Sunday, February 27, 2011

Vitabu vya Chap Chap

Wengi wetu tunalalamika kuwa utamaduni wa kusoma vitabu umefifia au kufa miongoni mwa wa-Tanzania. Malalamiko haya yako sana katika hii blogu yangu. Kwa mfano, soma hapa.

Labda kuna haja ya kufafanua kitu tunachokilalamikia, maana wa-Tanzania hao hao inaonekana wanasoma sana vitabu ambavyo vinatungwa papo kwa papo kuhusu masuala kama vile mapenzi.

Vitabu hivi vinaandikwa haraka na kuchapishwa haraka na ndio maana naviita vitabu vya chap chap. Ni vijitabu, kwani vina kurasa chache tu.


Mwaka jana nilipokuwa Tanzania nilinunua kitabu cha aina hiyo kiitwacho "Pata Mambo, Part 5 ," kilichoandikwa na Fuad Kitogo (Dar es Salaam: Elite Business). Ingawa hiki ni kijitabu cha kurasa 40 tu, kinashughulikia masuala mengi kama inavyooneka katika picha ya jarida hapo juu.

Hivi vitabu vya chap chap si vitabu vyenye kiwango cha kuridhisha kitaaluma, bali vinawavutia na labda kuwaridhisha wasomaji wa ki-Tanzania. Katika ukurasa wa kwanza kuna maelezo haya: "Kitabu hiki ni mwendelezo wa vitabu vya Pata Mambo kuanzia namba moja vinavyopendwa kusomwa nchi nzima."

Kuwepo kwa vitabu hivi na kupendwa kwake ni changamoto kwetu sisi tunaodai kuwa utamaduni wa kusoma vitabu umefifia Tanzania. Labda uvivu tunaoulalamikia uko kwenye kusoma vitabu vikubwa vinavyotumia muda na fikra zaidi katika kuvisoma, tofauti na hivi vya chap chap ambavyo ni rahisi kuvisoma na kuvimaliza.

Friday, February 25, 2011

SUPER MUHOGO: Unga Safi wa Muhogo

Katika pita pita zangu, nimeona tangazo kwenye blogu ya Lady JayDee la wajasiriamali wa Chanika, Dar es Salaam, wanaouza unga wa muhogo. Wamemwomba Lady JayDee awawekee tangazo hilo kwenye blogu yake, naye amefanya hivyo.

Nimevutiwa na jambo hili. Njia madhubuti ya kujenga uchumi wa nchi yetu ni kuzalisha bidhaa na kuziuza nje, ili tupate fedha za kigeni. Kuuza bidhaa zetu nje kunaleta ajira nchini.

Hili ni jambo rahisi kulielewa. Hata mimi ambaye sikusomea somo la uchumi nimeandika kuhusu suala hili katika kitabu changu cha CHANGAMOTO, nikielezea namna mbali mbali jinsi wa-Tanzania tunavyohujumu uchumi wa nchi yetu. Mfano moja ni jinsi tunavyozishabikia bidhaa za kutoka nchi za nje, bila kutambua kuwa tunawapa ajira watu wa nchi zingine. Wakati huo huo, wa-Tanzania wanalalamikia uhaba wa ajira nchini. Tunapaswa kuuza bidhaa na huduma kwa wengine.

Kutokana na yote hayo, nimevutiwa na hao wajasiriamali wanaouza unga wa muhogo. Nimeamua kusaidia kutangaza biashara yao hapa kwenye blogu yangu. Nawatakia mafanikio tele katika kuboresha maisha yao na kuinua uchumi wa nchi.

Wednesday, February 23, 2011

Makala ya "Kwanza Jamii" Yaendelea Kupeta

Niliwahi kuandika kuhusu makala yangu ya kwanza kuchapishwa katika gazeti la Kwanza Jamii, "Maendeleo ni Nini," ambayo hatimaye ilichapishwa huku Marekani, baada ya mimi kuombwa niitafsiri kwa ki-Ingereza. Soma hapa.

Wahenga walisema: dunia ni mduara, huzunguka kama pia. Bila kutegemea, tarehe 20 Oktoba nilipata barua pepe kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa ni mhariri mkuu wa jarida la Monday Developments. Ujumbe wa msingi wa barua yake ni huu:

We cover issues and trends in international development and humanitarian assistance, and are a publication of InterAction—an alliance of 200 U.S.-based international development organizations focused on the world’s poor and most vulnerable people.

