwa kutumia nguvu ya taasisi au cheo cha mtu. Tuwatie shime na tusimame nao katika wakati huu wa kihistoria.


Pamoja tunaweza, mpaka kieleweke!

Tuesday, November 16, 2010

Mzee Kataraia Amekipenda Kitabu Hiki

Blogu yangu hii ni kama kisebule changu binafsi. Naamua nini cha kukiweka hapa, na sidhani kama ninasukumwa na ukweli kwamba watu wanasoma ninayoandika. Yeyote anayepita hapa na kuchungulia, ni hiari yake. Niliwahi kujieleza hivyo katika makala hii hapa.

Basi, leo napenda kuelezea nilivyokutana na Mzee Kataraia juzi, tarehe 14, mjini Minneapolis. Hatukuwa tumefahamiana. Lakini mara tulipotambulishwa, alianza kunielezea jinsi alivyokipenda kitabu changu cha Africans and Americans.

Niliguswa, nikamsikiliza kwa unyenyekevu. Ingawa napenda kuandika makala na vitabu, na watu wengi wananielezea wanavyopendezwa na kufaidika na maandishi yangu, napata taabu kustahimili sifa. Ila huwa namshukuru Mungu kwa kunipa vipaji, niendelee kutekeleza wajibu wa kuwanufaisha viumbe wake. Hii ndio tafsiri yangu. Sifa zote na shukrani namrudishia Muumba.

Nikiwa namsikiliza, Mzee Kataraia aliendelea kunieleza jinsi alivyosafiri sehemu zingine hapa Marekani, akawaonyesha wa-Tanzania kadhaa kitabu hiki, nao wakakisoma. Aliniambia kuwa wiki hizi alizokuwa hapa Marekani, ameshafanya safari kadhaa kwa ndege. Wakati wa kungojea ndege, ameona watu wakisoma kwenye kompyuta zao, na ndege ikiwa hewani amewaona watu wakisoma vitabu. Hapo nami nikamwunga mkono, kuwa nami nimeona sana tabia hizo hapa Marekani.

Maongezi yetu yalikuwa mafupi sana, labda dakika tano tu, kwa sababu tulikuwa katika shughuli nyingine za kusalimiana na kuongea na watu. Lakini kwa dakika zile chache nilipata picha kuwa Mzee Kataraia ni m-Tanzania wa pekee.

Kwanza, kama ninavyoandika katika blogu hii mara kwa mara, si rahisi kumkuta m-Tanzania anayevutiwa na vitabu, labda vitabu vya udaku. Halafu niliguswa na moyo wa Mzee Kataraia wa kuwakumbuka wengine. Alivyoona amekuta kitu cha manufaa, ameenda kuwaonyesha wengine, wanufaike. Nimeguswa.

Sitamsahau Mzee huyu. Nitajiona nina bahati iwapo nitakutana naye tena. Nimegundua huyu ni Mzee aliyeelimika. Kwa mtazamo wangu, kama nilivyosema katika mahojiano Radio Mbao, ishara muhimu ya kuelimika ni kuwa daima na kiu ya kutafuta elimu.

Monday, November 15, 2010

Tumesoma Masimulizi ya "Popol Vuh"

Leo katika darasa langu mojawapo tumemaliza kuongelea masimulizi ya kale ya Popol Vuh. Ni masimulizi ya zamani sana ya taifa la wa-Maya wa Amerika ya Kati. Wa-Maya wa zamani waliishi maeneo ambayo leo yanahusisha nchi za Mexico, Guatemala, Belize na Honduras. Walikuwa maarufu kwa mafanikio waliyofikia katika nyanja mbali mbali, kama vile ujenzi wa miji, ugunduzi wa hati ya kuandikia lugha yao, utafiti wa sayari, na utengenezaji wa kalenda.

Nilisikia juu ya Popol Vuh kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 1982 kutoka kwa Profesa Harold Scheub, nilipokuwa nasomea shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu Cha Wisconsin-Madison. Hata hivi hatukusoma kitabu hiki. Sasa nimefurahi kuwa katika darasa langu tumefanikiwa kukisoma na kukijadili, ingawa mambo yake mengi si rahisi kueleweka kwetu watu wa leo, wa tamaduni tofauti kabisa na ule utamaduni wa wa-Maya wa zamani.

