Kila mwaka, ninapokuwa Tanzania, napiga picha nyingi niwezavyo na kuja nazo huku Marekani. Mwaka huu nimepiga picha nyingi sehemu nilizopata fursa ya kuzitembelea: Arusha, Dar es Salaam, Lushoto, Morogoro, Moshi, na Tanga.
Watu ambao wameishi Tanzania tu wanaweza kuuliza kwa nini napiga picha hata sehemu ambazo si za pekee au muhimu. Siwezi kuwalaumu. Huku ughaibuni mambo ni tofauti, na napenda nitoe fununu kidogo.
Mbali na kufundisha hapa katika chuo cha St. Olaf, ninashughulika na programu zinazopeleka wanafunzi Tanzania na sehemu zingine za Afrika. Kazi yangu ni kuwaandaa hao wanafunzi, kwa kuwaeleza mambo ya utamaduni, maisha, elimu, na kadhalika yahusuyo nchi hizo wanakokwenda.
Picha zangu hizi ni hazina inayonisaidia katika shughuli hizi. Mbali ya kuwaelimisha, zinawahamasisha katika kupenda kuja Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Wiki iliiyopita, niliporejea hapa chuoni kutoka Tanzania, mkuu wa idara yangu ya ki-Ingereza aliomba nitundike picha za Tanzania kwenye ubao wetu wa matangazo. Niko katika harakati ya kuziandaa. Ni fursa ya kuitangaza Tanzania, nami nimeipokea kwa furaha. Picha hizi zitakaa hapo kwa wiki kadhaa, labda miezi.
Napangia kutundika picha za Chuo Kikuu Dar es Salaam, maeneo ya miji niliyoitembelea na vijiji mbali mbali. Nitatundika picha za matukio mbali mbali. Nitatundika picha za makanisa na misikiti, nikizingatia kuwa wa-Marekani hawajazoea kuona misikiti, na mbaya zaidi, wengi wana mawazo potofu kuhusu misikiti na u-Islam, kama nilivyogusia hapa. Hizi picha zitachangia kuwaelimisha.
Jambo la ziada ni kuwa ninazunguka sehemu mbali mbali hapa Marekani nikitoa mihadhara kuhusu masuala kama elimu na tamaduni, kama inavyoonekana katika blogu zangu. Basi, katika mizunguko hiyo, picha zangu ni hazina mojawapo na nyenzo ya kuelimishia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
4 comments:
Mwalimu, tunazisubiri hizi picha kwa hamu. Naamini utatushirikisha.
Shukrani kwa ujumbe. Baadhi ni hizi ambazo zimeanza kutokea kwenye blogu zangu. Nitaendelea kuzileta hapa.
Ni kweli mwalimu, unafundisha na kuonyesha kwa vitendo, kwa mfano ukiwafundisha au kuwaelezea kuhusu mlima Kilimanjaro au twiga na una picha yake huyo mtu ataelewa zaidi.
Kwahiyo unapoielezea Tanzania kwa wazungu na kuwaonyesha hali halisi katika picha kila mmoja atavutika na kuitafuta vyema nchi hii, na hapo utakuwa umeitangaza.
Hongera na sisi inabidi tukupe ahsante kwa kuipenda sana nchi yako
Shukrani, emu-three, kwa ujumbe wako. Ni kweli unavyosema kuhusu umuhimu wa vielelezo.
Miezi michache iliyopita nilinunua kitabu kiitwacho Going Visual: Using Images to Enhance Productivity, Decision Making and Profits."
Kitabu hiki kinaelezea vizuri umuhimu wa picha katika nyanja mbali mbali, si elimu tu. Kinaanza kwa kutukumbusha kuwa hata wale binadamu wa mwanzo kabisa walioishi mapangoni, walichora picha kwenye kuta za mapango, katika kujieleza.
Post a Comment