One of our upcoming issues will be discussing the topic: Is development the new colonialism? While researching the subject, I came across your article “What is Development? Colonialism Deconstructed” and found it very refreshing. As a journal geared primarily toward global NGO staff, I thought your critique of the term and notion of development would be an interesting point of view to our readers—who often only see their side of the issue.

I wonder if you might consider adapting your article to run in our publication? Our readership includes NGOs, universities, the UN, World Bank, and offices of the U.S. government –exactly the audience who should be exposed to the points you raise.

Sikusita; nilikubali ombi la kuikarabati makala yangu na juzi nimeipeleka. Mhariri amejibu na kushukuru akisema, "You raise interesting points that our NGO readership should consider as they perform their work."

Makala hii, pamoja na zingine nilizochapisha katika Kwanza Jamii imo katika kitabu cha CHANGAMOTO, ambacho kinapatikana mtandaoni, kama inavyoonekana upande wa kulia wa ukurasa huu, na pia Dar es Salaam, simu namba 0754888647 au 0717413073. Nilikichapisha kitabu hiki ili kuwapa wa-Tanzania wengi iwezekanavyo fursa ya kuyafahamu mawazo yangu, kwa lugha ya ki-Swahili.

Nilifanya hivi ingawa najua kuwa vitabu havithaminiwi miongoni mwa wa-Tanzania. Nimejiepusha na lawama. Hatimaye nitapenda kukitafsiri kitabu hiki kwa ki-Ingereza, hasa baada ya kuona jinsi makala hii moja niliyoitafsiri inavyopokelewa na wale wasiojua ki-Swahili.

Naweka taarifa hii hapa iwe changamoto kwa watoto na vijana wetu. Wajizatiti na shule na elimu, kama nilivyofanya na ninavyoendelea kufanya maishani mwangu, bila kuyumbishwa na chochote. Manufaa yake huonekana baadaye.

Sunday, February 20, 2011

Tanzania Yetu ....

Wimbo huu hapa unatukumbusha tulikotoka, na mategemeo yetu miaka ya mwanzo ya Uhuru na hata baada ya "Azimio la Arusha." Tulipata Uhuru tukiwa na matumaini makubwa, na mojawapo alilieleza vizuri Mwalimu Nyerere:

Sisi tunataka kuwasha mwenge, na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, ili umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki, na heshima palipojaa dharau
.

Monday, February 14, 2011

Mwanafunzi Wangu Kaniacha Hoi

Leo kaja ofisini mwanafunzi wangu ambaye amerejea siku chache zilizopita kutoka Tanzania, ambako alikuwa ameenda kujifunza masuala ya huduma za hospitali. Alikuwepo kule kwa mwezi moja.

Kabla ya kwenda Tanzania, alikuwa amechukua somo langu moja. Halafu, alipokuwa anaandaa safari ya Tanzania, tulikutana nikamweleza yale ninayowaelezea wa-Marekani kabla hawajaenda Afrika, kuhusu hali ya Tanzania, na hasa kuhusu tofauti za tamaduni kama nilivyozielezea katika kitabu cha Africans and Americans.

Alivyokuwa Tanzania, alikuwa akiangalia shughuli za madaktari katika hospitali moja mkoa wa Arusha. Kutokana na lengo lake la kuwa daktari, amejifunza mengi. Siku za mapumziko alisafiri hadi Dar es Salaam na Zanzibar, hifadhi za Ngorongoro, Serengeti na Lake Manyara. Pia alipanda Mlima Kilimanjaro.

Tulipomaliza maongezi, alinipa picha, bila mimi kutegemea, aliyopiga akiwa kileleni Mlima Kilimanjaro. Nimeguswa sana na zawadi hii. Raha moja kubwa ya ualimu ni kugusa mioyo, akili, na maisha ya wanafunzi. Nimevutiwa na ubunifu wa mwanafunzi huyu. Sikutegemea kuona jina langu linapepea juu ya Mlima Kilimanjaro. Labda ni changamoto, nijikongoje ili nami siku moja nikafike pale.

Sunday, February 13, 2011

Kitabu Kuhusu Mtume Muhammad

Kati ya vitabu ninavyosoma wakati huu ni Muhammad: A Biography of the Prophet, kilichoandikwa na Karen Armstrong. Ni kitabu murua kwa jinsi kinavyoelezea mazingira aliyoishi Mtume Muhammad na harakati alizopitia katika kutimiza majukumu yake kama Mtume.