Popol Vuh ni masimulizi kuhusu mambo mengi yahusuyo jinsi dunia ilivyoumbwa, na matukio mbali mbali yaliyofuatia, yakiwahusisha miungu na mashujaa wa aina aina. Ni masimulizi yenye uzito, kwani yanabeba mambo ya imani, maadili, utabiri na falsafa. Baadhi ya masimulizi ya Popol Vuh yanatukumbusha masimulizi ya vitabu vya dini kama Biblia au Quran, na pia masimulizi mengine kama Gilgamesh, au hata masimulizi maarufu ya wa-Kerewe, alivyoyaandika Mzee Kitereza katika kitabu chake cha Bwana Myombekere na Bibi Bugonoka na Ntulanalwo na Buliwhali.

Kusoma vitabu vya aina hii ni jambo jema sana, kwani linatupa mwanga kuhusu hali halisi ya yale waliyopitia na kuwazia wanadamu sehemu mbali mbali za dunia.

Friday, November 12, 2010

Huduma ya Vitabu Gesti

Tarehe 29 Oktoba nilikuwa Chicago, kuhudhuria mkutano wa washauri wa programu ya masomo iitwayo ACM Botswana. Vyuo vingi hapa Marekani vinaendesha programu za kupeleka wanafunzi nchi mbali mbali, nami ni mshauri katika programu kadhaa.

Nilifikia katika hoteli ya Best Western River North. Nimeshalala hapo mara kadhaa, ninapohudhuria mikutano ya ACM Botswana na ACM Tanzania. Safari hii niliona hoteli hii imeanzisha huduma ya vitabu.Nilivyoingia chumbani, niliona tangazo kwenye meza ndogo ya taa, pembeni mwa kitanda.

Nilipoliangalia karibu zaidi, niliona kuwa ni tangazo la huduma ya vitabu.


Nilifuatilia. Nikateremka chini, kuelekea sehemu ya mapokezi. Wakati nashuka kwenye lifti, baada ya kufika chini kabisa, nikaona kuwa ukutani pana tangazo kuhusu huduma ya vyakula katika hoteli hii, na pia hii huduma ya vitabu, pamoja na uwepo wa hoteli hii katika mtandao wa Facebook, pia kuwa hoteli ina blogu yake. Hoteli imeanzisha huduma ya vitabu katika kuchangia maendeleo ya jamii.

Halafu karibu na sehemu ya mapokezi ndipo wameweka kabati la hivi vitabu. Nililisogelea nikaona kuna vitabu vya aina aina.
Na utaratibu ni kuwa mgeni anakaribishwa kuvisoma, na hata kuvichukua, na pia kuchangia vitabu.


Jambo hili lilinifurahisha. Nikaanza kuwazia gesti zetu za Tanzania. Kitu cha kwanza nilichokumbuka ni jinsi taa ndani ya gesti za Tanzania zilivyo. Mara nyingi taa katika chumba iko juu sana na mwanga wake ni hafifu. Huwezi kusomea. Mazingira ya kusoma, kwa ujumla hayako. Gesti nyingi ziko pamoja na baa, ambapo muziki na kelele ni mtindo mmoja, na varangati za hapa na pale.

Cha kushangaza pia ni kuwa katika gesti nyingi Tanzania, kuna nakala ya Biblia. Sijui utaratibu huu wa kuweka Biblia ulianzaje. Pia najiuliza kama kuna m-Tanzania yeyote anayesoma Biblia gesti. Sifa na heshima za gesti tunazijua. Hazifanani na sifa na heshima ya Biblia. Nashangaa kwa nini sisi wa-Kristu tunaruhusu kitabu cha dini yetu kuwekwa katika mazingira ya namna hii.

Tuesday, November 9, 2010

Mdahalo wa Dr. Slaa, ITV, Utumike Mashuleni

Mimi ni mwalimu, mwenye uzoefu wa kufundisha tangu mwaka 1976, nilipoanza kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na hatimaye kutoa mihadhara katika vyuo vikuu sehemu mbali mbali duniani.

Kutokana na wadhifa wangu, napenda kusema kuwa ingekuwa bora iwapo mdahalo wa Dr. Slaa ITV ungesambazwa mashuleni, kwani una mambo muhimu ya kuwafundisha vijana wetu. Jambo la kwanza ni kuwa mdahalo ule unatoa changamoto kuhusu masuala ya nchi yetu, ni kichocheo cha fikra.