Kitabu hiki kinagusa na kuelimisha sana sio tu kuhusu historia ya u-Islam, bali pia kuhusu upekee wa Mtume Muhammad, kama Karen Armstrong anavyosema:

If we could view Muhammad as we do any other important historical figure we would surely consider him to be one of the greatest geniuses the world has known
(uk.52). (Tafsiri yangu: Kama tungemtazama Muhammad kwa namna tunayowatazama watu wengine muhimu katika historia, ni wazi tungemtambua kama mmoja wa watu wenye vipaji vya ajabu kabisa ambao dunia imepata kuwafahamu).

Karen Armstrong ni maarufu kwa msimamo wake kuhusu u-Islam. Anaelezea sana historia ya zile anazoziita hisia potofu kuhusu u-Islam na zilivyoanza na kuenea. Lakini, pamoja na kutafiti na kuandika sana kuhusu u-Islam, Karen Armstrong ni mtafiti wa dini zingine pia, kama vile u-Kristu u-Juda, na u-Buddha. Ni mmoja wa watu wanaoongoza hapa duniani kwa umakini wa kuandika kuhusu dini.

Pamoja na kusoma kitabu cha Muhammad na kufuatilia maandishi mengine ya Karen Armstrong, na pamoja na kufuatilia mihadhara na mahojiano aliyotoa sehemu mbali mbali za dunia, nafuatilia pia maandishi na matamshi ya wengine kuhusu mchango wa Karen Armstrong. Nimebaini kuwa kuna malumbano kuhusu mchango wake, ambalo ni jambo la kutegemewa katika taaluma.

Kitabu cha Muhammad ni kizuri na muhimu sana. Nafurahi kukisoma, kwani kinanifungulia milango ya kuyafahamu maisha na mchango wa mtu ambaye ametoa mchango mkubwa sana duniani. Ni kitabu muhimu kwa yeyote mwenye nia ya kumwelewa Mtume Muhammad na kuuelewa u-Islam.

Karen Armstrong, ambaye alikuwa sista katika Kanisa Katoliki, ambalo ndilo dhehebu langu, anatuonyesha mfano mzuri, kwa kujibidisha katika kuzifahamu dini za wengine. Naamini kuwa iwapo sote tungefanya hivyo, kungekuwa na maelewano mazuri baina ya watu wa dini mbali mbali.

Thursday, February 10, 2011

Kitabu Kinapopigwa Marufuku

Kati ya mambo yanayosumbua sana akili yangu ni kitabu kupigwa marufuku. Sijui kama wewe unaafiki kupigwa marufuku kwa kitabu chochote.

Katika historia ya vitabu, ambayo ni karne nyingi, vitabu vingi vimepigwa marufuku sehemu mbali mbali za dunia, kwa sababu mbali mbali. Vingi vinaendelea kupigwa marufuku.

Tafakari matukio mawili ya kupigwa marufuku vitabu ambayo yametokea Tanzania. Kitabu kimoja ni Satanic Verses cha Salman Rushdie. Kuna watu waliona ni lazima kipigwe marufuku. Kingine ni Mwembechai Killings cha Dr. Hamza Njozi. Nacho kuna watu waliona ni lazima kipigwe marufuku.

Mtazamo wangu kuhusu suala hili nimeuelezea katika kitabu changu cha CHANGAMOTO, ambacho ni cha uchochezi. Labda nacho kitapigwa marufuku.

Tuesday, February 8, 2011

Blogu Imenisaidia Darasani

Leo wakati muhula mpya unaanza hapa Chuoni St. Olaf, nimekutana na wanafunzi nitakaowafundisha somo la kuandika kwa ki-Ingereza. Kama kawaida, siku ya kwanza huwa ni ya kujitambulisha, kuelezea habari za somo, maana yake, falsafa na maadili yangu kama mwalimu, maana na mikakati ninayotumia katika kufundisha.

Katika kujitambulisha, huwa nawaeleza wanafunzi kuhusu nyumbani kwangu, shule nilizosoma, na nilivyoingia katika kazi ya ualimu, na imani yangu kuwa Mungu alitaka niwe mwalimu.

Leo wakati naanza kuelezea habari za nyumbani kwangu, nilikumbuka kuwa nilishaandika kwenye blogu. Basi, niliwasha kompyuta iliyomo darasani nikafungua blogu na wao wenyewe wakasoma kwenye skrini kubwa habari za Litembo.

Blogu imenisaidia kufikisha ujumbe wangu kwa ufanisi, kwani mbali ya maelezo kuna picha. Picha zinajieleza vizuri kuliko pengine hata maneno, jambo linalosisitizwa katika ule usemi kuwa picha ni sawa na maneno elfu. Niliwaambia kuwa nina picha nyingi za nyumbani kwangu na Tanzania kwa ujumla. Ni wazi kuwa ninazo fursa tele za kuendelea kuwajulisha walimwengu habari za kwetu.