Jambo la pili ni kuwa vijana wetu wakiona jinsi Dr. Slaa anavyoyakabili masuali, kwa ufasaha, ufahamu, na kujiamini, wataona mfano wa kuiga na kigezo cha kujipima. Wataelewa kuwa wana wajibu wa kujielimisha sana.

Wengi tunafahamu jinsi kiwango cha elimu kilivyoporomoka nchini, kiasi kwamba hata kwenye mahojiano ya kutafuta ajira, wa-Tanzania wanapata taabu. Kwa mfano, taarifa zimezagaa kuwa wa-Tanzania wanaogopa kushindana na wa-Kenya.

Sisi miaka tulipokuwa tunasoma hatukuwa tunawaogopa wa-Kenya, wala wa-Ganda, wala wengine wowote. Tulisoma nao pale Chuo Kikuu Dar es Salaam, bila kuwaogopa kwa lolote. Kwa hali hii, ni muhimu vijana wetu wapewe kila aina ya msaada na changamoto ya kuwajengea mwamko mpya. Mdahalo wa Dr. Slaa una mchango kwa upande huo.

Vile vile, mdahalo huu wa Dr. Slaa unatoa mfano mzuri wa uwajibikaji katika kuitumia lugha ya ki-Swahili. Haipendezi kuona wale tunaowaita viongozi, kama vile wabunge, mawaziri, na wakurugenzi, wakishindwa kukitumia ki-Swahili ipasavyo, na badala yake wanachanganya lugha. Hii ni dalili ya kutoelimika vizuri, na kutoiheshimu lugha yetu ya ki-Swahili.

Nafahamu kuwa wa-Tanzania wengine wakisoma ujumbe kama huu wangu, watarukia mambo ya ushabiki wa vyama vya siasa. Mimi ni raia ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa. Kwa wadhifa wangu kama mwalimu, naangalia maslahi ya vijana wetu kielimu.

Wanaopenda kudhania kuwa mtu akitoa maoni kama yangu basi anahusika na chama fulani cha siasa nawaomba waelewe kuwa msimamo wangu kama mtu asiye mwanachama wa chama cha siasa ni kuwa mifumo ya siasa tunayoifuata Tanzania ni ya kikoloni mambo leo. Haijalishi kama ni chama kimoja au vyama vingi. Haitajenga demokrasia. Nimeelezea hayo katika kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii.

Wednesday, November 3, 2010

Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM

Ingawa alikuwa mwanzilishi wa CCM, kwa nia njema ya kuendeleza mapinduzi katika nchi yetu, miaka ilivyozidi kwenda Mwalimu Nyerere alishuhudia jinsi CCM ilivyobadilika na kuwa mzigo kwake na pia tishio kwa usalama wa Taifa.

Mwaka 1993 Mwalimu alichapisha kitabu kiitwacho Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (Harare: Zimbabwe Publishing House, 1993). Pamoja na mambo mengine katika kitabu hiki, Mwalimu alisema kuwa kuna kansa katika uongozi wa CCM. Nanukuu baadhi ya maneno yake:

Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa Vyama vya Upinzani, kinaweza kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, "potelea mbali:" wakachagua Chama cho chote, ilimradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM. Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa Nchi yetu unataka yasemwe
. (Ukurasa 61)

Mwalimu hakuishia hapo, bali aliongezea namna hii:

Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi isingekuwa ni jambo la kutisha sana kama tungekuwa tumeanza kuona Chama kizuri cha upinzani kinachoweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM. Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliofanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa Vyama Vingi. Nilitumaini kuwa tunaweza kupata Chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM; au ambacho kingekilazimisha Chama cha Mapinduzi kusafisha uongozi wake, kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao. Lakini bado sijakiona Chama makini cha upinzani; na wala dalili zo zote za kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM. Bila upinzani mzuri wa nje, na bila demokrasia halisi ndani ya Chama cha Mapinduzi, Chama hiki kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu. Kwa hali yetu ya kisiasa ilivyo nchini hili si jambo la kutarajia bila hofu na wasi wasi
! (Ukurasa 66)

Ni wa-Tanzania wangapi wenye utamaduni wa kusoma vitabu? Ni wangapi wanaosoma vitabu vya Mwalimu Nyerere? Ni wazi kuwa umbumbumbu miongoni mwa wa-Tanzania ni neema kwa CCM.