Thursday, February 3, 2011

Mji wa Moshi, Tanzania

Moshi ni mji maarufu kaskazini mwa Tanzania, chini ya Mlima Kilimanjaro. Siufahamu sana mji huu, ingawa nimepita hapo mara kadhaa, na hata kulala, mara mbili tatu.






Kama ilivyo katika miji mikubwa ya Tanzania, Moshi kuna hoteli nzuri za kufikia wageni. Wakati moja nililala katika hoteli hii hapa kushoto.









Moshi ni maarufu kwa usafi. Wa-Tanzania wanajua kuwa uongozi wa Moshi una sheria kali kuhusu usafi. Hapo kushoto nipo kituo cha mabasi, pasafi kama vile pamepigwa deki. Nilikuwa safarini baina ya Arusha na Dar es Salaam. Nimechoka, shaghalabaghala; msafiri kafiri na kitabu changu cha Under Kilimanjaro.

Tangu mara yangu ya kwanza kuingia mjini Moshi, nilivutiwa na msikiti unaoonekana kushoto, ambao uko pembeni mwa kituo cha mabasi.







Wakati mmoja nilikuwa Moshi na wanafunzi kutoka Chuo cha Colorado, niliowaleta nchini kuwafundisha kuhusu mwandishi Ernest Hemingway alivyosafiri nchini mwetu akaandika juu yake. Niliwapeleka hadi Chuo cha Mweka, kinachoonekana kushoto. Kiko nje kidogo ya mji.

Ninapokuwa katika mji wowote napenda kujua maktaba ilipo. Hapo kushoto ni maktaba ya mkoa. Niliingia ndani, nikaona ilivyo nadhifu. Ina majarida na vitabu kiasi cha kuridhisha, nikifananisha na maktaba nilizoziona mikoani Tanzania. Nilivutiwa kuwaona watu wakisoma, sio watoto wa shule tu, kama ilivyo kwenye maktaba zingine.

Nilitembea kutoka Lutheran Uhuru Hostel kuelekea barabara kuu itokayo Arusha, nikaiona hoteli hii inayoonekana kushoto. Nilivutiwa na tangazo la mchemsho, ingawa sikupata kuingia ndani. Hamu ya kuingia nilikuwa nayo, kwa mategemeo ya kupata chakula cha ki-Chagga. Ni suala muhimu la kuzingatiwa siku za usoni, panapo majaliwa.

Wednesday, February 2, 2011

Kauli ya Mufti Simba Kuhusu wa-Islam na Elimu

Nimesoma kwa furaha taarifa kuwa Mufti wa Tanzania, Shekhe Mkuu Issa Shaban Simba, amewataka wa-Islam Tanzania wajibidishe na elimu ili kujikomboa kimaisha. Amenukuliwa akisema, "Huu ni muda mwafaka kwa waislam kuanza kujikita na kukazania zaidi suala la elimu, na si kubaki kulialia pekee kuomba kuchaguliwa na kupewa vyeo serikalini, hivyo tuchangamke tusiendelee kubaki nyuma tupige hatua kama wenzetu." Soma taarifa hii hapa.

Nilikuwa njiani kuandika makala kuhusu suala la elimu katika historia ya u-Islam, ili kuiweka katika blogu hii. Baadhi ya mambo niliyopangia kusema ni kwamba u-Islam, tangu mwanzo, ulihimiza suala la elimu katika taaluma mbali mbali. Mtume Muhammad alisisitza suala hilo na waumini wakafuata kwa makini. Anayosema Mufti Simba ndio ukweli kwa mujibu wa dini ya ki-Islam.

Makala yangu inakuja. Kwa leo napenda tu kusema kuwa msisitizo wa Mufti Simba kuhusu elimu unatuhusu sisi wote, si wa-Islam peke yao. Ninaandika sana kuhusu suala hilo kwenye blogu na sehemu zingine, kama vile kitabu cha CHANGAMOTO, nikilalamika kuhusu uvivu uliokithiri miongoni mwa wa-Tanzania katika suala la elimu. Kwa hivi namwunga mkono na kumpongeza Mufti Simba kwa kusimama kidete kuongelea suala hilo. Yeye kama kiongozi wa wa-Islam amewataja wao, lakini ukweli ni kuwa nasaha zake zina manufaa kwa wa-Tanzania wote.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...